Muhimbili wanatekeleza kwa vitendo agizo la JPM

NA ANGELA KIWIA

Hospitali ya Taifa Muhimbili imetekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dk. John Magufuli la kubuni mkakati wa kupunguza idadi ya wagonjwa wanaotibiwa nje ya nchi.
JAMHURI limefanya mahojiano maalumu na Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, kuhusiana na utekelezaji wa agizo hilo la rais.
JAMHURI: Utekelezaji wa agizo la rais umefikia wapi?
Aminiel: Kwanza tuliangalia kwanini watu wanakwenda kutibiwa nje ya nchi, tukaangalia sababu ndiyo tukazifanyia kazi.
Kulikuwa na sababu ambazo ni baadhi ya matibabu kutopatikana nchini kutokana na kutokuwa na vifaa tiba pamoja na wataalamu wake. Tukaamua kuanzia hapo, tukapata ufumbuzi.
Utoaji wa huduma hiyo ni utekelezaji wa azima ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa matibabu ambayo yalikuwa hayatolewi ndani ya nchi.
JAMHURI: Ni wagonjwa wapi waliokuwa wakisafiri zaidi kwenda kutibiwa nje ya nchi?
Aminiel: Wagonjwa wa figo ndio waliokuwa wakiongoza kwenda kutibiwa nje ya nchi ambapo kwa miaka 15 wagonjwa 230 walipelekwa India kupatiwa matibabu.
Kila mgonjwa mmoja alikuwa anagharimu kiasi cha Sh milioni 80-100. Lakini waliofanyiwa kwetu baada ya kuanza kutoa huduma hii gharama yake ni Sh milioni 21.
Pia vifaa vya kusaidia kusikia kwa watoto hili nalo lilikuwa ni tatizo. Tayari hospitali yetu inao wataalamu wa tiba hii ambao wamefanya upasuaji kwa watoto 11 na kuwapandikiza vifaa vya kusaidia kusikia kwa gharama ya Sh milioni 36, kwa mgonjwa mmoja.
Mgonjwa mmoja alipokuwa akipelekwa nje ya nchi alikuwa akigharimu kiasi cha Sh milioni 80-100. Hapa utaona ni kiasi gani pesa zinavyookolewa.
Ikumbukwe kifaa cha kusaidia kusikia ndicho kinachogharimu fedha nyingi, kwani kinanunuliwa kwa Sh milioni 30, zinazobaki ni huduma za upasuaji na mambo mengine.
Aina ya tatu ya wagonjwa walikuwa ni wagonjwa wa tiba ya radiolojia ambao kwa sasa wanapatiwa matibabu hapa hapa nchini kwa gharama nafuu zaidi.
Mgonjwa mmoja alikuwa akiigharamu serikali Sh milioni 96 akipelekwa nje ya nchi, lakini hapa kwetu anatibiwa kwa Sh milioni 8.
JAMHURI: Wagonjwa wote waliokuwa wakisafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu walikuwa wakilipiwa na nani hasa?
Aminiel: Aliyekuwa akigharamia matibabu ilikuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
JAMHURI: Je, wagonjwa waliopatiwa matibabu haya mapya wamegharamiwa na nani?
Aminiel: Wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji ambao ni kupandikizwa figo, vifaa ya kusaidia kusikia kwa watoto na tiba ya radiolojia hawakulipia matibabu. Huduma zilizotolewa zote zimelipwa na serikali, wametibiwa bure.
Hospitali yetu imekuwa ikitumia kiasi cha Sh milioni 500-600 kila mwezi kwa ajili ya kulipia wagonjwa wasio na uwezo. Hapa utaweza kuona ni kiasi gani cha pesa kinatumika kutoa huduma ya afya kwa Watanzania.
JAMHURI: Mpaka sasa ni wagonjwa wangapi wameshapatiwa matibabu haya mapya katika hospitali hii ya taifa?
Aminiel: Ikumbukwe kuwa wakati tunaanza kutekeleza agizo la rais tulianza kuangalia mambo yanayohitajika ili kuweza kufanikisha agizo hilo.
Kwanza, tulipeleka wataalamu 20 nchini India kupata mafunzo kwa miezi mitatu. Wakati walipokuwa huko tulishughulika na miundombinu itakayowawezesha kufanya tiba.
Novemba mwaka jana upasuaji wa kwanza wa figo ulifanyika kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi. Kwa sasa tayari wagonjwa 19 wamepandikizwa figo na wanaendelea vizuri.
Wakati tunaanza kupandikiza figo, tulikuwa tunaalika wataalamu kutoka India, wataalamu 15 walikuja tulipoanza, lakini kila siku zinavyosogea na madaktari wetu wanavyopata uzoefu idadi ya wataalamu imepungua na kufikia wanne tu.
Uwezo wa wataalamu wetu umekua sasa kwa asilimia 75, hivyo tutakapofanya kambi nyingine tatu tutakuwa hatuhitaji tena wataalamu kutoka nje ya nchi.
JAMHURI: Idadi ya wagonjwa wa figo inaonekana kuwa kubwa, je, mkakati wenu ni upi ili kuwapatia huduma wote?
Aminiel: Hapa kwetu tuna mkakati wa muda mfupi na wa muda mrefu.
Mkakati wa muda mfupi ni huu unaofanyika sasa, ni kuhudumia/kufanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa watano kwa mwezi mmoja. Mkakati huu utaendelea kwa kipindi cha miaka miwili ambacho tunasubiri kukamilika kwa jengo letu la kisasa.
Baada ya kukamilika jengo hili ambalo litakuwa na sakafu moja kwa ajili ya upandikizaji figo, tutakuwa na uwezo wa kufanya upandikizaji wa figo kwa mgonjwa mmoja kila siku, hivyo kwa mwezi tutahudumia wagonjwa 20 na wagonjwa 200 au 240 kwa mwaka.
JAMHURI: Tiba ya radiolojia ni tiba mpya nchini, je, inafanyikaje?
Aminiel: Hospitali ya Taifa Muhimbili imeanzisha kwa mara ya kwanza hapa nchini utoaji wa huduma za tiba ya radiolojia (Interventional Radiology) ambapo kabla ya uanzishwaji kwake wagonjwa waliokuwa wanahitaji huduma hizi walikuwa wakienda nje ya nchi.
Tiba hii inahusisha utaalamu wa kutumia vifaa vya radiolojia kama X-ray, MRI, CT-Scan na Ultra-Sound kutibu moja kwa moja ugonjwa au kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi.
Kwa wastani wa mgonjwa mmoja kutibiwa uvimbe kwenye sehemu ya kinywa (sclerotherapy for haemangioma) inagharimu kiasi cha Sh milioni 2. Kutokana na ugonjwa huo mgonjwa anahitaji kutibiwa hatua nne ili kukamilisha mzunguko wa tiba hiyo, hivyo kugharimu Sh milioni 8.
JAMHURI: Ni wagonjwa wangapi wameshapata huduma hii mpaka sasa na kiasi gani cha fedha kimetumika?
Aminiel: Watoto 11 wasiosikia wamewekewa vifaa vya kusaidia kusikia na kugharimu Sh milioni 88. Iwapo wangepelekwa nje ya nchi wangetumia zaidi ya Sh bilioni moja. Gharama ya matibabu kwa mgonjwa mmoja hapa kwetu ni Sh milioni 8, badala ya Sh milioini 96 zinazohitajika nje ya nchi.
Huduma ambazo zimeanza kutolewa kupitia njia hiyo kwa sasa ni kuondoa uvimbe kwenye sehemu ya kinywa, uso na shingoni (sclerotherapy for haemangioma and lymphangioma).
Pia kuweka mirija kwenye figo ambazo mirija ya kutoa mkojo imeziba (nephrostomy tube placement), kuzibua mirija ya nyongo iliyoziba (percutaneous trans hepatic biliary drainage) na kuzibua mirija ya uzazi iliyoziba (fallopian tube recanalization). Tiba nyingine ni kunyonya usaha ndani ya tumbo (abscesses drainage).
JAMHURI: Tiba hii imeanza kutolewa lini?
Aminiel: Tumeanza kutoa tiba hii Novemba 27, mwaka jana na tunajivunia juhudi za kuokoa maisha ya binadamu pamoja na kuokoa kiasi cha Sh bilioni 3.96.
Kutokana na kuwepo kwa huduma hii nchini kutasaidia wananchi wengi kunufaika na kuipunguzia serikali na baadhi ya watu mzigo wa kulipa fedha nyingi kwa matibabu nje ya nchi.
Ikumbukwe kuwa katika kuimarisha huduma za afya nchini, serikali imetenga Sh bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kisasa hapa Muhimbili. Jengo hili litakuwa na ghorofa saba ambalo litahusisha huduma za matibabu ya kibingwa. Hii yote ni kupunguza na kuondoa rufaa za wagonjwa kutibiwa nje ya nchi.
JAMHURI: Jengo hili litakuwa kwa ajili ya wagonjwa wa aina gani?
Aminiel: Litakuwa na vyumba vinne kwa ajili ya watu mashuhuri (VIP), chumba kimoja chenye hadhi ya juu (Presidential level suit), vyumba vya upasuaji wa kawaida viwili, vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) vyenye vitanda vitano pamoja na sehemu ya ICU ya kupumzika yenye vitanda 10 tu.
Pia kutakuwa na sakafu maalumu kwa ajili ya huduma za upandikizaji figo ambapo kutakuwa na vyumba viwili vya upasuaji vinavyoingiliana (theatre), ICU itakayokuwa na vitanda vitano na ICU itakayokuwa na vitanda 10 (step down ICU).
Kutakuwa na sakafu maalumu kwa ajili ya upandikizaji wa chembechembe za damu zilizomo katikati ya mifupa (bone marrow transplant) na vitanda 10 vya ICU.
Vitanda 10 kwa ajili ya sehemu ya kupumzika baada ya mgonjwa kutoka kwenye chumba cha ICU (step down), vitanda 10 kwa ajili ya ‘daycare’ kwa ajili ya wagonjwa wa bone marrow. Eneo la mazoezi ya viungo (physiotherapy), vitanda 10 vya watoto wachanga, vyumba vinane vya mama wajawazito na ofisi za madaktari na wauguzi.
Jengo hili litakuwa na maabara inayojitegemea, famasi, uhasibu, watunza kumbukumbu, huduma za mionzi kama Utra- sound, X-ray, vyumba v