url-1Sehemu ya tatu ya ripoti hii ya Jaji Joseph Warioba iliyochapishwa wiki iliyopita, kwa kiasi kikubwa ilizungumzia maadili ya viongozi na hatua ya viongozi kufanya biashara wakiwa madarakani kwa kuuza hadi vidani vya wake zao kwa wafanyabiashara. Wiki hii, tunakuletea sehemu ya nne yenye mambo na mapendekezo muhimu. Endelea…

 

1. KUSAFISHA UONGOZI ULIOPO NA KUJENGA MAADILI YA VIONGOZI WA BAADAYE

1. Mwananchi mmoja ametoa wazo kwamba kinachotakiwa hapa nchini ni kuunda “TUME YA UKWELI” (TRUTH COMMISSION). Tume hiyo itakuwa na kazi nne kubwa:-

(i) Kuainisha vigezo vya maadili ya uongozi na misingi ya uwajibikaji kwa kila mhusika endapo amekiuka kwa namna moja au nyingine vigezo hivyo.

(ii) Kupokea viapo (declarations) vya viongozi mbalimbali wa nchi hii,  yaani waliomo serikalini, mashirika na vyombo vingine vya Serikali, viongozi wa vyama vyote vya siasa, viongozi wa vyombo vya umma (civic organizations) na kadhalika. Viapo hivyo vitahusu mali walizonazo; jinsi walivyozipata, lini walizipata, na wapi mali hizi zilipo.

(iii) Kufanya uchunguzi juu ya uhakiki wa viapo hivyo, kama kweli wametamka kila walichonacho, na kuwataka wale ambao wamekiuka maadili ya uongozi kama yalivyoainishwa katika (a) hapo juu kuwajibika ipasavyo ikiwa wao wenyewe watakuwa hawakujihukumu binafsi

Aidha adhabu ya viongozi hao itakuwa ni kujivua uongozi na uwezekano wa kuwa viongozi tena isipokuwa kama watakuwa wamesamehewa na Rais katika Bunge kwa “Azimio Mahsusi.” Wahusika ambao watasema kweli, wataruhusiwa kubakia na mali zao.

(iv) Kuwachukulia hatua za kisheria wale ambao watakuwa wamedanganya ikiwa ni pamoja na kuwafilisi mali zao zote ambazo wamezipata kinyume na mapato yao halali, iwe zilitamkwa katika viapo vyao au la.

2. Tume inayaafiki maoni haya na kupendekeza kwamba yakubalike kimsingi. Kwa kuanzia Kamishna wa Maadili achukue hatua zifuatazo:-

(i) Ahakikishe kwamba kila kiongozi anayetakiwa kutamka mali zake kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya mwaka 1995 anafanya hivyo ndani ya muda usiozidi miezi mitatu.

(ii) Kufanya uhakiki wa fomu zote ambazo zimewasilishwa kwa Kamishna wa Maadili ili kujihakikishia kwamba kila mhusika ametaja mali zake zote. Mali hizo zitangazwe hadharani ili na wananchi pia wafahamu.

(iii) Endapo kuna kiongozi au viongozi ambao watadhihirika kwamba hawakusema kweli, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Aidha, viongozi wahusika watakiwe kujiuzulu mara moja.

(iv) Endapo kutakuwa na viongozi ambao hawatajaza fomu zao kwa wakati uliowekwa, wao pia wachukuliwe hatua za kisheria.

3. Kwa msingi huo itakuwepo haja ya kurejea Sheria ya Maadili; sheria inayounda Tume ya Kudumu ya Uchunguzi na Sheria ya Kuzuia Rushwa ambazo zote zinaguswa na pendekezo hili. Maana ya pendekezo hili ni kwamba Sheria ya Maadili ya Taifa iwatake wale wote wanaoongoza vyombo vikuu vya umma – iwe ni vya kiserikali au la, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa na vya wananchi (civic organizations) watangaze mali zao bayana.

 

II: KUIMARISHA UONGOZI NA NAMNA YA KUPATA UONGOZI MPYA

4. Chimbuko la sifa za uongozi linatokana na utaratibu wa kuwapata viongozi pamoja na misingi inayotawala utaratibu huo. Tunao viongozi wa aina mbili katika nyanja za kisiasa. Kwanza ni wale waliochaguliwa na wananchi na pili ni wale walioteuliwa kushika nyadhifa na kisiasa.

Viongozi walioko chini ya mfumo wa utumishi wa Serikali na ambao wameteuliwa na Rais, mfumo unahitaji wafanyiwe upekuzi. Udhaifu uliojitokeza katika udhibiti wa viongozi walioko chini ya utumishi wa Serikali hautokani na hitilafu katika taratibu zilizopo bali umesababishwa na utovu wa usimamizi na uwajibikaji.

Hali hii inaweza kurekebishwa kwa urahisi kwa kuzingatia matumizi ya kanuni za utumishi. Hata hivyo kuna dosari kubwa katika nyanja ya uongozi wa kisiasa. Uchaguzi wa madiwani, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge uliopita umeonyesha bayana kushamiri kwa rushwa kuanzia katika uteuzi wa wagombea hadi kwenye uchaguzi wenyewe.

Baadhi ya wagombea waliojihusisha na vitendo vya rushwa wamefanikiwa kupita na ni madiwani, wawakilishi na wabunge. Kwa vile viongozi wa namna hii wamepata ushindi kwa kutumia rushwa haitakuwa rahisi kuwategemea wawe ni mfano bora wa uongozi.

 

MAPENDEKEZO 

5. Si jambo la kubishaniwa kuwa uongozi wa nchi unalalamikiwa sana kuhusika na vitendo vya rushwa. Kuna haja ya kuchukua hatua madhubuti kusafisha safu za uongozi ili kurejesha heshima ya uongozi na imani ya umma kwa viongozi.

Baada ya zoezi la kusafisha safu za uongozi, kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba viongozi wanaobaki na wale wapya hawatumbukii katika matatizo. Aidha, upo umuhimu wa kuanza mara moja kuwalinda viongozi wapya. 

Baadhi ya tabia mbaya ni pamoja na mazoea ya viongozi na watumishi wa ngazi za juu za serikali, mashirika ya umma na vyama vya siasa kufanya urafiki wa karibu na wafanyabiashara matajiri, kupokea zawadi kutoka kwa marafiki hao, kutumia madaraka yao vibaya kwa kufanya maamuzi yanayowanufaisha binafsi badala ya kujali masilahi ya Taifa.

Tabia hizo zinaongeza udhaifu wa kuwadhibiti watendaji wa chini yao katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Kwa hali hiyo inapendekezwa kwamba hatua zifuatazo zichukuliwe bila kuchelewa:

(i) Viongozi na watumishi wa Serikali, mashirika, vyama vya siasa na vyama vingine vya umma (Civil Organisations) wakipokea zawadi kutoka kwa mtu yeyote lazima waziwasilishe kwa uongozi wa juu wa mahali pao pa kazi.

Uongozi wa mahali hapo utaweka thamani ya zawadi hizo na kumtaka mhusika ailipie. Vinginevyo zawadi hiyo itauzwa kwa mtu yeyote na fedha inayopatikana itakuwa sehemu ya mapato ya Serikali au chama husika.

(ii) Viongozi wajihadhari sana na kujenga tabia ya kutembeleana majumbani na wafanyabiashara na matajiri ambao sio ndugu wala marafiki wa viongozi au watumishi wanaohusika. Kwa msingi huo pia viongozi na watumishi wa Serikali watanabahi na kuhatarisha kazi zao kwa kutembelewa majumbani na kupelekewa zawadi wao wenyewe au familia zao.

Aidha, wazingatie kwamba shughuli za kiofisi zifanyike ofisini. Kwa hiyo ni juu ya viongozi au watumishi wahusika kuhakikisha jambo hili linatendeka. Wao ndio wanajua mipaka kati ya ndugu na marafiki na wale wanaowatafuta kwa ajili ya shughuli za kiserikali na kadhalika.

(iii) Ili kuhakikisha kwamba kila mtu anawajibika kwa shughuli alizokabidhiwa, iko haja ya kuweka mipaka au kuainisha madaraka kati ya watendaji wakuu wa wizara, idara na mashirika ya umma na mawaziri au wajumbe wa bodi za mashirika.

Kazi ya waziri na wajumbe wa bodi ni kutayarisha sera (Policies) na kudhibiti utekelezaji wa sera hizo. Wenye jukumu la kuzitekeleza ni watendaji wakuu na wakuu wa idara mbalimbali za Serikali na mashirika.

(iv) Uongozi ni dhamana ambayo mtu amekabidhiwa na umma. Kwahiyo ni muhimu kwa kila kiongozi kuhakikisha kwamba dhamana hiyo inalindwa na kutumiwa kwa manufaa ya umma na taifa zima kwa ujumla.

Aidha, heshima ya taifa lolote inategemea heshima ya viongozi wake mbele ya umma. Kwahiyo wakuu wa idara, wizara na mashirika ya umma, wanategemewa kuwajibika kwa ubovu wowote  ambao unatokea katika sehemu zao za kazi au kuhusiana na tabia zao wenyewe binafsi ambazo zinaliletea taifa fedheha.

Hivyo ni juu yao kujiwekea taratibu zitakazowawezesha kujua yanayotendeka chini ya himaya zao na kuwawajibisha wanaohusika kabla aibu hiyo haijawakumba wao wenyewe. Mathalani idara, wizara au shirika fulani likilalamikiwa juu ya rushwa, kiongozi wa idara au wizara ile au shirika lile awajibike. Kanuni hii inawahusu viongozi wa wilaya na mikoa pia.

(v) Ili kumlinda Rais asihusishwe na uteuzi wa viongozi wengi kupitia uwezo wake wa kuwafahamu, taratibu za zamani za kutumia Tume ya Uajiri Serikalini, Tume ya Serikali za Mitaa, Tume ya Jeshi la Polisi na Magereza, Tume ya Mahakama, Tume ya Walimu na kadhalika, zimeimarishwa ili Rais ahusike na uteuzi wa viongozi wachache tu wa juu kabisa.

Aidha, sehemu kubwa ya uteuzi pia itokane na mapendekezo ya tume hizi kupitia Idara Kuu ya Utumishi ambayo misingi yake ya kupendekeza mtu inajulikana. Kazi ambazo zinahitaji kushindaniwa na watumishi wote wa Serikali zitangazwe na kusailiwa na tume zinazohusika ndipo mapendekezo yapelekwe wa Rais au vyombo vinavyohusika kwa uteuzi wa mwisho.

Kwa njia hiyo, wakuu wa idara wa Serikali watapata fursa ya kuchunguzwa vizuri (to be vetted) kabla ya kuajiriwa katika ngazi ambazo watahusika moja kwa moja katika kuishauri Serikali.

Kwa upande wa mashirika ya umma, Rais awajibike kuteua Mwenyekiti wa Bodi tu. Isipokuwa kwa watendaji wakuu wa mashirika nyeti kama BoT na NBC, watendaji wakuu wengine wa mashirika watateuliwa na bodi zao baada ya kufuata taratibu za usaili.

(vi) Taratibu za kuwapekua watumishi wa sehemu nyeti za Serikali, kama watumishi wa masjala za siri, watumishi wa wizara nyeti kama Ikulu, Ulinzi, Mambo ya Ndani, Mambo ya Nje na kadhalika ni muhimu zirejeshwe haraka iwezekanavyo.

(vii) Watu wapewe kazi kutokana na ujuzi na uwezo wao, uadilifu wao kazini, na tabia zao kwa ujumla. Kazi nyeti wasipewe watu ambao historia zao hazijulikani sawasawa, lakini ni muhimu pia kwamba watu wasipoteze nafasi za kupandishwa vyeo kwa sababu historia zao hazijulikani. Ni juu ya viongozi wa idara, mashirika au wizara zinazohusika kuhakikisha kwamba wanakuwa na taarifa kamilifu za kila mtumishi aliye chini yao.

(viii) Masuala yanayopelekwa kwa Rais kwa uamuzi yapelekwe ndani ya majalada ya wizara inayohusika. Pale ambapo suala hilo limejadiliwa kwa muda mrefu na kuna majalada zaidi ya moja ambamo mjadala uliendeshwa (yaani volumes mbili au tatu), majalada hayo yote yaambatanishwe. Hii itampa Rais fursa ya kujua historia ya suala hilo kama akitaka na hata kujionea mawazo ya watu wa chini pia, jambo ambalo linamwezesha pia kujua watu wengi zaidi katika utumishi wa Serikali yake.

(ix) Idara ya Habari irudishe utaratibu wa kuwa na gazeti la Serikali la kurasa mbili au nne ambalo litatolewa kwa wiki au kwa mwezi kwa bei nafuu na ambalo litaelezea kinaganaga maamuzi ya Serikali na taratibu mbalimbali za Serikali.

Zamani gazeti kama hilo lilijulikana kama “Habari za Leo” na lilitolewa kila wiki bure tu. Hatua hii itausaidia umma kujua yanayoendelea ndani ya Serikali pamoja na haki zao ambazo hawapaswi kuzilipia. Gazeti hilo pia liwaelekeze wananchi mahala pa kupeleka dukuduku zao wanapoonewa na vyombo vya umma.

(x) Mtindo wa majaribio katika miundo na utekelezaji uachwe. Pale ambapo uamuzi ulikwishakufanyika baada ya uchambuzi wa kina na utekelezaji unaendelea, hali hiyo isibadilishwe, isipokuwa kwa sababu nzito sana na zenye maelezo yanayojumuisha wataalamu na watendaji wanaohusika.

 

III. UDHIBITI WA VIONGOZI

6. Akijadili uzoefu wake kuhusu juhudi za kupambana na rushwa katika nchi yake, Kamishna wa Kamisheni Huru ya Kupambana na Rushwa ya huko Hong Kong ameandika kwamba: “Katika jamii yoyote rushwa itaweza kupunguzwa ikiwa wananchi kwa ujumla wanaamini kwamba uongozi wa nchi  una dhamiri ya dhati ya kuipiga vita rushwa; kwamba uongozi wa juu kabisa unaonyesha mfano wa kweli wa uadilifu na tabia njema ya maadili ya taifa; na kwamba faida kutokana na maendeleo ya uchumi zinapenyeza kumfikia mwananch wa kawaida katika jamii ile.”

7. Tume imeyanukuu maneno haya si kwa sababu ya ukweli wake tu, bali kusisitiza umuhimu wa kusafisha safu za juu za viongozi. Viongozi waliopo na wapya hawawezi kuona umuhimu wa vita hivi mpaka Rais na Serikali yake aonyeshe kwa vitendo kwamba hakika wakati wa kuwavumilia wanafiki, wabadhirifu, na walarushwa umepita. Hatua hiyo itawafanya wananchi wawe na imani zaidi ya Rais na Serikali yake, na itawawezesha wananchi kushiriki katika kuwafichua walarushwa kwa imani kwamba Serikali yao itawachukulia hatua.

8. Njia pekee ya kuwadhibiti viongozi ni kuwaonyesha kwamba Serikali haitamvumilia kiongozi anayekiuka maadili. Hivyo Serikali iainishe wazi wazi maadili ya viongozi na yatangazwe kwa kila mwananchi. Kiongozi anayekiuka maadili hayo awajibishwe bila huruma au upendeleo. Miongoni mwa maadili hayo ni: 

(i) Kutokutumia cheo chake kujinufaisha yeye mwenyewe, familia yake, au mahali anapotokea. Kiongozi yeyote atambue kwamba yeye ni kiongozi wa taifa hili na hawezi kutumia juhudi za taifa kunufaisha kikundi kidogo cha watu bila kujali mipango ya kuendeleza taifa zima kwa ujumla.

Tunapenda kusisitiza hapa kwamba kinachokatazwa ni kutumia “juhudi za taifa” kwa manufaa ya wachache. Kiongozi hazuiwi kuwahamasisha jamii zake au watu wa wilaya yake au kijiji chake kuweka juhudi katika kujiendeleza wenyewe na hivyo wakaweza kuvutia huruma za wahisani kutoka nje ya wilaya hiyo au kijiji hicho hata kutoka nje ya nchi kuwaongezea nguvu.

(ii) Kutokutumia vyombo vya Serikali au shirika kuendeleza biashara zake au za jamaa zake. Mathalani tabia ya kiongozi kupanga eneo kubwa la nyumba za shirika la umma na yeye mwenyewe kuipangisha sehemu hiyo kwa watu wengine kwa kodi kubwa zaidi ya ile ambayo yeye anailipa. Kitendo hicho ni kibaya zaidi kama yeye ndiye pia kiongozi wa shirika hilo.

(iii) Kutunza mali ya umma kama anavyotunza mali yake binafsi. Tabia yoyote inayoonyesha ufujaji na kutozingatia maadili ya kiuchumi ya idara, shirika au wizara anayoisimamia katika kutumia mali ya umma iweze kuadhibika kwa kumwachisha au kumfukuza kazi na hata kumchukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kumfilisi mali yote ambayo ameichuma kwa  njia za ubadhirifu.

(iv) Tabia ya aina yoyote isiyolingana na maadili ni aibu kwa taifa. Ni muhimu viongozi wakuu wa Serikali, mashirika ya umma, vyama vya siasa na kadhalika wajue kwamba macho ya watu wote yako juu yao. Ni vema wakawa mfano wa tabia njema katika jamii. Kiongozi anayekumbwa na kashfa yoyote inayokiuka maadili aachishwe kazi mara moja ikiwa atakataa kujiuzulu mwenyewe.

(v) Kila kiongozi awajibike kujua na kuelewa taratibu za utendaji kazi katika eneo analolisimamia awe mkweli, kila wakati aonyeshe ubunifu katika kuwaongoza wananchi na watumishi wenzake kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, hasa wanyonge na hivyo maendeleo ya Taifa kwa jumla. Asiwe mbabaishaji na anaposhindwa akiri kushindwa.

(vi) Viongozi waachane na tabia ya kuendesha mambo kwa operesheni ili wasikike. Viongozi washindane katika kufanikisha sera mbalimbali zilizokubaliwa na siyo katika kujitangaza juu ya mambo wanayobuni, hata kama hayakufaulu. Tujenge tabia ya kutangaza matokeo mema ili yawe shule kwa wengine. Kwa njia hiyo viongozi watakuwa waangalifu sana katika kutamka mambo.

(vii) Viongozi wawe na tabia ya kuandika hotuba zao ili wawe na hakika kwamba yale yanayotamkwa ni kweli yalikusudiwa yasemwe mahali pale yalipotamkiwa. Hotuba hizo ziwekwe kwenye kumbukumbu maalumu ili viongozi wa juu wanapotembelea sehemu za kazi mikoani na wilayani waweze kukagua na kudhibiti yale yaliyotamkwa kuona kama yamefuatiliwa na vitendo au ilikuwa ni kujifurahisha tu. Hatua hii itawalazimisha viongozi kujifunza kufikiri kabla hawajasema kitu na kufuatilia utekelezaji wa maagizo yao.

(viii) Viongozi wa mikoa na hasa wa wilaya wajenge tabia ya kuandaa taarifa za miezi mitatu mitatu ambazo siyo zaidi ya kurasa tano, zikionyesha tathmini ya maendeleo ya sehemu zao kwa takwimu. Serikali isaidie kutayarisha muundo (format) wa taarifa hizo. Mikoa iwasilishe taarifa kwa wakuu wao.

 

IV: NAMNA YA KUDHIBITI WATOA RUSHWA WAKUBWA

9. Katika kusafisha safu za uongozi, bila shaka itadhihirika kwamba kuna baadhi ya matajiri ambao ndio hasa wamekuwa washiriki katika kuwaharibu viongozi. Aidha kwa sababu ya udhaifu wa taratibu za udhibiti huko nyuma, uko uwezekano kwamba hata viongozi wetu wazuri wamejitumbukiza katika mkumbo wa kutumia vyeo vyao kujinufaisha kwa sababu ya kurubuniwa na matajiri hawa. Ili kuhakikisha kwamba tabia mbaya za matajiri hawa pia zinakomeshwa, inapendekezwa kwamba hatua zifuatazo zichukuliwe mara moja:-

(i) Watu wote ambao watabainika na kwamba wamekuwa chanzo cha upotoshaji wa haki na ukiukaji wa taratibu zilizowekwa waadhibiwe bila huruma ama kwa kutaifisha na kuzifilisi mali zao kwa mujibu wa sheria. Mifano hai ni kama ile ya kujenga majengo katika maeneo yaliyokusudiwa kujenga ama huduma za umma kama maduka, zahanati, shule na kadhalika; au mahali ambapo palikusudiwa kuwa burudani kwa umma. Ni dhahiri kwamba maamuzi kama hayo lazima yawe yalifanyika kinyume na taratibu.

(ii) Matajiri hawa pia watakiwe kujieleza kwa utaratibu utakaowekwa na Serikali ni viongozi gani wanazo hisa katika kampuni zao na walizilipiaje. Kama walilipiwa na kampuni, hisa hizo zitwaliwe na Serikali. Lakini kama walinunua kwa fedha zao wenyewe na ziachwe vivyo hivyo.

(iii) Ni muhimu kampuni iseme kweli. Ikibainika kwamba haikusema kweli, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya kampuni hiyo.

(i) Aidha madhambi ya kiongozi yanayotokana na taarifa hizo za kampuni yawe ni sababu tosha ya kumvua uongozi kiongozi huyo kama ambavyo imekwisha kupendekezwa.

10. Ili kuwawezesha viongozi hawa, hasa wajumbe wa bodi mbalimbali za  mashirika ya umma kutekeleza wajibu wao kikamilifu inapendekezwa kwamba:

(i) Wajumbe wateuliwe kwa kuzingatia ujuzi, uwezo, na uadilifu wa hali ya juu na sio kwa vyeo kama Mbunge, Katibu Mkuu, Meya na kadhalika. Aidha kila inapowezekana, wateuliwe wajumbe wenye uzoefu wa shughuli zinazohusika.

(ii) Mjumbe yeyote ambaye ni mtumishi wa umma asiwe kwenye bodi zinazozidi tatu.

(iii) Pale ambapo sheria inayounda shirika ndiyo inatumika kufanya uteuzi wa wajumbe wa bodi, sheria hiyo ibadilishwe ili kutoa nafasi kwa waziri anayehusika kuteua watu ambao watakuwa na muda wa kutosha. Iwe mwiko kwa waziri kuteua wajumbe kutokana na undugu au urafiki.

(iv) Viongozi na watumishi wa umma walioko katika nyadhifa za kufanya maamuzi makubwa ya kitaifa kama mawaziri, manaibu mawaziri, Spika, Gavana wa Benki Kuu, Katibu Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu wake na Inspekta Jenerali wa Polisi wasiteuliwe kuwa wajumbe wa bodi za mashirika.

 

Je, unajua wiki ijayo Ripoti ya Rushwa ya Jaji Warioba aliyoiandaa mwaka 1996 lakini hadi leo inazungumza matatizo ambayo hayajaondoka miaka 20 baadaye anapendekeza nini? Usikose nakala ya JAMHURI upate mwendelezo wa ripoti hii muhimu.

1647 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!