TAIFA LETU, AMANI YETU

A. UTANGULIZI
“Fumbua Kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote
walioachwa peke yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; uwapatie
maskini na wahitaji haki yao” (Mithali 31: 8-9).
Wapendwa wana KKKT,
Watukuka, watu wote na familia ya Mungu katika Taifa letu,
“Amani iwe kwenu!; Kristo Amefufuka (Yohana 20:19).
Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka, alipowatokea wanafunzi wake wakiwa
wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, aliwasalimu na kujifunua kwao kwa
salaamu ya kuwatakia amani. Wapendwa watu wa Mungu, katika umoja wetu, sisi
maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), tunawasalimuni nyote
kwa kuwatakia amani. Bwana wetu Yesu Kristo Amefufuka kweli kweli –
Haleluya!. Yeye ni amani yetu, na pia ni amani kwa watu wote wenye mapenzi
mema. Kwa kufufuka kwake, upendo umeishinda chuki; unyenyekevu
umeushinda ubabe; nuru imelishinda giza; haki imeshinda udhalimu; msamaha
umeshinda visasi; ujasiri umeshinda hofu; na kwa hiyo uzima umeshinda kifo.
Mwaka 2017, Kanisa letu limeadhimisha miaka 500 ya Matengenezo ya Kanisa.
Tukiwa wana Matengenezo tumekumbushwa tena kuwa mwanadamu
anaokolewa kwa Neema ya Mungu tu: Wokovu Hauuzwi; Mwanadamu
Hauzwi wala kununuliwa; na Uumbaji hauuzwi. Kanisa zima na dunia kwa
ujumla tunaitwa kusimama pamoja na kuueleza ukweli huu unaoziweka huru
dhamiri zetu (Yohana 8:31-32).
Matengenezo (Reforms) ni dhana ya kibiblia. Tangu zama za Agano la Kale,
Mungu kwa nyakati mbalimbali aliteua wajumbe wake kuwasilisha ujumbe wake
kwa jamii na kwa watawala wa dunia. Kwa Umungu wake, aliwainua wanawake na
wanaume kwa makusudi ya kutoa unabii yaani, ujumbe wa Mungu kwa jamii au
watawala. Wakati mwingine aliinua manabii kuwasemea wasiokuwa na sauti.
Unabii na Matengenezo ni njia ya Mungu katika kusimika utawala wa haki na
unaostawisha uhuru na amani.

2

Kwa namna ya pekee, manabii kama Daniel, walionya juu ya uongozi unaojenga
uhalali wake katika wingi wa watu wanaokubaliana na uongozi huo hata kama ni
katika makosa. Haikuwa rahisi kibinadamu kuukosoa mfumo kama huo lakini
Mungu alitumia manabii kuzungumza na mfumo wa namna hiyo. Unabii wa
Daniel 3:7 unasema, “Kwa hiyo watu WOTE, mara waliposikia sauti za
baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari, na sauti za ala nyingine za
muziki, walianguka kifudifudi na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo
Mfalme Nebkadneza aliisimamisha”. Hapa tunaona kosa la kiongozi
kutengeneza sanamu, linasababisha kosa la watu wanaokubali kuiabudu hiyo
sanamu. Tumetafakari na kusadiki kuwa, kosa la kiongozi au mfumo,
haliwaondolei hatia wanaomfuata kiongozi au kuufuata mfumo, hata kama watu
hao walikula kiapo cha kutii maongozi ya kiongozi huyo na mfumo wake. Mbele
ya Mungu hakuna ile kanuni ya kuwajibika kwa pamoja. Kila mtu kwa dhamiri
yake anawajibika mbele za Mungu. Kwa upande mwingine, pamoja na uwajibikaji
wa mtu binafsi, Nabii Ezekieli anatukumbusha na kutuonya kuwa tusipoonya na
kusimama katika zamu yetu, hatia na damu ya wasio na hatia, itadaiwa mikononi
mwetu (Ezekiel 33: 8-9).
Adhimisho la kufufuka kwa Yesu Kristo (Pasaka) na maadhimisho ya miaka 500 ya
Matengenezo ya Kanisa, yanatusukuma kutafakari utume wa Kanisa katika jamii
kwa nyakati zetu. Tunaalikwa kupeleka ujumbe wa amani kwa watu wote na
kusimama kwa ujasiri katika kuwasemea wasio na sauti katika jamii ili kuenzi
roho ya Pasaka na Matengenezo katika nyakati zetu. Kama Kanisa na kwa nafsi
zetu mmoja mmoja, tunaitwa kwa upande mmoja, kufundisha, kushauri na kutia
moyo. Kwa upande mwingine, tunaitwa kuonya, kukaripia, kukemea na kuelekeza
kwa uvumilivu wote na upendo (2 Timotheo 4: 1-5).
Wajibu huu kwetu sisi maaskofu ni wito na utume usiokwepeka; na kwa watu
wote wa imani, wajibu huu hauna mbadala. Tunaagizwa kuchochea ujenzi wa
madaraja ya maridhiano katika upendo na amani, na kuwa kinyume na mifumo
yote inayoendeleza chuki na marafakano. Kwa kufanya hivyo, imetupasa kusema
wazi wazi ujumbe wa amani, upendo, heshima, utu, ustahimilivu na maelewano.
Mfumo wowote unaojengwa katika utii wa sheria bila upendo; heshima bila
uhuru; na amani bila haki, unajengwa katika msingi usio imara. Kupuuza wito huu
kuna madhara kwa jamii yetu. Ni sawa na kujenga nyumba juu ya mchanga
(Mathayo 7: 26). Tunasihi kwa machozi mengi, tuwe wajenzi wenye akili wajengao
nyumba zao juu ya mwamba (Mathayo 7:24). Mwamba tunaotakiwa kujenga taifa
letu lenye dini mbalimbali, vyama mbalimbali, na makabila mbalimbali, umetajwa
katika sala kuu ya taifa letu, yaani, “DUMISHA UHURU NA UMOJA”. Bila Uhuru
hakuna umoja uwezao kuleta maendeleo; na bila umoja wa kitaifa, uhuru wetu

3

hauleti amani endelevu. Kwa sababu ya nguvu ya dhamiri safi iliyo dira ya taifa
letu, tunalazimika kumtii Mungu kuliko mwanadamu (Matendo 5:29).
B. TAIFA LETU NA AMANI YETU
Tunapoadhimisha sikukuu ya kukumbuka kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo,
tunatambua kuwa utume wa Kanisa letu katika taifa letu, unafanyika katikati ya
changamoto kadhaa. Kwa kuwa Kanisa ni sehemu ya jamii, linaguswa na
changamoto hizo. Katika kukaa pamoja na kuliombea taifa letu, sisi maaskofu wa
KKKT, tumetafakari na kubaini changamoto hizo. Kwa njia ya salaam za Pasaka,
tunaleta kwenu changamoto tatu ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na
viongozi wake.
1. Jamii na Uchumi
Kiini cha Utume wetu katika jamii kinatuingiza kwa nia njema katika maisha ya
uchumi na mshikamano wa kijamii. Neno la Mungu linatufundisha kuwa
“Mwanadamu hawezi kuishi kwa mkate peke yake” (Luka 4:4). Pia neno la
Mungu linatuhakikishia kuwa Bwana wetu Yesu Kristo alikuja ili tuwe na
uzima tele (Yohana 10:10). Tunawiwa katika umoja wetu wa ubaba,
kuipongeza serikali yetu kwa jitihada inazofanya kuboresha maisha ya
wananchi. Tumeshuhudia jitihada na nia njema kuhusu uvunaji na umilikaji wa
raslimali za nchi kwa manufaa ya taifa zima. Aidha, tunapongeza jitihada za
ukusanyaji wa kodi ili kuiwezesha serikali kugharamia huduma za jamii. Hata
hivyo, bila kukatisha tamaa jitihada hizo, tunawiwa kushauri yafuatayo:
I. Sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa maendeleo, si washindani
wa serikali katika kuchangia maendeleo ya taifa. Mazingira yasiyo rafiki
kuhusu wadau hawa, ni kikwazo kisicholeta mshikamano kati ya serikali
na sekta binafsi na mashirika ya dini katika kuleta maendeleo. Jitihada za
makusudi na za mara kwa mara zifanyike kuondoa dhana ya ushindani
kati ya serikali na wadau hawa ili kuimarisha mahusiano mema kati ya
serikali na sekta binafsi.
II. Ili mfumo wa ukusanyaji wa kodi uwe endelevu; jitihada za kukusanya kodi
ziendane na elimu kwa mlipa kodi. Msisitizo wa uzalendo wa kulipa kodi
uende sambamba na ustawi wa walipa kodi katika shughuli zao za
biashara. Mivutano isiyo na tija kati ya walipa kodi (wafanya biashara) na
mamlaka ya ukusanyaji wa kodi, inastawisha uadui unaopunguza
makusanyo ya kodi na kujenga ushawishi wa rushwa. Mfumo wa kodi
unaowafilisi wafanya biashara, haulengi kujenga uchumi wa viwanda.
III. Kutokana na ongezeko kubwa la vijana wasio na ajira; jitihada za wazi na
za makusudi zifanyike ili msukumo wa uchumi wa viwanda ufikie
matumaini yanayoshikika miongoni mwa vijana wasio na ajira. Sekta

4

binafsi, wawekezaji na wadau wengine, wahakikishiwe usalama wa mitaji
yao kisheria. Hili likifanyika ni kichocheo kizuri cha ujenzi wa viwanda.
IV. Uchumi wa viwanda (vidogo na vikubwa) uendane na uwekezaji katika
sekta ya kilimo maeneo ya vijijini. Kilimo na ufugaji ndizo sekta zenye
wigo mpana wa viwanda vinavyogusa maisha ya watanzania walio wengi.
Utozaji holela wa kodi na ushuru wa mazao unakatisha tamaa wadau wa
kilimo. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja, na
wakulima/wafugaji na wawekezaji kwa upande wa pili, si kivutio cha
uwekezaji katika sekta ya kilimo.
2. Maisha ya Siasa
Kwa umoja wetu katika utume, tunatambua siasa safi na uongozi bora kuwa ni
misingi iliyoongoza maisha ya siasa katika taifa letu. Ujio wa vyama vingi
mnamo 1992, haukuondoa umuhimu wa misingi hii bali ulipanua matumizi ya
demokrasia iliyojengwa katika uhuru wa mawazo. Taifa ni mkusanyiko wa
taasisi na watu mbalimbali, wenye lengo moja lakini kwa njia mbalimbali.
Kutokana na wingi huu, taifa letu daima ni juu ya vyama, taasisi na makundi.
Taifa huongozwa na katiba iliyo kiini cha sheria zote. Taifa haliongozwi na
ilani za vyama. Serikali haiongozwi na ilani za vyama. Serikali huongozwa na
katiba, sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi na tunu za taifa). Serikali
husimamiwa na bunge huru lililo sauti ya wananchi. Wananchi ndilo
chimbuko la madaraka ya bunge. Bunge halisimamiwi na ilani, chama
chochote wala mtu awaye yote. Kwa umoja wetu na kwa nyakati zetu, hivi
sasa tunashuhudia matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi iliyolilea taifa
letu. Baadhi ya matukio hayo ni:
I. Hofu iliyojengwa katika matukio halisi yakiwamo utekaji, utesaji, kupotea
kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji
yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi
mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.
II. Kupungua na hatimaye kutoweka kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika,
na kupata habari. Kwa mwenendo huu, kuna hofu kuwa hata uhuru wa
kuabudu uko mashakani.
III. Kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge,
Mahakama, na Tume ya Uchaguzi. Hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa
kwa serikali za Mitaa.
IV. Kukosekana kwa mazingira ya haki na uhuru wa kuchagua na
kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi zote zimeghubikwa na
ubabe, vurugu, hila, na vitisho.

5

V. Utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye mwelekeo wa kiitikadi.
Hatua hii imeimarisha ubaguzi wa kiitikadi katika taifa letu na kukuza
migawanyiko.
VI. Kushamiri kwa chuki mioyoni mwa watu ambalo ni chimbuko la visasi,
kukata tamaa, na ushiriki mdogo wa wananchi katika chaguzi na maisha
ya siasa.
VII. Udhalilishaji wa kauli njema isemayo “Maendeleo hayana chama”.
Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika
chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta
maendeleo. Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu
anajiuzuru chama fulani, eti kwenda kuleta maendeleo katika chama
kingine? Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya watu
wanaokufa, kujeruhiwa na uharibifu wa mali.
Mambo haya ni tishio linalohatarisha umoja na amani ya nchi yetu.
3. Masuala Mtambuka
Kanisa ni alama ya uwepo wa utume wa kuleta na kutunza matumaini katika
jamii. Ukimya wa Kanisa katika masuala yanayoigusa jamii ni ukwepaji wa
wajibu wake. Lakini pia sauti ya Kanisa isiyomilikiwa na mtu isipokuwa Mungu
tu, ni chachu ya amani na matumaini. Kwa dhamiri safi inayotokana na
utambuzi wa “Wakati wa Mungu”(Kairos) katika taifa letu, tunawiwa
kutambua masuala mtambuka yanayogusa maisha ya watu kipekee na kwa
njia nyingi na kuyatolea ushauri ufuatao:
I. Kuhitimisha mabadiliko ya mara kwa mara katika mfumo wa elimu nchini
ili kuondoa mwanya wa kila mtendaji mkuu wa wizara kuja na sera yake.
Elimu ni kitovu cha ustawi wa taifa, kisiwe kinachokonolewa
chokonolewa kila wakati. Sekta zote nchini hujenga mafanikio yake
katika mafanikio ya mfumo thabiti wa elimu.
II. Uwezeshaji wa vijana kupata mikopo ya elimu ya juu uwe shirikishi na
usiokuwa na “ubaguzi” kati ya wanafunzi wa vyuo binafsi na wale wa
serikali; sayansi na sanaa; wazazi maskini na wenye nafasi; waliosoma
shule binafsi na wale wa shule za serikali, n.k. Kwa kuwa huu ni mkopo,
jitihada ziwekwe zaidi katika urejeshaji wa mkopo huo kwa kuzingatia
kuwa huu ni mkopo kwa mtoto siyo kwa mzazi.
III. Vyombo vya usimamizi wa sheria na utoaji haki vionekane vinatenda
haki sawa kwa watu wote na makundi yote bila kuacha ishara za fadhila
au kukomoana.
IV. Wajibu wa serikali kikatiba katika kulinda uhai wa raia wake, uonekane
unatekelezwa bila kuacha mwanya wa kuituhumu serikali. Ukiachwa
mwanya katika ulinzi wa uhai wa raia, waweza kutumiwa na mamluki

6

kujichukulia sheria mkononi kwa niaba ya serikali. Damu isiyo na hatia
ina madhara kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo. Mpaka sasa tumeshuhudia
umwagaji wa damu unaotusuta sisi sote na mamlaka zote. Mungu
anatusuta watanzania kama alivyomsuta Kaini: “Sauti ya damu ya
ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi” (Mwanzo 4:10).
V. Uhai wa mtu una thamani isiyopimika. Ni wajibu usiokwepeka kuulinda
na kuutunza uhai kwa vitendo halisi. Endapo uhai umepotea katika
mazingira yoyote, uchunguzi huru na wa haki ufanyike na taarifa
zitolewe kwa wakati muafaka ili kujenga jamii yenye imani kwa serikali na
vyombo vyake. Matukio ya mauaji ya askari wetu, mauaji ya raia,
majaribio ya kuwaua wanasiasa, utekaji, na uteswaji visipochunguzwa na
kutolewa taarifa, ni shina la hofu na uchungu katika jamii. Jamii iliyojaa
hofu na uchungu, haiwezi kuwa na maendeleo wala kuwa na roho ya
uzalendo.
VI. Ili kulipatia taifa letu ufumbuzi wa mambo yote tuliyotaja na kushauri
kwa wakati huu na ujao; tunaisihi serikali ya awamu ya tano, kurejea
mchakato wa upatikanaji wa KATIBA MPYA ya wananchi,
iliyopendekezwa na wananchi kupitia Tume ya Warioba. Watanzania
wengi wanaona na kuamini kuwa KATIBA MPYA ina majibu ya kukidhi
mahitaji ya taifa letu kwa sasa na baadaye. KATIBA MPYA ni zao la utashi
wa Watanzania kupitia tume ya Warioba iliyokuwa na uwakilishi mpana
wa taifa letu.
VII. Aidha, tunawashauri raia wema, kwa njia za kidemokrasia kupitia
majukwaa ya kikatiba yaliyo katika maeneo yao, kudai upatikanaji wa
KATIBA MPYA. Itapendeza ikiwa KATIBA MPYA itapatikana kabla ya
uchaguzi mkuu ujao. Mambo mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu
ya tano yatadumu iwapo kuna KATIBA MPYA inayolinda mazuri. Kiongozi
mzalendo si mbadala wa KATIBA MPYA. Tanzania yenye amani na
maendeleo ni tunda la itikadi zote, dini zote, makabila yote na makundi
yote chini ya KATIBA MPYA.

C. HITIMISHO
Kufufuka kwa Yesu Kristo ni kiini cha Matengenezo ya Kanisa. Kwamba, katikati ya
jamii iliyokata tamaa na kutawaliwa na hofu, Kristo alifufuka na kuleta matumaini
mapya. Kwamba, katikati ya wasiwasi wa Kanisa kupoteza nguvu ya utume wake,
Roho Mtakatifu aliongoza Matengenezo ya Kanisa. Kwa hiyo Matengenezo ni
endelevu katika jamii ya watu na taasisi zao. Muasisi wa Matengenezo Dr. Martin
Luther yungali analiwajibisha Kanisa kuzingatia utume wake unaoleta matumaini
mapya kila siku. Waliobatizwa wote ni wamisionari tunaotumwa na Bwana wetu
Yesu Kristo (Yohana 20:21). Imetupasa kuwa nuru na chumvi ya jamii na kuwa
mawakala wa uhuru, umoja na amani.

7

Taifa letu lilipata uhuru mwaka 1961 bila kumwaga damu. Roho ile ile ya
majadiliano na maridhiano iliyokuwamo ndani ya waasisi wa taifa letu, inatakiwa
kila wakati. Uhuru ulioletwa kwa majadiliano, utunzwe na kulindwa bila ulazima
wa kumwaga damu ya watanzania. Uhuru na Umoja ndizo ngao zetu
zilizolitunza taifa kwa zaidi ya miaka 50.
Sisi tulio maaskofu kwa neema ya Mungu, tunaleta wito kwenu wenye imani
katika dini mbalimbali, kuliombea taifa letu. Kuwaombea wote wenye madaraka
ili wajaliwe hekima, busara na upendo kwa taifa na watu wake. Kupitia jumuia
ndogo ndogo na sharika zote, waombee viongozi wetu ili Mungu awajalie na
kuwatunuku kiu ya kutenda haki, kusikiliza kuliko kusema, kuelekeza kuliko
kuamrisha, kuunganisha kuliko kutawanya, kupenda watu kuliko kutamani
kupendwa na watu, kutamani kutumika kuliko kutumikiwa (Marko 10:45),
kuheshimu kuliko kuheshimiwa.
Ujumbe wa Pasaka unatuhimiza kuthamini uhai. Bwana wetu Yesu Kristo alikubali
kufa ili kuhifadhi uhai wetu. Kwa kufa kwake na kufufuka, amekomesha kifo na
mawakala wake. Tunaitwa kuthamini uhai na kutoruhusu tena watu kuteswa na
kuuawa. Kwa hekima yote na unyenyekevu, tunasihi tena, kwamba ikubalike kuwa
hitaji la watanzania walio wengi kwa sasa ni KATIBA MPYA. Katiba Mpya ipatikane
ili kukuza na kuimarisha mfumo wa utawala utakaolinda uhai wa watu, raslimali
za nchi, tunu za taifa, uhuru wa mihimili ya dola, na uwajibikaji wa viongozi kwa
wananchi.
Tunawatakia Pasaka njema ya mwaka 2018, na Mungu awabarikini nyote.
Ni sisi
1. Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo, Mkuu, KKKT na Dayosisi ya Kaskazini
2. Askofu Dkt. Benson K. Bagonza, Dayosisi ya Karagwe
3. Askofu Dkt. Stephen I. Munga, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki
4. Askofu Dkt. Alex S. Mkumbo, Dayosisi ya Kati
5. Askofu Blaston Gaville, Dayosisi ya Iringa
6. Askofu Dkt. Abednego N. Keshomshahara, Dayosisi ya Kaskazini Magharibi
7. Askofu Andrew P. Gulle, Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria
8. Askofu Dkt. Emmanuel Makala, Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria
9. Askofu Chediel E. Sendoro, Dayosisi ya Mwanga
10. Askofu Charles R. Mjema, Dayosisi ya Pare
11. Askofu Elias Kitoi Nassari, Dayosisi ya Meru
12. Askofu Dkt. Solomon Massangwa, Dayosisi ya Kaskazini Kati
13. Askofu Jacob Mameo Ole Paulo, Dayosisi ya Morogoro

8
14. Askofu Michael Adam, Dayosisi Mkoani Mara
15. Askofu Isaya Mengele, Dayosisi ya Kusini
16. Askofu Job Mbwilo, Dayosisi ya Kusini Magharibi
17. Askofu Renard Mtenji, Dayosisi ya Ulanga Kilombero
18. Askofu Ambele Mwaipopo, Dayosisi ya Ziwa Tanganyika
19. Askofu Dkt. Alex G. Malasusa, Dayosisi ya Mashariki na Pwani
20. Askofu Dkt. Edward Mwaikali, Dayosisi ya Konde
21. Askofu Levis L. Sanga, Dayosisi ya Kusini Kati
22. Askofu Amon Mwenda, Dayosisi ya Ruvuma
23. Askofu Lucas Y. Mbedule, Dayosisi ya Kusini Mashariki
24. Askofu Amon Kinyunyu, Dayosisi ya Dodoma
25. Askofu Nicolaus Nsanganzelu, Dayosisi ya Mbulu
26. Askofu Mteule Isaack Kissiri Laiser, Dayosisi Teule ya Magharibi Kati
27. Askofu Mteule Wilson Sanga, Dayosisi ya Kusini Kati

Arusha, 15 Machi 2018

By Jamhuri