Wizara ya Maliasili na Utalii imekumbwa na kashfa nyingine. Safari hii askari wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) na Pori la Akiba la Kijereshi wilayani Busega mkoani Simiyu, wakituhumiwa kubaka wanawake.

Habari zilizoifikia JAMHURI zinaeleza kwamba askari hao pia wanatuhumiwa kuwapiga wanawake na wanaume kwa kutumia mijeledi na wakati mwingine kuwajeruhi kwa risasi.

Wakazi wa Kijiji cha Kijereshi wamewalalamikia askari hao, kuwa wamekuwa wakifanya udhalilishaji na unyama huo wakati wanapowakamata watu walioingia kimakosa kutafuta kuni na kulisha mifugo katika maeneo hayo ya uhifadhi.


Wanakijiji hao wameanika malalamiko hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti, aliyefuatana na wajumbe wengine wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo katika mkutano wa hadhara kijijini hapo,  hivi karibuni.“Mheshimiwa mkuu wa mkoa, askari gemu wenu wa pori la akiba hapa Kijereshi, wamefikia hatua ya kuwakamata na kuwafanyisha ngono kwa lazima mama zetu, dada zetu na watoto wetu. Huu ni unyama usiovumilika. Wanafanya hivyo kwa sababu wao wamevaa magwanda ya kijeshi na wana bunduki.


“Pia wanalazimisha mifugo ya wanakijiji iingie porini kwa nguvu ili waikamate watoze pesa kwa ajili ya kutanua matumbo yao… ukikataa unapigwa risasi. Sasa kama Serikali itashindwa kutusaidia sisi, uvumilivu utatushinda,” alisema David Mashauri na kupigiwa makofi na umati wa wanakijiji wenzake.


Baada ya kusikia hivyo, Mabiti alimwagiza Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Salum Msangi, kushughulikia malalamiko hayo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha askari watakaothibitika kujihusisha na vitendo hivyo wanachukuliwa hatua za kisheria.


“RPC Salum Msangi, nakuagiza uchukue hatua za kukomesha mara moja unyama wanaofanyiwa wananchi wangu… sitaki kusikia tena malalamiko kama haya, askari wanaohusika wakamatwe na kupelekwa mahakamani mara moja. Huu upuuzi siutaki?” alisema Mabiti.


Hata hivyo, amewataka wakazi wa Simiyu kuheshimu hifadhi hizo kwa kuhakikisha hawaingii kinyume cha sheria.


By Jamhuri