Kuna wakati niliwahi kufikiria kuwa naweza kuwa mkimbiaji mzuri wa mbio ndefu kama ambavyo akina Juma Ikangaa, Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na wengine, nifanye hivyo ili kutoa aibu kwa Taifa langu ambalo limeshindwa kupata wakimbiaji bora kwa kipindi kirefu hadi historia ya nchi yetu inapotea katika ulimwengu wa riadha.

Kimoyomoyo nikasema kichwa kinapenda lakini mwili unakataa, huwa naenda katika viwanja vya mpira na kushuhudia mapambano mengi ambayo mwisho wake huwa ni kusema nafuu jana tulifungwa chache, nafikiria niwe mchezaji kama yule wa Ulaya, lakini ukweli uko palepale sitaweza kukopi na kupesti.

Tumefika hapa kwa pongezi baada ya mkuu wa kaya kuingia kivyake Ikulu, aliingia kwa staili yake kiaina, vijana wa leo wanasema nitoke vipi, ndivyo alivyotoka na singo yake inakubalika Afrika Mashariki na kwingineko barani Afrika na hata katika nchi za Dunia ya Kwanza.

Ameingia kwa staili ambayo wengi wangependa wawe wao, lakini ndiyo hivyo, mzee wa kumaanisha, kamaanisha na yupo ndani ya ulingo anatumbuiza muziki ambao wachezaji ni wengi na kila mtu anafikiria jinsi ya kwenda spidi na mirindimo ya muziki na kumaliza naye muziki.

Siku kadhaa wamejitokeza wachezaji wengine, wachezaji ambao yeye amewachagua kwa maana ya kumsaidia, matarajio ya Watanzania wengi ni kuona jinsi ambavyo wao wataingia katika kasi ambayo tayari ni kubwa na inataka spidi ya supa soniki kuweza kukabiliana nayo.

Baadhi ya wasaidizi wamekuwa wakionyesha dhahiri kuwa kazi yao waliyopewa hawaiwezi spidi ya baba mwenye nyumba, wapo waliodiriki kupita mle mle, na wapo waliojaribu kusema kama yeye, wapo waliofanya kama yeye lakini hawawezi kuwa yeye kwa kuwa namna ya utokaji wa mwenyewe ni dhahiri kasi ni tofauti.

Wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge lake pale Dodoma, kuna mambo mengi sana aliyosema, wapo waliodhani hakuna atakayeweza kutekeleza yale aliyokuwa anayaahidi mbele ya wananchi kupitia Bunge lile, wapo waliosema ni kasi ya nguvu ya soda na wengine ambao kazi yao duniani kubishana wanasema wazi kabisa kuwa hawezi.

Ukweli umedhihiri kwa muda mfupi aliokaa pale katika nyumba kuu na kufanya mambo makuu ambayo kwa kawaida ya Watanzania hawakuwahi kufikiria kwamba yangewezekana, wale ambao walionekana miungu watu katika taasisi mbalimbali waliondolewa kupisha kasi mpya, na wengine waliamua kubadilika tabia ili kuweza kukabiliana na madhara ambayo yangewakuta.

Alizungumzia majipu na kwamba yeye tumpe kazi ya kuwa mkamuaji na sisi tumsaidie kumuombea kwa kuwa kazi hiyo ni ngumu na inahitaji kufanyika kwa Taifa letu, wakati akisema hayo maneno muda mwingi alikuwa anamuomba Mungu amsaidie katika kutekeleza hilo, kwa hakika jambo hili linaendelea na Watanzania tumuunge mkono na kumuombea.

Ameweza kuonesha kwamba kumbe kila kitu kinawezekana kama tukiamua, kwa muda mfupi tumeona mabadiliko makubwa ya utendaji serikalini, kwa muda mfupi tumeona makusanyo ya mapato, kwa muda mfupi tumeona vigogo wengi wakiacha ofisi zao kwa tuhuma.

Leo kuna viongozi wengi ambao wamekuwa wakiiga staili yake ya utendaji huku wakitumia maneno ambayo aliyakataa akiwa analihutubia Bunge lake. Alikataa maneno kama tuko katika mchakato, mipango inafanyika, linafanyiwa kazi na mengine mengi ambayo yapo kisiasa zaidi badala ya utendaji.

Tumeshuhudia wasaidizi wengi wakifanya mbwembwe zake lakini bado wanatumia maneno ambayo alikuwa hayataki, kwa mawazo yangu unapoiga ni vema ukafanya vizuri zaidi kuliko kuharibu na katika hili kuna baadhi ya wasaidizi wanaonekana kabisa kupishana mawazo na mtazamo na mkuu wa kaya, nina hofu na siku zijazo huenda wakakutana mahali ambapo hakuna atakayeweza kujua walikuwa na lengo gani.

Matarajio ya wengi katika jopo lake la wasaidizi ni kuona wao wakiingia ndani zaidi badala ya kufanya yale ambayo tayari ameanza nayo kwa nafasi yake kama mkuu wa kaya, tungeona mfano wa anachokitaka mkuu kwa kuonesha mfano badala ya kuimba nyimbo ambazo tayari mkuu keshaimba.

Matatizo ya Watanzania ni mengi sana ambayo mkuu wa nchi hawezi kuyashughulikia yote kwa wakati mmoja, wasaidizi tungewaona katika mambo mengine wakirekebisha badala ya kutafuna-tafuna yale maneno ya kisiasa ya mchakato na maboresho.

Mwisho wa kuiga haupo mbali sana kwa sababu staili aliyoingia nayo mwenyewe inajulikana, ni vema kila mtu akajitafakari atoke vipi na aweze kukabiliana na wimbo wake, hapo ndipo dhana ya ubunifu inapohitajika, lakini kama wote watapita mle mle basi ni dhahiri kuwa copy and paste imetimia. 

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri