Ufuska kwa Marekani, uozo wa TBS kipi ni hatari zaidi?

Makachero wawili wa Serikali ya Marekani wamejiuzulu kwa kuwajibika, baada ya kukumbwa na kashfa ya kufanya ufuska nchini Colombia.

Wiki tatu zilizopita, maofisa 15 wa Jeshi na Idara ya Usalama wa Taifa walitangulia mjini Cartagena, Colombia, kuandaa na kusimamia ulinzi na usalama wa Rais Barack Obama, aliyehudhuria mkutano wa siku mbili wa Umoja wa Nchi za Amerika unaoitwa kwa kifupi OAS.

Kashfa hiyo iligundulika baada ya kachero mmoja kukiuka makubaliano ya malipo ya kulala usiku kucha na kahaba waliyekubaliana amlipe dola 800 za Marekani, lakini kulipokucha akampa dola 30 pekee na kuibua zogo la aina yake nje ya chumba alimokuwa amepanga katika Hotel de Caribe.

Kahaba huyo aliungwa mkono na mwenzake aliyekuwa amechukuliwa na kachero mwingine na kusababisha polisi waitwe ili kuokoa jahazi.

Mwanzo wa yote ni hatua ya makachero 11 kati yao kushiriki sherehe ya usiku na wawili kati yao kurudi hotelini walikofikia, huku wakiwa wamechukua makahaba kwa siri.

Wakati makachero hao wakiamua kujiuzulu wenyewe kwa tuhuma za kufanya ufuska huku wakiwa katika kazi hiyo maalumu, Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hapa nchini inaonyesha kuwapo kwa uozo mkubwa wa uongozi katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kuhatarisha uhai wa maisha Watanzania.

Katika toleo lake la Jumanne iliyopita, gazeti hili liliandika kwa kirefu kuhusu uozo huo wa kutisha huku Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Charles Ekelege, akiendelea kuliongoza bila yeye mwenyewe kutafakari, kupima na kuchukua hatua stahiki katika upande wa kwanza. Kuna madai kwamba amekuwa akilindwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami.

Katika taarifa yake iliyotikisa Mkutano wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliomalizika Jumatatu iliyopita, CAG ameainisha undani kuhusu uozo mkubwa unaofanywa na TBS dhidi ya maisha ya Watanzania.

Mbali na kuruhusu kuingizwa sokoni kwa bidhaa mbalimbali za nyumbani, pikipiki na kadhalika, kuna nyingine huingizwa nchini huku zikiwa na kiwango kikubwa cha hewa yenye sumu (carbon monoxide).

Bidhaa nyingine ni pamoja na maharage, ngano, vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini, oili za magari, mafuta ya magari, mafuta ya ndege, mbolea, betri, siagi aina ya Blueband, sabuni za unga aina ya Omo, vifaa vya ujenzi na kadhalika.

Chukulia mfano wa mamilioni ya walaji wa maharage, chapati, maandazi, kaimati na vyakula vingine vinavyotengenezwa kwa unga wa ngano, kisha ufikirie wangapi waliolishwa ‘sumu’ kwa kula bidhaa hizo zilizothibitishwa na TBS kwamba ni bora na kuathiri afya zao polepole na kimyakimya!

Fikiria Watanzania waliokula maharage hayo na vyakula mbalimbali vilivyotengenezwa kutokana na unga huo wa ngano ulioingizwa nchini kutoka nje, wale ambao sasa huenda wakaugua magonjwa makubwa ya hatari kama saratani.

Niambie Watanzania wangapi wanamiliki na kuendesha pikipiki zenye kiwango kikubwa cha hewa yenye sumu na abiria wao – wale wanaoivuta na kuijaza kwenye mapafu bila kujua chochote. Pia fikiria itakuwaje hapo baadaye kuhusu afya zao endapo si kuzikwa kaburini kutokana na uozo huo wa TBS!

Kana kwamba haitoshi, maisha ya watumiaji wa magari na ndege nayo yapo hatarini muda wote. Hali hiyo inatokana na vyombo hivyo vya usafiri wa nchi kavu na angani kutumia mafuta feki ya kulainishia mitambo na kuzungushia injini zake ili zifanye kazi.

Kila wanapokuwa safarini, wasafiri hao hufanana na watu waliojimwagia petroli na kupita karibu na moto, hivyo wanaweza kupata ajali wakati wowote kutokana na kutumia mafuta yasiyokuwa salama. Ndege inapokuwa angani inaweza kuanguka wakati wowote na kuua, na wale wanaotumia usafiri wa magari, nayo yanaweza kupinduka muda wowote na mahali popote.

Ajali hizo, kwa mfano, zinaweza kutokea kutokana na injini kupasuka na kuzimika ghafla huku gari likiwa kwenye mwendo mkali, tena inawezekana ikawa mahali ambako jiografia yake yenyewe ni ngumu kujinusuru katika hali yoyote.

Fikiria, Watanzania wangapi wanakunywa chai au maziwa ya moto yaliyohifadhiwa kwenye chupa maalumu za kuhifadhi joto (thermos) wakati kumbe hazifai! Chupa hizo za chai huwa na chembechembe hatari za sumu kwenye ‘mayai’ yake (vacuum flask), lakini wateja wanazinunua na kuzitumia bila kujua chochote kwa vile TBS inakuwa imethibitisha kuwa zina ubora wakati kumbe ‘zinawaua’.

Sema, ni wangapi wamekunywa vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini wakati havikidhi kiwango na kuhatarisha maisha yao wenyewe, lakini wamefanya hivyo bila kujua chochote ila ‘kwa ruhusa ya TBS’ inayojua madhara yake!

Wakati maisha yao yakiwa hatarini kwa viwango tofauti, wengine katika hesabu ya maelfu miongoni mwao wanakabiliwa na magonjwa hatari kama saratani kutokana na kutumia siagi aina ya Blueband isiyokuwa na kiwango. Wananunua na kuzijaza nyumbani kwa ajili ya kukaangia mboga au kupaka mikate kwa ajili ya chai ya asubuhi, lakini kumbe wanajijazia sumu na kuwaua polepole na kimyakimya!

Ekelege na wenzake wanaelewa pia kiasi gani wanaruhusu mbolea feki itumike kwa kilimo na kusababisha wakulima wapoteze nguvu zao nyingi bila faida yoyote. Wanapoteza muda wao mrefu wakihangaika shambani na kutumia akiba zao za fedha kununua mbolea, lakini wanapoitumia ili kukuzia mazao wanayolima, inaharibu ardhi yao kwa vile haina kiwango ingawa imethibitishwa na TBS kuwa ina ubora wote unaotakiwa.

Katika hali hiyo, shirika hilo la umma linashiriki kwa makusudi kuhujumu uchumi wa nchi kwa kusababisha njaa inayoweza kuzuilika, halafu linafanya hivyo huku wakati huohuo likiwalisha sumu mamilioni ya watu wakiwamo wakulima.

Linashiriki kuwaua kwa kuruhusu wale vyakula vyenye sumu kutoka nje ya nchi, hatua inayokuja baada ya kuanza kwanza kuwapelekea mbolea inayonyausha mazao wanayolima, kuharibu ardhi yao kwa kuidumaza ili isifae tena kwa kilimo, au vinginevyo!

Sipati maneno mazuri ya kuandika kuhusu uozo mkubwa uliofichuliwa na CAG pale TBS, lakini wahusika wote wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Ekelege, hawaonyeshi angalau tu mwelekeo wa kujutia ‘madudu’ yao hayo na ‘kununua’ dhambi hadi kwa Mungu.

Hawajali kuwa maisha ya duniani yakiisha yanayofuata wakosefu wote wanatupwa kwenye moto unaowaka milele, lakini ukitajiwa majina yao unakuta wote wanaamini Biblia Takatifu au Quran Tukufu! Hawataki kutafakari, kupima na kuchukua hatua stahiki kutokana na taarifa hiyo ya CAG ili kuwajibika kwa taifa na kutubu kwa Mungu. Kila nikiisoma ingawa sihusiki na chochote, najikuta natetemeka na kukosa hata usingizi.

Swali linaloumiza kichwa changu ni je, hivi ufuska uliofanywa mara moja tu na makachero wa Marekani na uozo uliojichimbia TBS kipi ni hatari zaidi?

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0713 676 000 na 0762 633 244