Benki ya dunia imetangaza inasitisha mikopo mipya kwa Uganda kutokana na nchi hiyo kupitisha sheria kali dhidi ya watu wa jinsia moja walio katika mahusiano ya kimapenzi.

Benki hiyo ilisema sheria hiyo inayoharamisha LGBTQ iliyopitishwa miezi michache iliyopita inakwenda kinyume na misingi na maadili ya benki ya dunia ambayo haibagui yeyote kwa misingi ya jinsia, jinsi au rangi yake katika azma yake ya kutokomeza umasikini duniani.

Tangu kupitishwa kwa sheria hiyo inayotoa adhabu kali kwa wana LGBTQ, nchi kadhaa ikiwemo Marekani na Umoja wa Mataifa umelaani utawala wa Uganda kwa kuridhia kupitishwa kwa sheria hiyo.

Sheria ambayo Rais Yoweri Museveni alitia saini Mei 29 ina kifungu cha hukumu ya kifo kwa “mapenzi ya jinsi moja yaliyokithiri.”

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Benki ya Dunia mwaka 2020 inabainisha kuwa “imetoa zaidi ya dola bilioni 10 katika ufadhili” kwa Uganda tangu 1963.

Kampeni ya Haki za Kibinadamu na Baraza la Usawa wa Kimataifa ni miongoni mwa mashirika zaidi ya 100 ya utetezi ambayo yameitaka Benki ya Dunia kusitisha mikopo kwa Uganda.

Takriban wanachama kumi na wawili wa Congress wiki iliyopita walisisitiza matakwa haya katika barua waliyotuma kwa Rais wa Benki ya Dunia Ajay Banga.

Wizara ya Mambo ya Nje mwezi Juni ilitangaza kuwa Marekani ilikuwaimeweka vikwazo vya hati za kusafiria (viza), dhidi ya maafisa wa Uganda.

Uganda imekuwa na msimamo mkali na wa wazi dhidi ya mapenzi ya jinsi moja, ikiyataja mapenzi ya jinsi moja kama kinyume na maadili ya utamaduni wa Uganda.

By Jamhuri