Na Joe Beda Rupia

Birth-day au birthday. Siku ya kuzaliwa. Huwa si siku maarufu sana kwa kweli katika maana halisi ya ‘siku ya kuzaliwa’! 

Huwa haifahamiki. Kwa nini? Kwa sababu mtoto anayezaliwa hajulikani. Hasa kama mtoto mwenyewe anatoka katika familia ya kawaida.

Siku ya kuzaliwa hubaki ikifahamika na kujulikana kwa wazazi na labda ndugu wachache wa karibu. 

Walau siku ya kufa ndiyo hufahamika na kujulikana na idadi kubwa zaidi ya watu mbali na wazazi na ndugu wa karibu.

Hii ndiyo maana kumbukumbu za kifo ndizo husimama kama kumbukumbu sahihi ya maisha ya mtu husika. Hapo ndipo kwetu tunakuwa na Karume Day na Nyerere Day.

Leo ni kumbukizi ya kifo cha Edward Moringe Sokoine. Waziri Mkuu maarufu zaidi nchini. Katika nafasi hiyo, Sokoine anachuana na watangulizi wake wawili; Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Rashid Mfaume Kawawa.

Nyerere anazungumzwa zaidi lakini Kawawa ni miongoni mwa wale wanaofahamika kama ‘unsung heroes’. Ni mwamba, Simba wa Vita, anayehitaji siku maalumu ya kumzungumzia.

Lakini kweli Sokoine ni maarufu. Mzalendo? Ndiyo. Ni mzalendo kwa tafsiri nyingi tu mbali na ile ya kuendesha vita ya uhujumu uchumi.

Siku moja Mabele Marando amewahi kuzungumzia ‘uzalendo’ wa Sokoine akisema katika ziara yake Kibaha akiwa waziri mkuu, akapelekwa sehemu kwa ajili ya chakula cha mchana.

Pale akawakuta watoto wa shule wakimsubiri huku wanaimba. Kabla ya kuingia kwenye chakula, akawauliza wenyeji wake; hawa watoto wapo hapa tangu saa ngapi?

 Akajibiwa kuwa ni tangu asubuhi. Akahoji; wamekula? Hakuna jibu. Mwenyewe akaelekeza watoto wale wapewe chakula kilichoandaliwa kwa ajili yake, msafara na wengineo.

Akamalizia kwa kusema: “Mimi ninarudi Dar es Salaam; wengine kila mtu akale kwake.”

Haya. Huyo ni Sokoine ambaye alizaliwa Agosti 1, 1938. Leo ni kumbukumbu ya siku ya kifo chake kilichotokea Morogoro kwa ajali ya gari.

Kesho ndiyo kesho. Miaka 100 ya Mwalimu Nyerere! Si kawaida sana. Lakini Nyerere ni Nyerere tu.

Waliokuwapo wakati anazaliwa au hata kuwa na habari tu kwamba kuna ‘kamtu’ kamezaliwa wamebaki wachache sana duniani. Kama wapo.

Kwa hiyo wengi tuamzungumzia Nyerere tunayemfahamu au tuliyemsikia. 

Ndiyo maana hata mimi, na kwa umri wangu, inabidi nimzungumzie Nyerere wa aina hiyo. Nyerere Baba wa Taifa. Nyerere Rais mstaafu. Nyerere Mwenyekiti wa SSC.

Ndiyo. Kama hauna habari kuwa Nyerere alikuwa Mwenyekiti wa SSC shauri yako.

Ni miaka 100 sasa tangu azaliwe (Aprili 13, 1922). Miaka 37 tangu aondoke madarakani (Novemba 1985). Miaka 32 tangu ang’atuke CCM (Agosti 1990). Miaka 23 tangu aage dunia (Oktoba 14, 1999). 

Ninaijua sababu ya kifo chake. Nimewahi kuiandika mara kadhaa. Haijawahi kupingwa. Ilikuwa hivi:

Baada ya kustaafu, Mwalimu alikuwa akisafiri kwa ndege kwenda Butiama kupitia Mwanza. Akifika Mwanza alikuwa akichukua gari kwa safari ya kijijini kwake.

Barabara ya Mwanza – Butiama inapita Mlango Mmoja, Buzuruga, Nyakato, Igoma, Kisasa, Magu na kwingineko.

Katikati ya Nyakato na Igoma kuna kiwanda cha Mwatex; moja ya viwanda vikubwa sana nchini enzi Mwalimu akiwa madarakani. 

Naam! Walau watu 3,000 walikuwa na ajira ya kudumu na maelfu ya vibarua kama ilivyokuwa Urafiki, Kiltex, Sunguratex na kwingineko.

Kila alipokuwa akifika hapo, alikuwa akimwambia dereva wake asimame; Mwalimu anatelemka kwenye gari, anakitazama kile kiwandaaaaa, anatikisa kichwa. Anapanda gari na kuendelea na safari.

Yaani haelewi! Kiwanda hiki kimekufakufaje? Siku moja akamwona mlinzi, akamuuliza; kuna waajiriwa wangapi hapa? Mlinzi akamjibu: “Tupo wawili. Mimi na mlinzi mwenzangu.” Nyerere akachooooka kabisa!

Kiwanda kilichokuwa na maelfu ya wafanyakazi sasa wamebaki wawili tu? Tena hao wawili hata mshahara hawapewi wanalazimika kuuza vipuri vya kiwanda kuhudumia familia zao!

Jambo hili lilimtesa sana Mwenyekiti wa South-South Commission – SSC, Mwalimu Nyerere na kwa hakika hiki ndicho kilichosababisha kifo chake.

0679 336 491

By Jamhuri