Uvuvi ni vurugu tupu

 

B: Idara ya Uvuvi

 697. Samaki ni moja ya maliasili muhimu kwa afya na uchumi wa taifa. Samaki wanapatikana katika mito, maziwa, mabwawa na baharini. Kwa kuzingatia umuhimu wa maliasili hii serika ilitunga sheria ya msingi ya “The Fisheries Act No. 6 of 1970,” ili kusimamia hifadhi, ulinzi na matunzo yake kwa ajili ya manufaa ya taifa zima.

Sheria hii inampa Waziri anayehusika na Wizara ya Maliasili uwezo wa kutunga na kuweka kanuni na taratibu za kusimamia na kudhibiti uvunaji na utunzaji wa samaki katika maziwa na bahari. Aidha, kanuni na taratibu hizo zinaeleza aina za leseni, jinsi ya kuzipata na viwango vya ada kwa kila aina ya leseni ya uvuvi wa samaki.

 

Aina za Leseni za Uvuvi wa Samaki

698. Kuna aina nne (4) za leseni katika sekta ya uvuvi nazo  ni:

 (a)  Leseni za kuvua

(b) Leseni za ukusanyaji wa bidhaa za uvuvi

(c)  Leseni za biashara ya samaki humu nchini

(d) Leseni za kuuza nje ya nchi samaki na mazao yatokanayo na uvuvi.

 

Mamlaka za kutoa leseni

 699. Mamlaka za kutoa leseni za uvuvi na bidhaa zitokanazo na uvuvi ziko katika ngazi tatu yaani Idara ya Uvuvi Makao Makuu, Mkoani na Wilayani.

 

(i) Ngazi ya Wilaya

 Maofisa Uvuvi waliopo kwenye Halmashauri za Miji au Wilaya, wana uwezo wa kutoa leseni kwa ajili ya uvuvi wa samaki kwa vyombo vidogo visivyozidi urefu wa mita kumi na moja (11.0) na leseni za ukusanyaji wa bidhaa za uvuvi kama vile majongoo, mwani, makombe, n.k.

 

(ii) Ngazi ya Mkoa

 Maofisa Uvuvi wa mikoa hutoa leseni za uvuvi kwa vyombo ambavyo vinazidi urefu wa mita kumi na moja (11.0) ambavyo viko katika mikoa yao. Vile  vile hutoa leseni za marudio za kuuza bidhaa zitokanazo na uvuvi nje ya nchi kwa wafanyabiashara waliopo kwenye mikoa yao.

 

 (iii) Ngazi ya Idara ya Uvuvi Makao Makuu

 Mkurugenzi wa Uvuvi hutoa leseni zifuatazo:

 (a)  Leseni za kuuza nje ya nchi bidhaa zote zitokanazo na uvuvi hususan kwa waombaji wapya wa leseni.

 (b) Leseni za uvuvi wa kamba kwa vyombo vyenye urefu usiozidi mita 11.0.

 

(c)  Leseni zote zinazohusu wavuvi na wafanyabiashara ambao siyo raia wa Tanzania.

 

Taratibu za kutoa leseni

 700.  Leseni zitolewazo na Wilaya:

 (i) Mwombaji anajaza fomu ambazo hupatikana Ofisi za Uvuvi za Wilaya au kwenye vituo vya kupokea samaki. Kwenye fomu hiyo mwombaji anatoa maelezo binafsi, shughuli anayotaka kufanya na eneo atakalofanyia shughli hiyo na kuiwasilisha kwa Afisa Uvuvi (W).

 (ii) Afisa Uvuvi akishapokea fomu ya maombi atafanya ukaguzi kujua eneo linalohusika na pia kukagua chombo ili kujua hali ya usalama wake,  vifaa na wezo. Akiridhika na maelezo yaliyotolewa pamoja na ukaguzi aliofanya hutoa leseni hiyo.

 701. Leseni za biashara ya samaki humu humu nchini hutolewa na Maafisa Biashara wa Wilaya au Mkoa unaohusika. Mwombaji wa leseni ya biashara ya samaki anapaswa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Biashara.

 

702. Leseni Mpya zitolewazo mikoani

(i) Mwombaji hujaza fomu kuanzia wilayani na baadaye kuiwasilisha kwa Afisa Uvuvi Mkoa.

 (ii) Afisa Uvuvi Mkoa akiipokea fomu atakagua chombo na eneo linalohusika kwa waombaji wapya.

 (iii) Afisa akiridhika na ukaguzi pamoja na maelezo binafsi yaliyotolewa hutoa leseni kwa mwombaji.

 

703. Masharti ya kuzingatia kabla leseni haijatolewa

 (i) Mwombaji awe na sehemu nzuri na inayofaa kuhifadhia samaki.

Awe na uwezo wa kudhibiti ubora wa samaki.

(ii) Awe na nyenzo na vifaa vya kutosha.

(iii) Chombo cha kuvulia kiwe na cheti cha kudhihirisha kwamba kinaweza kusafiri baharini, cheti cha ukaguzi, vifaa vya kuongoza chombo, vifaa vya uvuvi, maeneo mazuri ya malazi na sehemu nzuri ya kuhifadhi chakula na maji.

(iv) Kwa waombaji wa leseni za marudio, waombaji lazima wawasilishe taarifa ya matumizi ya leseni inayoisha muda wake wa kutumika.

 

704.  Leseni zitolewazo na Idara ya Uvuvi Makao Makuu

 Leseni za kuuza nje ya nchi bidhaa za uvuvi

 (i) Mwombaji hujaza fomu ya maombi Fomu Na. 5(b) na kuipitisha kwa Afisa Uvuvi wa Wilaya na Mkoa wake na kisha kuziwasilisha Makao Makuu ya Idara.

 

Masharti ya Kutimiza

 (ii) Leseni za kuuza nje ya nchi bidhaa za uvuvi kwa wazalendo hazina masharti magumu, isipokuwa kwa wageni ni sharti wawekeze kwenye viwanda au ufugaji wa samaki.

 

705. Leseni za uvuvi wa kamba

 Waombaji wa leseni za kuvua kamba hujaza Fomu na kutakiwa kutimiza masharti yafuatayo:

 (i) Kujaza fomu za maombi kikamilifu na kuambatisha picha mbili (side view) za chombo.

 (ii) Uthibitisho wa ulipaji kodi ya mapato.

 (iii) Uthibitisho wa kurejesha fedha za kigeni – hasa kwa waombaji wa leseni za kurudiwa.

 (iv) Uwekaji dhamana (security bond) kwa wenye vyombo vya nje.

 (v) Kuingia mkataba na serikali kwa waombaji wenye vyombo vya kigeni.

 (vi) Kuwasilisha taarifa za uzalishaji.

 (vii) Kuwa na hati ya usalama wa chombo.

 (viii) Hati ya ukaguzi wa chombo.

 (ix) Hati za kufanya kazi nchini kwa “foreign crew.”

 (x) Ubora wa malazi, maji safi ya kunywa na chakula kwa wafanyakazi melini.

 (xi) Kuwa na taarifa safi kuhusu uzingatiaji wa masharti ya leseni kwa wale wanaohitaji kuongeza muda.

 (xii) Kuingia mkataba na Chama cha Wafanyakazi wa Melini.

 (xiii) Kuwa na uwezo wa kulipa ada ya leseni inayotakiwa.

 

706. Leseni za uvuvi wa kamba kwa vyombo vikubwa

 (i) Kujaza fomu za maombi.

(ii) Kuwa na chombo kinachofaa kwa shughuli zinaoombewa leseni.

(iii) Chombo kuwa “sea worthy.”

(iv) Hati ya mkaguzi wa chombo.

(v) Chombo kiwe na ukubwa wa wastani ili kulinda mazingira. (Vipimo ambavyo imekubalika kitaalamu ni uzito uziozidi tani 150, urefu usiozidi mita 25.0, injini zenye H.P.500 au pungufu.

(vi) Kama ni wageni wawekeze kwenye viwanda vya kutengeneza samaki hapa nchini.

(vii) Hati ya ulipaji wa kodi ya mapato (renewal licence).

(viii) Uzingatiaji wa masharti ya leseni kwa msimu uliopita (renewal licence).

(ix) Urejeshaji wa fedha za kigeni kutokana na mauzo ya msimu uliopita (renewal licence).

(x) Kuwa na uwezo wa kulipa ada za leseni.

 

Leseni za uvuvi na kuuza nje bidhaa za uvuvi kwa watu ambao siyo raia wa Tanzania

707. Idara ya Uvuvi Makao Makuu hutoa leseni za uvuvi na kuuza nje ya nchi bidhaa za uvuvi kwa wawekezaji ambao miradi yao imepitishwa na Kituo cha Uwekezaji Vitega Uchumi. Jambo muhimu linalozingatiwa ni kuona kwamba shughuli za wawekezaji hawa haziingiliani na zile za wafanyabiashara wadogo wadogo au wavuvi wazalendo.

 

Maeneo yenye matatizo (Mianya ya Rushwa)

Leseni za uvuvi wa kamba

708. Rasilimali iliyopo ni ndogo na inaonyesha kupungua kila mwaka. Idadi ya waombaji leseni ni kubwa kuliko kiasi cha kamba wanaoweza kuvunwa. Hadi sasa kuna waombaji zaidi ya mia mbili ambao hawajapatiwa leseni za kuvua kamba kutokana na upungufu huo.

Ili kulinda, kuhifadhi na kudhibiti rasilimai iliyopo isitoweke, idara imelazimika kutoongeza vyombo vya uvuvi wa kamba vyenye urefu unaozidi mita 11.0 na GRT.20, kupunguza idadi ya vyombo vyenye ukubwa wa zaidi ya GRT.150 na (Horse Power) HP.500 kwa awamu pamoja na kugawa maeneo yanayovuliwa kamba katika kanda ili kuwapa kamba waliopo kwenye kanda nyingine muda wa kukua na kuzaliana.

 Uhaba huu umeifanya Idara kugawa kanda za uvuvi kwa upendeleo baada ya kupokea rushwa.

 

Je, unafahamu Jaji Warioba katika ripoti hii aliyoiandaa mwaka 1996 alizungumza nini kuhusu marufuku ya baadhi ya zana za uvuvi? Ingawa ripoti hii imeandikwa mwaka 1996, inaendelea kuwa na maudhui yenye uhalisia na yenye kuonyesha upungufu uleule hadi sasa na hivyo inastahili kufanyiwa kazi. Usikose JAMHURI wiki ijayo. Mhariri.

1372 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!