Wakfu ni nini?

Image result for sheria

Sheria ya Mirathi na Usimamizi wa Mali, Sura ya 352 ndiyo sheria inayoeleza masuala yote ya msingi kuhusu habari nzima ya wakfu. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Kifungu cha 140, wakfu  ni  kutoa mali  kulingana na sheria za Kiislamu  kwa ajili ya dini, hisani au kwa ajili ya watu/mtu wa familia fulani.

Suala la wakfu huenda sambamba  na  suala la wadhamini.  Kwa mujibu wa kifungu hicho, wadhamini ni watu/mtu  ambaye ndiye hupewa jukumu la kusimamia mali ya wakfu.  

Kama  ni  nyumba  yenye  wapangaji,  basi mtu au watu hao ambao  ni  wadhamini  ndio watahusika  na  kukusanya kodi  pamoja  na mambo  mengine yote yanayohusu nyumba. Na kama kuna  maendelezo  yoyote ya ukarabati au vinginevyo, hawa ndio watahusika. 

 Maelekezo ya mtoa wakfu lazima yafuatwe

Siku zote mtoa wakfu hutoa mali kwa malengo maalumu. Yaweza kuwa ni malengo ya  kiimani au vinginevyo. Mtoa  wakfu anapotoa nyumba/kiwanja kama wakfu hutoa kwa maelekezo ya  namna na  jinsi kitakavyotumika. 

Na mali hiyo itapaswa kutumika kulingana na maelezo yaliyotolewa na mtoa wakfu. 

Ni kosa mali ya wakfu kutumika kinyume cha maagizo ya mtoa wakfu. Ikiwa itatumika kinyume, basi kuwe na sababu za  msingi ambazo zinalazimisha hivyo. Ziwe ni sababu  ambazo hakuna namna isipokuwa ni lazima kufanyika hivyo.  Kifungu cha 150(1) cha sheria ya  mirathi na usimamizi wa mali kinasema kuwa matumizi ya mali za wakfu ni lazima  yazingatie nia na malengo ya mtoa wakfu. 

Isipokuwa kifungu hicho kinasisitiza kuwa nia na malengo ya mtoa wakfu yatafuatwa tu pale ambapo  nia  na  malengo  hayo yatakuwa halali kisheria. 

Ikiwa mtoa wakfu ameelekeza matumizi ambayo hayakubaliki kisheria, basi maelekezo  hayo hayatafuatwa.  Lakini ikiwa  hayapingani na sheria yoyote, basi ni sharti kuyafuata.

 Ifahamu Tume ya Wakfu

Kuna chombo cha kisheria kinaitwa Tume/Bodi ya Wakfu Tanzania (Wakfu Commission of Tanzania). Kazi  kubwa  ya chombo hiki ni kusimamia na kuratibu mali zote za wakfu.  Wakfu ili uweze kulindwa na sheria hii hutakiwa kusajiliwa.  Chombo hiki ndicho kinachohusika na usajili. 

Kifungu cha 145(6) kinasema kuwa mali ya wakfu inatakiwa kusajiliwa ndani ya miezi mitatu  tangu iwe mali rasmi  ya  wakfu.  

Pia kamati  ya wadhamini ambayo ndiyo inasimamia mali za wakfu nayo hutakiwa kusajiliwa ndani ya  miezi  mitatu tangu  kuundwa kwake. Pia mgogoro wowote unaotokana na mali ya wakfu husuluhishwa na chombo hiki.

 Nini ufanye mali ya wakfu inapotumika vibaya?

Wakati mali ya wakfu inapotumika vibaya au kufujwa, yeyote  mwenye masilahi anaweza kuibua malalamiko. Kifungu cha  146 cha Sheria ya Mirathi na Usimamizi wa Mali kinasema kuwa malalamiko yatapelekwa  kwenye Tume/Bodi ya  Wakfu. 

Lakini pia kifungu hicho hicho kinatoa mamlaka kwa tume yenyewe  kuchukua hatua hata kama hakuna mtu  aliyelalamika. Tume itachukua hatua mara moja itakapoona mali ya wakfu inatumika  kinyume cha malengo ya mtoa  wakfu au kuna ufujaji  unaofanywa. 

Kifungu hicho kinasema kuwa Tume/Bodi itafanya  uchunguzi na ikigundua kuwa kuna mambo hayako sawa katika usimamizi wa wakfu, basi inaweza kuichukua ile mali ya wakfu na kuiweka chini ya usimamizi wake au kuteua wadhamini  wengine ili kusimamia vema mali hiyo. 

Yapo mengi kuhusu wakfu, lakini kwa leo ni hayo.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

By Jamhuri