Wiki ya Maji ni fursa maalumu ya sekta ya maji nchini kujitathmini kwa kujilinganisha na nchi nyingine duniani katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya maji.

Maji ni kichocheo muhimu cha maendeleo katika sekta mbalimbali za uchumi hapa nchini, ikiwemo kilimo, biashara, utalii na viwanda. Katika kutambua umuhimu na thamani ya maji katika maisha ya binadamu na uchumi wa dunia kwa ujumla, mwaka 1993 Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira na Maendeleo lilipitisha azimio rasmi la kuadhimisha Siku ya Maji Duniani kila mwaka ifikapo tarehe 22 Machi.

Wizara ya Maji imekuwa ikiratibu na kuadhimisha siku hii muhimu kuanzia mwaka 1988. Haya yamefanyika kwa kuwashirikisha wananchi na wadau wa maji.

Maadhimisho haya yanakwenda sambamba na Azimio Na. 47/193 la Umoja wa Mataifa (UN) linalozitaka nchi wanachama kuadhimisha Siku ya Maji Duniani kila mwaka tarehe 22 Machi, siku hii kwa Tanzania inakuwa ni kilele cha Wiki ya Maji. Siku hii itashuhudiwa kwa mara ya kwanza jijini Dodoma.

Lengo kuu la maadhimisho haya hapa nchini ni kuungana na mataifa mengine duniani katika kutathmini utekelezaji, mafanikio, changamoto na kuainisha mikakati ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira na kusimamia utunzaji wa rasilimali za maji nchini.

Maadhimisho yatakwenda sambamba na kaulimbiu ya Wiki ya Maji Duniani, 2019 inayosema:

“Hakuna Atakayeachwa: Kuongeza Kasi ya Upatikanaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa wote katika dunia inayobadilika kitabia nchi.”

 

Madhumuni mahususi ya maadhimisho

Miongoni mwa madhumuni ya siku hii ni kama ifuatavyo; kuelimisha jamii kuhusu Sera ya Maji na majukumu yao katika kuitekeleza, kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa Programu ya Maji, hali ya huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Wiki ya Maji Tanzania

Katika kuadhimisha Wiki ya Maji, Wizara ya Maji inashirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya maji katika kutathmini utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira pamoja na uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.

Wiki hii inakwenda sambamba na shughuli mbalimbali zinazohusiana na utoaji wa huduma ya maji na utunzaji wa vyanzo vya maji nchini. Maadhimisho hayo yanafanyika katika viwanja vya St. Gasper Dodoma.

Tofauti na miaka mingine, maadhimisho haya kwa mwaka huu 2019, yatakuwa na sura tofauti. Tofauti inatokana na kukamilika kwa mapitio ya Programu ya Maendeleo ya Sekta  Awamu ya Pili (WSDP II).

Kwa kuzingatia makubaliano ya kikao cha pamoja kati ya wadau wa maendeleo na serikali kilichofanyika tarehe 22-23 Oktoba, mwaka jana jijini Dodoma, na miongoni mwa maazimio yaliyokubaliwa na kuwekwa katika mpango wa utekekelezaji, ni kuadhimisha Wiki ya Maji kwa mwelekeo tofauti na miaka mingine ambapo mikutano mbalimbali ya wataalamu itafanyika.

Hivyo, mikutano ifuatayo itafanyika; Kongamano la Kisayansi kuhusu sekta ya maji (Water Scientific Conference); Mkutano wa Mapitio ya Sekta ya Maji (Joint Water Sector Review); uliokuwa unafanyika mwezi Novemba kila mwaka na Siku Maalumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA Day); ambapo EWURA itatumia fursa ya maadhimisho ya Wiki ya Maji kuwashirikisha wadau kuhusu shughuli za udhibiti katika sekta ya maji.

Maadhimisho yatafanyika kwa siku tano, yatajumuisha washiriki takriban 300, kutoka makundi anuwai wakiwemo kutoka maeneo yafuatayo; wizara za kisekta, wawakilishi wa mikoa na halmashauri nchini, taasisi na mamlaka zote chini ya Wizara ya Maji, wadau wa maendeleo katika sekta ya maji, taasisi zisizokuwa za serikali, makampuni ya ujenzi katika sekta ya maji, makandarasi katika sekta ya maji, taasisi za dini na  Sekta Binafsi (TPSF).

Please follow and like us:
Pin Share