*Wataalamu waonya usafiri Ziwa Victoria si salama
*Wahoji nchi ilivyojiandaa kukabili majanga mapya
*Wengi wakumbuka yaliyotokea kwa MV Bukoba
*Waziri Mkuu aeleza ya moyoni, kivuko kuvutwa

Na Mwandishi Wetu, Ukara

Wahandisi na wataalamu wa majanga wamesema Tanzania inakabiliwa na hatari kubwa mbele ya safari iwapo serikali haitafanya uamuzi mzito katika usafiri wa majini, JAMHURI limeelezwa.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti wilayani hapa Ukerewe, wahandisi wawili walioomba wasitajwe majina gazetini wamesema meli zinazomilikiwa na serikali zinapaswa kuchunguzwa zaidi.
“Mheshimiwa Rais ana nia njema na nchi hii, ila sheria na taratibu za kuendesha meli zilizopo ni za hatari. Tunajua huu ni wakati wa kupeana faraja, kwani tuko msibani, lakini ni bora tuyasema haya ili tume itakayoundwa iyachunguze na nchi yetu iondokane na tatizo hili milele,” amesema mhandisi kutoka mkoa jirani na Mwanza aliyefika kisiwani hapa kutambua mwili wa ndugu yake.
“Meli hizi hazina bima. Hazifanyiwi ukaguzi wowote. Watu wanaoziendesha sifa zao haziainishwi kisheria kama meli za wafanyabiashara binafsi. Kwa kweli nasema kuna usiri mkubwa katika kuendesha meli zinazomilikiwa na serikali na hili wanalifanya makusudi kutafutia ndugu zao kazi.
“Ndiyo maana utaona nahodha halisi amemkabidhi mtu ambaye alikuwa ‘mwendesha mtumbwi’ jukumu la kuendesha meli na kwa kuwa hakusomea kazi hii, amejua kwa uzoefu na hana maadili ya kazi akawa anaongea na simu, anasoma meseji wakati kivuko kinatembea na matokeo yake amekipindua naye akafa… hii ni hatari kubwa. Tuidhibiti,” amesema.
Mtaalamu wa majanga mmoja naye amezungumza na JAMHURI na kueleza hatari mpya iliyopo mbele ya taifa letu. “Serikali inajitahidi inanunua meli kubwa na za kisasa. Lakini ni lazima iwe na mfumo wa uokozi na kudhibiti majanga. Kwa mfano mwaka 1996 ilipopinduka meli ya MV Bukoba kama serikali ingenunua kreni ya kunyanyua meli majini, leo wasingekufa watu wengi kiasi hiki.
“Kreni hiyo ingefika ikainua hii meli na kunusuru maisha ya watu. Lakini miaka 22 baada ya ajali ya MV Bukoba bado kivuko kimeanguka nchi haina msaada wowote. Na sasa nchi yetu inanunua meli kubwa, lazina iwekeze katika kreni za uokozi. Hivi hiyo siku meli hiyo kubwa ya kubeba watu 1,200 kwenda Bukoba kikipinduka mambo yatakuwaje? Ni lazima tujiandae kudhibiti majanga, bila hivyo siku zijazo tutalia tena,” amesema mtaalamu huyo.
Maofisa watatu waliokuwa wanasimamia kivuko cha MV Nyerere kilichopinduka na kuua watu 224 wamekamatwa, wakiwa vilabuni wanalewa pombe, huku wenzao watano wakifikia ndani ya kivuko, JAMHURI limeelezwa.
Habari za uhakika zinasema maofisa watatu waliokuwa mnadani Ukara walikamatwa wakiwa wanaburudika bila kujua kuwa kwa kushindwa kusimamia kazi yao sawa sawa wamesababisha maafa.
‘Nahodha’ wa kuazima aliyekuwa anaendesha Kivuko cha MV Nyerere anaelezwa kuwa alikuwa anazungumza na simu wakati wanakaribia kutia nanga. “Nahodha alikuwa anazungumza na simu. Alipokaribia daraja (gati) kuja kuhamaki akakuta daraja ameliacha kushoto. Kwa hiyo akakata ghafla, meli ikaenda upande na kupinduka,” amesema.
Akizungumzia ajali hii, mtaalam huyo amekumbushia yaliyotokea wakati wa ajali ya MV Bukoba: “Wakati ule tuliisamehe serikali kwa kusema labda tulikuwa bado taifa changa. Tulishuhudia watu wanakata meli eti kutoa watu, ikazima moja kwa moja. Zamu hii tunajiuliza, imekuwaje wakasitisha uokoaji saa tatu usiku eti giza limeingia?
“Wakati serikali imesitisha uokoaji, wavuvi wameendelea kuopoa miili kwa kutumia karabai na mitumbwi. Sitaki kuamini kuwa kila siku tunaendelea kujifunza. Tutahitimu lini? Majanga kama haya si ya kuchekea. Kwa nchi kama China watu waliofanya uzembe wa kiwango hiki wanapigwa risasi. Nadhani hata sisi tufikirie kwenda huko kwa watu wanaofanya makosa ya wazi kama haya ya kujaza meli kupita kiasi,” ameongeza.

Waziri Mkuu azungumza

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amezungumza na JAMHURI na kuliambia kuwa hali ni ya masikitiko makubwa katika Kisiwa cha Ukara, ila serikali imeamua kuwafariji wananchi. “Unajua wananchi wamefiwa. Wanahitaji comfort (faraja). Yaani wananchi wanafarijika kuona kwamba tuko nao.
“Tunazunguka pale kwenye corridor, tunaingia chumba hiki tunaangalia miili na wao wanakagua, wanatambua miili, wanasema huyu ni ndugu yangu, anaandaliwa… wanasafirisha wanakwenda kuzika nyumbani na viongozi wakiwapo. Sasa siwezi kutoka hapa yaani mpaka nione mwili wa mwisho… mpaka ile meli waiinue, tukague, tujue ile meli ina miili mingapi tufanye maamuzi,” amesema.
Hadi Jumapili jioni, miili 224 ilikuwa imeopolewa. Wanaume zaidi ya miaka 18 walikuwa 71 na watoto wa kiume wenye umri chini ya miaka 18 walikuwa 10. Wanawake wenye umri zaidi ya miaka 18 ambao miili yao imeopolewa ni 126, na watoto wa kike wenye umri chini ya miaka 18 walikuwa 17.
Hivyo, jumla ya wanaume waliothibitika kufariki dunia hadi sasa ni 81 na wanawake ni 143, idadi inayofanya jumla kuu ya watu wote waliothibitika kufariki dunia katika ajali hiyo kufikia 224. Hadi tunakwenda mitamboni, watu 219 walikuwa wametambuliwa na watano walikuwa hawajatambuliwa na ndugu zao.
Ukichanganya watu hao 224 waliofariki dunia na 41 waliookolewa, idadi ya watu waliokuwa wamebebwa na kivuko hicho sasa imethibitika kufikia 265.
Awali Waziri Mkuu Majaliwa amesema wakati anahutubia taifa kwenye ibada ya mazishi kuwa ajali hiyo ni tukio lililoacha majonzi makubwa. Kivuko cha MV Nyerere kilibeba abiria wengi na mizigo kuzidi uwezo wake.
Amesema kutokana na tukio hili la kusikitisha serikali imefanya juhudi za kuopoa miili, kutoa pole ya Sh 500,000 kwa kila mwili na vyombo ya uokoaji vinaendelea kutambua miili inayopatikana.
Majaliwa amesema serikali inaunda tume kuchunguza ajali hiii itakayojumuisha wataalamu na vyombo vya usalama kubaini chanzo cha ajali. Tume hiyo itatangazwa hivi karibuni.
Serikali imeanza kuchukua hatua kwa kuwakamata maofisa waendeshaji wa kivuko hicho kwa mahojiano ya awali na wote waliohusika watachukuliwa hatua.
“Tayari tumewakamata maofisa wote waliokuwa wanahusika na usalama wa majini (wilayani Ukerewe).
Meli ya MV Nyehunge imeletwa kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma kwa wakazi wa visiwa vya Ukerewe wakati serikali ikifanya utaratibu wa kupata kivuko cha kudumu.
“Baadhi ya fedha zitakazopatikana kupitia michango katika akaunti iliyofunguliwa kwa ajili ya maafa zitatumika kujenga uzio na mnara katika makaburi ya waliokufa kwenye ajali hiyo. Mnara huo utakuwa na orodha ya watu waliofariki dunia katika ajali hiyo kwa ajili ya kumbukumbu.
“Tumefungua akaunti ya MV Nyerere namba 31110057246,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza kuwa fedha zitakazopatikana zitasaidia waathirika na sehemu yake itatumika kujenga uzio na mnara wenye majina ya wote waliofariki dunia.
Ameeleza kuwa anatarajia kuendelea kuwepo kisiwani Ukara mpaka shughuli ya uopoaji wa miili itakapomalizika. “Mimi nitaendelea kubaki Ukara mpaka zoezi litakapokamilika la uopoaji na kuzika miili itakayokosa ndugu.
“Tutaivuta meli kuileta ufukweni, huku mnaita mwaloni. Tutaendelea na mazishi pale tutakapopata mwili mwingine, nami nitaendelea kubaki Ukara kusimamia zoezi hili,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema serikali imeendelea kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Victoria kwa kuanza kujenga meli kubwa ya kwenda Mkoa wa Kagera na vivuko vipya vya Ukara na Bugolora.
“Taifa limepata msiba mkubwa sana, wito wetu ni tushikamane. Ni majonzi makubwa sana, wafiwa wanahitaji faraja. Tujipe moyo, ni mapenzi ya Mungu. Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aendelea kuwaponya majeruhi wote na awalaze marehemu wote mahali pema peponi. Amina,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Muhagama, ametangaza namba ya Tigo Pesa ya kutoa mchango. Namba hiyo imesajiliwa kwa jina la RAS Mwanza. 0677030000 ambapo kwa watakaoguswa wanaombwa wachangie.
Maiti zilizotambuliwa ni 219 ambazo zimechukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya maziko. Ambao hawajatambuliwa wamechukuliwa vipimo vya utambuzi (DNA) waweze kutambuliwa na ndugu zao baadaye iwapo watajitokeza. Katika ajali hiyo watu 41 waliokolewa wakiwa hai.
Kivuko kilibeba watu zaidi ya 265 kwa idadi iliyopo sasa, wakati uwezo wake ni kubeba watu 101.
Mhandisi Kamwelwe amesema mazishi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, kisiwani Ukara, Ukerewe, mkoani Mwanza yatakuwa ya kitaifa ambapo viongozi wakuu wa kitaifa wanatarajia kushiriki mazishi hayo.
Hadi tunakwenda mitamboni uokoaji na uopoaji wa miili ya watu waliokuwa kwenye kivuko cha MV Nyerere ulikuwa unaendelea, ikiwamo kuvuta kivuko hicho kisha kukigeuza na kukisogeza ufukweni, kazi inayotarajiwa kufanyika kwa kipindi cha wiki moja.
Vikosi vya uokoaji Mkoa wa Mwanza viliongezewa nguvu na vikosi vya Mkoa wa Mara katika eneo la tukio kuongeza kasi ya kuopoa miili ya watu waliopinduka na kivuko hicho.
Uongozi wa Wakala wa Meli, Mkoa wa Mwanza umetambua wafanyakazi wa kivuko watano ambao wamepoteza maisha akiwemo nahodha, fundi, karani, mlinzi na mkuu wa kivuko. Kivuko hicho kilikuwa na wafanyakazi wanane.
Mamia ya wakazi wa Ukerewe walikusanyika nje ya Kituo cha Afya cha Bwisya kutambua miili iliyoopolewa kwenye ajali iliyotokea wakati wakisafiri kutoka Kisiwa cha Bugolora kwenda Ukara kwenye gulio.
Kivuko cha MV Nyerere kilichokuwa kinafanya safari zake kati ya Bugolora na Kisiwa cha Ukara katika Ziwa Victoria kilizama huku taarifa za idadi ya watu waliokuwemo ndani ya kivuko zikiwa bado zina utata.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana amesema kivuko hicho kilizama wakati kikielekea katika Kisiwa cha Ukara mchana wa Septemba 20.
Kivuko cha MV Nyerere kilinunuliwa na kuanza kutoa huduma mwaka 2004. Kilifungwa injini mbili mpya zenye thamani ya Sh milioni 191 Julai mwaka huu. Kivuko cha MV Nyerere kina uwezo wa kubeba tani 25 sawa na abiria 101 na magari matatu kwa wakati mmoja.
Taarifa za awali zimeeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kivuko hicho kubeba zaidi ya abiria 400, pamoja na mizigo mingi ambayo ilikuwa ni magunia ya mahindi, kreti za bia na soda. Kivuko cha MV Nyerere kilipinduka Septemba 20, mwaka huu saa nane mchana.

Jukumu la nahonda

Nahodha wa meli mzoefu, Ibrahim Bendera, amesema vyombo vinavyotumia bahari au maji vipo vya aina mbili ambavyo vinasimamiwa na sheria mbili kwa Tanzania. Kuna vivuko ambavyo vina sheria yake maalumu inaitwa Ferris Act No. 173 ya Tanzania, lakini meli nyinginezo zinatumia Sheria inayoitwa Merchant Shipping Act ya Mwaka 2003.
Anasema sheria hizo mbili, hazitambui meli za serikali. Kifungu cha 15 cha Ferris Act hakitambui kwamba meli za serikali lazima zifuate sheria hiyo. Kifungu cha 3(2)(d) cha Sheria ya Shipping Act hakitambui meli ya serikali kufuata sheria hiyo.
“Kifungu hicho cha 3(2)(d) kinasema: Kwanza inaanza (a) meli za polisi, (b) meli za jeshi n.k. mpaka (d) meli zote za serikali hazitakiwi kufuata sheria hiyo. Ukija kwenye Ferris Act kifungu cha 15 kinatamka kabisa kwamba meli za serikali hazitakiwi kufuata sheria hiyo. Sasa hizo sheria mbili ndiyo zinatoa msimamo nahodha afanye nini.
“Bila sheria hizo serikali inajua yenyewe inapata wapi msimamo nahodha wa chombo chake aweje,” amesema Kapteni Bendera.
Swali: Tumemsikia rais wakati akielezea tukio lenyewe, taarifa alizopewa ni kwamba hata nahodha hakuwemo kwenye chombo.
Jibu: Sasa yeye kaambiwa kwamba nahodha hakuwemo kwenye chombo, sasa hatuwezi kujua na kama ni nahodha wa kivuko, sifa zake si lazima zifuate Merchant Shipping Act.
“Kama kivuko ni cha serikali, yeye Mheshimiwa Rais ndiye anajua sheria ya serikali inasemaje kuhusiana na elimu, unahodha wa mtu ambaye anaendesha meli ya serikali.
“Unapoenda kwenye boti ya polisi wenyewe wanajua nahodha wa boti ya polisi anakuwaje, ukienda kwenye boti ya navy wenyewe wanajua na pia kama nilivyokueleza mwanzoni hizi sheria mbili haziwahusu wanaofanya kazi ndani ya meli za serikali. Kwa hiyo, lazima hiyo tume atakayokuwa ameunda itatueleza.
Swali: Ajali nyingi hapa nchini mara nyingi huwa tunasikia kwamba chanzo chake ni kuzidishwa kwa shehena na hata hii tumesikia kwamba abiria walikuwa wamezidi, shehena ilikuwa ni kubwa zaidi. Nafasi ya nahodha ni ipi kabla chombo kung’oa nanga?
Jibu: Kwanza hiyo dhana kwamba chombo hiki kimezama kwa sababu ya mizigo mingi au abiria wengi (si sahihi), kwanini kisizame Ukerewe kilipoanzia? Mbona kilikuwa kinaelea pale?
Kwanini kimezama baada ya kupita maili kadhaa karibu na Ukara ndipo kimezama? Unajua technically, unajua ule ‘mleoleo’ wa meli, yaani ship stability kuna kitovu cha uzito tunaita centre of gravity. Kuna sehemu inaitwa metacentric height ambayo pale inapogeuka upande mmoja kwenda upande mwingine.
Sasa inatakiwa ikiwa iko stable, iko sawa sawa inatakiwa ikienda upande mmoja irudi, inaitwa righting moment. Sasa kwa meli hizi za serikali sijui kama in stability booklet.
Kwa sababu ingekuwa ni meli iliyosajiliwa chini ya Merchant Shipping Act ningekuhakikishia kwamba kutakuwa na mkataba wa kimataifa wa Safety Life at Sea wa mwaka 74, yaani SOLAS Convention inayosimamia hiyo meli.
Sasa kama nilivyokueleza mwanzoni, meli za serikali hazitakiwi kufuata hizi sheria mbili. Sijui wanafuata utaratibu gani, nahodha wake anatakiwa ajue nini na afanyeje. Hiyo tume atakayokuwa ameunda rais itatuambia.

Mhandisi ashangaza wengi

Kitendo cha Mhandisi Alphonse Charahani wa Kivuko cha MV Nyerere siku tatu baada ya ajali akiwa hai kimeshangaza wengi. Charahani ameokolewa Jumamosi, Septemba 22, alfajiri akiwa hai. Alikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Bwisya, Ukara akapatiwa matibabu ya awali na baadaye akapelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando.
Inaelezwa kuwa Charahani alijipaka grisi karibu sehemu zote za mwili hali iliyozuia maji kupenya kwenye ngozi yake akabaki anapumulia kwa juu katika sehemu ya wazi iliyokuwa haina maji.
Rais John Magufuli amehutubia na kutangaza siku nne za maombolezo ambapo bendera zinapeperushwa nusu mlingoti tangu Ijumaa. Ameagiza watendaji wote waliohusika na kadhia hii kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

Jukwaa la Wahariri latoa salamu

Jumapili Septemba 23, 2018 Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alituma salamu za pole kwa Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli, wafiwa, wanafamilia ndugu na jamaa kwa kusema:
“Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za kupinduka kwa kivuko cha MV Nyerere kilichokuwa kinatoka Bugolora kwenda Ukara, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza, Septemba 20, mwaka huu. Hadi sasa taarifa zilizopo ni kuwa zaidi ya watu 200 wamepoteza maisha katika ajali hiyo.
“Ajali hii inarejesha kumbukumbu mbaya kwa Watanzania kwani inawakumbusha ajali za MV Bukoba (1996) katika Ziwa Victoria ambako watu zaidi ya 800 walipoteza maisha, MV Spice Islander (2011) katika Bahari ya Hindi, ambako zaidi ya watu 200, walipoteza maisha, huku MV Skagit nayo ikizama kwenye bahari hiyo hiyo na kupoteza maisha ya watu karibu 150 mwaka 2012.
“TEF inatoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli, familia za wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki.
“Tunafikiri wakati umefika wa Tanzania kuzuia kuendelea kushuhudia majanga kama haya ambayo kwa hakika yanataka kugeuka kuwa utamaduni wa uendeshaji wa vyombo vya majini nchini.
“Tunaisihi serikali, wananchi na wadau mbalimbali kuongeza elimu ya udhibiti wa majanga, huku tukijenga utamaduni wa kuheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa usalama wa abiria.
“Tunaamini utafanyika uchunguzi wa kina na waliohusika na uzembe huu uliogharimu maisha ya Watanzania watafikishwa katika vyombo vya sheria.
“Tunaomba katika kipindi hiki kigumu tuwe na utulivu, tuendeleze umoja na mshikamano wa Watanzania, huku tukivisihi vyombo vya dola vinavyofanya uchunguzi kuharakisha uchunguzi na kuwatendea haki waliohusika kwa mujibu wa sheria.
“Tunaomba Mungu awape nafuu manusura waliojeruhiwa na pumziko la milele Watanzania wenzetu waliopoteza maisha. Amina.”

Wataalamu wanena

Timu ya wataalamu kutoka Songoro Marine wamemwambia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuwa watatumia muda wa wiki moja kuvuta kivuko kilichoanguka na kukifikisha ufukweni kwa kutumia tingatinga.

TEMESA

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Musa Mgwatu, amesema TEMESA watahakikisha wananunua mafuta kwa ajili ya kusafirisha miili ya maiti kutoka Ukara kwenda Bugolora kwa ajili ya kivuko cha MV Nyehunge ambacho sasa kinatumika kwa shughuli za usafirishaji na uokoaji.
Temesa imegharamia majeneza kwa ajili ya maziko, pamoja na kufanya manunuzi ya vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya kunyanyua kivuko cha MV Nyerere ikiwa ni pamoja na tingatinga, air bugs na kamba ngumu (wire rocks).

Mkuu wa Majeshi

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo, amesema ingawa wataalamu wamesema kuwa kazi ya kuvuta kivuko itachukua siku saba, kutokana na mtambo uliokuwa unategemewa kuwasili visiwani humo itawachukua muda mfupi zaidi.
Amesema wanaweza kutumia siku mbili au tatu kukisimamisha tena kivuko hicho cha MV Nyerere ambacho kimepinduka.

Mazingira ya kuzama MV Nyerere

Mashuhuda walionusurika wanasema walianza safari kuelekea Ukara huku kivuko hicho kikiwa na idadi kubwa ya watu na mizigo, na kwamba kabla kivuko hicho hakijaanza safari baadhi walimuonya nahodha kutojaza mizigo, lakini hakutaka kuwasikiliza.
Wanaeleza kuwa hali hiyo haikuwazuia wao kupanda katika kivuko hicho na kuianza safari kutoka Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara na kwamba siku hiyo safari ilienda haraka sana tofauti na ilivyozoeleka kwa kivuko hicho kutembea polepole.
Inaelezwa kuwa wakati kivuko hicho kikikaribia kutia nanga pwani ya Ukara, kilishindwa kulielekea ghati na badala yake kilianza kuelemea upande mmoja, hali inayotajwa kusababishwa na nahodha ambaye kwa wakati huo alikuwa anazungumza na mtu kupitia simu yake ya kiganjani.
Kutokana na mizigo mingi ambayo siku hiyo ilikuwa imepakiwa kwenye kivuko hicho, inaelezwa kuwa uzito ulianza kuegemea upande mmoja na kwamba magunia ya mahindi na kreti za soda na bia vilianza kutumbukia kwenye maji. Wakati huo huo maji yalianza kuingia kwenye kivuko hicho.
Mashuhuda wanasema kivuko kilikuwa kimepakia magari mengi, hata sehemu ambayo abiria walipaswa kusimama palipangwa magari pia.
Inaelezwa kuwa kabla kivuko hicho kuanza safari abiria waliwahoji wafanyakazi kwanini wanaruhusu magari kuingia wakati kimejaa, lakini wafanyakazi hao hawakujali, badala yake waliwajibu kwamba wasiwapangie kazi.
Hadi tunakwenda mitamboni kazi ya uokozi ilikuwa inaendelea na serikali ilikuwa imetangaza mchakato wa kuunda tume ya kuchunguza ajali hii.

Ends…

1087 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!