Kujenga Tanzania: Nini kifanyike? (2)

Sehemu ya kwanza ya makala hii, mwandishi alitihimisha kwa kueleza mambo manne yaliyoamuriwa kutokana na Kamati iliyoundwa kuhusu mfumo wa elimu nchini. Moja ya yaliyokubaliwa ni kuwa mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi iwe ile ile kwa wote na ingeweza kufanyika kwa lugha yoyote ile ya Kiswahili au Kiingereza. ENDELEA..
 
Lakini ile Integration Committee kwa kujua Tanganyika huru watakuwapo mabalozi kutoka nchi mbalimbali na watakuwapo wataalamu kadhaa wakifanya kazi serikalini au katika mashirika, iliona busara kubakiza shule chache tu (zilibaki shule 11) za Kiingereza kwa hao watoto wa wageni.
Hatua hiyo ya mapendekezo kutoka ile Kamati ilikuwa na lengo la kuondoa tofauti katika elimu ya watoto wa Tanganyika huru. Aidha, kwa mapendekezo yale shule zote za madhehebu, niseme wazi hapa shule za misheni (religious schools) na zile za mataifa (racial schools) zilitakiwa kupokea watoto wowote wale na si wa medhehebu yao au wa taifa lao tu.
Hivyo sasa Waislamu au watoto wasiokuwa na madhehebu ilikuwa RUKSA kusoma katika shule za misheni na vivyo hivyo watoto Wakristo ruksa kusoma katika muslim schools. Aidha, watoto Waafrika sasa waliweza kuingia katika shule za Wazungu au Wahindi. Ni hatua mojawapo ya kujenga utaifa maana watoto wote wasome pamoja, wacheze pamoja na wakue pamoja kitaifa. Hii ilivunja udini na ubaguzi wa kitaifa.
 Baada ya Uhuru, Serikali ilichukua hatua madhubuti na za wazi wazi kuwezesha watoto wote wa nchi huru ya Tanganyika kupata elimu sawa katika shule popote humu nchini. Ndipo mwaka 1970 Serikali ilitaifisha shule zote za madhehebu na za mataifa (religious and racial schools) zote sasa zikawa ni shule za Serikali chini ya Wizara ya Elimu. Wizara nayo ikabadilishwa jina na kuitwa Wizara ya Elimu ya Taifa kuendesha shule zote.
Huu utaifishwaji wa shule za madhehebu na za mataifa ulisaidia sana kuleta mageuzi katika elimu. Watoto wa shule za sekondari walichanganyika sana. Kutoka Kagera wakatawanywa shule zote nchini. Kutoka Kilimanjaro wakapelekwa kote nchini. Kutoka Lindi, Ruvuma na Rukwa wakatawanywa kote nchini. Hii ilifaa sana. Kwanza maeneo yale yasiyokuwa na shule nyingi watoto wao wote waliofaulu darasa la nane walipata nafasi mikoa mingine.
Pili, ukabila ulianza kutoweka, maana kila shule ya sekondari ilipata mchanganyiko wa makabila.
Tatu, udini ulitoweka maana kila mtoto wa dini yoyote alipelekwa shule alikopangwa na akachanganyika na watoto wengine wa dini mbalimbali. Madhehebu ya RC, UMCA, CMS, Moravianna, Wahindi na Waismailia waliokuwa na shule nyingi za madhehebu yao sasa walionja utaifa; maana walipokea watoto wengine wasiokuwa wa madhehebu yao, lakini walikuwa Watanganyika. Mtoto Issa alisoma Umbwe wakati mtoto Venance alisoma Kinondoni Muslim. Huu ulikuwa MSETO wa manufaa katika kujenga umoja na utaifa wetu.
Isitoshe, watoto wa nchi hii waliweza kujua ukubwa wa nchi yao na tofauti ya mandhari (vegetation). Kwa hili walipata jiografia halisia ya nchi na kupanua wigo wao. Matokeo ya mchanganyiko ule hivi sasa Wachaga na Wahaya wamejua Kusini kulivyo na hii imewezesha watumishi waliositasita kwenda kufanya kazi Kusini enzi za ukoloni sasa wako radhi kuhamishiwa kule. Wamejua kulivyo baada ya kusoma shule za huko. Kwa vile Kusini sasa kumefunguka kwa kupata barabara za lami (Dar es Salaam – Lindi – Songea na Dar – Mbeya – Sumbawanga). Na upo mvuto wa gesi asilia, basi watu watakimbilia huko wakitokea mikoa mbalimbali.
Ili kuijenga Tanzania yenye utaifa ilivyokusudiwa na Baba wa Taifa, Serikali ilibuni utaratibu wa kuwa na JANDO LA KITAIFA kwa watoto wote. Jando hili lilikuwa kuwakusanya watoto wote wa nchi hii na kuwaweka pamoja ili kuwakomaza katika moyo wa utaifa na uzalendo. Hii iliwapa fursa watoto wa nchi hii kuishi pamoja, kufanya kazi pamoja na kucheza pamoja. Jando lile likaitwa “JESHI LA KUJENGA TAIFA”. Hapa ndipo mahali pekee Baba wa Taifa alisema wavulana wote na wasichana wote watapikwa pamoja katika jungu kubwa na wakishaiva watatoka na kuwa WATANGANYIKA (nationals and patriots). Zanzibar kuna ‘jando’ kama hili kwa lengo la kuwajengea UZANZIBARI wazawa wote wa Visiwani. Wenzetu ‘jando’ lao linaitwa “JESHI LA KUJENGA UCHUMI”.
Wasomaji vijana hawawezi kujua hali ilikuwaje siku zile za zamani.  Enzi za ukoloni kila mbinu ilitumika kutuweka katika matabaka. Wakaleta mfumo wa elimu kwa kila taifa – Waafrika, Wazungu na Waasia. Idara ya Elimu ndiko kitovu cha mfumo wa matabaka ulikoanzia. Kulikuwa na mkurugenzi mmoja tu wa elimu na naibu mkurugenzi mmoja tu. Lakini kukawa na wasaidizi wanne tofauti. Kila msaidizi alikuwa na madaraka kamili kuendesha mfumo wake wa elimu:-
Alikuwepo Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Waafrika (Asistant Director of Education for African Education).
1.   Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu kwa wasio Waafrika – Wazungu, Wahindi na Magoa (Assistant Director of Education for Non Africans, European, Asian, Goans and other non – native communities).
2.   Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Ufundi (Assistant Director Technical Education, notably at two Trade Schools – Ifunda & Moshi and Technical Institute Dar es Salaam)
3.   Mkurugenzi Msaidzi Elimu ya Wanawake (Assistant Director of Education for Women’s and Girls Education of all communities).
Watoto wa Afrika elimu yao ilisimamiwa na Kamati ya Ushauri tu (Advisory Committee for African Education) wakati elimu kwa Wazungu ilisimamiwa na Mamlaka ya Elimu iliyoitwa (European Authority for Education). Ile ya Wahindi ilisimamiwa na Mamlaka ya Elimu (Indian Authority for Education).
Kumbe kwa wageni wale wengine kama vile Magoa, Waarabu na kadhalika waliundiwa Kamati ya Ushauri tu iliyojulikana kama Advisory Committee for other Non – Native (including Goan) Education.
Kwa mfumo huo wa matabaka elimu kwa watoto isingalikuwa na mfumo mmoja. Hapo mfumo wa elimu uliwagawanya watoto wa nchi hii katika matabaka na walikuwa na fikra hizo za matabaka.
 Si mnaona ubaguzi wenyewe? Hata Magoa hawakuhesabiwa kama Waasia- walibaguliwa na kuwekwa kundi la wageni (aliens) kama Waarabu, Wasomali na kadhalika. Kumbe Magoa na Wahindi ni wale wale tu wote wanatoka kule India.
Kuondoa uchafu na upuuzi wote wa matabaka namna ile Serikali ya Tanganyika ilifumua mfumo wote wa elimu ya nchi hii na kuijenga upya ikiwa sasa ni elimu ya Taifa kweli na sawa kwa wote.
Nimesema huko juu kuwa Taifa liliunda jando lake la kitaifa kulea watoto wake kwa pamoja. Ikatungwa na sheria kuhalalisha uundwaji wa National Service – yaani Jeshi la Kujenga Taifa, sheria ile ni Na. 16 ya 1964 kwa huku Bara. Visiwani nako jando lao liliundwa mwaka 1977 na kuitwa Jeshi la Kujenga Uchumi badala ya zile kambi za vijana. Nako ilitungwa sheria Na. 5 ya 1979 kuhalalisha JKU.
Ikaonekana hata ile sheria Na. 16 ya 1964 ya JKT ilibagua vijana wa nchi hii. Sheria iliwataka wavulana na wasichana wa elimu ya msingi tu ndio wajitolee. Sasa wale wasomi je? Kwa vipi vijana wa nchi hii wabaguane?
Vijana wa Tanu Youth League (TYL)-Umoja wa Vijana wa TANU- walipofanya mkutano wao Arnaoutoglou 1965 walimuuliza Mwalimu, “Vipi Taifa hili linawabaguwa vijana katika makundi mawili- la wasomi na la kabwela?” Wale wa darasa la saba ndio wanajitolea katika Kambi za JKT na kujengewa utaifa, wale wasomi aka! Hawaendi, tutakuwa na Taifa moja kweli? Huo sasa ulikuwa ubaguzi wa kielimu katika nchi yetu.
 
>>ITAENDELEA

418 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons