Sisi wanadamu tunajua sana viumbe hawa wawili – kinyonga na popo. Tunaishi nao. Kila kiumbe ana tabia na sifa maalumu zinazowatofautisha na wanyama au viumbe wengine.

Kinyonga anajulikana sana kwa ile hali yake ya kujibadilisha badilisha rangi ya ngozi yake kulingana na mahali alipo. Ni kigeugeu hasa.  Akiwa penye majani mabichi naye hujibadilisha rangi ya ngozi yake ikawa kijani. Akija penye mchanga au penye nyasi kavu naye hujibadilisha na kuwa kama pale alipo. Amejaliwa kuumbwa hivyo ili aweze kujikinga au kujiepusha na maadui zake asionekane kiurahisi.

Lakini kujibadilisha rangi huko pengine kunamsaidia kupata mawindo yake (chakula) kiurahisi pia. Hali hii ya kigeugeu ya kinyonga kitaalamu inaitwa kamefleji (camouflage)- ni aina ya udanganyifu wa mwonekano tu, yeye anabaki kinyonga tu hata iweje.

Haya, yupo kiumbe popo. Sote tunamjua popo. Lakini kisayansi (zoologically) popo anaingia kundi lile kubwa la wanyama wajulikanao kama “mammalia” yaani wanyama wanyonyeshao. Lakini hadithi zetu shuleni zinasema popo hujiganga kuwa yeye si mnyama, bali ni ndege kundi (kizuolojia) linajulikana kama “aves”. Lakini akibanwa huko kwa akina ndege mara moja popo hujiokoa kwa kudai yeye si mwenzao maana yeye ni mnyama! Mateteo yake ni kwamba wanyama tunazaa watoto na kunyonyesha, hivyo hakuna ndege anayezaa na kunyonyesha. Pale wanyama wanapombana popo anawajibu mimi ni ndege hauoni nina mbawa na naruka? Mnyama gani anaruka? Hapo sasa tunaiona tabia ya popo ni kigeugeu kama kinyonga vile.

Tunaposema u-popo maana yake ni hiyo tabia ya kukwepa lawama au majukumu upande mmoja ili unufaike na mastahili ya ule upande mwingine. Hapa chini nitaonesha mifano ya wenye tabia hizi za u-kinyonga na u-popo katika Taifa letu huru la Tanzania. Hiyo tabia ya u-popo na u-kinyonga inaonekana miongoni mwa viongozi wetu wa vyama vya siasa.

Kwa nini nianze na maelezo namna hiyo? Hii imetokana na tatizo linalojitokeza katika siasa ya vyama hapa nchini. Kila chama cha siasa kina itikadi yake, tunayoijua kama IMANI ya CHAMA (The CREED of the PARTY).

Viongozi wanaoamini itikadi hiyo wana wajibu wa kuilezea na kuitangaza kwa wafuasi wao. Viongozi hao wanatakiwa wawe na msimamo thabiti wa ITIKADI yao hiyo, na waieleze kinagaubaga kwa wanachama wao. Kukejeli au kukosoa chama kingine si namna nzuri ya kueneza itikadi, bali ni uchochezi.

Hapo wanapoielezea itikadi yao hiyo viongozi hawa wanatakiwa waoneshe kwa maneno na kwa matendo yao misimamo yao kwa itikadi ile. Umma utawaamini na hapo utapokea itikadi hiyo na kuifuata. Mimi ninapwelea matamshi ya baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa kimsimamo. Viongozi wa siasa wanapotoa sera za vyama vyao na kuitangaza imani ya vyama vyao ni kweli wanatuthibitishia uhalisia wa hali zao wenyewe?

Shaka yangu mimi inatokana na angalizo lililomo katika Maandiko Matakatifu. Tunajua kila tamko litokalo kinywani mwa mtu linasukumwa na kiungo tukiitacho “ulimi”. Maandiko yanatuonya hivi, na nukuu: “…Angalieeni twatia lijamu katika vinywa vya farasi ili watutii, hivi twageuza mwili wao wote. Tena angalieni merikebu ingawa ni ubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, kokote anakoazimia kwenda nahodha.

“Vivyo hivyo, ULIMI nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu, ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili unajisi, huwasha moto, moto mfulizo wa maumbile… Bali ULIMI hakuna awezaye kuufuga, ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti…” (Yakobo sura 3 mistari ya 3 – 6 na wa 8).

Hivyo basi, kwa kutumia ulimi viongozi wetu, wawe wa siasa au wa Serikali wanaweza kueneza sumu miongoni mwa wananchi wote wanaosikia matamshi hayo.

Si hivyo tu, bali matamko hayo ya viongozi yanaweza kuamsha hisia miongoni mwa wasikilizaji kama vile cheche za moto zinavyowasha moto katika nyasi kavu za msituni. Hapo ndipo unatokea moto mkubwa unaumaliza msitu na hata usiweze kuzimwa kwa urahisi. Katika mwili wa mwanadamu, moto huo ndio hasira zinazoamshwa na maneno ya viongozi na chuki zinazozuka miongoni mwa wananchi wa taifa moja hilo hilo na kusababisha mifarakano, mvunjiko wa amani ugomvi na hata vifo.

Kumetokea matamko hatarishi katika nchi yetu. Matamko kutoka UKUTA na pia kutoka UVCCM. Taifa limeingia katika hali tete ya maisha. Matamshi yote hayo yametolewa toka vinywa vya viongozi wenye dhamana ya kulinda itikadi ya vyama vyao. Ulimi umetumika kutoa matamshi hayo. Viongozi wa vyama vya siasa wanajua jukumu la ulinzi na usalama wa raia ni la Serikali. Na Serikali imetamka kupitia ulimi huo huo kuwa HAKUNA MAANDAMANO ya aina yoyote katika nchi hii. Kampeni za uchaguzi zilimalizika Oktoba 2015. Sasa ni kipindi cha uzalishaji – ni KAZI tu.

Hebu tufikirie, uongozi wa siasa unapodai hili au lile ni uzalendo kweli huo? Ni moyo wa utaifa kweli huo? Kuweka nchi katika hali TETE (Kiingereza CONFRONTATION) ni dalili kubwa ya msukumo wa u-mimi au u-sisi, yaani ni silika ya ubinafsi. Tutaaminije matamko ya viongozi ambao huko nyuma waliwahi kutamka katika mikutano ya hadhara na wakaapa. Lakini baada ya mazingira kubadilika, viongozi wale wale wakameza matamshi yao, wakayakana na kujibaraguza kama vile hawakuhusika na matamshi namna ile.

Nijaribu tu kukumbusha wasomaji wa makala zangu nini ninachokisema. Ulimi una hatari kweli. Kuna wakati gazeti moja likiitwa “Sauti Huru” toleo lake No. 346 la Alhamisi tarehe 30 Julai 2014 uk. 2 lilinukuliwa tamko la kiongozi wa CHADEMA kuwa hawatampokea Lowassa katika chama hicho hata ikiwaje, labda kiongozi mkuu wa chama hicho awe ameshakufa. Kwa Kiingereza maneno ya kiongozi yule yalisomeka “…over my dead body”.

Haukupita muda ukatokea mfarakano katika CCM na kwa mazingira yale mapya kiongozi mkuu wa CHADEMA kamkumbatia Lowassa na kusema, namnukuu: “Chama hiki siyo Mahakama ya kuendelea kuwatuhumu watu kwa kashfa mbalimbali (taz. Uhuru toleo Na. 22193 la Jumamosi tarehe 29/07/2015 uk. 2 ibara ya 3).

Hapo wasomaji sijui ukigeugeu huo wa kiongozi unamaanisha nini? Mimi kwa imani yangu ya ukristo (ukatoliki) nilijiuliza mara kadhaa mbona Biblia inakataza kukiuka kiapo? Tunasoma maneno haya, “…ndugu zangu, msiape wala kwa mbingu, wala kwa nchi, wala kwa kiapo kinginecho chochote. Bali “NDIYO” yenu iwe ndiyo, na “SIYO” yenu iwe siyo. Msije mkaangukia hukumu” (Yak. 5 mstari 12).

Pale kiongozi anapoapa, “…..over my dead body” ni kiapo cha kisiasa hicho. Sasa kukivunja ni kujitakia hukumu kutoka kwa wanadamu wale waliosikia akiapa!

Mfano wa pili juu ya tabia hii ya kigeugeu ya viongozi imetokea mwaka huu kule Dodoma, bungeni. Imesemekana, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni aliibana Serikali katika kipindi kile cha maswali na majibu ya papo kwa papo siku ya Alhamisii tarehe 19 Mei, 2016. Kiongozi aliuliza kwa nini Serikali imeshindwa kutekeleza ule mradi wa shamba la miwa tangu mwaka 2006 kule Bagamoyo?   Likajibiwa vizuri tu na Waziri Mkuu.

Kumbe wajuaji na wafuatiliaji wa matamshi ya viongozi wakashangazwa na swali lile. Wakaja na hoja hii. Mbona kiongozi huyu amepinga vikali sana ule mradi wa Serikali wa kupanua KIA (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kule Kilimanjaro), lakini anashabikia shamba la miwa la Bagamoyo, kuna nini? 

>>ITAENDELEA

By Jamhuri