Uchambuzi wa Mkali, wiki iliyopita ulikomea akisema kwamba Uhuru wa wananchi kuishi popote kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki (EAC) unatakiwa uwe, kwa lugha ya kiingereza wanasema, “reciprocal”, kwa maana ya raia kutoka nchi wanachama wanakuwa huru kuhamia Tanzania, kwa sababu nafasi za kuishi hao watu kwa amani zitakuwa zipo. Kadhalika, Watanzania wanatakiwa wawe huru kuhamia kwenye hizo nchi shiriki ambako nako nafasi za wao kuishi kiamani pia ziwe zimeandaliwa; walakini hali halisi inasema Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ardhi ya kuwawezesha Watanzania kufungua maskani kule haipo hata kidogo; na uhamiaji wa upande mmoja tu hautakuwa “free movement” ambayo inadaiwa bali ni uvamizi “invasion” ambao utazaa vita ya sisi kwa sisi isiyokwisha. Hii ni “commonsense” si “rocket science”.

 

Sasa enedelea: Mfano wa karibu wa hii hali ambayo inaliwinda jimbo la Afrika Mashariki leo, tuangalie yaliyowapata wananchi wa Nigeria kati ya mwaka 1967 na 1970. Mnamo 1914 serikali ya kikoloni, bila kuwashirikisha wananchi wenyewe, iliunda Shirikisho la Nigeria kati ya: nchi za Nigeria ya Kaskazini na Nigeria ya Kusini. 

Hizi zilikuwa nchi mbili tofauti kama vile ilivyokuwa Rhodesia ya Kaskazini (Zambia) na Rhodesia ya Kusini (Zimbabwe); na leo viongozi wa Afrika Mashariki wanachelea kuitisha kura za maoni kuhusu shirikisho kwa sababu wanafahamu wazi wananchi wao walio wengi hawautaki huu mradi; kama wakoloni walivyosita kuitisha kura za maoni Nigeria.     

Kadri miaka ilivyopita, wananchi wa Nigeria ya Kusini ambako kulikuwa na uhaba mkubwa wa ardhi walihamia kwa wingi huko Nigeria ya Kaskazini chini ya tiketi ya uraia wa shirikisho (Federal citizenship).

Lakini ilipofika miaka ya 1960, kubaguliwa kwa Wanigeria wa Kusini walioishi Kaskani kulipamba moto katika nyanja za uajiri, utoaji wa zabuni, kufutwa kwa hati za kumiliki ardhi na hatimaye watu bungeni waliongea waziwazi wakiwataka Wanigeria ya Kusini walio Kaskazini warudi kwao.

Sasa sijui hiyo “kwao” ilikuwa wapi wakati kisheria hii sasa ilikuwa nchi moja! Na baada ya miaka 50 hawa waliokuwa wanaambiwa warudi kwao ni watu waliozaliwa na kukulia Kaskazini; kwao waliyoijua ilikuwa si Kusini.

Wabaguzi walipohisi ubaguzi na unyanyasaji haukuleta mabadiliko kwa kasi waliyoitaka basi mauaji yalifuata, yaliyofikia kilele 1966 – mwaka ambao wananchi wa kabila la Waibo 30,000 waliokuwa wanaishi Kaskazini waliuawa; hili ndilo chimbuko la kujitenga kwa jimbo lililojiita Jamhuri ya Biafra, kulikosabisha vita ya wao kwa wao ya Julai 1967 hadi Januari 1970. Vita hii iligharimu maisha ya watu karibu milioni tatu. 

Itakuwa ni sawa na uhaini kuruhusu kifo cha Mtanzania hata mmoja kesho na keshokutwa kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe itakayosabishwa na: uroho wa ardhi wa viongozi wa Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi; au kutokana na viongozi wa Afrika Mashariki kuoneana aibu kuelezana ukweli; ama kwa sababu viongozi walibebana kwa maslahi yao binafsi. 

Kuna mambo mawili muhimu hapa ya kuzingatia, kwanza, ni kwamba hilo shirikisho la kinafiki litakapokujuvunjika vita vitakujafuata. Na watakaokufa vitani; watakaokufa kwa njaa; na watakaosota kwenye makambi ya wakimbizi hawatakuwa viongozi au familia zao, bali watu kama wewe na mimi – watoto wa maskini; tumeyaona hayo huko Kenya 2007/8.

Pili, linalojitokeza ni kuwa wenzetu wanatuingiza kwenye huu mtego wa Shirikisho kwa mahesabu, kisayansi – hatua kwa hatua. Watanzania tunaonekana tunajiingiza tu kichwa kichwa tena na macho tumefumba.

Tukumbuke kuwa mfarakano wa Jumuiya ya kwanza mwaka 1977 haukazaa vita kwa sababu halikuwa Shirikisho, na hicho kipengere walikifahamu hao waliovunja Jumuiya hiyo. Leo umuhimu wa Shirikisho haupo kata kidogo.

Lakini wao wanashinikiza Shirikisho ili sisi tusidiriki kujitoa, baada ya kuingia, (kama wao walivyojitoa kwenye Jumuiya 1977) kwa sababu chini ya Shirikisho “sheria” itairuhusu Serikali kwenda vitani; tena watakaofanya kazi hiyo ni maswahiba wao wa Ulaya na Marekani wenye silaha zinazoitwa “drones” yaani ndege za kivita ambazo hazichui marubani.

Watanzania hatutajua kilchotupiga, uzoefu wetu wa vita tulioupata zama za ukombozi wa Afrika, hautatusaidia. Hayo ndiyo mahesabu yao. Tukishapiga saini ya kuingia kwenye shirikisho, basi tumekwisha kuwa mateka; na kwao wao hiyo saini itakuwa ni bima ya kuwawezesha kuvamia ardhi yetu kisheria.

Baada ya wananchi wa kabila la Waibo 30,000 walioshi Kaskazini ya Nigeria kuuawa, Waibo walipewa kila sababu ya kujitoa kwenye Shirikisho hilo. Lakini kipengere cha Shirikisho ndicho kilitumiwa kuhalalisha vita iliyoua watu karibu milioni tatu na zaidi.

Umoja wa Afrika ulipeleka majeshi Comoro kuzuia kujitenga kwa jimbo la Anjouan mwezi Machi, mwaka 2008. Wakati jimbo la Mayotte liliokataa kuingia kwenye Shirikisho likabaki linatawaliwa na Ufaransa, leo hii wala halisumbuliwi. Sisemi Mayotte ilitoa uamuzi nzuri, la hasha, ninalosema ni kwamba demokrasia ni uhuru wa kuchagua ikiwa ni pamoja na kuchagua kwa makosa.

Shirikisho, si mradi wa kujiingiza aidha bila tafakari ya kina au muafaka wa raia walio wengi katika nchi. Hivyo basi, ni maoni yangu kuwa Rais Jakaya Kikwete, aliteleza kulitangazia taifa kupitia Bunge kuwa Tanzania haitajitoa kwenye mradi wa Shirikisho la Afrika Mashariki, baada ya kukutana na marais wa Kenya na Uganda alipokuwa Afrika Kusini. Kuingia kwenye Shirikisho maana yake Watanzania kuachia uhuru wao, na uhuru ni mali ya wananchi si ya rais, serikali au si mali ya Bunge. Maamuzi ya Watanzania kupitia kura za maoni (referendum) iwe ndiyo njia pekee ya kuingilia kwenye Shirikisho, kama kuna tija ya kujingiza huko, ambayo haipo.

Rais wa awamu ya pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, kama angaliitisha “referendum” kabla hajatoa ahadi ya kujishirikisha kwenye hili janga la Shirikisho, leo tusingalikuwa hapa tulipo; tusiendeleze makosa. Lakini taifa linao muda wa kutosha wa kusahihisha kosa hili, na kama hatulisahihishi baada ya kubainika kama ilivyo hivi sasa basi historia isije kumlaumu Alhaji Mwinyi.

Kiongozi yeyote, anapokula kiapo cha kulinda Katiba pamoja na nchi pia anakula kiapo cha kutosema uongo, ingawa msamiati wa “sitasema uongo” huwa haupo; lakini unakuwepo katika tafsiri yake; kwa mantiki ipi? Mathalani, wakati wa kuapishwa unaposema, “… nitailinda na kuitetea katiba na wananchi wa nchi yangu; Mungu nisaidie”, Taifa huwa halina sababu ya kutoamini kuwa unasema kweli; hiyo imani ya Taifa huwa ni sehemu ya kiapo chako. 

Hivyo basi, viongozi wa Afrika Mashariki wasivunje viapo vyao kwa wajindanganya au kuwadanganya wanachi wao kuwa vita kama ya Biafra haiwezi kutokea: kwani mauji ya sisi kwa sisi yamejitokeza Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda.

Tutawezaje kudai kuwa vita aina ya Biafra haiwezi kutokea hapa kwetu, hasa tukizingatia kuwa tatizo la ardhi lililokuwa ndio msingi wa vita ya Biafra ni kubwa zaidi Afrika Mashariki leo kuliko lilivyokuwa Nigeria nyakati hizo?

 

Kukokota miguu

Washirika wetu watarajiwa kwenye “Shirikisho” la Afrika Mashariki wanaposhindwa kujibu swali la ardhi ndipo wanaishia kututukana Watanzania kuwa tunakokota miguu kwa makusudi ya kuhujumu juhudi za kuunda umoja wa Afrika Mashariki na kwa mwendelezo umoja wa Afrika.

Kwa nini ninasema kuwa ni matusi kuwashutumu Watanzania kuwa wahujumu wa umoja. Kwa sababu ilikuwa ni Tanzania iliyotangaza kuwa tayari kusitisha uhuru wake ili kuwasubiri wenzetu kwa lengo la kuungana mara tu baada ya kutoka kwenye ukoloni.

Ilikuwa ni “… Rais Nyerere wa Tanzania aliyesimamisha maendeleo ya nchi yake ili kuhakikisha ukombozi wa nchi zingine zote ambazo zilikuwa katika mapambano dhidi ya tawala za kikoloni.” 

Hapa, ninanukuu kauli ya Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, aliyoitoa wakati wa mazishi ya Rais mstaafu, Nelson Mandela alipokuwa anamkaribisha Rais Kikwete wa Tanzania, kutoa rambirambi za nchi yake. Na haya matusi yanakera mno tunapozingatia kuwa wakati Watanzania walipokuwa wanasimanisha maendeleo yao na wanajeshi wao walipokuwa wanapoteza maisha katika nyanja mbalimbali za vita vya ukombozi wa Afrika, serikali huru za Kenya na serikali za kibaguzi za makaburu wa Afrika Kusini zilikuwa zimekumbatiana kibiashara; marejeo yafanywe kwenye Maktaba ya Congress ya Marekani

Tanzania isikubali kuvuruga misingi ya amani kwa sababu yoyote ile; sembuse juhudi za kuunda shirikisho na serikali ambazo sifa yake kubwa ni usaliti – hususani serikali huru za Kenya: ambazo zimesaliti wapigania uhuru wao wa Mau Mau; Serikali zilizopiga marufuku kwa muda wa miaka 40 Chama Cha Siasa kilichopigania uhuru wa nchi – Mau Mau.

Fauka ya hili, kwa kudiriki kufanya biashara na serikali za kibaguzi za Makaburu, zilisaliti juhudi ya ukombozi wa Afrika, na kwa mwendelezo juhudi za kuunda umoja wa Afrika – kwani hatuwezi kuungana wakati bado tunatawaliwa.

Mandela alipofunguliwa aliuomba ulimwengu usilegeze vikwazo vya uchumi dhidi ya nchi yake hadi hapo ubaguzi wa “apartheid” utakapotanguliwa. Lakini Kenya ilisaliti ombi hilo kwa kuruhusu ndege za shirika la ndege la Afrika Kusini kutua Nairobi.

Imani ya kuunda shirikisho na serikali hizi inatoka wapi? Ni matumaini ya bahati ya kuwa Kenya labda itakuwa tofauti kesho na keshokutwa? Nchi haziendeshwi kwa mahesabu ya matumaini ya bahati mzuri eti! 

Kadhalika hizo Serikali za Uganda, Burundi na Rwanda nazo pia ni saliti; kwani kuulea mfumo unaoruhusu wachache kuhatamia ardhi na kuwaacha walio wengi mikono mitupu huwa ni kitendo cha kuwasaliti hawa walio wengi nchini. Haya matusi ya kukokota miguu, yanakera zaidi, tukizingatia kuwa Mwalimu Nyerere aliwahi kuwasihi viongozi wenzake kuhusu umuhimu wa kuunda Shirikisho mara baada ya uhuru miaka ya 1960 na kwamba yeye alikuwa ridhaa kuchukua nafasi yoyote ya chini kwenye Serikali ya Shirikisho, (the Federal hierarchy) kwa maana ya kwamba: Rais aidha atoke Kenya na Makamu awe kutoka Uganda au kinyume chake; yeye atachukuwa nafasi nyingine yoyote baada ya hizi mbili kuzibwa, ili mradi shirikisho liundwe. 

Lakini Mzee Jomo Kenyatta wa Kenya na Dk. Milton Obote wa Uganda walikataa; ni nchi zipi hapa zilaumiwe katika kukokota miguu kwenye kuunda shirikisho?

Mwaka 1967, badala ya Shirikisho tukaishia kwenye Jumuiya ambayo (kwa matakwa ya Wakenya na Waganda) ilitupilia mbali masuala ya ardhi na uraia. Hata hivyo ilikuwa ni Jumuiya mathubuti na yenye tija kwa wananchi wa Afrika Mashariki; tena lilikuwa Jumuiya ya kwanza kwa ubora duniani; lakini maslahi binafsi ya wachache yaliua Jumuiya hiyo.

Itasaidia iwapo watu wa Afrika Mashariki hatutajifanya wenye kumbukumbu fupi. Jumuiya ya kwanza iliuawa na wawekezaji wa nje kupitia Kenya, waliohofu kuimarika kwa Ujamaa, kupitia Azimio la Arusha la Tanzania na Chata ya Kabwera “Common Man’s Charter” ambayo ilikuwa ndio azimio la Ujamaa la Uganda lilioanzishwa na Dkt.  Milton Obote na Idi Amin Dada alikuwa mbioni kulifufua.

Kadhalika itakuwa ni vema kama hatutakuwa tunasahau kwamba tangazo la kuvunja Jumuiya mwaka 1977 lilitolewa wakati ndege karibu zote za Shirika la Ndege la Afrika Mashariki zilikuwa zipo nchini Kenya na zikabaki huko; na si hilo tu bali vyombo vya habari Kenya vilipiga vigelegele na vifijo; bila kuzitaja tafrija “Champagne Parties” zilizohudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu Serikalini huko Kenya katika kusherehekea kifo cha Jumuiya. Hii maana yake ni nini? Ni kuwa tukio zima halikuwa ni ajali; bali lilikusudiwa, lilipangwa na kutekelezwa kwa weledi.

Miaka 30 baadae, wawekezaji wale wale wa nje kupitia magazeti na viongozi wale wale wa Kenya walikuwa ndio masogora wa kushabikia ufufuaji wa shirikisho; je, ufufuzi huu leo ni kwa manufaa ya nani? Jibu ni kwa manufaa ya hao wapiga debe wenyewe, ndiyo sababu mradi mzima umesukwa kukidhi matakwa ya nje zaidi kuliko ya ndani (external rather than internal integration); na “Treaty” ya Afrika Mashariki yenyewe ndio shahidi azizi. Ninahisi, viongozi wetu Tanzania wameisoma hii “Treaty” kijuujuu sana kama wameisoma. 

     Ninapenda kusisitiza mambo machache fauatayo: kwanza, Afrika Mashariki aihitaji shirkisho, bali Jumuiya ya kiuchumi ya 1967-1977; na kuipata hiyo inabidi kutaifisha mashirika yote ya ndege, reli, bandari, posta na simu na kuweka katika mikono ya serikali za Afrika Mashariki kwa manufaa ya wananchi wa Afrika Mashariki. Wawekezaji wa nje wasiingizwe kabisa kwenye miradi hii. Hiyo ndio mikakati ya kuinua uchumi wa jimbo hili, hatuhitaji Jumuiya inayoruhusu raia kufungua viduka vya mkono kwenye nchi jirani; wakati njia kuu za uchumi zimo mikononi mwa waja wanaoendeleza unyonyaji wa jimbo letu pengine kupita hata nyakati za ukoloni.

Pili, hakuna suala au “element/aspect” yoyote ya ushirikiano wa msingi wa Afrika Mashariki ambao hauwezi kutekelezeka kwa sababu tu eti hatuna kitu kinachoitwa Shirikisho. Hakuna. Madhumuni ya ushirikiano ni kuimarisha uchumi ili kuboresha maisha ya wananchi na wala si kujenga himaya. Wakati wa ujenzi wa himaya umepita, (viongozi wasipoteze muda wao kwenye hilo) na hii ndiyo sababu ulimwengu unashuhudia mfumuko (proliferation) wa mataifa (nation-states) duniani, pamoja na propaganda zinazoenezwa kwa gharama kubwa na mataifa ya viwanda na taasisi zao kama Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) za kufagilia ulaghai wa kitu kinachoitwa “globalization”; na bado hiyo globalization wala haijaua utaifa popote duniani. Sasa Watanzania tunapotetea ustaarabu wetu, watu waliouza kila walichokuwanacho wanataka kutuzuga; kutufanya maafkani yaani hatuna akili timamu; “… Kwa nini tunashindwa kuona ubora wa Shirikisho?” Jibu ni kwa sababu ubora wenyewe haupo au ni hafifu mno iwapo upo.    

Kadhalika, kudai kuwa Afrika Mashariki ushirikiano wao hauwezi kuwa kamili bila kuwepo shirikiso ni umbembe na utapeli usio na aibu. Jumuiya ya Afrika Mashariki ya 1967-1977 ilikamilika na kujitosheleza kiasi cha kwamba hadi leo hakuna Jumuiya yoyote duniani ambayo inaisadifu ile kwa ubora. Hata Umoja wa Ulaya (European Union) hivi sasa wala haiifikii Jumuiya ile. Jumuiya ya 1967/77 si tu ilikuwa na sera za pamoja, bali (assets) mali za pamoja: shirika la ndege, reli, bandari, posta & simu na mengine mengi lakini kulikuwa hakuna shirikisho, pasipoti ya pamoja au hicho kinachoitwa, “land sharing”.  Ulazima wa vitu hivi leo unatokea wapi?

Bado kuna Viongozi Afrika Mashariki wanaosema eti sisi tujifunze na yanayojiri kwenye Umoja wa Ulaya (European Union)! watu hawa wanaishi katika sayari gani? Kwa taarifa yao basi, Umoja wa Ulaya wanajaribu kunukuru kutoka kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kwanza ya 1967 hadi 1977; tusijifedheheshe.

Suala la kulizingatia hapa ni kuwa mataifa ya nje kama Uingereza, Ujerumani, Uholanzi, Italia na Marekani pamoja na taasisi zao – Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF), zenye kuwekeza Afrika Mashariki, hasa Kenya, zitawashinikiza Watanzania waingie kwenye mtego wa shirikisho; lakini lengo halitakuwa ni kuendeleza maslahi ya Watanzania au wananchi wa Afrika Mashariki. Bali maslahi yao binafsi. Hizi ndizo nchi zinazohatamia ardhi huko Kenya, Uganda na kwingineko na kusababisha uhaba wa ardhi unaoleta vita za mara kwa mara, wala si kudura ya mungu.

Watanzania kusijifanye wataaradhi wa kutatua migogoro ya Afrika Mashariki kwa kutoa ardhi yetu, kwani matokeo yake yatakuwa ni kujenga amani ya watu wengine kwa kubomoa amani yetu wenyewe. Waswahili wanauita huo ukarimu wa mshumaa, unaowaangazia wengine wakati wenyewe unateketea. 

Wenzetu walipodhani hawakuwa na matatizo ya ardhi miaka ya 1960 hawakutaka kusikia mambo ya kuunda Shirikisho; leo, ukweli wa mficha maradhi kifo humumbua, hawa wameumbuliwa halafu, wanajifanya eti ndiyo wapenzi wakubwa wa Shirikisho! Kwanza, shirikisho la Afrika Mashariki limepitwa na wakati; pili sababu za kufufua shirikisho hilo hazijitegemei, hivyo si msingi imara wa kujenga hilo jengo. Afrika Mashariki inahitaji ushirikiano wa kiuchumi wa 1967 hadi 1977, si shirikisho hili.

 

Harid Mkali ni mtunzi wa vitabu na mwandishi wa habari. Mkazi wa London, Uingereza. Anapatikana kupitia simu namba: +447979881555; barua pepe: [email protected]  na tovuti:  www.haridmkali.com

By Jamhuri