Siku ya Ijumaa Novemba 5, mwaka huu 2021, katika Hoteli ya Golden Tulip, Kiembe Samaki, Zanzibar, kulifanyika kumbukizi ya maisha ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, marehemu Maalim Seif Sharif Hamad (Allaah Mtukufu Amrehemu) na kuzindua taasisi ya kumuenzi, uzinduzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, na kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Daktari Hussein Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, kwa kuwataja wachache.

Awali ya yote, tunayo sharafu kubwa kuwapa kongole wale waliofikiria kumuenzi kiongozi huyu wa mfano marehemu Maalim Seif Sharif Hamad (Allaah Mtukufu Amrehemu) kwa kuunda taasisi ya kumuenzi – Maalim Seif Foundation, kwa kushirikiana na taasisi ya Kijerumani – Friedrick Naumman Foundation for Freedom (FNF). Kwa hakika wamefanya jambo adhimu.

Pamoja na mjadala wa wanazuoni wa Hadithi juu ya udhaifu katika Hadithi isemayo: “Yakumbukeni (Yatajeni) mema ya wafu wenu.” Hadithi ya Bibi Aisha (Allaah Amridhiye) na nyinginezo ambapo Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amekataza kuwatukana wafu, zinatuelimisha kuwa wafu yatajwe mazuri yao na tusiwaseme vibaya wala tusiwatukane.

Katika kongamano la Kumbukizi ya Maisha ya Marehemu Maalim Seifu Sharifu Hamad, Rais Samia amemtaja marehemu Maalim Seif akisema: “Ni nadra kumpata mtu kama Maalim Seif”.

Kwa nini?

Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ni mwanasiasa aliyepitia changamoto anuai na aliyeonja machungu ya siasa lakini wakati wote alikuwa tayari kuunyoosha mkono wake kwa ajili ya mapatano na maridhiano. Kwa Tanzania na hususan Zanzibar, hauwezi kuutamka msamiati wa amani bila ya kumtaja marehemu Seif Sharif Hamad (Allaah Mtukufu Amrehemu).

Jambo la suluhu na maridhiano ni jambo kubwa sana na kheri kama tunavyosoma kwenye Qur’aan Tukufu, , Sura ya 4 (Surat An-Nisaai), Aya ya 114, kuwa: “Hakuna kheri katika mengi ya wanayoshauriana kwa siri, isipokuwa kwa yule anayeamrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi tutakujampa ujira mkubwa.”

Na ndivyo tulivyomuona marehemu Maalim Seif Sharif Hamad baada ya mengi yaliyopita akitamka hadharani kuwa: “Mheshimiwa Rais, mwisho nitoe wito kwa Wazanzibari wote waliopo ndani na nje ya nchi wakubali kunyoosha na kupokea mkono wa maridhiano.”

Hii ni kauli nzito isiyoweza kutamkwa na mwenye moyo mwepesi, ndiyo maana nilipoandika taazia (Obituary) ya marehemu Maalim Seif Sharif Hamad nilitumia anuani “Buriani, Maalim Seif Sharif Hamad…Ulikuwa tumaini, utabakia mfano.” 

Kwa marehemu Maalim Seif Sharif Hamad nilikuwa nimeakisi mwisho wake mwema akipigania kwa nguvu zake zote maridhiano yanayobeba umoja, mshikamano, udugu na maelewano kwa Wazanzibari na Watanzania, kwa ujumla – Allaah Mtukufu Amrehemu Rehema Kunjufu. 

Nukuu ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, marehemu Maalim Seif Sharif Hamad inaonyesha kwa uwazi kabisa ukubwa wa msiba ugongao nyoyo ulioipata Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kwa kuondokewa na mwana halali wa Zanzibar, Tanzania na Afrika, ambaye wakati wote aliyaweka mbele masilahi ya nchi na watu wake kuliko masilahi yake.

Maalim Seif Sharif Hamad aliyezaliwa kisiwani Pemba Oktoba 22, 1943, na kufariki dunia katika Hospitali ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam Februari 17, mwaka huu 2021 na hatimaye kuzikwa kijijini kwao Mtambwe, Pemba,  Februari 18, 2021, alikuwa kiongozi ambaye maisha yake na hatima yake imebeba mafunzo makubwa kwa anayetaka kujifunza na kuzingatia na hususan utayari, uvumilivu na kusamehe.

Desemba 23, 2020 gazeti hili lilichapisha makala katika safu hii ya ‘Uga wa Kiislamu’ yenye anuani: Sulhu ya Hudaibiyyah na kilichotokea Zanzibar.’ 

Katika makala hiyo kwa niaba ya wadau wa Safu hii ya ‘Uga wa Kiislamu’ tulimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Daktari Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa ukomavu aliouonyesha mapema kabisa aliponyoosha mkono wa udugu na kutaka maridhiano na kutenga nafasi kwa Chama cha ACT-Wazalendo katika serikali yake pamoja na maneno ya faraja katika hotuba zake, na tulimpongeza aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kwa kudhihirisha kwa mara nyingine uungwana wake wa kuweka mbele masilahi ya nchi na wananchi.

Si siri kuwa marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ni mwanasiasa aliyevuka milima na mabonde ya kisiasa na kupata tajriba isiyotiliwa shaka ya maumivu ya kisiasa, lakini pamoja na yote hayo kila alipotafakari na kuzingatia thamani ya amani, udugu, mshikamano na maridhiano alinyoosha haraka mkono wa maridhiano bila ya kujali machungu na changamoto alizopitia na shinikizo la baadhi ya wafuasi wa chama chake waliokuwa tayari ‘liwalo na liwe’.

Wakati wote Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa mwepesi wa kukubali suluhu na maridhiano na kuwa mstari wa mbele kupigania umoja, mshikamano na masilahi ya nchi na watu wake. 

Miongoni mwa mifano ya wazi ya juhudi zake za kuwanasihi Wazanzibari ni usia wake huu ufuatao: “Ndugu zangu, hivi vyama vipo kwa sababu haiwezekani katika nchi watu wote wakawa na fikra sawa. Haiwezekani. Haiwezekani kabisa katika nchi watu wote wakawa wana fikra sawa. Tofauti ya fikra na mawazo itakuwapo lakini si sababu, kwa sababu ya vyama tuhasimiane, tugombane, vyama…vyama ni vitu vya kupita, ndugu zangu, lakini nchi ipo…nchi ipo.”

Maalim Seif Sharif Hamad ametusisitizia umuhimu wa kuweka mbele masilahi ya nchi kuliko masilahi ya vyama vyetu vya siasa ambavyo leo vipo lakini vitapita kama vilivyopita vyama vya TAA, TANU, ASP, HIZBU AL-WATWANY na vinginevyo.

Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa na tabia njema na unyenyekevu na ninakumbuka siku alipofanya ziara Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), aliacha usia muhimu unaopaswa kuwa muongozo wa uhusiano kati ya viongozi wa dini na wanasiasa. Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad alisema: “Mheshimiwa …, Kiongozi wangu, sisi wanasiasa kwenu ni waumini wenu na watoto wenu mnaotulea kiroho. Msitukweze na kutuogopa, tuongozeni. Tuleeni kwa usawa bila ya upendeleo. Tukifanya vyema tuombeeni dua, tupongezeni na tutieni moyo na tukifanya vibaya na hasa pale tunapokuwa katika mizozo, migogoro, hasama na kutoelewana tuiteni, tukosoeni na tupatanisheni.”

Kwa hakika, maneno haya ya marehemu Maalim Seif Sharif Hamad (Allaah Mtukufu Amrehemu) yamekuwa yakijikariri kichwani mwangu juu ya dhima ya viongozi wa dini ya kuwalea waumini wao wanasiasa waliogawanyika katika vyama mbalimbali kwa usawa na kuwaongoza, kuwapongeza, kuwakemea na kuwaonya pale inapostahili.

Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad katika siku za mwishoni mwa uhai wake alitoa ujumbe mzito sana ambao unapaswa  kuzingatiwa pale alipotuusia kuwa: “Sasa ninasema tuna dini moja. Inawezekana kuna madhehebu lakini hata madhehebu Unguja si tatizo hata siku moja; Sunni wapo wanafanya shughuli zao, Ibadhi wapo wanafanya shughuli zao, Mashia wapo wanafanya shughuli zao, kabisa hatuna mtafaruku huo kabisa. Sasa kama dini ni moja na majority (idadi kubwa) ya Wazanzibari ni Sunni, enhe, sasa kwa nini tugombane? Hata msikitini mnafukuzana! Hata msikitini hutaki kuswali na mwenzako! Sunni mwenzako! Muislamu Sunni mwenzako, hutaki kuswali naye! Unadhani unamridhisha Mwenyeezi Mungu? Au unamkasirisha Mwenyeezi Mungu? Je, tunaziweza adhabu za Mwenyeezi Mungu? Tunaziweza adhabu za Mwenyeezi Mungu? Kwa hiyo, ndugu yangu …ndugu zangu, nasisitiza umoja, umoja, umoja. Sawasawa? Kwanza ni kukumbushana, vyovyote itakavyokuwa sisi ni wamoja…Wazanzibari ni wamoja. Na ukweli ni kwamba, tangu Rais Mheshimiwa Dokta Husein Mwinyi alipoapishwa, kauli ambayo amekuwa akiitoa na kurudia kuitoa ni kwamba tunataka umoja wa nchi yetu. Na si kauli tu lakini hiyo kaitafsiri kwa vitendo…. Hawa wenzetu ambao si Waislamu, pamoja na uchache wao, wanaheshimiwa katika nchi hii kabisa kabisa. Kama kuna uvumilivu wa kidini katika dunia hapanapo kuliko Zanzibar. Kabisa kabisa. Leo hapa kunawezekana mna Mkristo lakini kavaa kanzu na kofia humjui. Inawezekana. Kwani hata Rais Magufuli anavaa kanzu na kofia na koti juu. Kwa hivyo ninasema sisi tunafanana sana, hata wakati wa Ramadhani hapa, ndugu zangu, hasa siku za nyuma, ilikuwa pamoja na Wakristo wanaruhusiwa kula Ramadhani lakini humuoni Mkristo akila barabarani. Kama ni kula anakula ndani. Kwa nini? Kwa kuheshimu Waislamu.” 

Tunamuomba Allaah Mtukufu Amrehemu mja wake Maalim Seif Sharif Hamad…Alikuwa tumaini, atabakia mfano kwetu na kwa vizazi vijavyo. 

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Simu: 0713603050/0754603050

313 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!