Wiki iliyopita, Mkutano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulikuwa na vibweka na vimbwanga vingi vyenye kuacha kinywa wazi kwa mshangao na hamaki kwa mtu yeyote makini mwenye kuujali mustakabali mwema wa nchi yake.

Hata hivyo, pamoja na vibweka na vimbwanga vilivyotokea kwenye kikao hicho, ukweli unabaki kuwa kilikuwa kikao chenye moja ya miswada muhimu yenye kipekee unaokwenda kuweka jiwe jipya la msingi kwa Tanzania tunayoihitaji kuijenga kwa miaka 50, au hata 100 ijayo.

Mjadala wa Septemba 4 na 5, mwaka huu, ulihusu muswada wa marekebisho ya rasimu ya Katiba mpya. Mjadala huu ulipaswa kupata umuhimu wa kipekee na kuwaondoa wabunge kutoka kwenye vivuli vya kofia na majoho ya vyama vyao, na kuufanya kuwa mjadala usiokuwa na itikadi wala ushabiki wa kivyama maana ni mjadala unaobeba mapigo ya moyo ya Taifa lenye idadi kubwa ya watu wasio wapenzi, wanachama wala mashabiki wa chama chochote cha siasa.

 

Ulipaswa kuwa mjadala wenye maono na mapenzi makubwa kwa Tanzania na vizazi vyake vijavyo bila kujali maslahi ya muda mfupi yasiyo na tija kwa vizazi hivyo.

Kilichotokea kwenye mjadala huo ni ‘msiba’ na maafa yasiyoelezeka kwa Taifa lenye nia ya dhati ya kuweka msingi imara na mwafaka wa kitaifa kupitia Katiba mpya. Lakini pia yaliyotokea yanadhihirisha kuwa kuna waheshimiwa wamepewa dhamana na wananchi ya kwenda kuwasemea na kuwatetea, lakini wao wanasema yao yenye maslahi yao kama kakikundi ka watu huku maslahi mapana ya wananchi yakiachwa ufukweni yakielea na kupigwa na mawimbi ya usaliti.

Mtikisiko ulianzia Septemba 4 kwenye kikao cha jioni baada ya wabunge wote wa kambi ya upinzani (Chadema, CUF, na NCCR-Mageuzi) isipokuwa Augustine Mrema wa TLP, kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge kutokana na kutoridhishwa na namna Naibu Spika, Job Ndugai, alivyokuwa akiwatendea wabunge wa kambi hiyo, kutokana na kutokupata majibu ya kuridhisha kwenye hoja zao za miongozo ambazo kimsingi zilikuwa zimebeba mzizi wa mjadala husika.

Walipotoka wabunge wa kambi ya upinzani unaweza kutafsiri kuwa walitoka na akili zilizokuwa na hoja za mjadala ule.

Wabunge karibu wote wa chama tawala waliokuwa ukumbini kila aliyepata nafasi ya kuchangia, badala ya kuchangia hoja muhimu iliyoko kwenye mjadala, wao walielekeza mashambulizi na hoja zao za nguvu kwa kambi ya upinzani iliyokuwa nje ya ukumbi wa mjadala na nje ya muswada wa marekebisho ya Katiba ya mpya.

 

Hayo yalifafanyika huku Naibu Spika akiwa kimya kana kwamba mjadala uliwahusu wabunge waliotoka, au kana kwamba aliamua kuhalalisha wabunge walioko ndani ya ukumbi waruhusu akili zao juu ya mjadala, zitoke nje ya ukumbi ziambatane na kambi ya upinzani na wao wabaki na akili za kuwashambulia wenzao, badala ya kushambulia mjadala kwa hoja ili kukidhi matakwa na matarajio ya wananchi juu ya suala muhimu la Katiba mpya.

 

Siku iliyofuata ikawa zaidi ya jana yake. Hii ilikuwa baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, kusimama na kuomba mwongozo kama kanuni zinavyohitaji, lakini alinyimwa na kuambiwa akae chini. Huku Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema, akitakiwa asimame achangie, Mbowe alisema:  “Mheshimiwa Naibu Spika, nina hoja naomba nisikilizwe.”

 

Kama kawaida, Naibu Spika ‘akatunisha msuli’ na kuwataka askari wajiandae ili waingie kumtoa. Baada ya Mbowe kugoma kutolewa na askari hao ikawa ni vuta nikuvute kati ya askari na Joseph Mbilinyi  aliyekuwa akipinga askari kutumia nguvu kumtoa kiongozi wa upinzani. Kilichotokea wote tunakijua.

Mbowe alipoamua kutoka mwenyewe wabunge wa kambi ya upinzani wote bila kujali itikadi zao na vyama vyao wakaamua kutoka nje, na ukumbini wakabaki wabunge wa chama tawala pamoja na Mrema anayejinasibu kuwa si kibaraka wa CCM. Kilichotokea kwa wachangiaji walioanza kuchangia mjadala ule ni aibu kwa chama tawala, wabunge na wananchi waliowachagua wabunge hao.

 

Wengi, kama kawaida, hawakugusa yaliyo ya msingi kwenye mjadala uliohusu marekebisho ya muswada wa Katiba. Walianza kuwashambulia wabunge wa upinzani waliotoka nje, hasa wa Chadema. Mfano, mbunge wa Nzega alienda mbali zaidi na kuanza kuzungumzia maisha binafsi ya kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani na mkewe, mpaka muda wake unakwisha hakuwa amechangia chochote chenye mashiko kilichohusu mjadala husika.

 

Akiwa ‘anatapika nyongo’ zake, Naibu Spika alionekana kufurahia kana kwamba ndiyo alikuwa anaongea hoja zilizo kwenye mjadala.

Kauli ya kusikitisha na yenye majonzi ilitoka kwenye kinywa cha Mbunge Lusinde. Alisema; “Tanzania haihitaji Katiba mpya, bali wananchi wanahitaji barabara, maji na zahanati.” Huyu unaweza kujiuliza kuwa kauli hizi katumwa na nani wakati wananchi wengi kwa umoja wao sasa wanajadili Katiba mpya wanayotaka iwe bora itakayoweka misingi bora kwa nchi yao!

 

Aliyepaswa kumsahihisha Lusinde alitakiwa kuwa Kapteni Komba alipopata nafasi ya kuchangia. Lakini alivyoanza kuongea ilibidi nifunge runinga na kuondoka maana ilikuwa ni aibu kusikia maneno ya hovyo kutoka kwake.

Kwa muhtasari, kama tukipima hoja za wabunge hao na wenzao wengine waliochangia, tunaweza kuwa na hitimisho kuwa kupatikana Katiba mpya kutakuwa kwenye jasho jingi kutokana na baadhi ya wabunge wa chama tawala wasiojua kuwa Watanzania wanataka nini, lakini Bunge lijalo la Katiba litakuwa na mvutano mkubwa kwa kuwa hakuna busara ya kusiliza hoja za wachache na kuzipa nafasi kama jinsi inavyokuwa sawa kwa wengi kuburuza wachache.


By Jamhuri