Shirika la Afya Duniani (WHO) hivi karibuni limeripoti – mwanandoa mmoja kati ya sita duniani ana tatizo la ugumba. Kwa miaka mingi watu wamekuwa wakielekeza lawama zao kwa wanawake linapokuja swala kukosa mtoto katika ndoa – hasa katika nchi za Kiafrika.

Lakini sasa inajulikana kuwa utasa kwa wanaume huchangia karibu 50% ya kesi zote. Na wanaume duniani kote – Afrika ikiwemo – wanakabiliwa na tatizo la kupungua kwa idadi na ubora wa mbegu.

Kuna sababu nyingi za utasa wa kiume. Hata hivyo, ni wazi kwamba uchafuzi wa mazingira una mchango mkubwa katika kupungua kwa uzazi duniani kote. Wasiwasi unaongezeka kuhusu kemikali zinazopatikana katika bidhaa binafsi kama sabuni, shampuu na dawa za kunyunyuzia nywele, na vile vile vifungashio vya chakula, chupa za maji na vitu vingine.

Vichafuzi vingine vinaonyesha dalili za kuingia kwenye mnyororo wetu wa chakula ni kemikali za kuulia wadudu na dawa. Utafiti wa hivi karibuni katika maabara uligundua athari katika mazingira ya baharini, na pia katika mito na maeneo ya kilimo.

Utafiti unaeleza, “uchafuzi huu unatia wasiwasi” unaweza kuchangia tatizo la utasa kwa wanaume.

Utafiti unaeleza madhara ya vichafuzi kama vile dawa na viua wadudu katika uzazi wa wanaume. Kemikali zinaweza kuathiri uzazi kwa wanaume kwa kuingia katika ubongo au kuingia kwenye viungo vya uzazi kama vile korodani. Umma unatakiwa kufahamu madhara ya uchafuzi wa mazingira kwa uzazi.

Mambo ya kuyafahamu

Ugumba ni ugonjwa wa mfumo wa uzazi wa mwanaume au mwanamke unaokuja kwa kukosekana kupatikana ujauzito baada ya miezi 12 au zaidi baada ya kujamiiana mara kwa mara bila kinga.

Ugumba huathiri mamilioni ya watu – na una athari kwa familia na jamii zao. Makadirio yanaonyesha kuwa takriban mtu mmoja kati ya watu sita walio katika umri wa uzazi duniani kote hupata ugumba katika maisha yao.

Katika mfumo wa uzazi wa mwanamume, ugumba husababishwa zaidi na matatizo katika utoaji wa shahawa, kutokuwepo au viwango vya chini vya manii, au umbo lisilo la kawaida la manii.

Katika mfumo wa uzazi wa mwanamke, utasa unaweza kusababishwa na aina mbalimbali za kasoro za yai, mvuko, mirija ya uzazi, miongoni mwa mambo mengine.

Ugumba upo wa aina mbili. Ugumba wa awali ni wakati mimba haijawahi kupatikana na mtu, na ugumba wa pili ni wakati angalau mimba moja ya awali imepatikana.

Utunzaji wa kizazi unajumuisha kuzuia, utambuzi na matibabu ya utasa. Upatikanaji wa huduma ya uzazi bado ni changamoto katika nchi nyingi; hasa katika nchi za kipato cha chini na kati. Utunzaji wa uzazi haupewi kipaumbele katika vifurushi vya kitaifa vya bima ya afya kwa wote.

Athari kwa wanaume

fd
Maelezo ya picha, Utafiti unaeleza kwamba kwa wanyama wote, ikiwa ni pamoja na wanadamu, uchafuzi wa mazingira huingilia utendaji wa homoni.

Utafiti unaeleza kwamba kwa wanyama wote, ikiwa ni pamoja na wanadamu, uchafuzi wa mazingira huingilia utendaji wa homoni.

Kizuizi kinacholinda manii. Mara tu uchafu hasa kemikali zinapovuka kizuizi hicho, huhamia kwenye sehemu za korodani ambapo manii huzalishwa na inaweza kuingiliana na seli zinazohusika katika uzalishaji wa manii. Seli hizi pia zina jukumu muhimu katika kudhibiti utengenezaji wa homoni. Vichafuzi vinaweza kuharibu seli hizi moja kwa moja au kuingilia utendaji wao.

Vichafuzi hivyo pia vinaweza kuharibu moja kwa moja vinasaba katika chembechembe za mbegu za kiume, na kusababisha mabadiliko ya kijeni ambayo yanaweza kuathiri ubora wa mbegu za kiume na uwezo wa kurutubisha yai. Hii inaweza kusababisha utasa au kuhatarisha afya ya watoto.

Njia za kujilinda

Uchafuzi unaotokea kwenye udongo, maji na hewa huonekana. Hatua za udhibiti ni pamoja na kupunguza matumizi ya baadhi ya viuatilifu au dawa, na kubuni njia mbadala salama. Kuna hatua za ulinzi za kibinafsi za kuchukua, kama vile kutumia vichungi vya hewa na maji, na kupunguza matumizi ya bidhaa za plastiki ambazo zinaweza kuwa na uchafu.

Kampeni za afya kwa umma zinaweza kuongeza ufahamu kuhusu hatari za kuambukizwa, au uundaji wa teknolojia mpya ambazo zinaweza kutambua na kuhesabu uchafu katika mazingira kwa usahihi zaidi.

Watu, hasa wanaume, wanapaswa kufahamishwa kuhusu ongezeko la utasa wa kiume na jinsi ya kuboresha afya zao wenyewe na kuepuka kuathiriwa na vichafuzi ambavyo vinaweza kupunguza nafasi zao za kuwa baba.

Makala haya kwa msaada wa mtandao wa BBC Swahili

By Jamhuri