RIPOTI YA RUSHWA YA JAJI WARIOBA – 27

Z’bar inaiyumbisha TRA

 

1.     Sukari

(a)  Bill of Landing No. 3 & 4 (Inv. No. ETL/1300C/95 Metric Tons 2,000

(b) Bill of Landing No. 5 & 6 (Inv. No. ETL/1300D/95 Metric Tons 2,000

(c)  Bill of Landing No. 1 (Inv. No. ETL/1300F/96 Metric Tons 6,000

 Mizigo inayohusiana na Bills of Landing 3, 4, 5 na 6 iliondolewa bandarini tarehe 24 Aprili, 1996 na “Bill of Landing” 1 tarehe 1 Mei 1996. Mizigo yote hii ilihifadhiwa kwenye Bonded Warehouse No.84 ya Mohamed Enterprises Ltd, na ilikuwa bado iko humo wakati Tume inaanza uchunguzi.

Aidha, Tume imebaini pia kuwa ECCO Traders Ltd,  imeitumia Tanzania Commodities Trading Company viberiti, mchele, sukari, mawe ya tochi na unga wa ngano. Wakurugenzi wa Tanzania Commodities waliozungumza na Tume walisema mipango yote ya kuagiza mizigo hii ilifanywa na Mohamed Enterprises (T) Ltd. Anuani inayotumiwa na ECCO Traders Ltd ni anwani ya Habib Bank AG. Zurich ya London.

Mara tu Tume ilipoanza kufuatilia bidhaa hizo Mohamed Enterprises (T) Ltd, ilifanya mpango wa kuzilipia ushuru. Kati ya tarehe 15 Agosti na 21 Agosti 1996 ushuru wa Shs 808,157,787/- ulilipwa. Mwishoni mwa Septemba 1996 Shs. 100,000,000/- zikalipwa kama ushuru. Gulam Dewji wa Mohamed Enterprises (T) Ltd, ameahidi kumalizia malipo ya ushuru wa kiasi kilichobaki.

Tume ilimhoji Gulam Dewji anayemiliki kampuni ya Mohamed Enterprises. Alikiri yeye ndiye aliyefanya mpango wa kuagiza bidhaa hizi ili kumsaidia binamu yake Murtaza Alihussein ambaye ndiye mmiliki mkubwa wa Tanzania Commodities Trading Co. Ltd., kwa vile alikuwa bado mgeni kwenye biashara hiyo.

Alikiri kwamba bidhaa hizo zilikuwa zinakuja nchini lakini baada ya kubaini kuwa ulikuwepo mchele ulioletwa na Serikali ya Japan kama msaada alijua kuwa soko halitakuwa zuri hapa nchini na hivyo akatafuta soko Uganda kupitia Uganda Commodities Trading Co. Ltd.

Hata hivyo bidhaa hiyo ilipofika hapa nchini yakawepo matatizo ya kupata mabehewa kutokana na usafirishaji wa mizigo kwa ajili ya wakimbizi wa Rwanda na Burundi na ndipo akatafuta soko humu humu nchini. Kama usemi huu ni kweli asingejaza Road Customs Transit Declaration ambayo inaonyesha mizigo ilipaswa kusafirishwa kwa barabara na siyo reli, na haikupaswa kuhifadhiwa kwenye Bonded Warehouse.

 Kitendo cha kampuni kulipia bidhaa hizo ushuru baada ya kubaini kwamba uchunguzi ulikuwa unafanywa na Tume kinatia mashaka kuhusu ukweli na maelezo ya Gulam Dewji kwamba alikuwa amekosa mabehewa na hivyo kulazimika kutafuta soko humu nchini.

 Tanzania Commodities Trading Co. Ltd, ilikuwa ikimilikiwa na Bharial Keshawji Tanna na Gulamabbas Hassanal Fazal Dewji (Gulam Dewji). Tarehe 5 Julai 1995 milki ya Kampuni hiyo ilibadilika na kumilikiwa na Murtaza Alihussein, mwenye hisa 99 na Mussa Amlima mwenye hisa 1.

Murtaza Alihussein ni binamu ya Gulam Dewji ambaye ndiye amekuwa msimamizi mkuu wa kampuni hiyo. Katika kipindi cha mwaka mmoja Mohamed Enterprises (T) Ltd haikuagiza chakula kutoka nje ya nchi, wametumia Kampuni ya Tanzania Commodities kufanya hivyo.

 Tume imepata nakala ya barua ya ECCO Traders Ltd, iliyotiwa saini na Gulam Dewji kama Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni hiyo kwenda kwa Tamilnad Mercantile Bank Ltd ya 100/104 Kazi Sayed Streed, Mandri, Bombay India ikielekeza watume pesa za mauzo ya mbaazi zenye thamani ya US$ 102,654 zilizosafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Bombay na meli “UMFOLOZI” kwa akaunti ya ECCO iliyoko kwenye Habib Bank Ag Zurich ya London.

Alipohojiwa alisema alifanya hivyo kwa maelekezo ya wenye kampuni ya ECCO na kwamba yeye siyo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo. Tume imeshindwa kukubali maelezo hayo. Kutokana na maelezo ya Gulam Dewji na yale ya viongozi wa Tanzania Commodities Tume imeridhika kwamba ujanja ulitumika kuwezesha ukwepaji wa kodi.

Tanzania Commodities ilikuwa mali ya Gulam Dewji hadi mwaka jana wakati hisa zake zilipohamishiwa kwa Murtaza Alihussein na Mussa Amlima. Tume ilipowahoji hawa wawili walisema hawakutoa malipo yoyote kununua kampuni hiyo bali Gulam Dewji aliwakopesha.

Walikiri pia kwamba mipango yote ya kuagiza bidhaa inafanywa na Gulam Dewji na mizigo ikifika bandarini inashughulikiwa na Mohamed Enterprises, ikiwa ni pamoja na kutafuta soko na kuhifadhi nyaraka zote. Tume inaamini Tanzania Commodities bado ni mali ya Gulam Dewji na Murtaza na Amlima ni wafanyakazi wake kama walivyokuwa kabla ya kubadili milki ya kampuni kwenye makaratasi.

Tume inaamini ama Gulam Dewji pia anamiliki ECCO Traders Ltd, au ana uhusiano wa karibu na kampuni hiyo. Aidha, barua aliyoandika kama Mkurugenzi Mtendaji wa ECCO akiagiza pesa za mauzo ya mbaazi zihamishiwe Uingereza inaonyesha jinsi wafanyabiashara wanavyotorosha fedha nje ya nchi.

 Gulam Dewji anadai anazo nyumba tatu Dar es Salaam na tatu Arusha na mbili Singida. Hata hivyo kwa mtu mwenye biashara kubwa kiasi hicho mali isiyohamishika iliyoko nchini ni ndogo sana na hii imeifanya Tume iamini kuwa rasilimali yake kubwa iko nje ya nchi.

 Tume ilipata  majina ya wafanyabiashara wengine wanaotumia mbinu kama hizi kukwepa kulipa kodi. Taarifa hizo zimepelekwa kwenye vyombo vinavyohusika kwa kufanyiwa kazi.

 

MAPENDEKEZO:

503 (i) Idara ya Forodha ipatiwe vifaa vya kisasa vya mawasiliano kati ya Makao Mkuu, vituo vya forodha katika barabara zinazopitisha magari ya mizigo ya ‘transit’ na vituo vya mipakani pamoja na magari ya doria ili kuweza kudhibiti usafirishaji wa mizigo hiyo.

(ii)Wakati utaratibu wakupata vifaa unaandaliwa Idra itengeneza ‘perforated manifests’ ambazo wenye magari ya mizigo watapaswa kuonyesha katika kila kituo cha Forodha kilichoko katika njia wanazopitia. Katika kila kituo Afisa Forodha atapaswa kuchana kipande kutoka manifest hiyo na kukihifadhi kwa ajili ya udhibiti.

(iii)Magari yakishapakia mizigo ya Transit yaanze safari moja kwa moja badala ya kuzagaa humu jijini au kuchelewa njiani.

 (iv)Mikataba ya ‘Transit Cargo’ baina ya nchi yetu na nchi majirani iandaliwe upya ili iweze kuwawajibisha Maafisa wa Idaraya Forodha wa nchi hizi kupeana taarifa kuhusu usafirishaji wa mizigo baina ya nchi hizi.

 (i) Uchambuzi wakina ufanyike wa kuwabaini wasafirishaji ambao hawakufikisha mizigo nchi jirani ili wafutiwe leseni zao za usafirishaji pamoja na magari yao kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.

 (ii) Idara ya Forodha iwajue wasafirishaji wenye maadili mazuri ya biashara amabo watakuwa wanasafirisha mizigo kwenda nchi jirani.

 (iii) Utaratibu wa kutoa vibali vinavyoruhusu ‘Transit Goods’ kulipiwa kodi na kuuzwa hapa nchini ufutwe na kama kuna sababu za msingi zitakazozuia migizo hiyo isiweze kupelekwa nchi jirani, kwa mfano vita, basi kibali cha kuuza mizigo hiyo nchini kitolewe na Kamishna wa Forodha na sio mtumishi mwingine wa Idara.

 

TRANSHIPMENT YA MIZIGO YA ZANZIBAR

 504. Hii  ni mizigo inayoagizwa mahsusi kwa ajili ya Zanzibar na kushushwa Bandari ya Dar es Salaam ikisubiri meli au  jahazi la kuipeleka Zanzibar. Mizigo hiyo huhifadhiwa bandarini au katika kituo cha Bandari cha Ubungo hadi hapo usafiri utakapopatikana.

 

Utaratibu wa kusafirisha mizigo

Mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar

 (i) Wakala wa wenye mizigo anatakiwa kujaza fomu ya dhamana (Customs Bond (CB 9) kwa ajili ya transhipment cargo. Mizigo hii husafirishwa na meli kubwa tu ili kuondoa mwanya wa mizigo kupakuliwa ufukoni mwa bahari.

(ii) Wakati anasafirishamzigo anajaza fomu nyingine C42 inayomsaidia kutoa mzigo.

(iii) Mizigo ikishafika Zanzibar na kupakuliwa, Afisa Forodha anajaza fomu ya ‘Port Landing Certificate’ (C14) kudhihirisha kwamba mzigo umefika Zanzibar. Nakala ya fomu hiyo hupelekwa Dares Salaam kumwezesha Wakala aliyesafirisha mizigo kufuta Bond aliyowekea mizigo hiyo.

 

Mizigo kutoka Zanzibar kuja Dar es Salaam

(iv) Mizigo  mingi inasafirishwa kati ya Bara na Zanzibar kwa kutumia majahazi. Jahazi moja lina uwezo wa kubeba mali za container tatu hadi nne. Kiutaratibu jahazi lenye mzigo likitoka Zanzibar kuja Bara linatakiwa kujaziwa fomu ya Export Coast Cargo.

Jahazi likifika Dar es Salaam Dhow Whart mwenye mzigo anatakiwa kufuata taratibu zote za Forodha kabla ya kuondoa mizigo yake. Pale ambapo pana viwango tofauti vya kodi mwenye mzigo anatakiwa kulipa tofauti ya kodi.

506. Kutokana na usimamizi duni wa Idara ya Forodha Bara na Visiwani pamoja na kutoheshimu sheria ya forodha, mizigo inayopitia njia ya Zanzibar inatoa mwanya mkubwa wa kuvuja kwa mapato ya Serikali ya Muungano. Akifunga mjadala wa ‘Financial Laws, Miscellaneous Ammendments 1996’ Waziri wa Fedha Profesa S. Mbilinyi alieleza Bunge kwamba Serikali ya Muungano imekuwa inapoteza shilingi bilioni sita (6) kwa mwezi kutokana na bidhaa zinazoingia nchini kwa kutumia njia zifuatazo:

(i) Baadhi ya waagizaji wana maduka makubwa Tanzania Bara na Visiwani na wanaagiza bidhaa za pande zote mbili. Wafanyabiashara kwa kushirikiana na watumishi wa Idara wamekuwa  wanaondoa makontena bandarini na kituo cha Ubungo na mizigo kupakuliwa jijini kisha makotena matupu kupelekwa Zanzibar kwa ushuhuda tu.

 (ii) Wafanyabiashara wamekuwa wanaagiza bidhaa kwa ajili ya matumizi Tanzania Bara, lakini kutokana na viwango vidogo vya kodi huko Visiwani wanabadilisha Manifest ya bidhaa ili zikashushwe visiwani. Baada ya kulipiwa kodi bidhaa hizo hurejeshwa Bara.

 507. Utaratibu huu una athari zifuatazo katika uchumi:

(i) Kodi ya Ushuru na Mauzo inalipwa pale ambapo bidhaa zisipotumika. Kwa kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepunguza viwango vya kodi ikilinganishwa na viwango vya Serikali ya Muungano wafanyabiashara hawa wamekuwa wanalipa kodi Zanzibar na bidhaa kuuzwa Bara.

(ii) Shughuli za Forodha ni shughuli za Muungano, Zanzibar imetoa unafuu wa kodi na hivyo kukiuka Sheria ya Forodha.

(iii) Kamishna Msaidizi wa Zanzibar anawajibika kwa Serikali mbili. Yeye anatakiwa kutekeleza majukumu yake kulingana na Sheria ya Forodha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kuwajibika kutekeleza maamuzi na maagizo yote kuhusu kodi yatakayotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ijapokuwa anafahamu ni batili.

Wakati umefika wa kuhakikisha kwamba Katiba inatekelezwa ipasavyo  kuhusu madaraka ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ya Serikali ya Muungano. Hapana budi Kamishna wa Mapato kwa Kanda ya Zanzibar awajibike kikamilifu kwa Kamishna Mkuu.

(iv) Kwa kuwa hakuna udhibiti mzuri wa majahazi baadhi ya mizigo inadhaniwa kuwa inapelekwa Zanzibar lakini haifiki huko Visiwani bali inarudishwa kuuzwa Bara. Ujanja huu unazinyima serikali zote mbili mapato.

(v) Hata kama viwango vya kodi vingekuwa sawa katika pande zote mbili, Zanzibar inakabiliwa na tatizo la ulegezaji wa masharti ya ukaguzi. Baadhi ya mizigo imekuwa inaondolewa bandarini Zanzibar wakati wa Jumamosi na Jumapili au wakati wa saa ya mapumziko siku za kazi bila ya kulipiwa kodi yoyote. (Weekend and Lunch clearance).

508. Wafanyabiashara wa Zanzibar wana ndugu zao au wakala katika Bara la Arabuni ambao huwanunulia bidhaa, kuziweka kenye containers na kuisafirisha hadi Zanzibar. Mawakala hawa hawaweki ‘Packing List’ ya bidhaa hizo ndani ya kontena ili kumwezesha Afisa Forodha kufahamu aina na idadi ya mali iliyopo. Matokeo yake ni kuruhusu mizigo mingi kutoka bandarini bila ya kulipiwa kodi.

509. Mfanyabiashara au Wakala wake amekuwa anakula njama na watumishi wa Idara ya Forodha hapa Dar es Salaam na kuweka dhamana ya maneno badala ya fedha taslimu. Kwa kuwa hawajibiki tena kupeleka mizigo hiyo Zanzibar, jahazi hubadilisha mwelekeo kurudi Bara au nchi jirani na kushusha mizigo.

510. Pale ambapo wameweka dhamana ya fedha taslim, mizigo hiyo hupakiwa ndani ya majahazi na kuondoka bandarini, lakini mizigo hiyo haipelekwi Zanzibar. Mfanyabiashara au Wakala wake huenda Zanzibar kupiga mhuri makaratasi ya Transhipment Form pamoja na Landing Certificate na kuziwasilisha Idara ya Forodha kufuta dhamana.

 511. Kwa mizigo inayotoka Zanzibar, yameundwa magenge katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo yanajumuisha Maofisa wa Forodha, mawakala, Polisi na watumishi wengine wa bandari kuondoa mizigo hiyo sehemu ya gati ya majahazi bila ya kulipa kodi.

 Wafanyabiashara wamekuwa wanapanga bidhaa ya bei ghali mwishoni mwa makontena na kuweka zile za bei rahisi na ambazo zinalipiwa kodi ndogo karibu na mlango wa makontena. Hata hivyo kwa kuwa shughuli zote hizi zimeundiwa njama, hata ile iliyoko langoni mwa kontena hailipiwi kodi.

 

 MIZIGO ILIYOSHUKA BANDARI YA DAR ES SALAAM KWENDA ZANZIBAR NA KUTOKA ZANZIBAR KUJA DAR ES SALAAM KATIKA KIPINDI CHA JANUARI, 1995 HADI DESEMBA 1995

 

Chanzo: Idara ya Forodha

 

Thamani ya mizigo iliyoletwa bara ni kubwa ikilinganishwa na udogo wa kodi iliyokusanywa kwa vile kodi iliyokusanywa ni ‘Defferential Duty’ tu.

 

MAPENDEKEZO:

 512. (i) Mizigo yote inayoagizwa kwa ajili ya matumizi ya Zanzibar ikipakuliwa kutoka kwenye meli ihifadhiwe katika eneo maalum huko bandarini na kamwe isiende kuhifadhiwa Ubungo.

 (ii) Waagizaji wapewe muda maalum wa kuhifadi mizigo hiyo na kama watashindwa kuisafirisha ndani ya muda uliokubaliwa basi mizigo hiyo ikabidhiwe Idara ya Forodha ili inadiwe.

(iii) Mizigo yote ya Transhipment kwenda Zanzibar iwekewe dhamana ya fedha taslimu na taratibu zote za transhipment zifuatwe ili kuimarisha udhibiti wa mizigo hiyo.

 (iv) Mamlaka ya Mapato kwa kushirikiana na vyombo vya dola iweke utaratibu wa doria katika ukanda wa pwani ili kudhibiti uingizaji holela wa bidhaa.

513. (i)  Kwa kuwa shughuli za Idara ya Forodha ni za Muungano, Serikali ya Zanzibar itakiwe kuzingatia Katiba na kuitekeleza ipasavyo kwa kuweka viwango sawa vya ushuru katika pande zote mbili za Muungano.

 (ii)Idara ya Forodha Kanda ya Zanzibar iimarishe shughuli za Ukaguzi wa Mizigo bandarini. Kila anayeagiza mizigo atakiwe kuwa na ‘Packing List.’

 

MISAMAHA YA KODI

514.  Misamaha ya kodi imekuwa ikiongezeka hasa baada ya kuanzishwa kwa Kituo cha Uwekezaji Rasilimali  nchini. Pamoja na nia nzuri ya kuwavutia wawekezaji, baadhi yao wamekuwa wanatumia fadhila hiyo vibaya. Aidha, baadhi ya watumishi wa serikali katika vitengo vinavyotoa misamaha ya kodi wamejihusisha na wawekezaji katika kukwepa kodi.

 Kwa mfano, katika mwaka 1989, Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya Shs. 139.2 bilioni. Bidhaa zenye thamani ya Shs. 51 bilioni zilisamehewa kodi ikilinganishwa na bidhaa za thamani ya Shs.88.2 bilioni zilizolipiwa kodi. Kwa hiyo asilimia 36.6 ya thamani ya bidhaa zilisamehewa kodi.

515. Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Mapato inampa madaraka Waziri wa Fedha kutoa misamaha ya kodi pale anapoona kufanya hivyo ni kwa manufaa ya umma. Aidha, Sheria ya Forodha inatoa uhuru na mamlaka kwa Kamishna wa Forodha kutoa maamuzi yanayohusu ukadiriaji wa kodi na taratibu za ulipaji wake.

Ingawa sheria hizi ni nzuri, madaraka haya yamekuwa yanatumiwa vibaya kwa kutofuata taratibu zilizowekwa katika kutoa misamaha hiyo na hivyo kuathiri mapato ya serikali. Aidha, baadhi ya watumishi wa serikali katika vitengo vinavyotoa misamaha ya kodi wameshirikiana na wawekezaji katika kukwepa kodi.

Ili kukidhi nia ya serikali ya kuwa na chombo imara na huru kitakachoweza kukidhi makusudio hayo, Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka imependekeza serikalini kwamba sheria iliyounda Mamlaka ya Mapato ifanyiwe marekebisho ili kudhibiti misamaha ya kodi inayotolewa kwa hisani ya Mamlaka husika, Discretionary exemptions zote zifutwe na misamaha yote iwe ni ‘statutory’ na ionyeshwe katika sheria husika.

516. Chini ya sheria ya forodha, Kamishna wa Forodha ana madaraka ya kusamehe au kupunguza (Waivers) kiasi cha dhamana inayowekewa mizigo inaosafirishwa kwenda nchi jirani. Pamoja na uzuri wa utaratibu huu, unaweza kutumiwa vibaya na mhusika.

Kwa mfano mteja anayetakiwa kuweka adhamana ya Shs. 600 milioni na ana nia ya kuuza mzigo huo hapa nchini atatumia njia yoyote ile ili aweze kupata waiver kutoka kwa Kamishna. Kwa kiasi hicho cha fedha akitoa rushwa ya asilimia mbili tu ni fedha nyingi sana. Mbaya zaidi na kwamba mteja akitoa rushwa hiyo atapata waiver na mzigo haupelekwi kunakotakiwa bali huuzwa hapa nchini.

 517. Utaratibu wa utoaji wa misamaha ya kodi siyo tu umeinyima serikali mapato bali pia imetoa mwanya kwa baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha kupokea rushwa.Taarifa ya Kamati ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya mwaka 1995 iliyochunguza suala la misamaha ya kodi iliyotolewa na kituo cha Kuwekeza Rasilimali (IPC) na Hazina katika kipindi cha Aprili –Septemba 1994 imedhihirisha wazi kwamba baadhi ya viongozi wamekuwa wanatumia uwezo wao vibaya kutoa msamaha wa kodi. Uchambuzi wa misamaha hiyo umeonyesha mambo yafuatayo:

(i) Jumla ya misamaha yote ya kodi Shs. 21.7 bilioni

 (ii) Misamaha ya kodi ambayo mafaili yake yalipitiwa na Kamati    Shs. 17.4 bilioni

 (iii) Misamaha ya kodi ambayo mafaili yake hayakuonekana Hazina Shs. 4.3 bilioni.

 (iv) Misamaha ya kodi iliyotolewa kihalali …………………Shs. 16.2 bilioni.

 (v) Misamaha ya kodi iliyotolewa pasipo halali………………..Shs. 17.4

 (vi) Misamaha ya kodi iliyoidhinishwa na IPC na Hazina (na Importation List kupitishwa na IPC………..Shs. 7.2 bilioni

 (vii) Misamaha ya kodi iliyotolewa na IPC lakini Importation List haikupitishwa na IPC………………..Shs. 4.1 bilioni.

 

Taarifa ya Kamati hiyo ilipendekeza kwamba Maofisa wa Hazina waliotoa misamaha kinyume cha taratibu wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria mara moja. Uchambuzi huu unaonyesha wazi kwamba Wizara ya Fedha imekuwa inatumia madaraka yake vibaya kutoa misamaha kwa wateja amabo kiutaratibu hawangestahili kupata misamaha hiyo.

518. Kamati ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali imegundua kwamba kuna baadhi ya misamaha ya Shs. 4.1 bilioni iliyotolewa na IPC lakini orodha ya bidhaa zilizoagizwa haikupitishwa na IPC. Hii inadhihirisha kwamba kwa kutumia kivuli cha IPC, Hazina ilikuwa inaruhusu baadhi ya mizigo ambayo ingetakiwa kulipiwa ushuru kufaidi misamaha ya IPC isivyo halali. Lakini baya zaidi ni kwamba alioongeza idadi ya bidhaa hizo katika orodha hiyo walichukua rushwa ili kutimiza jukumu hilo.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 alipendekeza nini juu ya misamaha ya kodi? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu ule ule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

1413 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons