Serikali ya Israel imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kurejesha uhusiano unaolenga kuziimarisha nchi hizi mbili kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Ayelet Shaked wakati wa Kongamano la Tano la Biashara na Uwekezaji kati ya Israel na Tanzania.

“Tunamshukuru sana Rais Magufuli kwa kufungua ubalozi wa Tanzania nchini kwetu na tunataraji kuuzindua rasmi juma lijalo”, alisema Waziri Shaked.

Ameongeza kuwa kwa zaidi ya miongo minne Tanzania na Israel hazikuwa na mahusiano ya kiuchumi wala ya kisiasa na kuongeza kuwa sasa nchi yao iko tayari kuwekeza nchini.

Waziri huyo ameeleza kuwa ni mara yake ya kwanza kufika Afrika na yuko tayari kuja na familia yake kwa ajili ya kufanya utalii Zanzibar na kwenye mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewakaribisha waisraeli kuwekeza nchini kwani Tanzania ni kitovu cha uwekezaji kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kutokana na amani iliyopo. Pia ameitaja nchi hii kuwa ni lango la biashara kwa nchi za kiafrika zinazoizunguka.

“Israel mnakaribishwa kuwekeza hapa Tanzania kwani mazingira ya uwekezaji ni mazuri, tunayo ardhi nzuri kwa kilimo, tunayo maziwa, mito kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, hivyo hakuna mtakachokikosa endapo mnataka kuwekeza kwenye kilimo”, alisema Waziri Mwijage.

Waziri Mwijage amesema Tanzania iko tayari kwa uwekezaji katika kilimo, viwanda vya dawa, TEHAMA, utalii, uzalishaji wa sukari na uongezaji thamani kwenye madini, na hivyo kuwahakikishia kuwa Serikali inaunga mkono suala la uwekezaji.

Naye balozi wa Israeli kwa nchi za Tanzania , Kenya, Uganda, Malawi na Shelisheli, Mhe. Noah Gal Gendler amesema Serikali ya Rais Magufuli imeonyesha mabadiliko makubwa ya ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi kwa muda mfupi.

“Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 46 hakuna waziri hata mmoja kutoka Israeli amewahi kuitembelea Tanzania, lakini ndani ya wiki mbili wamefika mawaziri wawili toka nchini mwetu”, alisema Gendler.

Ameongeza kuwa katika kuimarisha sekta ya Afya, Israeli itajenga wodi za wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, na kituo huduma kwa watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Kongamno hili ni la tano kufanyika hapa nchini likiwa na lengo la kuonyesha fursa za uwekezaji zitakazotekelezwa baina ya wafanyabiashara wa Israeli na Tanzania. Kongamano hili ni fursa kwa sekta binafsi kuitumia vizuri ili kuongeza tija katika biashara hususan katika kilimo na uwekezaji katika ujenzi wa viwanda.

1469 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!