Timu ya soka ya Alliance ya jijini Mwanza, imealikwa kushiriki mashindano ya kimataifa yanayojulikana kama International English Super Cup 2013, huku ikiahidi kurejea nchini na ushindi.

Mashindano hayo yatawashirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 12 na 14.

Akizungumzia na JAMHURI hivi karibuni, Katibu wa timu hiyo ya Alliance, Kessy Mziray, amesema wanatarajia kuondoka hapa nchini kwenda Uingereza Julai 28, mwaka huu.

 

“Lakini kabla ya kuondoka kwenda Uingereza tunatakiwa kuwa tumewaandikia wenyeji wetu barua ya uthibitisho wa kushiriki kwetu kufikia Mei, mwaka huu,” amesema Mziray.

Kwa mujibu wa Mziray, ikiwa Uingereza timu hiyo itapata pia fursa ya kutembelea timu maarufu za Man United, Arsenal na Swansea.


“Tutakuwa Uingereza hadi Agosti 6, mwaka huu, lakini kabla ya kuanza mashindano, tutatumia siku tatu kutembelea timu hizo maarufu nchini humo,” ameongeza.


Kwa sasa uongozi wa timu hiyo unafanya maandalizi ya ziara hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na uongozi wa Mkoa wa Mwanza kupata vibali muhimu.


Mkurugenzi wa Alliance Sports Academy, James Bwire, amesema ziara hiyo itawahusisha watu 19 wakiwamo wachezaji na viongozi, na kwamba gharama kwa kila mmoja ni Sh milioni nne.


Timu hiyo ina matumaini ya kuibuka na ushindi mnono katika mashindano hayo ya nchini Uingereza, kwani ina historia ya kutwaa ushindi karibu mashindano yote iliyokwishashiriki ndani na nje ya nchi.


“Tumejiandaa na tunaendelea kujiandaa zaidi, tuna uhakika wa kurudi na ushindi kibindoni kama ilivyo kawaida yetu kila tunaposhiriki mashindano mbalimbali,” ametamba Mziray.

 

Katika hatua nyingine, katibu huyo amesema timu hiyo inajiandaa kushiriki mashindano ya kirafiki nchini Kenya, kati ya Aprili 14 na 17, mwaka huu.


“Baada ya ziara hiyo ya nchini Kenya, tutakwenda Uganda kushiriki mashindano mengine ya kirafiki kuanzia Aprili 27 hadi 29, mwaka huu,” ameongeza Mziray.


Mashindano hayo ya Kenya na Uganda yatawashirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 12, 14 na 17.


Alliance Sports Academy ilianzishwa na Bwire kwa ajili ya kuibua na kuwaendeleza watoto na vijana wenye vipaji vya soka ndani na nje ya Mkoa wa Mwanza, pamoja na kuwagharamia masomo kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.

 

Please follow and like us:
Pin Share