MAONI YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA SHERIA NA KATIBA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU KUHUSU
MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA, YA MWAKA 2013

(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)

 

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,

Huu ni Muswada wa marekebisho ya pili ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Sheria za Tanzania. Kama Bunge lako tukufu litakavyokumbuka, Sheria hii ilifanyiwa marekebisho ya kwanza kwa kupitishwa kwa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Na. 2 ya mwaka 2012, mwezi Februari ya mwaka jana. Mabadiliko hayo ya kwanza yalihusu Sehemu ya Tatu na ya Nne ya Sheria hii, na yalilenga vifungu mbali mbali vinavyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba na utekelezaji wa majukumu yake.

Muswada huu wa sasa unalenga kufanya marekebisho katika Sehemu ya Tano ya Sheria inayohusu ‘Kuitisha Bunge Maalum.’ Sambamba na mapendekezo haya, kuna mapendekezo ya kufanya marekebisho katika Sehemu ya Sita kwa kufuta vifungu vya 32 hadi 36 vya Sheria vinavyohusu utaratibu wa kura ya maoni kwa ajili ya kuhalalisha ‘Katiba Inayopendekezwa.’ Marekebisho haya yamewekwa katika aya ya 57 ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni, 2013. Mapendekezo ya Muswada huu ni muhimu lakini yana utata mkubwa.

Mheshimiwa Spika,

 

Katika kutekeleza majukumu yake ya kuuchambua Muswada huu, Kamati ya Bunge lako tukufu ya Katiba, Sheria na Utawala ilikutana na wadau wengi mbali mbali. Hivyo, kwa mfano, Kamati ilipata maoni ya taasisi za kidini na za kiraia; taasisi za elimu ya juu na za kitaaluma; vyama vya siasa na asasi nyingine. Kwa sababu ambazo Kamati haikuelezwa vizuri na uongozi wa Bunge hili tukufu, mapendekezo ya Kamati kwenda Zanzibar kwa lengo la kukusanya maoni ya wadau wa Zanzibar juu ya Muswada huu muhimu kwa mustakbala wa Jamhuri ya Muungano yalikataliwa.

Kwa maana hiyo, ni muhimu Bunge lako tukufu lifahamu ukweli huu kwamba wadau pekee walioshirikishwa kutoa maoni yao juu ya Muswada ni Watanzania Bara tu. Wazanzibari hawakupatiwa fursa hiyo na hawakushirikishwa kabisa, licha ya Sheria yenyewe kuwa na mambo mengi yanayoihusu Zanzibar. Kwa vile wadau wa Zanzibar walishirikishwa kikamilifu kutoa maoni yao kuhusu Muswada uliopelekea Sheria hii kutungwa mwaka 2011, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni kwa nini uongozi wa Bunge na wa Serikali umeona si busara na sahihi kuwapatia Wazanzibari fursa ya kutoa maoni yao kuhusu Muswada huu wa kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inawahusu pia Wazanzibari na nchi yao.

 

URAIS WA KIFALME KWA MARA NYINGINE TENA!!!!

Mheshimiwa Spika,

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepigia kelele jitihada za serikali hii ya CCM kudhibiti mchakato wa Katiba Mpya kwa kuendeleza kile tulichokiita miaka miwili iliyopita, “… kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.” Hapo tulikuwa tunazungumzia mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wajumbe na watendaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na tulisema kwamba mamlaka hayo yalikuwa na lengo moja tu: “kuhakikisha kwamba matokeo ya kazi ya Tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa na Rais na Serikali yake na chama chake cha CCM.”

 

Mheshimiwa Spika,

Katika Maoni yetu wakati wa kutungwa kwa Sheria hii mwezi Novemba mwaka 2011, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipinga vikali mapendekezo ya kumwezesha Rais kuteua Wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Bunge lako tukufu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Tulisema yafuatayo kuhusiana na jambo hili: “… wajumbe … wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba kwa mujibu wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi kuwa, wawakilishi wa wananchi. Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala taasisi zao kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada Mpya unapendekeza wateuliwe na Rais.”

Kwa sababu ya upinzani huo, mapendekezo ya kumfanya Rais kuwa mteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum wasiokuwa wabunge na Wawakilishi yaliondolewa katika Muswada huo wa Sheria hii. Badala yake, kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria iliyotungwa na Bunge lako tukufu kiliweka wazi kwamba “wajumbe mia moja sitini na sita [watateuliwa] kutoka …” taasisi zilizotajwa katika kifungu hicho.

Mheshimiwa Spika,

Ni kweli kwamba kifungu cha 22(1)(c) kama kilivyotungwa kilileta giza badala ya mwanga katika suala la uteuzi wa wajumbe hao. Kama tulivyoieleza timu ya wataalamu wa Serikali kufuatia mkutano wetu na Rais Jakaya Kikwete uliofanyika Ikulu tarehe 26 Novemba, 2011: “Toleo la Kiswahili la Sheria linasema kwamba wawakilishi wa makundi mengine ‘watakaoteuliwa kutoka’ kwenye makundi yaliyoorodheshwa. Toleo la Kiingereza linasema wajumbe hao watakuwa ‘drawn from’ (kwa tafsiri ya Kiswahili ‘watachukuliwa kutoka’). Maana za maneno haya hazifanani na wala hayako wazi kuhusu nani ‘atakayewateua’ au ‘kuwachukua’ wajumbe hao kutoka kwenye taasisi zao.”

Kwingineko katika mkutano wetu na Rais Kikwete tulimweleza kwamba: “Wajumbe 166 wengine wanaowakilisha taasisi nje ya Wabunge na Wawakilishi hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala na taasisi zao kwani Sheria haisemi ni nani atakayewateua na/au kuwachagua.” Kwa sababu hiyo, tulipendekeza kwamba “Sheria iweke wazi kwamba wajumbe hawa ‘watateuliwa na’ taasisi zilizotajwa. Hii itaondoa utata juu ya uwakilishi wao na juu ya mamlaka yao ya uteuzi.”

 

Mheshimiwa Spika,

Mapendekezo ya marekebisho yaliyoko kwenye Muswada huu yanaonyesha wazi kwamba ushauri wetu kwa Rais Kikwete na kwa timu yake ya watalaamu umepuuzwa. Badala yake, serikali hii sikivu ya CCM imeamua kuturudisha nyuma kwa zaidi ya miaka miwili kwa kuibua tena pendekezo la kumfanya Rais kuwa mteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Wabunge au Wawakilishi wa Zanzibar. Hii ni kwa sababu aya ya 3 ya Muswada inapendekeza kwamba wajumbe hao sasa wateuliwe Rais. Hiyo ni sawa na kusema kwamba kilichokuwa hakifai miaka miwili iliyopita sasa kinafaa; na kilichokataliwa wakati ule sasa kinakubalika!

Ili kuficha ukweli kwamba mwenye mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum wasiokuwa Wabunge au Wawakilishi ni Rais, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Muswada unapendekeza kuongezwa kwa vifungu vidogo vipya viwili katika kifungu cha 22. Kwanza, inapendekezwa kuwe na kifungu kidogo cha (2A) ambacho kitamruhusu Rais kualika kila kundi lilioainishwa katika kifungu kidogo cha 1(c) “kuwasilisha kwake orodha ya majina ya watu wasiozidi watatu ili kuteuliwa kuwa wajumbe.” Pili, inapendekezwa kuwe na kifungu kidogo cha (2B) kitakachomlazimu Rais kuzingatia sifa na uzoefu wa watu waliopendekezwa, na usawa wa jinsia wakati wa kufanya uteuzi wa wajumbe hao.

 

Mheshimiwa Spika,

Mapendekezo ya kumpa Rais mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalum hayakubaliki na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliomba Bunge lako tukufu lisiyapitishe kuwa Sheria. Kwanza, mapendekezo haya yanarudisha dhana kwamba wajumbe hawa watakuwa watu wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM. Rais Kikwete na chama anachokiongoza ni wadau wakubwa wa mchakato wa Katiba Mpya na wana maslahi halisi na makubwa ya kuhakikisha kwamba matakwa ya chama chao ndio yanakuwa Katiba Mpya ya nchi yetu.

Ushahidi wa maslahi haya ya CCM ni kile kinachoitwa Ufafanuzi Kuhusu Rasimu ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wanachama na Viongozi wa CCM uliotolewa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM tarehe 10 Juni, 2013. Katika Ufafanuzi huo, CCM imekataa mapendekezo yote muhimu yaliyoko kwenye Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume. Needless to say, Rais Kikwete ni Mwenyekiti wa vikao vyote vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Kumpa Rais, na Mwenyekiti wa CCM Taifa, mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalum litakaloijadili – na kuikubali au kuikataa – Rasimu ya Katiba ambayo chama chake kimekwishaikataa ni sawa na kuipa CCM fursa nyingine ya kujaza Bunge hilo na makada wake kwa lengo la kutekeleza matakwa ya chama hicho.

Pili, hata bila wajumbe hawa kuteuliwa kwa namna inayopendekezwa, tayari CCM peke yake ina zaidi ya 72% ya wajumbe wote wa Bunge Maalum wanaotokana na Wabunge na Wawakilishi. Kumpa Mwenyekiti wa CCM mamlaka ya kuteua wajumbe wengine zaidi, kama inavyopendekezwa katika Muswada huu, ni kutoa mwanya kwa CCM kutumia kivuli cha makundi ya kiraia, taasisi za kidini na makundi mengine ili kujiongezea wajumbe wengine zaidi, na hivyo kuhakikisha kwamba Bunge Maalum litatekekeleza matakwa ya kuendeleza status quo.

 

Kwa maneno mengine, Serikali hii ya CCM na Wabunge wake inataka Mwenyekiti wao wa Taifa ayachagulie makanisa na awachagulie Wakristo wawakilishi wao katika Bunge Maalum; awachagulie Waislamu wa BAKWATA, Baraza Kuu, JUMAZA na taasisi nyingine za Kiislamu wawakilishi wao katika Bunge hilo; avichagulie vyama vya siasa vinavyoipinga CCM wawakilishi wao; awachagulie wafanyakazi, wakulima, wafugaji, wahadhiri, wanafunzi, wafanyabiashara, walemavu na makundi mengine ya kijamii wawakilishi wao katika Bunge Maalum! Kama ni hivyo, hilo halitakuwa Bunge Maalum la Watanzania, bali litakuwa Bunge Maalum la CCM na Mwenyekiti wao. Hili halikubaliki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na, tunaamini, halitakubalika kwa wananchi wa Tanzania katika ujumla wao.

 

Tatu, kwa jinsi yalivyo kwa sasa, mapendekezo haya hayawezi kutekeleza matakwa ya kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria kinachotaka wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na wabunge au wawakilishi kuwa mia moja sitini na sita. Hii ni kwa sababu, hata kama watu wote waliopendekezwa na makundi yaliyoainishwa na kifungu hicho watateuliwa kuwa wajumbe, bado idadi yao itakuwa wajumbe ishirini na saba kwa kuwa makundi yenyewe yako tisa tu! Muswada uko kimya juu ya wajumbe wengine mia moja thelathini na tisa watatoka wapi na watateuliwa na nani na kwa utaratibu upi.

 

Kuna hoja kwamba utaratibu wa uteuzi wa wajumbe unaopendekezwa na Muswada unafanana na uteuzi wa wajumbe wa Tume ulioko kwenye kifungu cha 6(6) cha Sheria ambapo Rais alialika vyama vya siasa, jumuiya za kidini, asasi za kiraia, n.k., kuwasilisha orodha ya majina ya watu ili kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume. Hoja hii sio sahihi. Kwanza, Tume ya Katiba sio sawa na Bunge Maalum. Tume ni chombo cha kitaalamu chenye majukumu ya kitaalamu ya kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti pamoja na Rasimu ya Katiba. Uhalali wa Tume unatokana na utaalamu wa wajumbe wake na weledi katika kutekeleza majukumu yao ya kitaalamu.

 

Kwa upande mwingine, Bunge Maalum ni chombo cha uwakilishi ambacho wajumbe wake wana majukumu ya kisiasa ya kuwakilisha wananchi wa makundi mbali mbali kwenye kazi ya kisiasa ya kuandika Katiba Mpya. Uhalali wa Bunge Maalum unatokana na upana na ubora wa uwakilishi wake wa makundi mbali mbali ya kisiasa na kijamii. Chombo cha uwakilishi cha aina hii lazima kitokane na wananchi na/au makundi ya kijamii kinachoyawakilisha ili kiwe na uhalali wa kisiasa. Dhana ya Rais – na Mwenyekiti wa CCM – kuteua Wajumbe wa Bunge Maalum inavuruga au kuondoa kabisa dhana ya uwakilishi wa wananchi na uhalali wa kisiasa katika mchakato wa Katiba Mpya.

By Jamhuri