Ndugu Rais niliugua sana kifuani mwangu nilipokutafuta nami nisikuone siku ile Watanzania tulipokuwa tunamuaga Sir George Clement Kahama  katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Uliikosa fursa ya kuzisikia busara na hekima za Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi – Mtanzania pekee aliyejaliwa kuwa Rais mara mbili katika nchi inayodaiwa kuwa moja. Alikuwa Rais wa nchi ya Zanzibar na tena akawa Rais wa nchi ya Tanzania.
Namfahamu Mzee Mwinyi tangu Kipata, Kariakoo na kule Tandika. Nimesikia hotuba zake nyingi! Lakini nilikuwa sijawahi kuyasikia maneno yaliyojaa busara na hekima kubwa kama ya siku ile! Mwinyi aliuchoma moyo wangu aliponikumbusha kuwa mimi ni udongo na kwamba iko siku nitarudi kwa udongo!
Maandiko yanasema; “Ulitoka kwa udongo utarudi kwa udongo!” Baba Watanzania tukiwa tuli kabisa katika majonzi mazito, Mzee Mwinyi alisema; “Sisi wote hapa, ni mali ya Mwenyewe Mwenyezi Mungu! Hapa duniani tunapita tu!”
Ndugu Rais, laiti ungekuwapo, nina hakika nawe pia ungeikumbuka siku ya kupita kwako! Siku ambayo utakuwa umelala mavumbini ukisubiri ufukiwe katika mavumbi hayo, kwa kuwa humo ndimo ulimotoka! Imeandikwa; “Mwanadamu kumbuka, wewe ni mavumbi na mavumbini utarudi!”
Ulipoongea na wahariri ulisema wachora katuni wanakuchora mpaka siku nyingine unalazimika kujitazama vizuri katika kioo. Majuzi walikuchora tena, uso vilevile. Mbele yako yuko mwananchi amekaa juu ya gema, lakini anawaza sana. Juu yake wamechora picha ya ugali. Alionekana ni, ‘choka-mbaya’. Ilikuwa wazi kuwa kwake siku hiyo ugali ulikuwa haufikiki!
Upande wa pili wamekuchora pia ukiwa juu ya gema. Kati yako na yule masikini kuna korongo refu sana. Eti kwa kumhurumia masikini wako ambaye hawezi kupata hata mlo mmoja kwa siku, baba eti umembebea mataruma, yaani vyuma vya reli mpya (standadi geji) unampelekea! Hapa Wakongo wangesema ‘akili mu kichwa’.
Baba yule lofa mwenye kuvaa matambara anawaza ugali ambao kwa siku hiyo kwake ulikuwa haufikiki, alituwakilisha wengi! Kwa kuwa hatuna uhakika wa bajeti yetu, hela ya kula kwa siku hutolewa kila asubuhi ya siku hiyo hiyo. Sijui, lakini Baba, ningekuwa karibu na mama yetu Janet, ningemuuliza hali yenu kibajeti ilikuwaje ulipokuwa mwalimu tu hujaanza kufikiria hata kuwa mbunge. Lakini mama yetu najua unasikia.
Leo, Baba akirudi mwambie vijana wako wale wazee wastaafu wa TTCL walikuja kuulizia ile nyongeza yao ya elfu hamsini iliyopitishwa na Bunge yeye akiwamo. Mwaka wa pili unaisha nyongeza haiongezwi! Yawezekana binafsi wakati huo akiwa mbunge na waziri hakuafiki kima cha chini cha pensheni kwa wastaafu kiwe laki moja, lakini huo ulikuwa uamuzi wa Bunge nzima! Wengine wamelipwa, hawa wastaafu wa TTCL pekee wamekosa nini?
Ndugu Rais, juzi binti yangu karudi bila unga, kisa fedha niliyompa haikutosha. Zimepungua shilingi mia nne. Unga siku hizi unapanda bei kila asubuhi! Baba kubali wananchi wako tunakupenda. Kazi kubwa unayoifanyia nchi hii tunaithamini! Ukisema umetununulia ndege hakuna timamu anayepuuza jambo jema kama hili. Ila njaa tuliyonayo imeziba mishipa ya fahamu na kuiacha ile tu inayotambua kuwa ili uishi kesho uje uone matunda ya hizo ndege ni lazima kwanza uishi leo! Utaishi leo kwa kula chakula! Angalau ndege moja ingengoja wananchi wapate ugali kwanza!
Ndugu Rais nyakati za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kumwona kila mtu ni ndugu yako na kwamba binadamu wote ni sawa zimepita! Zimekuja hizi zetu za kukomoana na kutendeana unyamaunyama tu! Lakini hadithi nzuri aliotuachia Mwalimu Nyerere tunaisoma, nayo haitapata kupita hata mwisho wa nyakati! Yako mengi ya ulimwengu huu yatapita lakini Baba wa Taifa atabaki kuishi kati yetu! Vivyo hivyo tuwatendeavyo wengine sasa yatabaki kusomwa nyuma yetu! Jana kafungwa huyu gerezani bila hatia na leo huyu katekwa na kuteswa kama mnyama, naye bila hatia! Ole wao wamiliki wa unyama huu!
Wamejiondoa ufahamu na sasa wanajitengenezea visasi wao na watoto wao!
Katika hali kama hii Baba, waambie basi watu wako, ni wewe ambaye masikini wa nchi hii walikuwa wanakungojea, uje uwafungue minyororo ya umasikini wao au wamngojee Rais ajaye?
Mzee Mwinyi aliendelea kusema, “Tutakapokuwa tumekwishapita kitakachobaki nyuma yetu ni hadithi yetu tu. Waliobaki watakapokuwa wanatukumbuka watakuwa kama wanaosoma kitabu cha hadithi! Tunaposoma hadithi nzuri alioiacha Sir George Kahama, tujitahidi na sisi siku yetu itakapofika, tuje tuiache hadithi nzuri!”
Ndugu Rais ungejumuika na watu wako katika ule msiba, ukaisikiliza hotuba ya mzee Mwinyi, nina hakika  na wewe ungejiuliza maswali kama tulivyojiuliza wote! Ni hadithi ya namna gani tutakayoiacha nyuma yetu? Watoto wetu, ndugu na jamaa zetu tutawaachaje? Tunaambiwa hata kwa Mungu maswali ni hayahaya, “Uliwachungaje, niliokukabidhi uwachunge?”
Baba siku hiyo inakuja! Siku ambayo mwili ungali umelala, mavumbini mbele yao, ndipo mjane atasoma kwa sauti, “Mume wangu alipotea katika mazingira yakutatanisha wakati wa awamu ya tano na sijamwona tena mpaka leo!” Watoto, ambao sasa watakuwa wakubwa watasoma, “Baba yetu alitekwa nyara na kuteswa sana wakati wa awamu ya tano bila kuwa na hatia yoyote!” Wengine watasimulia jinsi wazazi wao walivyosota katika magereza bila kuwa na hatia! Wastaafu wa TTCL wachache watakaokuwa wamebakia watasoma, “Wengi wetu wametangulia baada ya kushindwa kujinunulia hata vidonge tu vya kutuliza homa kwasababu Baba alikazania vitu kuliko kuthamini utu wetu! Akashindwa kutulipa nyongeza ya sh. 50,000 tu! Baba ni nani hatailaani hadithi itakayowakumbusha awamu iliyoijaza nchi hofu, vitisho na wasiwasi?
Watakaotukumbuka juu ya makaburi yetu, nina hakika yatapasuka nyufa!
  Ndugu Rais, Mwinyi alituasa tujitahidi na sisi siku yetu itakapofika, tuje tuiache hadithi nzuri! Historia ya dunia hii haijawahi kuongopa! Hakuna popote katika kumbukumbu za ulimwengu huu ambapo udhalimu uliwahi kushinda! Wote waliotawala kwa mkono wa chuma waliishia majuto, kulia na kusaga meno!

By Jamhuri