Wakala wa Nishati Vijijini (REA), analalamikiwa kutoa zabuni za mabilioni ya shilingi na mamilioni ya dola kwa kampuni kadhaa za ndani na nje ya nchi katika mazingira yanayotia shaka, JAMHURI limeambiwa.
Miongoni  mwa wanufaika ni mmoja wa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tano, ambaye ingawa haonekani moja kwa moja, JAMHURI limepata uthibitisho wa ushiriki wake.
Zabuni hizo zinahusu Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu unaolenga kufikisha umeme wa gridi kwenye vijiji 3,559 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Thamani yote ya mradi huu ni shilingi zaidi ya bilioni 900; kiwango ambacho ni cha kihistoria katika awamu moja ya kusambaza umeme kupitia REA.


Tuhuma za upendeleo zimesababisha baadhi ya washiriki kulalamika, na miongoni mwa malalamiko hayo yameweza kurekebishwa, huku mengine yakitupwa.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini ‘madudu’ kadhaa kuanzia usajili na sifa za kampuni zilizopewa zabuni hadi kwenye nguvu za baadhi ya ‘vigogo’ walioshirikiana na baadhi ya kampuni hizo.
Miongoni mwa yaliyobainika; mosi, kuna kampuni zilizopewa zabuni lakini zikiwa hazikusajiliwa katika Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).
Pili, kuna kampuni ambazo hazikusajiliwa CRB, lakini zimeshirikiana na wabia (JV) ambao ni wa madaraja ya chini wasiostahili kupewa zabuni kubwa.


Tatu, kuna kampuni zilizonyimwa zabuni kwa kukosa sifa, lakini kampuni nyingine zenye udhaifu na sifa za aina hizo hizo zimeshinda zabuni.
Nne, kuna kampuni zilizopewa zabuni za mabilioni ya shilingi ilhali sifa zake kama zilivyoorodheshwa CRB haziziwezeshi kutunukiwa zabuni za kiwango hicho kikubwa. Miongoni kwa kampuni hizo zimo ambazo usajili wake ni wa kufanya kazi za ukandarasi kwa umeme wa majengo na si wa gridi (powerline).
Tano, JAMHURI limeweza kubaini baadhi ya kampuni za ndani zilizoanzishwa haraka haraka, zikiwa zimeshinda na kupewa mafungu (lots) zaidi ya moja ilhali zikiwa hazina uzoefu kwenye kazi hiyo.

Hali ya mambo
Kampuni ya Radi Service Limited iliyoingia ubia na kampuni za Njarita Contractor Ltd na Agwila Electrical Contractors Ltd, kati ya mafungu ya zabuni walizopata ni la dola 991,971.65 za Marekani; na Sh bilioni 7.393. Zabuni hiyo ni kwa mradi ulio katika wilaya za Mkinga, Muheza, Pangani na Bumbuli mkoani Tanga.
Pamoja na ushindi huo, imebainika kuwa kwenye usajili wake CRB, kampuni ya Radi ni ya Daraja la II na la III. Taarifa za CRB zinaonesha kuwa kampuni ya Agwila ni ya Daraja la V; na Njarita Contractor Ltd usajili wake ni wa Daraja la V.
Wabia hao wameshinda pia lot nyingine yenye thamani ya dola milioni 3.787; na Sh bilioni 25.61 katika wilaya za Nanyumbu, Masasi, Newala, Tandahimba na Mtwara Vijijini mkoani Mtwara. 


Kwa muktadha wa kazi zinazopaswa kufanywa kulingana na ukubwa wa zabuni iliyotangazwa, kampuni zenye sifa ya moja kwa moja (kwenye zabuni hii) ni za daraja la kwanza. Kampuni kwenye daraja hilo, hazina ukomo wa kiasi cha fedha zinazopaswa kulipwa kwenye kila fungu (lot).
Wakati hali ikiwa hivyo kwenye Daraja la I, madaraja mengine na ukomo wa kiwango cha fedha kwa kazi hiyo ya umeme wa gridi ni: Daraja la II (Sh bilioni 2), Daraja la III (Sh bilioni 1.2), Daraja la IV (Sh milioni 600), Daraja la V (Sh milioni 300) na Daraja la VI ni Sh milioni 150.
JAMHURI limeelezwa kuwa inapotokea kampuni zote wabia ikawa hakuna yenye Daraja la I, lakini zikiwa zimeungana, zinaruhusiwa kuandika barua CRB ili zipatiwe kibali kabla ya kuomba zabuni. Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kampuni hizo, kwa umoja wao licha ya kuwa wabia, hazikuwahi kuandika barua na kupewa kibali.


“Kampuni zote hizi tatu hakuna yenye Daraja la I, lakini wamepewa kazi ya mabilioni ya shilingi kwenye lots mbili; hiki ni kinyume cha taratibu na sheria,” kimesema chanzo chetu.
Nayo, kampuni ya Whitecity International Contractors Limited, imeingia ubia na kampuni ya Guangdong Jianneng Electric Power Engineering. Wabia hawa wamepangiwa kufanya kazi katika Mkoa wa Simiyu. Thamani ya lot hiyo kwa Mkoa wa Simiyu ni dola milioni 2.9 za Marekani; na Sh bilioni 22.
Wakati wakishinda zabuni hiyo nono, imebainika kuwa kwenye taarifa za Bodi ya Usajili wa Makandarasi, kampuni ya Whitecity International Contractors Limited imesajiliwa kwa kazi za umeme (Daraja la IV), majengo (Daraja la II), Civil (Daraja la IV) na Civil specialist (Daraja la II).
Kampuni ya Guangdong Jianneng Electric Power Engineering, hadi JAMHURI linaandika habari hii, haikuwa na usajili wowote CRB.


Zabuni nyingine yenye utata imetolewa kwa kampuni ya MF Electrical Engineering Limited ambayo imeingia ubia na kampuni ya GESAP Engineering Group Limited.
Kutoka CRB, imebainika kuwa MF Electrical Engineering Limited usajili wake ni wa Daraja la V; na kampuni ya GESAP Engineering Group Limited usajili wake kwenye masuala ya umeme ni wa Daraja la II.
Wabia hao wameshinda zabuni katika wilaya za Mlele, Mpanda na Tanganyika mkoani Katavi. Kwenye lot ya kwanza ambayo JAMHURI lina nakala yake, wanalipwa dola milioni 5 (zaidi ya Sh bilioni 10) za Marekani; pamoja na Sh bilioni 23.748.
Kwenye lot ya pili, wameshinda zabuni ya kufanya kazi katika wilaya za Kasulu, Buhigwe, Kigoma na Uvinza mkoani Kigoma. Thamani ya lot hiyo ni dola milioni 3.852 za Marekani; na pia Sh bilioni 19.899.
Shaka nyingine ipo kwenye kampuni ya Joe’s Electrical Ltd ambayo imeingia ubia na AT & C Pty na L’S Solution Limited. Uchunguzi umeonesha kuwa kampuni ya Joe’s Electrical Ltd ni ya kigeni. Hadi wabia hawa wanakabidhiwa barua za kusudio la kuwapa zabuni, kampuni za Joe’s Electrical, AT & C Pty Ltd na L’S Solutions Ltd hazikuwa na usajili CRB.


Pamoja na upungufu huo ulioonekana, REA imeweza kuwapa wabia hao ushindi wa lots mbili. Lot ya kwanza ni ya thamani ya dola za Marekani milioni 1.5; na Sh bilioni 15.695 kwa mradi kwenye vijiji vilivyoko wilaya za Bahi, Kongwa na Chemba mkoani Dodoma.
Lot nyingine waliyoshinda ni ya mkoani Kagera yenye thamani ya dola milioni 1.915 za Marekani; pamoja na Sh bilioni 17.958.
Chanzo chetu cha habari kimesema: “Ukiwa na kampuni ya kigeni kama ilivyo Joe’s hata kama ina Daraja la I, lakini akawa na mbia Mtanzania ambaye hana usajili, moja kwa moja hawastahili kupewa zabuni. Hapa unaona mgeni hana usajili, mwenyeji hana usajili…ni shida.”
Aidha, kampuni ya Al-Hatimy Developers Limited ambayo kwenye daftari la CRB inaonekana kuwa ni ya Daraja la II kwenye masuala ya umeme (siyo powerline), imepata zabuni yenye thamani ya Sh bilioni 59.816 kwa ajili ya miradi iliyoko katika wilaya za Chato, Nyang’wale, Bukombe na Mbogwe mkoani Geita.

Utata mwingine
Kampuni ya Power Magic Electrical Contractor and Suppliers, iliyokuwa imepewa barua ya kusudio la zabuni, imeondolewa dakika za mwisho kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kukosa sifa.
Iliondolewa kwa barua ya Mei 15, mwaka huu siku ambayo JAMHURI lilifanya mahojiano na viongozi wa ngazi ya juu wa REA katika ofisi zao zilizopo Mawasiliano Towers, Barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam. Miongoni mwa maswali waliyoulizwa yalihusu ‘kupewa zabuni’ kampuni hiyo licha ya kuwa usajili wake ni wa Daraja la V; na haikuwa na mbia.


Power Magic Electrical Contractor and Suppliers ilikuwa tayari imeshajihakikishia lots za mbili. Moja ikiwa na thamani ya dola milioni 2.86; pamoja na Sh bilioni 14.095. Kiasi hicho ni kwa ajili ya mradi wa umeme katika wilaya za Chamwino, Kondoa na Mpwapwa mkoani Dodoma.
Lot ya pili ilikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 4.32; pamoja na Sh bilioni 24 ambazo ni kwa ajili ya kutekeleza zabuni hiyo katika Mkoa wa Singida.
Utata mwingine umejitokeza kwa kampuni ya Nipo Group Limited inayopewa kazi katika Mkoa wa Arusha. Awali, ilionekana kuwa haina usajili CRB, lakini baadaye ikabainika kuwa ipo- ikiwa na usajili Daraja la V.


Kampuni hii imepewa zabuni yenye thamani ya dola milioni 2.011; na kiasi kingine cha Sh bilioni 15.545; ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya kazi za kiwango cha gridi. Haina mbia kama ilivyo kwa kampuni nyingine za Watanzania ambao hazina sifa.
Kampuni hii inatajwa kuwa na uhusiano wa karibu na mmoja wa mawaziri wenye umri wa kati, wanaotoka katika mmoja wa mikoa ya Kanda ya Kati. Mara kadhaa waziri huyo amesikika akieleza ‘alivyotokwa na jasho’ ili kuhakikisha washirika wake hao wanafanikiwa.
“Ameweza kuwatafuta washindani wa Nipo na wakati mwingine kwa kuwapigia simu akiwaonya na kuwatisha wasithubutu kutibua zabuni hii, akisema ametumia fedha nyingi kuipata,” kimesema chanzo chetu.
Jina la waziri huyo tunaendelea kulihifadhi kwa sasa kwa kuwa hajapatikana kuzungumzia madai hayo.
Mtu aliyejitambulisha kuwa ni Mkurugenzi wa Nipo (kupitia simu zilizowekwa kwenye fomu za maombi ya zabuni za REA), amezungumza na JAMHURI, na baadaye kupelekewa maswali akiombwa ayajibu. Hata hivyo, kwa wiki nzima amegoma kujibu maswali hayo.

Udhaifu kwenye uhakiki
Mei 16, REA kupitia tovuti yake, ilitoa taarifa iliyosomeka: “Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umekamilisha taratibu za zabuni kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (Turnkey III) na unawajulisha Wakandarasi [Makandarasi] walioshinda kwamba hatua inayofuata ni kupewa barua za tuzo (Award Letters) na kusaini mikataba.
JAMHURI limebaini udhaifu kadhaa katika kuwapata washindi wa zabuni. Miongoni mwa udhaifu unaotajwa ni kukosekana kwa ‘vetting’ miongoni mwa waombaji zabuni.
“Due diligence (chunguzi za kina) ya kukagua kampuni zinazoomba zabuni kule REA kabla ya kuzipa ushindi hakuna. REA wanatuma makandarasi waombaji wenyewe wajifanyie due diligence halafu wawapelekee taarifa. Hawaendi hata BRELA kujua kweli hizi kampuni zinazoomba zipo? Ofisi zake ziko wapi? Wenye nazo ni Watanzania kweli?” Kimesema chanzo chetu.
 
REA watoa ufafanuzi
JAMHURI limezungumza na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Injinia Gissima Nyamo-Hanga, aliyekuwa na wakurugenzi wengine wanne.
Injinia Nyamo-Hanga anasema utaratibu wote wa kuandaa, kutangaza, kuchambua na kuwatangaza washindi umefuata taratibu zote kisheria.
“Kisheria tulitimiza masharti yote, tukatoa hadi siku saba inavyoagizwa kisheria ili mwenye malalamiko ayalete. Tukapata malalamiko sita kutoka kampuni 43 kwenye lots 26. Kwa ujumla wote malalamiko yalikuwa manane. Wajibu wa mkuu wa taasisi (REA) ni kuyajibu, na kama yupo ambaye hakuridhika anakata rufaa PPAA [Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma].


“Kampuni mbili zililalamika, tukapata notisi na kutakiwa kuwasilisha vielelezo. Tukajibu notisi, na wakati huo kisheria tukatakiwa tusimamishe kila kitu. Tukafanya hivyo. Kesi ikasikilizwa na ruling (hukumu) ikatolewa Mei 12, 2017. Ikaonekana malalamiko ya wazabuni hayakuwa na uzito wa kisheria.
“Yote yaliyokuwa yamelalamikiwa kule PPAA yalionekana tumeyafanya huku REA kwa mujibu wa sheria za ununuzi. Ngazi hizi zimewekwa ili kuleta transparency. Hizi kazi ni nyingi, ziko complicated. Kunatakiwa ukaguzi wa ndani (REA) na nje kwenye public (kwa umma na kwa washindani wa zabuni),” amesema.
Lakini upande wa waliolalamika PPAA wanasema hukumu iliamuriwa kibabe kwa kuwa jaji hakutaka kupokea vielelezo vya ziada baada ya kubaini kuwa baadhi ya wazabuni walikuwa hawana sifa kama za usajili na za madaraja. JAMHURI limepata nakala ya hukumu hiyo wakati ikienda mitamboni.
Nyamo-Hanga anasema kwa mkandarasi wa nje aliyeomba zabuni endapo hayupo kwenye kanzidata ya REA, kimsingi akishashinda zabuni anatakiwa aende CRB apewe vielelezo ambayo ataviwasilisha REA. Kwa msingi huo, hadi kwanza mshiriki atangazwe mshindi ndipo apeleke vielelezo vya uhalali wake, ingawa REA wanasema vielelezo vyote hutakiwa viwasilishwe wakati wa kuomba zabuni.


“Waombaji wengi wa nje wanaomba kwa kushirikiana na local kupitia JV [Joint Venture] (ubia) wanapata temporary registration kutoka CRB. Huo ni mchakato maana watatakiwa walete vielelezo ili wapate zabuni, wakikosa, basi wanakosa zabuni,” anasema.
Ameulizwa kama haoni kitendo cha mwombaji kushinda ndipo aende CRB apewe vielelezo na kisha aviwasilishe REA hakiwezi kuchochea rushwa, na kuwa hakuna aliyehakikishiwa zabuni ya Sh bilioni 30 anayeweza kukosa vielelezo kwa njia za mkato, Injinia Nyamo-Hanga amejibu kwa kusema huo ndiyo ‘utaratibu uliopo kwa sasa.’
Kuhusu kiwango cha juu cha malipo kwa madaraja ya makandarasi (class limit), Mkurugenzi Mkuu anasema hilo suala lipo kisheria, lakini katika namna ya kuwasaidia Watanzania, imeonekana kunahitajika mabadiliko makubwa.
“Class limit ni moja ya malalamiko makubwa sana ya makandarasi wa ndani, na sisi tunasema hiyo kitu ifutwe kabisa. Kwenye Phase II (Mradi wa REA) wengi waliopata zabuni walikuwa wageni, lakini kazi zote zilifanywa na makandarasi wa ndani waliokuwa sub-contractors.
“Wageni walichukua fedha, wakalipa kidogo kwa kampuni za wazalendo, wakaondoka. Kuna barua nyingi za malalamiko ya makandarasi wa ndani kutolipwa na kampuni za kigeni,” amesema.
Nyamo-Hanga anasema endapo kuna malalamiko ya wasifu wa kampuni zilizopewa zabuni, muda bado upo kwa wananchi kuwasilisha maelezo ili hatua za kisheria ziweze kufuatwa.
Alipoulizwa juu ya kampuni ya Power Magic kuwekwa kwenye orodha ya waliokusudiwa kupewa zabuni licha ya kutokuwa na sifa, akasema: “Hao hatutafika nao hadi mwisho, bado tunaendelea kuwachuja kutokana na vielelezo tutakavyopata.”
Hata hivyo, JAMHURI limebaini kuwa wote waliopewa barua za kusudio la kupata zabuni; Mei 15, mwaka huu walikabidhiwa barua na hivyo kuitwa kwenye utiaji saini. Lakini siku hiyo hiyo kampuni ya Magic iliondolewa kwenye orodha ya ‘washindi’; na kuachwa wengine wanaotajwa kuwa na sifa kama zake. Miongoni mwa kampuni hizo ni Nipo Group Limited.


Injinia Nyamo-Hanga anatetea uwezeshaji wazawa akihimiza waungane ili waweze kupewa zabuni.
Anatoa mfano: “Kukiwa na jiwe la tani 3 mtu mmoja hawezi kulisukuma, lakini ukiwa na watu watano wanaweza kulisukuma. Tunawahimiza Watanzania waungane ili waweze kupata hizi zabuni kwa sababu hata kama hawana sifa za madaraja, kule CRB wanaweza kuonekana nguvu zao na kupendekeza wapewe kazi. Mtu mmoja mmoja si rahisi.
“Hizi fedha [zinazotumika kwenye miradi ya REA] – asilimia 95 ya funds za REA ni fedha za Watanzania wenyewe, ni fedha za humu humu ndani, kwa hiyo ni vizuri kwa manufaa ya uchumi wa nchi fedha hizi zikabaki kwa Watanzania wenyewe. Kuna umuhimu wa kuungana ili wapate hizi fedha, hiyo ndiyo sera ya uwezeshaji.”


Ameulizwa endapo REA hufanya uchunguzi kwa kushirikisha vyombo kama Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili kuwajua wenye kampuni zinazoomba zabuni, na kusema: “Hatuwezi kusema tuko perfect (sahihi) kwa asilimia 100. Kama nilivyosema bado tupo kwenye uchunguzi, tutafuatilia mengi hata kujua physical address ya hizo kampuni zinazoomba zabuni kama kweli zipo.
“Tunapoenda kusaini bado kuna vitu vingi kama bid security, bank statement, taarifa kutoka CRB na kadhalika. Suala la kuthibitisha uhalali wa hizi kampuni linaendelea bado,” anasisitiza. Wakati akisema hivyo, REA imeanza hatua ya mwisho ya kutiliana saini na washindi wa zabuni.
 
Takukuru wazungumza
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola, amezungumza na JAMHURI kuhusu kuwapo kwa malalamiko yanayoihusu REA kwenye Mradi Kamambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu.
Mlowola hakuwa tayari kukubali wala kukanusha habari za kuanza kwa uchunguzi wa suala hilo, akisema: “Nabanwa kisheria kulizungumza jambo lolote linaloletwa ofisini kwangu, na hasa hasa likiwa katika hatua za awali za uchunguzi. Nabanwa kisheria, lakini mambo tunayopokea ni mengi na inawezekana hilo likawa mojawapo au la! Kama lipo, wakati ukifika tutalieleza.”
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, hakupatikana kuzungumzia suala hili kwa kile kilichoelezwa na mmoja wa wasaidizi wake kwamba alikuwa katika msiba wa dada yake Musoma mkoani Mara.
 
Msimamo wa Rais John Magufuli
kwa Sheria ya Ununuzi
Desemba 2015, Tume ya Kurekebisha Sheria ilianza kuifanyia marekebisho Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 kama njia ya kuitikia mwito wa Rais John Magufuli ambaye aliahidi mabadiliko hayo wakati analizindua Bunge la 11.
Akizindua Bunge hilo, Rais Magufuli alisema: “Tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ili kuhakikisha kwamba mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi hafifu tunaiziba. Ni matarajio yangu tutakapoleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi [Ununuzi] ya Umma waheshimiwa wabunge mtatuunga mkono.”
Baada ya kauli hiyo, Tume ilitoa tangazo linalowataka wananchi na taasisi mbalimbali kutoa maoni ndani ya siku 30. Maoni na mapendekezo hayo yaliliwezesha Bunge kupitisha muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2016 iliyolenga kufumua mifumo ya kitaasisi iliyochochea wizi, rushwa na ufisadi. Sheria hiyo ilipitishwa Juni, mwaka jana.

Ukubwa wa Ununuzi wa Umma
Ukubwa wa ununuzi wa umma unaweza kuonekana kwa kuangalia kiasi cha fedha kinachotumika ikilinganishwa na pato la Taifa, ukubwa wa matumizi serikalini na bajeti ya Serikali.
Takwimu za utafiti wa ulinganisho wa ununuzi wa umma kwa nchi 10 uliofanywa na Benki ya Dunia (2015), zinaonesha kuwa nchi zinazoendelea hutumia wastani wa dola bilioni 820 za Marekani kwa mwaka katika ununuzi wa umma.
Huu ni wastani wa asilimia 15 hadi 20 ya pato la Taifa kwa nchi zinazoendelea. Katika nchi changa kiuchumi kama Tanzania, ununuzi wa umma unakadiriwa kuwa na wastani wa kati ya asilimia 60 hadi 70 ya matumizi yote ya Serikali. Katika nchi za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kimaendeleo (OECD), ununuzi wa umma hutumia takribani ya theluthi moja ya matumizi yote ya Serikali.
Hapa nchini, matumizi ya fedha kupitia ununuzi wa bidhaa na huduma yanachukua nafasi ya kwanza baada ya kutoa mishahara. Kwa mujibu wa Taarifa za Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma kati ya mwaka wa fedha wa 2007/2008 hadi 2014/2015, zinaonesha kwamba baadhi ya taasisi zilizokaguliwa katika kipindi hicho ziliingia mikataba ya ununuzi yenye thamani ya Sh trilioni 1.8 (2007/2008), Sh trilioni 2.963 (mwaka 2008/2009), Sh trilioni 3.075 (mwaka 2009/2010), Sh trilioni 4.532 (mwaka 2010/2011), Sh trilioni 4.325 (mwaka 2011/2012), Sh trilioni 4.884 (mwaka 2012/2013), Sh trilioni 4.859 (mwaka 2013/14) na Sh trilioni 4.349 (mwaka 2014/15).

By Jamhuri