Malawi waigwaya kipigo JWTZ

* Taarifa za kiintelejensi za Jeshi letu zawaogopesha

* Ndege za utafiti zaondolewa upande wa Tanzania

* Makamanda wasisitiza kuendelea kuulinda mpaka

* Waingereza walipotosha mpaka

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linaendelea kuimarisha ulinzi katika mpaka wa Tanzania na Malawi, licha ya taifa hilo dogo lililopo kusini mwa Afrika kuonyesha nia ya kutotaka kuingia katika vita, lakini pia gazeti la JAMHURI limebaini chimbuko la historia ya upotoshaji katika mpaka wa nchi hizi.

Makamanda wa JWTZ waliopewa dhima ya kuimarisha ulinzi katika eneo la mikoa ya Ruvuma na Mbeya, wameiambia JAMHURI kwamba pamoja na Malawi kuonyesha nia ya kutii maelekezo ya kutoendelea na utafiti wa mafuta na gesi katika Ziwa Nyasa, kauli hiyo haitoshi kulifanya Jeshi hilo lilale.Akizungumza kwa simu kutoka Ruvuma, mmoja wa makamanda hao aliyezungumza na JAMHURI kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema, “Hapa tupo, tutaendelea kuwapo kuilinda mipaka ya nchi yetu. Ndiyo kazi tuliyokabidhiwa, sasa kama wao wamesema hawana nia ya kuleta chokochoko, hayo ni yao wao.”

 

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, amesema mzungumzaji wa suala la mgogoro huo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. “Suala hilo linashughulikiwa na Wizara ya Mambo ya Nje,” amesema Nahodha alipoulizwa na JAMHURI. Raia wa Malawi wanaoishi jirani na mpaka wa Tanzania wamejaa hofu baada ya kuwapo taarifa kupitia vyombo vya habari zinazowakariri viongozi wa Tanzania wakisema wapo tayari kutumia hata njia ya vita kulinda aneo la Ziwa Nyasa, linalodaiwa na Malawi kuwa ni mali yake.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliliambia Bunge wiki moja iliyopita, kuwa Malawi wanapaswa kuacha kuendelea na utafiti wa gesi na mafuta katika eneo la Tanzania hadi hapo suluhu ya jambo hilo itakapofikiwa. Kauli yake ilitiwa nguvu na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa, aliyesema Tanzania ipo tayari kulinda mipaka yake kwa njia yoyote, hata ikibidi vita.

 

Wananchi katika Wilaya ya Chitipa iliyo jirani na Tanzania, wamekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wao baada ya kusikia taarifa hizo kupiti vyombo vya habari. Hofu ya wananchi hao inatokana na kutambua kwao uzoefu wa Tanzania katika medani ya kivita.

“Tunasikia taarifa kupitia Redio Tanzania wakisema wapo tayari kuingia vitani dhidi yetu (Malawi) kama tukiendelea na utafiti wa mafuta katika ziwa. Hii ina maana gani? Je, tuko salama? Nini msimamo wa Serikali yetu?” Amehoji mwananchi mmoja wa Chitipa. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Malawi, Uladi Mussa, amewajibu wananchi kwa kuwataka wawe watulivu.

 

“Nawahakikishia wananchi kuwa watulivu. Tunazungumza na Serikali ya Tanzania na mambo yatakwenda vizuri tu. Kama kutakuwapo matumizi ya nguvu tutakwenda katika Mahakama ya Kimataifa,” amesema Mussa. Hata hivyo, Waziri huyo aliendelea kusisitiza kuwa Ziwa Nyasa (wao wanaliita Ziwa Malawi tangu mwaka 1967) lote ni mali ya Malawi. “Hapa hakuna jambo. Tunatambua kuwa ziwa lote ni mali yetu. Madai haya yangekuwa yanatolewa na Msumbiji pengine kungekuwa na hoja, lakini si Tanzania. Tuna ushahidi wote wa mikataba vinavyoonyesha kuwa Ziwa Malawi ni mali ya Malawi,” amesema.

 

Awali, Mussa alisema Tanzania haina ubavu za kuizuia Malawi kuendelea na utafiti katika Ziwa Nyasa, ingawa kilichotakiwa na Tanzania ni kampuni na serikali ya nchi hiyo kuacha kuendesha utafiti upande wa nusu ya pili ya ziwa ambao ni mali ya Tanzania. Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Ephraim Chiume, pia amesisitiza kuwa ziwa hilo ni mali ya Malawi. “Tanzania wanaamini mpaka unapaswa uwe katikati ya ziwa. Madai yao wamejiegemeza kwenye sheria za kawaida za kimataifa ambazo zinasema kama nchi zinagawanywa na maji, mpaka wa nchi hizo uwe katikati ya maji. Msimamo wa Malawi ni kwamba madai hayo ya Tanzania ni ya kweli pale ambako kunakuwa hakuna mikataba/mkataba unaoelekeza mpaka,” amesema.

 

Mwaka 2011 Malawi iliipa zabuni kampuni ya Surestream kufanya utafiti wa athari za mazingira kwa ajili ya uchimbaji mafuta katika Ziwa Nyasa. Malawi inaamini kuwa mpaka sahihi ni ule uliowekwa kutokana na mkataba wa Heligoland uliotiwa saini mwaka 1890 kati ya Ujerumani na Uingereza. Wakati huo Tanzania ilikuwa chini ya utawala wa Ujerumani, ilhali Malawi ikiwa chini ya Uingereza.

 

Historia ya upotoshaji

Mkataba huo ulioingiwa mwaka 1890 ujulikanao kama Anglo-Germany Treaty ulienda sambamba na Mkataba ujulikanao kama Heligoland-Zanzibar Treaty wa mwaka huo. Huu ndiyo mkataba unaoipa kiburi Malawi. Mkataba huu una vifungu kadhaa, Lakini Malawi wanashikilia kifungu cha kwanza kinachosema mpaka wa Tanganyika na Malawi unaanzia Mto Ruvuma hadi eneo la Msinje hadi Ziwa Nyasa, kisha kujielekeza kaskazini mashariki na magharibi ya mwambao wa ziwa karibu na ncha ya Mto Songwe, wakati  kifungu cha nane cha mkataba huo kinasema wazi kuwa Ziwa Nyasa litatumiwa na nchi zote mbili kwa usawa kwa maana ya kwamba mpaka ni katikati ya ziwa.

 

Uingereza kwa upande wake, iliipatia Ujerumani Kisiwa cha Heligoland kilichopo umbali wa kilomita 46 kutoka mwambao wa Ujerumani. Kisiwa hiki kilikuwa kinatawaliwa na Uingereza. Kina wakazi 1,127 hadi leo na kina ukubwa wa kilomita moja. Hata hivyo, kabla ya kutiliana saini mkataba huu, chini ya Mkataba wa Berlin kwenye mkutano wa kugawa makoloni ya Afrika wa mwaka 1884/85, Ziwa Nyasa liliachwa kama ukanda huru.

 

Halikuwa miliki ya Mwingereza wala Mjerumani. Malawi wakati huo ilikuwa ikijulikana kama South East Central Africa.  Pamoja na mkataba huo, chapisho la mipaka la Agosti 18, 1900 Na. 3134 waandishi wa chapisho hili – Luteni E. L. Rhoades na Luteni W. B. Phillips walirejea katika Mkataba wa Berlin kwa kutoonyesha mpaka kuwa si mashariki mwa Ziwa Nyasa tu bali hata katikati haukuwekwa, hivyo eneo hilo likabaki kuwa ukanda huru. Hata hivyo, chapisho hilo linaonyesha wazi bandari za Kijerumani katika Ziwa Nyasa ikiwamo Langenburg.

 

Pia zipo alama za Wajerumani kama Wissmann Bay na Kaiser Bay katika Ziwa Nyasa. Ingawa halionyeshi mpaka lakini ni ushahidi kuwa Wajerumani waliendelea kumiliki sehemu ya Ziwa Nyasa hata baada ya mkataba huu wa 1890. Kisheria kwa matendo (by conduct) kwa kuwa Uingereza haikuwazuia Wajerumani kuendelea kutumia ziwa hili na kumiliki bandari, ni wazi Mkataba wa 1890 ulikufa kifo cha asili. Haufanyi kazi.

 

Si hilo tu, kwa Uingereza kulitambua hilo kati ya mwaka 1916 hadi mwaka 1934 machapisho rasmi ya Kumbukumbu za Makoloni yaliyochapishwa na Uingereza, yanaonyesha kuwa mpaka ni katikati ya Ziwa Nyasa. Hata chapisho la Usalama wa Taifa la Ujerumani la Mwaka 1916, linaendelea kuonyesha kuwa mpaka wa Tanganyika na Malawi ni katikati ya Ziwa Nyasa. Yapo machapisho mengi ya aina hiyo, ila lenye umuhimu zaidi ni hili la Wamalawi wenyewe.

 

Kwa mujibu wa mwanazuoni wa Sheria za Kimataifa, Ian Brownlie, katika kitabu chake cha ‘African Boundaries: A Legal and Diplomatic Encyclopaedia’, Wamalawi wenyewe wanatambua kuwa mpaka ni katikati ya ziwa. “Vyanzo rasmi vya kiserikali ya Nyasaland kati ya kipindi cha Mwaka 1932-1938 mara zote vinaonyesha mpaka ni katikati ya ziwa. Chapisho la ‘The Handbook of Nyasaland’ lililochapishwa na Serikali ya Nyasaland kupitia Wakala wa Serikali ya Uingereza kwa Makoloni mwaka 1932 ukurasa wa 200, lina ramani inayoonyesha kuwa mpaka ni katikati ya ziwa.

 

“Wilaya ya Nyasa Kaskazini kwa ramani iliyochorwa na Wamalawi inaonyesha kuwa mpaka wake ni katikati ya Ziwa Nyasa,” anasema Brownlie katika kitabu hicho alichokichapisha kwa mara ya kwanza mwaka 1962 na kurejea uchapishaji mwaka 1979.

Profesa huyo wa Sheria za Kimataifa anasema katika kitabu hicho kuwa Taarifa za Makoloni baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kuanzia mwaka 1948, Uingereza kwa kuwa ilikwishabaini sasa Tanganyika ingejitawala muda wowote, ndipo ilipochora ramani upya. Taarifa hizo katika Umoja wa Mataifa kati ya 1948 na 1962 zinabadili ramani ya zamani na kuonyesha kuwa mpaka ni mashariki mwa Ziwa Nyasa kwa maana kuwa ziwa lote linamilikiwa na Malawi.

 

Nyerere aliikana ramani mpya Mara tu baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Rais wa Kwanza wa Malawi wakati huo, Hastings Kamuzu Banda, kabla haijapata uhuru, alifika Dar es Salaam na kumwambia Mwalimu Nyerere kuwa wagawane Ziwa Nyasa na kuifuta kabisa Msumbiji katika ramani ya dunia. Mwalimu alimkejeli Banda na kutokana na nia hiyo mbaya, mwaka 1964 Mwalimu Nyerere kupitia Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) aliandaa tamko la Cairo, lililotaka mipaka isichezewe baada ya Uhuru.

 

Mwaka mmoja baadaye, 1965, Tanzania ilianza kuchora ramani zinazoonyesha kuwa mpaka wa Tanzania na Malawi ni katikati ya Ziwa Nyasa. Mwaka 1967 Rais Banda aliyekuwa ameipatia nchi yake Uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1964, alitishia kupigana vita na Tanzania iwapo Tanzania isingekubali kuwa ziwa lote la Nyasa ni mali ya Malawi. Nyerere alimtimua Banda na kumwambia yuko (Mwalimu) tayari kwa vita. Hali ilikuwa tete kwa kiwango cha kutisha. Lakini hatimaye Malawi ilifyata mkia na kuendelea kuwa kimya hadi mwaka huu walipoamua kutia kidole kwenye maji ya moto kuona kama yanaunguza kweli.

 

1322 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons