Uamuzi wa wawekezaji wilayani Hai, Kilimanjaro kumshtaki mkuu wa wilaya (DC) hiyo kwa Rais John Magufuli umepongezwa na baadhi ya wafanyabiashara na kuonekana kuwa ni mwanzo wa kumaliza vitendo vya kunyanyaswa.

DC wa Hai, Lengai ole Sabaya, anatuhumiwa na wawekezaji hao kuwa anawanyanyasa kwa kuwakamata, kuwaweka ndani na kuwaomba rushwa.

Kilio chao kilichowekwa kwenye maandishi, kimewasilishwa kwa Rais Magufuli, ambaye mara moja amewatuma Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango; na Waziri wa Uwekezaji, Angela Kairuki, kwenda Hai kupata ukweli wa madai hayo.

Wanadai kuwa licha ya kuwekwa ndani kwa saa 48 kwa amri ya Sabaya, wanabanwa kwenye mazingira ya kuombwa rushwa na mkuu huyo wa wilaya.

Waziri Mpango amezungumza na waandishi wa habari mjini Hai na kusema wawekezaji wanaolalamika ni pamoja na wa shamba la kahawa la Kibo/Kikafu, Trevor Robert, ambaye ni raia wa Zimbabwe. Mwekezaji huyo anasema aliwekwa rumande kwa saa 48 na akapokwa hati ya kusafiria kwa amri ya DC Sabaya.

Madai ya DC Sabaya ni kuwa mwekezaji raia wa Zimbabwe anadaiwa kodi ya Sh milioni 713 alizotakiwa awe amezilipa ndani ya siku saba.

Malalamiko mengine ni ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Tudeley Tanzania, Jensen Natai na Wakili wa kampuni hiyo, Edward Mrosso, ambao wote waliwekwa rumande kwa saa 48.

Mpango anasema mwekezaji raia wa Zimbabwe ameeleza kwenye malalamiko yake kuwa mbali ya kupokwa hati yake ya kusafiria, amedaiwa kuwa anaishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria.

Wawekezaji hawa wamemwambia rais kuwa mbali na kuzuiwa kuendelea na uwekezaji katika shamba la Kibo/Kikafu, wamechafuliwa majina yao kwa kuitwa wezi, matapeli na kuwa wameghushi namba ya utambulisho wa mlipakodi [TIN].

Waziri Mpango ameyaweka malalamiko ya wawekezaji hao katika makundi sita ya kudaiwa kukwepa kodi, akaunti zao kufungwa kwa maelekezo ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuwekwa ndani kwa saa 48, na kudaiwa rushwa ama kuwekwa katika mazingira yanayoashiria kudaiwa rushwa.

Wawekezaji hao wanasema mazingira ya uwekezaji nchini ni magumu na wanashindwa kuwashawishi wawekezaji wenzao kuja kuwekeza.

Mpango anasema lipo tatizo la mawasiliano kwa idara za serikali ambalo linachangia migogoro kama hiyo kutopatiwa ufumbuzi wa haraka.

Akatoa rai kwa idara za serikali kuanzia ngazi za halmashauri, mkoa hadi wizarani kufanya kazi kwa ukaribu na kuwa na mawasiliano ya karibu kwa kutatua changamoto mbalimbali za wawekezaji.

Sabaya amezungumza na JAMHURI na kukana tuhuma zinazoelekezwa kwake na wawekezaji hao.

Anasema baadhi yao ni wababaishaji kutokana na kile alichodai kwamba hawakuwa na mikataba ya uwekezaji katika shamba la kahawa la Kibo/Kikafu.

“Hao wawekezaji ni wababaishaji, hawana mkataba wowote na vyama vinavyomiliki hayo mashamba, pia hawajawahi kulipa kodi kwa hivyo vijiji na wanataka mpaka wapewe mkataba, sasa hao unawafanyaje?” amehoji.

Anasema hao waliolalamika kwa Rais Magufuli wameondolewa hadhi ya wawekezaji kutokana na kutofuata tararibu.

Kuhusu kupokwa pasi ya kusafiria, Sabaya anasema walitilia shaka maelezo yake kwamba alikuja kuwekeza kwenye kampuni iitwayo Kilimanjaro Farm ambayo kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, haipo wilayani Hai.

Kwa upande wake, Waziri Kairuki anasema lengo la serikali ni kuona uwekezaji unaendelea kuwepo na kufanyika katika mazingira rafiki na endelevu kwa nia ya kuwavutia wawekezaji zaidi.

Anasema wamefika Kilimanjaro ili kufahamu kwa undani malalamiko ya wawekezaji hao na madai ya kufungwa kwa akaunti za Kampuni ya KUZA AFRICA.

Anasema changamoto waliyoiona katika uwekezaji wa shamba la Kibo/Kikafu ni hatua ya mwekezaji wa awali, Kampuni ya Tudeley kuingia mkataba na Kampuni ya KUZA AFRICA bila kuvishirikisha vyama vya msingi vya ushirika vinavyomiliki mashamba hayo.

“Tupo hapa kuona kama taratibu za uwekezaji zilifuatwa, pia kupata maoni ya vyama vya ushirika vinavyoendesha mashamba haya kama wanataka kuendelea na mwekezaji wa awali ama huyo mpya,” amesema.

Mawaziri hao wamepata maoni ya viongozi wa wilaya na mkoa juu ya hali ya uwekezaji katika mashamba hayo.

Kampuni ya KUZA AFRICA ambayo ni kampuni ya Kijerumani imewekezaji katika kilimo cha parachichi Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya na mkoani Kilimanjaro.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, anasema: “Tumefikia mwafaka mzuri na tumekubaliana yule mwekezaji wa awali aje ili atupe fursa ya kusikilizana na kutoa fursa uwekezaji uendelee kwa manufaa ya wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na taifa kwa ujumla.”

Please follow and like us:
Pin Share