Magufuli apigwa bil. 100

Juhudi za Rais John Pombe Magufuli kuongeza makusanya ya kodi zinahujumiwa, baada ya uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI kubaini kuwa katika wilaya moja tu ya mpakani, anapoteza zaidi ya Sh bilioni 100 kwa mwaka.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa mji wa Tunduma unaoongoza kwa mapato katika halmashauri za mji nje ya Jiji la Dar es Salaam, umekuwa kitovu cha kuvuta shati kasi ya Rais Magufuli katika kukusanya kodi.

“Mji huu unatisha. Hapa kwa biashara inayoendelea, nchi kwa ujumla inapoteza hadi Sh bilioni 300. Kuna magendo haijapata kutokea. Kuna sigara zinavushwa kutoka Zambia zinaingia Tanzania mchana kweupe katoni nyingi tu.

“Hapa baiskeli, mikokoteni, magari, waenda kwa miguu, biashara kubwa ni magendo. Kuna vipodozi, sigara, pombe kali za kila aina, Heineken, hata konyagi ya Tanzania, nguo na kila unachofahamu kuwa kinauzika, kinavushwa mchana kweupe.

“Polisi wanajitahidi, lakini unaweza kuwahurumia. Watu wa hapa wakifahamu kuwa mtu fulani anaingilia biashara yao, wanachofanya ni kumuua. Hivyo, hata polisi waliopo hapa maisha yao yako hatarini wakijipendekeza kupambana na magendo. Labda kije kikosi maalumu cha makomandoo tunaowaona katika maadhimisha ya siku ya uhuru,” anasema mtoa taarifa.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Luteni Chiku Galawa, anakiri na kuthibitisha kuwa kiwango cha mauaji Tunduma kiko juu na kuwa biashara ya magendo inayoendelea hapo Tunduma inatisha wakati bidhaa za magendo kupitia Tunduma zinasafirishwa kwa treni za Tazara, kwenda katika karibu mikoa yote nchini, ila anayo dawa ya tatizo hilo.

 

Kinachoendelea Tunduma

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kutokana na hali ngumu ya uchumi, wenyeji wa Tunduma na wageni kutoka shemu mbalimbali za Tanzania wamepiga kambi mjini hapo. Mchana, baadhi wanalala ila usiku ukiingia, pikipiki, baiskeli, teksi bubu na Hiace zinaanza kufanya kazi ya kusafirisha bidhaa za magendo kwenda mkoani Mbeya, na baadaye mikoa mingine.

Pale Tunduma mjini, kuna mtaa wanauita Black Area. Mtaa huu umekaa kiajabu. Kama hujaambiwa au kupata fursa ya kukaribia kigingi cha mpaka wa nchi kati ya Tanzania na Zambia, unaweza kujikuta umewekewa kiti kunywa chai, miguu miwili ya kiti ipo ardhi ya Tanzania na miguu mingine miwili ipo ardhi ya Zambia.

Mwandishi ameshuhudia mambo ya ajabu. Mpaka huu hauna eneo linalotakiwa na sheria za kimataifa la mita 50 kila upande, lisilopaswa kukaliwa na mtu (no man’s land). Kuna wenyeji katika mji huu, nyumba kubwa imejengwa Zambia, choo na jiko vimejengwa Tanzania.

Maajabu yapo kwenye biashara. Baadhi ya picha zilizopigwa kwa siri kama zinavyoshuhudiwa, unakuta mfanyabiashara anauza mbao, duka la kupokelea pesa liko Zambia, na mzigo wa mbao uko kwenye ghala Tanzania. Wengine vifaa kama mbao, anakuwa amezilaza chini ila kisheria zinakuwa zimevuka nusu zimelala Tanzania na nusu nyingine zimelala Zambia.

“Ningejua ni mwandishi wala nisingezungumza na wewe, maana hapa sichelewi kuuawa wakijua mimi nimekueleza maovu yanayoendelea hapa. Kuna watu wanaishi kwa kutafuna kodi za Serikali. Hapa kuna wafanyabiashara wana maghala makubwa yamejaa bidhaa upande wa Zambia, na wala hawaguswi.

“Kwa Zambia wanaonesha kuwa bidhaa hizo zinakwenda Tanzania, hivyo hazilipiwi kodi na wakifika usiku wanaziingiza Tanzania zinaingia sokoni bila kulipiwa kodi. Hakika hapa Serikali inapoteza fedha nyingi haijapata kutokea. Sisi wenyeji tunaufahamu huu mpaka kama mpaka wa Nyerere na Kaunda. Hapa hakuna cha nchi mbili. Ukitaka unakuwa upande huu, ukipenda unakwenda kule. Hakuna cha passport wala nini,” anasema mtoa habari mwingine.

 

Sigara zapoteza Sh bilioni 30

Wakati uchunguzi wa JAMHURI ukibaini kuwa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) wanalalamika mauzo yao kushuka na hivyo kupunguza uwezo wao wa kulipa kodi za Serikali, imebainika kuwa nchi inapoteza hadi Sh bilioni 30 kutokana na magendo ya sigara yanayohusisha uuzaji wa sigara feki, za export na zilizokwepa ushuru. Kwa nia ya kunogesha habari hii, mwandishi anasimulia kwa uhalisia alichokiona Tunduma:

Nimekaa Tunduma kwa zaidi ya siku nane. Nimekuwapo mjini mchana na nimeamka usiku nikapita kwenye mitaa. Nimeshuhudia makubwa. Niliamua kuvuka mpaka kutoka upande wa Tanzania kwenda Zambia. Nimefika Zambia nikafika kwenye maduka yanayouza bidhaa mbalimbali.

Katika maduka matatu tofauti, nimeuziwa sigara kwa bei iliyoniaminisha kwa nini ni vigumu kudhibiti magendo ya sigara Tunduma. Wakati paketi 10 zikiuzwa kwa bei elekezi ya Sh 23,500 upande wa Tanzania, nikiwa Zambia, ambapo maduka yapo kwenye kigingi kabisa cha mpaka, nilinunua paketi 10 za Sweet Menthol (SM) na paketi 10 za Portsman kwa Sh 14,000 kila bunda.

Tofauti ya Sh 9,500 ni kubwa kumshawishi yeyote mwenye fursa ya kufanya magendo ya biashara hii kuifanya. Hii maana yake ni kwamba kama mtu anauza paketi 100 za sigara kutoka Zambia anazozivusha kwa kutumia kimfuko kidogo cha rambo, kwa siku anapata hela iliyostahili kuwa kodi ya Serikali ipatayo 95,000.

Muuza duka la kwanza, ambaye nilizungumza naye akila ugali ametulia tuli, bila kufahamu kuwa nafanya uchunguzi wa bidhaa za magendo zinazoingia nchini ikiwamo sigara, ambaye picha yake ipo gazetini, aliniambia hivi: “Kaka kama uko serious na una mtaji, sisi hapa tunakuuzia hata ukitaka katoni 100 za SM au Portsman.”

Kwa kujiamini kabisa akaniambia: “Sasa inategemea wateja wako wapo mkoa upi. Kama unataka kuingia kwenye biashara hii nishirikishe maana zipo sigara feki nyingi pia hapa Tunduma. Kama ni Dar es Salaam inabidi nikuchagulie ambazo sio feki, na hapo utapata faida hadi utapenda. Vinginevyo watazikataa utakula hasara.”

Baada ya kuambiwa hivyo, nikamwomba aniandikie risiti kwa kigezo kwamba nikirudi na hiyo risiti anitambue kuwa ndiye mteja aliyenunua paketi 20 “nzuri” za majaribio kwa wateja wake. Hakusita, akaniandikia risiti iliyochapishwa gazetini.

Nilipomuuliza anazipata wapi, hakusita: “Zipo kwenye maduka tunanunua kihalali na tunalipa kodi za biashara hii hapa Zambia hivyo wala Serikali haitusumbui.” Nilipomuuliza iwapo anafahamu kuwa hayo ni magendo, akasema: “Si jukumu la Zambia kuisaidia Tanzania kudhibiti magendo. Mzigo kama unatoka Zambia unaingia Tanzania, ni jukumu la Tanzania kuhakikisha kodi halisi zimelipwa. Hivyo, mimi sioni kosa kwa Zambia. Mbona Watanzania wanaingiza bidhaa nyingi huku usiku na mchana? Sisi ni ndugu tu,” anasema.

Katika duka la pili, niliuziwa sigara bila wasiwasi wowote, ila muuza duka hili, aliyeniambia ni Mzambia japo anaishi upande wa Tanzania akifunga duka jioni anakwenda nyumbani kwake upande wa Tanzania, amesema: “Sisi hapa ni ndugu. Kaka haya ni maisha. Hizi sigara zipo nyingi kadri unavyotaka. Ila angalia, feki zimeongezeka siku hizi. Mfano kama hizi. Ukitaka nakuuzia kwa Sh 13,000 kwa paketi 10, ila tukubaliane, ununue ukijua kuwa ni feki baadaye usirudi kwangu kulalamika.”

Hata hivyo, muuzaji huyu upande wa Zambia nilipomwomba kunipatia risiti, mwanzo alitaka kunipatia, lakini baadaye akasita. Akasema kitabu kimeisha, baadaye akasema kwanza hata hizo feki zipo chache. Alionekana kushtuka. Baada ya hapo nikaanza kuona hali inabadilika, akawa anatuma sms na matunda ya kutoka sms niliyashuhudia.

Baada ya kutoka dukani kwake, nilikwenda duka la tatu lililokuwa chumba cha saba kutoka duka alilomo. Nilimkuta mama ananyonyesha mtoto akiwa na vijana watu. Nikamwomba uniuzie sigara. Kwenye ‘shelfu’ za duka nilikuwa naziona sigara zile zile – Portsman na SM feki na halisi. Huwezi kuamini, mama huyu aliniambia: “Mimi hizi sigara siuzi.” Nikamwabia angalau aniuzie paketi 10 tu, akasema: “Sifahamu hata bei yake. Amezileta mume wangu, ameziacha hapa na akaniambia nisiziuze.”

Nilimbembeleza mno, akakataa katakata. Ghafla nilianza kuona watu kama wanakusanyika. Kila nilipoingia kwenye duka, ukimya ulitawala. Mazungumzo waliyokuwa nayo yakakoma. Nilikumbuka maneno ya mwenyeji wangu aliyeniambia: “Pale Tunduma wakifahamu kuwa kuna mtu anachunguza magendo wanawasiliana haraka sana. Ikibidi watamuumiza, watamwibia mali zake na hata kumuua asiwaharibie biashara zao.”

Bahati nzuri nilikuwa na mkoba wa laptop tu. Hoteli nilipokuwa nimefikia, nilikwishalipa pango la siku hiyo ila mizigo nilikuwa nimeiacha katika hoteli niliyofikia Mbeya. Akili ikachanganya haraka haraka. Nikarudi pale hotelini, nikaingia chumbani. Baada ya nusu saa nikatoka. Nikamuaga mhudumu kwamba narejea si muda. Nikakodisha gari kilomita 30 nikaenda kulala Vwawa.

Kesho yake baada ya kuzungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange, nilirejea Tunduma. Nilifika tena kwenye hoteli nilipofikia mhudumu akaniambia: “Kumbe kaka wewe ni mwandishi?” Nikamwambia ndiyo. Akasema: “Sasa jana umelala wapi?” Nikamwambia kwani sikulipa unanidai?

Akasema: “Hapana wamekuja marafiki zako wanakuulizia hapa zaidi ya mara nne usiku wanakisema wanataka mwende disko. Nikawaambia haupo umetoka, hawakuamini mpaka nilipowaonesha ufunguo na hadi mmoja nikamfungulia chumba akaangalia kwa jinsi alivyosisitiza.”

Nilichofanya, nililipia gharama za chumba tena, nikarejea mtaa wa Black Area. Nikavuka nikaenda Zambia. Huwezi kuamini. Wiki ijayo nitakuletea mwendelezo wa jinsi nilivyonunua viatu, kapero, nikanyoa nywele, nikaingia kwenye baa na maduka ya jumla nilikokuta chupa ya kinywaji kikali aina ya Gordons ya mililita 750 tunayouziwa Sh 36,000 Tanzania, upande wa Zambia inauzwa Sh 13,000 ya Tanzania.

Hapa ndipo vinywaji, vipodozi na bidhaa nyingine zinapolipotezea Taifa zaidi ya Sh bilioni 70 kwa mwaka. Usikose toleo la wiki ijayo. Je, unadhani pamoja na kulipia hotel nililala jioni hiyo baada ya kutoka Black Area? Nitajibu wiki ijayo.

Uchunguzi niliofanya, vijana wanafunga sigara kwenye maboksi ya maji na viroba. Baada ya hapo wanajitwisha kichwani na kuvusha kuja upande wa Tanzania, kisha vinapakiwa kwenye buti za magari, baiskeli, pikipiki na wakati mwingie Hiace.

 

Kodi inayopotea

Kuna wasiwasi na taarifa zisizothibitika kuwa huenda kuna kiwanda cha kutengeneza sigara feki zinazovuka mpaka kutoka Zambia kuja Tanzania. Hata hivyo, cha kushangaza sigara zenye nembo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania zipo upande wa Zambia kinyume cha sheria na niliweza kuzinunua kwa bei ndogo ya paketi 10 kwa Sh 14,000.

Afisa wa Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA) eneo la Tunduma, ameiambia JAMHURI: “Tunapata tabu kweli. Katika siku za karibuni kumekuwapo na  ongezeko kubwa la sigara zinazoingia sokoni bila kulipiwa ushuru upande wa Zambia. Tumewasiliana na TRA Tanzania kuwajulisha maana kasi hii inatisha.”

Uchunguzi umeonesha dalili kuwa sigara za export zinazouzwa na TCC kutoka Tanzania kwenda Zambia kwa mujibu wa sheria hazilipi kodi. Ingawa JAMHURI haikupata bei halisi ni kiasi gani sigara zinazouzwa nje ya nchi zinauzwa kwa paketi 10, bei elekezo kwa sigara zinazouzwa ndani ni Sh 23,500.

JAMHURI ilimewasiliana na maofisa wa TCC kupata bei hiyo bila mafanikio, ila habari za uhakika zinaonesha kuwa kitengo cha sigara za export chini ya TCC makao yake makuu yamehamishiwa Johannesburg, nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo, kwa kuwa kisheria bidhaa zinazouzwa nje ya nchi hazilipishwi kodi, ukiondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni asilimia 18 Sh 4,230 ya bei ya soko la ndani Sh 23,500 kwa paketi 10, kisha ukaondoa ushuru wa forodha, ambao ni Sh 28,024 kwa sigara 1,000 sawa na Sh 560.48 kwa paketi moja au Sh 5,604.8 kwa paketi 10, jumla ya kodi inakuwa Sh 9,834.8 (VAT + duty) kwa paketi 10.

Kwa mantiki hiyo bei ya export inakuwa chini ya Sh 13,665.2 kwa paketi 10 baada ya kampuni ya TCC kuongeza faida yake kidogo juu ya gharama za uzalishaji, hivyo inakuwa rahisi kwa wanaozipata kuziuza hadi Sh 14,000 bila kupata hasara.

Uchunguzi unaonesha kuwa baada ya TCC kuuza sigara hizo kwa Wazambia zikiwa zimewekewa stempu ya ushuru ya ZRA, ama Wazambia hawazipeleki Lusaka umbali wa kilomita zaidi ya 1,000 kutoka mpaka wa Tunduma, au wanatoa taarifa za uongo na kuzipanga kwenye maduka yaliyopo mpakani kwa faida kubwa zaidi bila kulipa kodi stahiki kwa Mamlaka ya Kodi Zambia.

“Hilo ndilo linalofanyika. Mzigo unapovuka kwenda Zambia, wanajua wanavyofanya wao, haulipiwi kodi, kisha sigara zinarejea Tanzania. Kinachoshangaza, ni hizi sigara halisi ambazo hazina nembo ya export zinatoka wapi upande wa Zambia, na kama zimelipiwa kodi halisi, mtu hawezi kuuza paketi 10 kwa Sh 14,000 mtaji wake ukakatika kwa karibu Sh 10,000 kwa kila paketi 10. Hapa kuna kazi ya kufanya na kuna majibu yanatakiwa,” kinasema chanzo chetu.

Zambia mwaka jana walilazimika kuongeza kodi ya sigara kutoka Kwacha 90 sawa na Sh 19,902.80 hadi Kwacha 200 sawa na Sh Sh 44,228.44 kwa sigara 1,000 kulinda viwanda vyao vya ndani, lakini ongezeko hili halijasaidia kudhibiti magendo ya sigara hadi wanashangaa. Kwa sasa kodi ya sigara ni kubwa Zambia kuliko Tanzania, lakini bado bei ya sigara kutoka Zambia zinazovuka mpaka ni karibu nusu ya bei inayouzwa na TCC kwa hapa ndani.

Tatizo lililopo Tunduma, lipo katika mji wa Ulumi, kuelekea Sumbawanga ambao matajiri wake wengi ni Wasomali. Sigara za export ndizo zilizotawala soko la mji huu hadi Sumbawanga. “Tatizo ni kubwa kuliko maelezo kaka. Mauzo ya sigara yameshuka hadi kwa asilimia 40, lakini hii inatokana na sigara feki. Kila kona ukienda wanauza sigara feki,” anasema mtoa habari wetu.

Katika mji wa Mpemba wilayani Momba, sigara za export ndizo zinazotamba. Sigara hizi zipo maeneo mengi nchini, ambapo huwa zinasafirishwa kwa treni za Tazara, lakini wafanyabiashara walio wengi wakifika eneo la Mlimba, zinashushwa na kupakiwa kwenye magari kisha zinasambazwa nchi nzima.

Uchunguzi unaonesha kuwa Kampuni ya TCC inauza sigara bilioni 5.4 kwa mwaka na kati ya hizo asilimia 10 zinaingizwa sokoni nchini kimagendo bila kulipiwa kodi sawa na sigara milioni 540. Kiasi hiki kwa viwango vya kodi vilivyopo hapa nchini ina maana Serikali inapoteza wastani wa Sh bilioni 30 kama kodi kwa mwaka ambayo inagetokana na ushuru wa bidhaa na VAT.

JAMHURI imeziona nyaraka za mawasiliano kadhaa kati ya TCC na Serikali wakilalamika kuwa wanapoteza mapato makubwa na Serikali inapoteza kodi kwa kiwango cha kutisha, huku wakitoa mafunzo juu ya sigara feki na zile zilizolipiwa kodi. “Tunashukuru Serikali imetupa ushirikiano mkubwa, ila inabidi tuongeze nguvu ya ushirikiano wa pamoja kupambana na suala hili ambalo ni tatizo kubwa,” anasema Afisa Mwandamizi wa TCC.

 

Jinsi ya kutambua feki

Wapo watu waliohoji inawezekanaje kutambua sigara feki? Uchunguzi wa JAMHURI umebainisha kuwa ni rahisi kubainisha sigara feki na zilizolipa kodi. Kitu cha kwanza ni kuangalia jinsi zilivyofungwa paketi kumi kumi. Ambazo ni feki plastiki iliyozifunga ni nyepesi na zinanesanesa.

Kitu kingine ni stempu ya ushuru ya TRA. Mtu anapokuta sigara zenye stempu ya ushuru ya TRA upande wa Zambia, hiyo inatosha kubaini kuwa si bidhaa halali kwani zenye stempu ya TRA zinapaswa kuuzwa Tanzania tu, na zile zenye stempu ya ZRA zinapaswa kuuzwa Zambia pekee na si Tanzania.

Kwa maana nyingine, sigara zinazouzwa maeneo mbalimbali nchini zikiwa na stempu ya ushuru ya Zambia hizo hazijalipa ushuru Tanzania. Jingine, makasha (packets) zina utofauti kwa zile za export kuwa na ming’aro huku za kuuza Tanzania rangi yake ikiwa imetulia.

Suala jingine, sigara halisi baada ya kubadilishwa sheria zina maneno makubwa meusi juu ya rangi nyeupe yanayosomeka “uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako”. Feki hazina maneno haya.

Afisa wa TCC amekanusha dhana kwamba huenda kuna watu ndani ya TCC wanaocheza mchezo mchafu kwa kushiriki biashara hiyo ya magendo ya sigara: “Hapana. Tuna ulinzi mkali dhidi ya matendo kama hayo na sigara zote zinazotoka kiwandani kwa ajili ya kuuzwa nje zipo chini ya ulinzi mkali.”

 

Kamanda wa Polisi Songwe

JAMHURI  imemhoji Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe juu ya uhalifu huu wa magendo eneo la Tunduma, na alikuwa na haya ya kusema: 

“Kama kuna jambo linanikosesha usingizi, basi ni Tunduma. Hayo ya magendo uliyosema, huenda hujaona kitu. Polisi wetu hawalali usiku kucha tunakamata bidhaa nyingi mno, ila kwa taarifa yako katika mpaka wa Zambia na Tanzania eneo la Tunduma tumekwishahesabu kuna njia za panya zaidi ya 320.

“Hili ni suala mtambuka, linalohitaji operesheni za pamoja za idara zote kukabiliana nalo. Hili suala la bidhaa kuvuka si sigara tu. Kuna vipodozi, sukari, vinywaji vikali na baridi, hii ni changamoto inayonikabili. Tatizo ni kubwa zaidi. Mpaka huu unaendelea na utata hadi kufikia mpaka wa Malawi na Tanzania. Ni shida.

“Mazingira ya Tunduma yana shida. Ule mpaka haufuati viwango vya kimataifa vya mipaka. Tunadhibiti magendo kwa tabu mno. Suluhisho ni kunyoosha ule mpaka uwe wazi. Ulijengwa kijamaa zaidi. Umeziona baiskeli zinavyovusha bidhaa? Hakuna “no man’s land”. Wanavusha madawa ya binadamu, wanyama… kuna watu wana maghala upande wa Zambia wanaishi Tanzania.

“Uhalifu Tunduma uko juu mno. Vijana wasio na kazi wanaongezeka. Hii ni shida, ila tunapambana nao kwa nguvu zote. Hata mauaji tunaendelea kuyadhibiti. Ni changamoto kwa kweli.”

 

RC atangaza suluhisho

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Luteni Chiku Galawa, amezungumza na JAMHURI na kusema tatizo la magendo Tunduma ni kubwa ila tayari Serikali imelipatia ufumbuzi. “Watu wa Songwe ni wataratibu na hili tatizo tutashirikiana kulimaliza. Binafsi sikufahamu kama kuna sigara za magendo. Nakwenda kulifanyia kazi. Tutashirikiana na Sigara wenyewe, TRA, Polisi, Usalama wa Taifa wote wanaohusika kukamata wanaofanya magendo hii.

“Tayari tumeanza. Pale Songwe mpaka una tatizo. Hakuna ‘no man’s land’. Sheria inataka mita 50 kila upande. Zambia wanasema wao wako tayari kuvunja nyumba zote zilizopo ndani ya mita 50 za mpaka. Na nyumba nyingi hizi wala si za Wazambia. Ni za Watanzania. Watanzania ndiyo wenye maduka huko Zambia.

“Mtu anakuwa na sigara upande wa Tanzania ukimgusa, anaruka anakanyaga upande wa Zambia. Huwezi kumfanya lolote. sheria za kimataifa zinakutaka ufuate taratibu za kuomba kumkamata kupitia Wizara ya Mambo ya Nje inayopeleka taarifa Mambo ya Ndani na polisi wapate kibali maalumu inaweza kuchukua hata mwaka.

“Sasa tunashirikiana na polisi wa Zambia, ila ukiwauliza wao wanasema sisi wafanyabiashara wetu wanalipa kodi hatuna tatizo. Ila sasa tunachotaka kufanya ni kuvunja nyumba zote zilizopo ndani ya mpaka. Tumeishirikisha Wizara ya Ardhi, tutavunja nyumba zote zilizopo ndani ya mita 50 upande wa Tanzania na Zambia, mpaka uwe wazo hapo ndipo tutamaliza tatizo.

“Ule mji haujapangwa, umejiotea tu. Na tangu Tunduma imeanza mpaka mwaka jana ndiyo wamepata halmashauri, ilikuwa Mamlaka ya Mji. Kabla ya hapo kalikuwa ka kata, maanake kijiji kinatawaliwa na sheria za ardhi za kijiji. Kuna sheria za ardhi mijini na sheria za ardhi vijijini.

“Sasa baada ya Tunduma kuwa halmashauri mwaka jana, ndiyo tumeanza taratibu na master plan tunaitengeneza ya Tunduma. Tumetoa zuio la kujenga, lakini unajua hali ilivyo kwa Tunduma… barabara kuu ya kwenda Sumbawanga, wamevunja wenywe na kusogeza nyumba majengo yao na siyo hiyo tu, hata za mitaani wamevunja wenyewe.

“Wanavunja wenyewe bila kulipwa na mtu. Wakiishakubaliana kwamba hapa tunapitisha barabara wanavunja wenyewe bila kulipwa. Ndiyo uzuri wa Tunduma. Watu wanakubaliana. Kwa hiyo nina imani hata hii. Hawa wanajua. Wanachotaka wanasema mkuu sisi tujengee soko tutahama wenyewe. Kwa hiyo ikiishapitishwa hii master plan tutavunja.

“Tunachotaka, halmashauri ikope fedha kwa maana ya kujenga soko kubwa, lakini siyo ndani ya no man’s land. Nje ya no man’s land. Wazambia waje kununua hapa. Na sisi tukiishavunja hawa wenzetu hawana tatizo. Kwa sababu kwanza waliojenga huko siyo Wazambia ni Watanzania. Na Mzambia anafaidi anapewa kodi.

“Kwa hiyo huo uchafu nimeukuta mimi. Kwa hiyo huwezi kuuondoa kwa kusimama siku moja unakwenda hatua kwa hatua na wewe unajua hali ilivyo kule Tunduma ilikuwa inahesabika ni sehemu ya vurugu. Na naaa… watu waliamini hivyo. Tunduma ukigusa tu, unaipata. Na mimi niliambiwa hivyo, lakini nikasema Tunduma nitaenda hawako hivyo.

“Nilivyokwenda nilikuta watu wako friendly, wamenipokea vizuri, tumekwishafanya nao usafiri na kwa kweli mimi naamini, lakini hii sasa mambo ya kuja kuweka hapa, nataka tuje tuweke alama, ili tujue mita zetu 50 zinaishia wapi. Mimi siyo mweka alama, mweka alama ni Wizara ya Ardhi,” anasema Luteni Galawa.

Idadi ya nyumba anazosema watazibomoa kusafisha mpaka hesabu ya haraka inaonesha kuwa ziko nyumba zaidi ya 3,000 katika eneo la mpaka. Je, unajua Luteni Galawa mpango huo atautekelezaje? Usikose JAMHURI wiki ijayo.

 

TRA wanena

Majaliwa Omar Ndungutu, ambaye ni Kaimu Afisa wa Mfawidhi wa TRA ofisi ya Tunduma, ameiambia JAMHURI kuwa hakuwa na taarifa za uwapo wa sigara feki, lakini wakati mwandishi akiwa ofisini kwake, Afisa wa Forodha kutoka Zambia, bila kujua kuwa aliyeko ofisini kwa Ndungutu ni mwandishi alifika na kuwasilisha malalamiko ya kuzidi kwa sigara feki za Portsman na SM.

“Tunashangaa sigara za magendo zimezidi kuwa nyingi. Nina jina la kampuni tunayoitilia shaka hapa kwetu Zambia kuwa ndiyo inayosambaza sigara hizi feki, naomba ninakutumia kwa WhatsApp vielelezo nanyi mlifanyie kazi. Sigara feki na zisizolipa kodi na ushuru zimekuwa nyingi kwa kiwango cha kutisha,” alisema Afisa huyo kutoka Zambia.

Kwa upande wake Ndungutu, ameiambia JAMHURI kuwa kama ni kuwapo kwa sigara feki na zisizolipa ushuru basi tatizo hilo litakuwa linatokea Zambia. “Hapa kwetu Tanzania TCC ambaye ni muuzaji pekee wa sigara akitaka kuuza sigara Zambia anaweka Custome Bond (dhamana ya ushuru). Sigara zikivuka, tunamrejeshea dhamana yake. Zikiishia ndani, TRA inachukua hiyo fedha.

“Kwa maana hiyo TCC wanafanya kila wanachoweza kuhakikisha sigara zinavuka kwenda Zambia waweze kurejeshewa bond yao. Sasa TCC wakileta malalamiko, sisi TRA tutafanya msako. Tunaomba watuandikie barua kuwa mauzo yao yameshuka, nasi tutafanya msako maana hiyo tunapoteza kodi na wao wanapoteza mauzo.

“Pili, itatupasa kufanya patro za pamoja kwa kushirikiana na vyombo vyote. TRA ina utaratibu wa kuwatuza watoa taarifa zinazothibitika kuwa za kweli. Tunaomba yeyote anayefahamu kama kuna kiwanda au mtu anayefanya hii magendo atujulishe. Tukimkamata tukapata hizo fedha, basi tutampa tuzo huyo mtu,” anasema Ndungutu.

Alipoulizwa juu ya taarifa kuwa TRA wanazo taarifa ya magendo ya sigara na bidhaa nyingine nyingi ila wanazifumbia macho kwa kuwa wao ni sehemu ya mchezo huo, akasema: “Sisi TRA na polisi tumekwishazoea haya mambo. Kila jambo baya huwa tunarushiwa sisi. Makosa hata yakifanywa na idara nyingine za Serikali, tuhuma zinaletwa kwetu. Wametugeuza kama dampo.

“Kila mara tunaangushiwa jumba bovu. Lakini kiuhalisia siyo kweli. Sisi hapa TRA hatutozi kodi. Tunaangalia documentation. Bidhaa za Transit hazilipi kodi kwetu hapa. Tunaangalia gari kama lilitoka Dar es Salaam limewekewa sili bado sili zipo au zimekatwa, basi hiyo ndiyo kazi yetu.”

Ndungutu anakiri kuwa kudhibiti magendo Tunduma ni kazi: “Kuna njia za panya zaidi ya 300. Mpaka ni mrefu sana. Kuna mwingiliano mkubwa mno. Unakuta nyumba imejengwa sebule iko Zambia, vyumba vya kulala vipo Tanzania. Hawa wenyeji wa hapa ni kabila moja la Wanyamwanga kwa pande zote mbili Zambia na Tanzania. Hujui nani yuko ujombani au ukweni… suluhisho ni kuwa na eneo la mpaka la mita 50 kila upande, ambalo kwa sasa halipo.”

Amesisitiza kuwa kazi ya TRA Tunduma ni kuchukua kumbukumbu kwa ajili ya kupata takwimu zinazosaidia mipango ya baadaye na si kutoza kodi. 

Richard Kayombo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipa Kodi wa TRA, ameiambia JAMHURI kuwa taasisi yake imekuwa ikipata malalamiko kutoka TCC wakieleza kuwapo kwa tatizo hilo na wanajipanga kufanya operesheni ya kukamata wanaofanya magendo ya sigara.

“Kwanza hili linaikosesha Serikali mapato, lakini pili inaleta ushindani usio wa haki katika soko la sigara jambo lisilokubalika. Ni lazima tupambane kuondoa tatizo hili. Tutafanya operesheni nanyi tutawajulisha,” amesema Kayombo.

Je, unajua bei za vinywaji, sukari, vipodozi ni kiasi gani upande wa Zambia hapo Tunduma ambavyo kwa ujumla wake vinaikosesha Serikali wastani wa Sh bilioni 70 kwa mwaka kama kodi kwa kuuzwa kwa njia ya magendo? Usikose nakala ya JAMHURI wiki ijayo.

2643 Total Views 3 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons