Yono Kevela ambaye ni mbunge mstaafu wa Jimbo la Wanging’ombe mkoani Njombe amewashauri Watanzania kuacha kuchangia michango mikubwa kwa watu wanaotaka kuoa ama kuolewa badala yake waongeze nguvu ya michango kwa watoto ili waweze kupata elimu.

Amesema hayo wakati akizungumza na wananchi katika mahafali ya 22 ya kidato cha nne ya shule ya sekondari Ilembula mkoani Njombe ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Amesema kuwa wapo baadhi ya vijiji kwenye wilaya hiyo kikiwemo kijiji cha Katenge wamekuwa na utaratibu wa kuchangia elimu jambo ambalo limewasaidia wanafunzi kuendelea na masomo.

“Kuna utaratibu wa kuchangia katika kijiji cha Katenge na hii imesaidia wanafunzi wengi wao wakiwa madaktari kuendelea na masoko hivyo hakuna sababu ya kuchangia michango mikubwa kwa watu wanaotaka kuoa ama kuolewa.

“Tuhangaike sasa hivi kwenye swala la elimu,kama mtoto amekosa ada ya kwenda kidato cha tano tuchangishane ili tuwezeshe huyo akasome,kwani hivi sasa vijiji vinavyofanya hivyo vina wasomi wengi kutokana na michango yao na wanaleta faida kwa vijiji vyao”amesema Kevela.

Hata hivyo amewashauri viongozi wa kisiasa waliopo madarakani kuwatumia wastaafu kwenye shughuli za maendeleo na kuacha imani potofu ya kunyang’anywa nafasi zao.

By Jamhuri