Kwa muda wa mwezi sasa nchi yetu ipo katika migogoro isiyomithilika. Yamekuwapo matukio yanayotia shaka iwapo sisi wazazi tuna hakika na tunachostahili kuwapatia watoto wetu. Kule Mwanza na Geita yametokea mauaji yaliyotokana na mapigano kati ya Wakristo na Waislamu wakigombea kuchinja wanyama.

Hapa Dar es Salaam yametokea mauaji ya askari polisi baada ya watu waliokuwa kwenye gari lililozibwa na karatasi nyeusi (tinted) kumfyatulia risasi. Kwa sasa tinted zinawekwa hadi kioo cha mbele. India wamepiga marufuku tinted kwani imethibitika zina uhusiano na uhalifu.


Vyama vya siasa kwenye mikutano ya hadhara vinaanzisha ajenda za kufarakanisha wananchi. Namba za Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, zinatolewa hadharani na baadhi ya Watanzania bila kufikiri kuwa namba zao zimesajiliwa wanazitumia kuwaporomoshea matusi.


Wafuasi wa dini ya Kiislamu wanapimana ubavu na polisi. Wanaamua kuandamana eti wamtoe gerezani kiongozi wao, Sheikh Ponda Issa Ponda. Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, analitangazia taifa kuwa wabunge wamezidi kutojiheshimu hivyo uongozi utazuia matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni.


Sisi baada ya kupitia kwa kina mwenendo na mwelekeo wa siasa katika nchi yetu, kiwango cha uhalifu na chokochoko za kiimani zinazoendelea kwa kiwango cha kuhoji nani ana mamlaka ya kuchinja na nani hana, tukaamua kuwa ni vyema tuweke rekodi.


Tumeamua kuandika maoni haya kuwaasa ndugu zetu Watanzania, kuwa tunapotea njia. Tunakwenda jehanamu. Tunaandaa mazingira ya Watanzania kupigana, kuuana, kudhalilishana na kuharibu mwelekeo wa nchi yetu.


Lugha zilizoanza kuzungumzwa za gesi ibaki Mtwara au Mtwara wafaidike kwanza, kisha baadaye tukaambiwa Kigoma kuna mafuta watafaidikaje, hatudhani kama zitatuacha salama. Maisha ya binadamu yana thamani kuliko kitu chochote. Watanzania tuukatae mkondo wa vurugu.


Watanzania tukatae kuchezea amani tuliyonayo, maana mbele ya safari tutajuta kwa kutouchukua ushauri huu. Hapa tulipo leo tukitoka tukatumbukia kwenye vurugu, tutalazimika kutafuta wasuluhishi wa kuturejesha hapa tunapopakimbia. Je, huo ndiyo urithi tunaotaka kuwaachia watoto wetu? Jibu ni hapana. Mungu ibariki Tanzania.


By Jamhuri