‘Woga ndio silaha dhaifu kuliko zote’

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, amezungumza jambo la maana sana.
Amewataka wananchi wasilalame tu, badala yake wachukue hatua dhidi ya ukiukwaji wa haki pale unapojitokeza. Amewataka watumie vyombo kama Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mahakama na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kutatua yale yanayowasibu kwa upande wa haki.
Profesa Kabudi amesema: “Jambo ambalo tumeliona hapa nchini watu wengi wanalalamika badala ya kuchukua hatua za kwenda kwenye mamlaka husika kutoa taarifa zinazohusu uvunjwaji wa haki zao au matumizi mabaya ya madaraka…”
Namshukuru na kumpongeza Profesa Kabudi kwa kuliona na kulisemea jambo hili. Wakati wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki, nilisafiri maeneo mengi nchini nikiwa na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa wakati huo, Dk. Diodorus Kamala.
Katika mkutano uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, mwananchi mmoja mwenye ulemavu (jina nimelisahau), alitofautiana na wenzake. Yeye aliunga mkono kuanzishwa kwa Shirikisho hilo. Wapo waliomzomea, lakini akawa imara. Hoja yake ikawa kwamba; “Woga ndiyo silaha dhaifu kuliko zote.” Aliamini woga wetu wa kuingia kwenye shirikisho kwa kuwahofu Wakenya, ungetuathiri kiuchumi. Yawezekana alikuwa sahihi au la! Hata hivyo, maneno ya ‘woga kuwa ndiyo silaha dhaifu’ nayakumbuka, na kwa kweli yamekuwa yenye msaada mkubwa kwangu.
Kwamba wananchi wanalalama, hilo si jambo la kificho. Kwamba wananchi wanaonewa, hilo liko wazi. Kwamba wananchi wana malalamiko mengi dhidi ya viongozi, watumishi na vyombo vya utoaji haki, hilo nalo si la mjadala. Je, tufanye nini?
Bila shaka kinachopaswa kufanywa na wananchi wanaoonewa, ni kuacha kulalamika tu – kama alivyosema Profesa Kabudi. Malalamiko pekee hayawezi kuondoa uonevu, dhuluma na vitisho wanavyofanyiwa wananchi. Lakini kwanini watu walalamike? Si kweli kuwa viongozi au vyombo vya utoaji haki vyote nchini hawafai au havifai. Kwa bahati nzuri wapo viongozi na watumishi wenye kutenda haki. Kuna vyombo vya utoaji haki ambavyo bado vimesimama imara kwenye maadili na utoaji haki. Kinachosumbua ni ile kasumba iliyojengeka katika jamii ya kuamini kuwa samaki mmoja akioza, basi wote wameoza. Kuna dhana ya kwamba ili mtu aweze kuhudumiwa vizuri katika Mahakama, Polisi au katika ofisi na taasisi yoyote ya umma, lazima atoe rushwa au awe anawajua viongozi au watumishi fulani fulani katika idara au taasisi fulani fulani.
Mara kadhaa wananchi wamefika polisi na waliponyimwa huduma fulani na polisi mwenye cheo cha chini, hawakuhangaika ‘kukata rufaa’ ili wamwone mkuu wa kituo au kiongozi wa ngazi ya juu zaidi. Walichofanya, ama ni kutafuta fedha za kuhonga, au walimtafuta ndugu, jamaa au rafiki anayejuana na ‘fulani’ katika kituo hicho cha polisi, awasaidie.
Kumekuwapo na ile dhana inayojulikana kama ‘stereotype’ ambayo inamfanya mtu, kwa mfano, ajiaminishe kuwa Wakurya ni wagomvi! Wachagga ni wezi! Wahaya ni wapenda majigambo! Wamaasai ni wezi wa mifugo, na kadhalika, na kadhalika.
Hii ni dhana potofu. Ni wajibu wa watu wenye uelewa kwenye jamii, kuwaelimisha wananchi ili hatimaye waamini kuwa si polisi wote ni waonevu, si mahakimu na majaji wote ni wala rushwa, si waandishi wa habari wote ni ‘wapenda mishiko’, si mawaziri wote wana roho mbaya, si madaktari na wauguzi wote hawana huruma kwa wagonjwa, n.k.
Wananchi wajue kuwa wanapoona hawakutendewa haki katika ngazi moja, ni wajibu wao kwenda ngazi ya juu. Bahati nzuri Rais Joh Magufuli ameshaweka msimamo wenye kuwabana viongozi na watumishi kuwahudumia wananchi. Mara kadhaa amesema malalamiko ya wananchi yanapofikishwa kwa viongozi wa ngazi za juu, maana yake walioko chini wameshindwa kazi.
Hii ni sahihi kabisa. Haiwezekani, kwa mfano, rais akaanza kuhangaika na masuala ambayo ni saizi ya mtendaji wa kitongoji au mtendaji wa mtaa. Si jambo la kiungwana kuona waziri mkuu akisumbuliwa na jambo lililopaswa kumalizwa na mkuu wa wilaya. Hii maana yake nini? Maana yake ni kuwa viongozi na watumishi wa umma sasa wanapaswa kuwajibika, kila mmoja, kwa nafasi yake ili kuwatumikia wananchi. Kama hivyo ndivyo, basi ni wajibu wa wananchi nao kuitumia fursa hiyo badala ya kulalama pembeni na kuyaumba matatizo na kero kwa hisia tu.
Nampongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala, ambaye tangu ashike wadhifa huo mkoani Kilimanjaro, amekuwa na utaratibu wa kusikiliza kero zinazowakabili wananchi. Huu unapaswa kuwa utaratibu wa kila mkuu wa wilaya, kila mkuu wa mkoa na viongozi wengine katika nafasi zao. Huo uwe utaratibu katika ofisi zote za umma.
Yule mwananchi wa Mtwara aliyesema “woga ndiyo silaha dhaifu kuliko zote”, yuko sahihi. Alimradi wananchi wanakuwa si wavunjifu wa sheria, hawana sababu ya kuwa waoga. Kumekuwapo tabia kwa wananchi kuwa waoga pale wanapotishwa. Mathalani, mwananchi anayefika polisi kuuliza sababu za ndugu yake kuwekwa rumande, anapotolewa macho tu na polisi anakuwa mwoga kweli kweli. Woga anaoupata ni kuwa kwa kuendelea kudai au kuhoji, naye atawekwa rumande! Huu ni woga mbaya.
Woga umechangia kuongeza idadi ya matukio ya mauaji na hata ushirikina katika jamii yetu. Kumekuwapo ushahidi usiotiliwa shaka kuwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na ile ya Magharibi wananchi ‘wanaisemea mioyo’ – kwa kuamini kuwa hawatendewi haki kwenye vyombo vya haki. Matokeo yake huamua kuisaka hiyo haki wao wenyewe kwa mauaji au kwa vitendo vya ushirikina.
Lakini pamoja na kuunga mkono mwito wa Waziri Kabudi wa wananchi kuacha kulalama, ni vema tukakiri kuwa kuna uonevu mkubwa katika baadhi ya vyombo vya utoaji haki nchini mwetu. Hali hii ndiyo iliyowafanya wananchi wengi, hata pale wanapotendewa haki – jambo ambalo ni haki yao – waone kuwa hiyo ni hisani.
Kwa mfano, imekuwa kawaida polisi kumkamata mtu asiye na hatia yoyote, akawekwa rumande  na pindi anapoachiwa, mwananchi huyo amekuwa ‘akiwashuruku’ waliomwachia! Anashukuru kwa sababu, ama hajui haki zake, au anazijua lakini woga tu unamfanya awe dhalili. Wananchi wakianzisha utaratibu wa kudai fidia pale wanapobaini hawakutendewa haki, naamini matukio ya uonevu ya aina hii yatapungua sana katika jamii yetu.
Haki ndiyo msingi mkuu wa umoja na upendo katika jamii yoyote. Haki inapolinganishwa na bidhaa, kwamba inapatikana kwa kuinunua, jamii itayumba na mambo ya hovyo yatatamalaki.
Tunao ushahidi wa wananchi ambao kesi zao zipo mahakamani kwa miaka 17 au 20. Wamefungua kesi wakiwa vijana, wamezeeka hukumu zikiwa hazijatolewa. Hawa ni wengi mno. Wapo wajane na yatima wanaoonewa au kuzungushwa na viongozi, na watumishi wa vyombo vya utoaji haki. Hao waache kulalama kama alivyosema Profesa Kabudi. Waende katika ngazi za juu ili waweze kutendewa haki.
Hatuwezi kuyapunguza au hatimaye kuyamaliza matatizo yetu kwa kulalama tu. Hili halipo kwenye haki tu, bali hata kwenye maisha yetu ya kila siku. Kulalama pekee hakuwezi kubadili maisha yetu. Hakuna aliyejenga nyumba ikakamilika kwa kuwa alitumia muda wake mrefu kulalama. Maisha kama ilivyo haki ya mtu, hupatikana kwa kuchukua hatua stahiki. Woga wa kudai haki ni silaha dhaifu inayotukwamisha wengi kwenye kudai haki na hata katika kuyaandaa maisha yetu.
Kila mmoja wetu aliyepata mwanga wa kuzijua haki za raia, na ashiriki kuwahamasisha wananchi kuzidai bila kuchoka. Awahimize waache tabia ya kulalama tu pembeni. Wananchi wenyewe ndiyo waamuzi wa aina ya jamii au Taifa wanalotaka kulijenga. Tuache kulalama.

1445 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons