Kuna wakati nahisi kama nchi yetu tunahitaji kuwa na ofisi za kijasusi, ambazo zimesajiliwa na zinalipa kodi kuliongezea Taifa mapato.

Nafikiria hivyo ninapokumbuka mambo ninayoona yanaingiliana na masuala ya kijasusi katika jamii yetu iliyokuwa na mshikamano mkubwa miaka michache iliyopita, ambapo kila Mtanzania alikuwa mlinzi wa amani katika nchi hii.

 

Nimekumbuka mambo mengi ya utekaji nyara ambayo kimsingi, hauna tofauti kubwa na ule ujasusi ninaoufahamu vizuri. Tumesikia baadhi ya wataalamu katika nyanja ya habari wakitekwa na kutendewa unyama kutokana na kazi yao wanayoifanyia jamii, wataalamu kama madaktari wakisokomezwa misituni na kuteswa kwa nia zao wanazozijua watekaji ninaowaita majasusi.

 

Lakini siku chache kabla ya matukio haya, tuliwahi kusikia watu wakiwateka watoto wadogo na kudai fedha nyingi kutoka kwa wazazi. Hata hivyo, ujasusi ule nasikia ulikomeshwa mapema na wajanja wachache waliokuwa wanawajua wahusika wa matukio hayo.


Hivi sasa masuala ya kutekana yanaonekana kushika kasi. Watekaji sasa hawataki fedha badala yake yaelekea wanapewa fedha na hao wanaowatuma, kwa fikra zangu watumaji ndiyo majasusi wakubwa kuliko hawa ambao wanakwenda kutekeleza walichoagizwa na hao wakubwa wanaokaa nyumbani kubuni mipango mingine ya  utekaji. Nchi yetu ninayoijua vizuri haikuwa  hivyo, watu tuliheshimiana sana.

 

Nchi yetu ninayoifahamu tangu ikiitwa Tanganyika, haikuwahi kuwa na matabaka ya watu wanaowatafuta wenzao kwa lengo la kuwadhuru kama ilivyo sasa kwa viongozi wetu, wataalamu, na watu wengine – iwe kwa sababu zozote zile za msingi na ambazo hazina msingi.


Naomba nichukue fursa hii kuiomba Serikali yetu ianzishe taasisi ambayo itakuwa ikisajili kampuni za kijasusi na zikajulikana ziweze kuingiza mapato ya Taifa, kwa sababu naona sasa zimekuwa kampuni za kinyemela na kulipa shida Jeshi letu la Polisi katika kudhibiti uhalifu huu.


Siku chache zilizopita, tumesikia viongozi wengi wa kisiasa wakiwa katika wimbi la kuuawa – iwe kwa kuwekewa sumu ama kuwindwa kama wanyama mbugani. Uchunguzi umefanyika na majibu hayajapatikana. Wapo waliokana kuhusika na wapo walioshukiwa kufanya hivyo pasi na ushahidi wa kujitosheleza.


Ubaya hulipwa kwa ubaya lakini katu ubaya wa mtu mmoja unaoonekana kwa kundi fulani tu, na kundi kubwa la jamii likawa linamkubali, hauwezi kuzimwa kwa kufanya ujasusi. Ni sawa sawa na kupalilia wimbi la kudai haki. Siamini katika kufanya mauaji kwa kiongozi wa siasa anayetetea wananchi ni suluhisho, suluhisho pekee ni kuondoa kero ambazo mwanasiasa huyo anazisimamia.


Nisingependa kuona ujasusi huu ambao katu katika maisha yetu ya Tanganyika ninayoijua, haukuwahi kutokea hadi kipindi hiki cha kuiva kwa demokrasia na kupembua mambo kwa jamii yetu kulivyokomaa. Ni haki ya msingi kila mmoja kueleza anachoona kinafaa kwa jamii yake, iwe kwa manufaa yake ama jamii inayomzunguka.

 

Hatuna sababu ya kuwa na walinzi wengi kwa viongozi wetu kwa sababu ya kuhofia usalama wao, hiyo nguvu tunapaswa kuwekeza katika kilimo na hata kufufua viwanda. Hatuna sababu ya kuendelea kuogopana Watanzania ambao tuliamini katika uzalendo na kuheshimiana na kupendana.


Naanza kuingiwa na wasiwasi kama kweli nchi yetu bado inamilikiwa na Watanzania ama tayari imekwishavamiwa na wageni wasio na utamaduni wetu tuliouanzisha tangu siku tulipopata Uhuru.


Chonde chonde Watanzania wenzangu tuangalie kama suala la kuwindana lina tija kwetu, tuangalie kama kuuana kutafuta makosa ambayo muuaji atakuwa ameyakwepa. Tujiulize kama hiyo ndiyo njia mwafaka ya kumaliza matatizo, vinginevyo lile suala la majirani zetu na kesi za The Hague ndiloo linakuja.

Wasaalam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.


Please follow and like us:
Pin Share