Demokrasia inatafsiriwa kuwa: mfumo wa kuendesha serikali iliyochaguliwa na watu kwa manufaa ya watu. Tafsiri haina tatizo, lakini yapo mambo yanavyoweza kutokea ndani ya mfumo huo ambayo yanaweza kusababisha hitilafu kubwa.

Kwa utaratibu wetu, kila baada ya miaka mitano vyama vya siasa “vinajinadi” kwa wapiga kura halafu ndani ya siku za mwishoni mwa mwezi wa Oktoba wa mwaka wa uchaguzi, wapiga kura tunapanga msululu kuchagua moja au zaidi ya wagombea wa vyama vilivyojitokeza kwenye uchaguzi.

“Kunadi” siyo neno ambalo mtu anayekusudia kujijengea heshima ndani ya jamii anaweza kulitumia mbele ya jamii anayokusudia kuitumikia. “Kujinadi” ni kutamka bei yako hadharani. Kwenye kanuni za masoko ni kuwa sokoni yupo muuzaji, na mnunuzi. Na wauzajihuja wa kila aina: wapo wauzaji waadilifu, lakini hali kadhalika wapo wababaishaji (nimesikia ndugu zetu Wamakonde wanawaita pakudumbadumba) ambao watakuuzia koroma lakini wakaipa jina na sifa za nazi.

Kwa maana tu ya kuwa wapo wagombea waadilifu na wale wababaishaji, basi labda siyo vibaya kusogeza mbele mjadala huu wa mchakato wa uchaguzi kuhusishwa pia na “kujinadi” kwa wagombea mbalimbali.

Hali ya uwepo wa wanaojinadi inaashiria kuwa wapo sokoni wakiahidi kuwa tukiwakubali wao, wanakuja na sifa kadha wa kadha, na watatekeleza mambo kadha wa kadha. Na tukishawishika tunawapigia kura kuwachagua.

Sifa nyingine ya mchakato wa uchaguzi ni uwepo wa wanasiasa wanaojinadi kuwa wanatuuzia nazi na, kweli, wakatuletea nazi pindi wanapochaguliwa. Wapo pia wale ambao wanaahidi pilipili, na kama wanavyoahidi, wakatuletea pilipili wanapochaguliwa.

Hoja yangu ya leo ni kuwa wapiga kura wa Tanzania tumezowea na tumekubali kuuziwa koroma inayoitwa nazi, lakini tukiuziwa pilipili na ikaja pilipili tunaanza kutafakari iwapo matokeo ya uchaguzi uliopita ni suala la kufurahia la kujutia.

Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi, Mhe. John Magufuli, alipozindua kampeni yake ya uchaguzi wa rais kwenye viwanja vya Jangwani mwaka 2015 aliahidi mengi, mojawapo likiwa kuhimiza wafanyabiashara wakubwa na wadogo kulipa kodi.

Nimejifunza hivi karibuni kuwa kuhimiza kulipa kodi ni pilipili kwa namna nyingi tu. Tena ukisikia baadhi ya maoni ya wapiga kura, na iwapo ingekuwa tunapima ukali wa pilipili kiuhalisia, unaweza kuamini kuwa ukali wa pilipili hii ungelalamikiwa hata nchini India ambako kwao pilipili ni jadi.

Naamini juu ya hoja kuwa ufuatiliaji kwa karibu wa ulipaji kodi umepunguza mzunguko wa fedha kwenye uchumi kwa sababu siyo pesa zote zilizokuwa kwenye mzunguko zilitokana na mapato halali. 

Asiyeweza kuelezea kwa kuridhisha kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ni jinsi gani amepata kipato hawezi kuendelea kutafuta fedha kwa njia hizo zisizoeleweka. Matokeo yake ni kuwa yule aliyekuwa ana magunia ya pesa enzi hizo, leo hii anabeba pesa zake kwenye mifuko ya nguo yake tu.

Matumizi mabaya ya pesa za serikali kwenye miradi ambayo ilikuwa haikamiliki, fedha iliyotokana na biashara ya meno ya tembo, na fedha inayotokana na madawa ya kulevya ni baadhi ya vyanzo vya mapato vilivyoingiza pesa kwenye uchumi ambazo sasa zimepungua kwa kiasi fulani. Kampeni dhidi ya mapato haya haramu zimeendeshwa na serikali za awamu zilizopita, lakini ni wazi kuwa zimeshika kasi kubwa katika kipindi hiki cha awamu ya tano.

Wapo wengi waliotegemea matumizi ya yule mkwepa kodi ambaye awali hakuandamwa na serikali kiasi cha kumkosesha usingizi. Ulikuwepo msululu wa watu ambao walifaidika na matumizi yake kutokana na bidhaa na huduma mbalimbali alizolipia.

 

>> ITAENDELEA

875 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!