Na Mussa Augustine,JamhuriMedia

Chama Cha ACT-Wazalendo kimemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,kulifuatilia sakata la malipo ya waathirika wa mabomu ya Mbagala na kuchukua hatua walioshughulikia suala hilo kwani kuna harufu ya udanganyifu,ubaguzi na uonevu.

Rai hiyo imetolewa leo Februari 1, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo Dorothy Semu ambapo amesema watu takribani 1361 wanadai fidia zao tangu 2009 baada ya mabomu kwenye ghala la silaha katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wanachi Tanzania( JWTZ) namba 671 KJ iliyopo Mbagala jijini Dar es Salaam.

Amesema kwamba mripuko huo umesababisha vifo, majeruhi, kuharibiwa kwa makazi na mali za watu pamoja na athari za kiafya ikiwemo magonjwa ya kifua kikuu,upofu wa macho na saratani,ambapo amebainisha kuwa wastani wa kaya 12000 ziliathiriwa na milipuko hiyo katika eneo la Mbagala pekee.

“Januari 28,2023 nilitembelea Mbagala kufuatilia suala hili baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa waathirika hao, nilifanikiwa kufuatilia na kuchambua taarifa mbalimbali ikiwemo orodha ya waathirika,malipo,risiti za malipo,kiasi cha bajeti kilichotumika na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na baadae kutembelea baadhi ya Waathirika hao”amesema.

Nakuongeza kwamba “ACT-Wazalendo tumeshangazwa sana kuona kwa zaidi ya miaka 14 tangu kutokea kwa milipuko hiyo kuna waathirika wapatao 1361 kutolipwa fidia yao.

Amesema kuwa malalamiko ya waathirika hao yapo katika maeneo mbalimbali ikiwemo la malipo kiduchu,utaratibu mbovu wa tathmini ya athari za mabomu,utaratibu wa malipo kutoeleweka.

“Wapo waliolipwa miezi kadhaa baada ya bajeti kwa usiri ambapi malalamiko mengi ya wananchi yanathibitishwa na ripoti ya CAG 2012/13 ilionyesha malipo ya fidia kwa waathirika wa mabomu ya Mbagala kulipwa kiasi Cha shilingi Bilioni 8 hayakuwa na nyaraka muhimu za kuthibitisha kama kweli malipo hayo yalifanyika kwa walengwa,kinyume chake adhabu hiyo wanapewa wananchi Kwa kunyimwa stahiki zao,vtisho na kebehi,” amesema.

Amesema kuwa jambo linaloumiza zaidi ni kuona viongozi wa Serikali kuanzia Halmashauri ya Temeke,ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Ndani kutumia vitisho kushughulikia suala hilo kwa kutaka kuzima vilio vya wananchi.

“Chama kimesikitishwa na kitendo kinachofanywa na Serikali cha kushindwa kuwangalia waathirika hao licha ya Bunge kuidhinisha bajeti ya shilingi Bilioni 17 na kwamba zimekwishatolewa kwa awamu takribani sita,” amesema.

By Jamhuri