Raia wa Afrika Kusini atupwa jela

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemhukumu Christine Lindiwe ambaye ni raia wa Afrika Kusini kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria.

Katika kesi namba 176 ya mwaka 2019, Lindiwe alisomewa shitaka la kuingia nchini kwa njia haramu, ambapo Agosti 14, mwaka huu alikamatwa katika kituo cha mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam.

Hakimu Mkazi, Vicky Mwaikambo, aliyesikiliza shauri hilo alisema Lindiwe anatuhumiwa kwa kosa la kuvuka mpaka na kuingia Tanzania bila kuwa na nyaraka muhimu zinazomruhusu kuvuka.

Katika kesi hiyo, Hakimu Mwaikambo ametumia kifungu cha sheria namba 45, kipengere cha (1) na (2) cha Sheria ya Uhamiaji (CAP 54 R. E 2016) kumtia hatiani raia huyo wa Afrika Kusini.

Hakimu Mwaikambo alimhoji Lindiwe kuhusu kuingia nchini bila vibali na uwezekano wa kuijisababishia matatizo.

Hata hivyo kabla ya kesi hiyo kuamuriwa na mahakama, mtuhumiwa alikabidhiwa nyaraka za shitaka lake na kutakiwa kuzisoma ili kuzihakiki na kubaini kama shitaka ni lenyewe.

Baada ya kuzisoma alikiri kosa mbele ya mahakama kwamba aliingia nchini kinyume cha sheria na taratibu za nchi zinavyotaka.