Kumbukumbu zangu hunikumbusha na kunielekeza kwamba vitu vina jozi, maumbo yana pande mbili na majambo yana sehemu mbili – ziwe zinafanana au hazifanani, ziwe hasi au chanya, jibu kamili ni mbili.

Mathalani, kuna mbingu na ardhi, usiku na mchana, ukweli na uwongo, shina na ncha. Kadhalika raha na tabu, mtoto na mkubwa, kijana na mzee, mwanamume na mwanamke na kadha wa kadhaa. Hata wana Kilwa Jazz Band waliwahi kuimba ‘hata ndege huishi wawili wawili.’ 

Fasihi inanielekeza kuangalia maneno mawili. Haki na batili. Mimi na wewe si wageni wa maneno hayo kusikia au yanavyotumiwa na baadhi ya watu katika kutenda haki na batili. Dunia leo inaogelea katika batili na ina tapatapa katika kutafuta haki.

Haki na batili ni dhana mbili kinzani katika maisha ya binadamu. Hata kwa wanyama, ndege na wadudu. Haki inapotaka kuendesha dunia, batili huchomoza haraka kuzuia haki isitimize kusudio lake. Sijafahamu kwa vipi inakuwa hivyo, labda kila moja ina silika yake ya kujichomoza.

Haki ni ukweli na uhuru wenye mwangaza. Batili ni uwongo na giza lililojaa upotovu. Kinyume cha haki ni batili. Kwa hiyo, siku zote duniani kuna mvutano na mapambano makali ya asili baina ya dhana hizo mbili. Lini yatakoma sielewi. Labda wewe msomaji unajua na nijuze nitambue.

Waumini wa dini duniani wanaeleza haki inatoka kwa Mwenyezi Mungu na inasimamiwa na malaika chini ya uangalizi wake. Batili inaendeshwa na watu waovu chini ya uongozi wa ibilisi aliyelaaniwa na Muumba wa ardhi na mbingu na vyote vilivyomo duniani.

Sheria na kanuni zimewekwa na binadamu wema kuheshimu na kulinda haki ya Mwenyezi Mungu. Lakini binadamu waovu usiku na mchana wanavunja sheria na kanuni zilizopo na kuunda zao za kukinza haki kutendeka. Hayo ni mapambano makubwa yanayohitaji umoja wenye nguvu kukabiliana nao.

Angalia yanayofanyika katika mabara yote duniani – Marekani, Asia na Uarabuni, Ulaya na Afrika jinsi batili inavyoenziwa na kuumuka mithili ya ngano iliyotiwa hamira. Vyama vya siasa na serikali zinavyoyumba katika uongozi na utawala kutokana na visingizio vya kutafuta haki za binadamu kumbe wanafanya batili. Hata viongozi wa dini wametumbukia katika hilo.

Tazama huko Asia, Afrika na Uarabuni watu wanavyouawa. Viongozi wa siasa na serikali wanavyong’ang’ania madaraka. Watoto wanavyoteseka na kuuawa bila ya hatia. Duniani wanawake wanavyodhalilishwa, wanavyofanywa kama bidhaa na mabango ya biashara. Wauza unga wanavyounda na kuimarisha mamia ya mateja na kupoteza utu na nguvu kazi ya watu.

Hapa nchini kuna migogoro ya wakulima na wafugaji katika mikoa mbalimbali. Uporwaji wa ardhi na mashamba ya wamiliki wa asili na kupewa wawekezaji, matajiri na wenye nguvu. Wenye haki wanapolalamika mbele ya sheria, vyombo vya sheria na mamlaka husika hufanya figisufigisu.

Hivi majuzi, kupitia vyombo vya habari, uchunguzi uliofanywa na gazeti JAMHURI, ulibaini kuna mgogoro kati ya wananchi wa Ng’wale, mkoani Mtwara, TPA (Bandari Mtwara) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo. Mgogoro huu una dalili ya kufukua makaburi. Kama hapana budi yafukuliwe ili haki itendeke.

Watanzania wazalendo tunahitaji maendeleo chanya. Maendeleo ya kuondoa umaskini, kujenga nchi ya viwanda, kuboresha na kuimarisha uchumi na kuinua kiwango cha bandari zetu nchini (ikiwamo ya Mtwara ), ambazo ni lango kuu la uchumi wetu. 

Baada ya kurejea taarifa za migogoro iliyopita mkoani Mtwara ya utumiaji wa gesi, stakabadhi ghalani, kiwanda cha saruji cha Dangote n.k na sasa wananchi wakazi wa kitongoji cha Ng’wale kutoshirikishwa na kuporwa ardhi yao, si jambo la masihara hata kidogo. Hapo lazima kazi ifanyike.

Kwa vile Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha haipendi batili na figisufigisu dhidi ya wananchi wake na kuweka nia ya kurudisha haki ya wananchi, naishauri Serikali Kuu kuingilia kutanzua mgogoro huo uliodumu kwa miaka 17.

Hali halisi kwa Serikali Kuu ya Awamu ya Tano isiache kuwaokoa wananchi wa Ng’wale kwa kuamini figisufigisu inayofanywa na baadhi ya bora viongozi wa ngazi ya chini na watendaji wa ofisi ya mkoa, kuhofia kufufua makaburi. Hiyo haitakuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli. Haiko hivyo ng’o.

881 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!