Wiki iliyopita, katika sehemu ya kwanza ya makala hii, nilielezea kilio cha muda mrefu cha Watanzania kuhusu hali ya jamii kimaisha siyo nzuri na sheria za nchi hazifuatwi, kama ilivyoandikwa na gazeti moja nchini, mwaka 2013.

Nilinukuu aya ya kwanza na ya 42 ambazo zilionesha ni kilio, dua na maombi kwa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Watanzania wakihitaji mabadiliko ya uongozi nchini, ili waweze kuishi maisha bora na kufuata sheria za nchi.

Maelezo yangu yalijisimika katika aya zilizoandikwa kwenye gazeti lile, na nikasukumwa kunukuu aya mbili ambazo zilitoa sura ya kilio na maombi kwa Mola, na kuwapa changamoto Watanzania katika uchaguzi wowote wa kitaifa ungetokea baadaye.

Aidha, niliahidi wiki hii kuleta aya ya 41 ya makala ile ambayo ilitoa mwelekeo na rais wa aina gani tulimhitaji kuongoza nchi na kufuta machozi ya kilio chetu Watanzania. Aya hiyo inasema hivi, nanukuu.

“Tanzania kwa kadri hali ilivyo sasa, tunahitaji kuwa na rais dikteta, lakini anayeweza kurejesha hali ya mambo kwenye mstari. Tunamhitaji rais atakayejitoa mhanga kuleta mapinduzi ya mabadiliko, rais asiyeogopa watu na asiye mbabaishaji katika mambo yanayohusu nchi. Rais mjasiri na mzalendo zaidi ya uzalendo ambaye ukimtazama tu usoni anamaanisha hivyo” mwisho wa kunukuu.

Aya hii ukiisona kwa umakini, huenda ukatoka na dondoo tano au zaidi ambazo zitakufanya utafakari na kupima katika mizania maelezo hayo yametafsiriwa barabara na Watanzania na hali ilivyo sasa?

Mimi nimepata dondoo zifuatazo ambazo ziliombwa kwa Mola.

1, Tunahitaji kuwa na rais dikteta, lakini….

2. Anayeweza kurejesha mambo kwenye mstari.

3. Tunahitaji rais atakayejitoa mhanga kuleta mapinduzi ya mabadiliko.

4. Rais asiyeogopa watu na asiye mbabaishaji katika mambo yanayohusu nchi.

5, Rais jasiri na mzalendo.

Dua au maombi haya yaliombwa katika gazeti, tarehe 27 Oktoba 2013 na majibu yalipatikana tarehe 25 Oktoba, 2015. Miaka miwili baadaye. Majibu hayo tayari yamekwishatoa makundi mawili yanayotofautiana kutoka kwa waombaji. (Watanzania).

Wapo wanaokubaliana na majibu ya maombi, ambao wanamshukuru Mwenyezi Mungu. Hii imedhihirishwa na kauli za viongozii wetu wa dini nchini na wananchi waliokuwa katika kilio kikubwa.

Vile vile, wapo wasiokubaliana na majibu ya maombi, ambao wanamshukuru nusunusu (shingo upande) Mwenyezi Mungu. Hii inadhihirishwa na kauli za viongozi wa siasa (baadhi) na watu wanaopenda dhuluma na uonevu wakilaumu na kutoa majina ambayo hayafanani na kauli zao za mwaka 2013.

Kalamu yangu imepokea rai, dua na maombi ya mwaka 2013 na majibu ya mwaka 2015 na kuona ipo haja ya kushukuru kilichopatikana kwanza. Pili, kupokea na kutekeleza kilichopo na tatu, tuombe tena tupate kile tunachodhani hakikupatikana kipatikane kwa salama na amani.

Ifahamike kuwa wakati wa kutekeleza jambo lolote, kuna kufanya vizuri au vibaya, ni maumbile. Zuri tunalichukua na kulitukuza. Baya tunaliacha na kulizika. Wakati wote huo tunakuwa pamoja katika utekelezaji siyo kutengana. Utengano na msuguano wa kauli na vitendo hauwezi kutusaidia kujenga Tanzania huru na salama.

Nawaomba vijana na Watanzania wenzangu; kila mara tukumbuke kauli na vitendo vyetu vilivyopita kabla ya kulaumu na kukejeli yanayofanywa na mamlaka ambayo kwayo tuliiomba. Tukifanya hivyo tunakosea. Kwa lugha ya dini tunakufuru. Mola tupishie mbali na hayo. Amin.

1541 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!