DODOMA

Na Mwandishi Wetu 

Kuelekea kilele cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania kitakachofanyika Desemba 9, mwaka huu, Waziri wa Madini, Dotto Biteko, amesema sekta ya madini imepata mafanikio makubwa kwa kuzuia utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi 

Biteko anasema utoroshaji wa madini kwa sasa ni ‘zilipendwa’ kwa sababu hauna faida na anayefanya hivyo anatafuta kwenda jela au umaskini.

Akizungumza mjini Dodoma wiki iliyopita kuhusu mafanikio hayo kuelekea kilele hicho, Biteko, anasema kwa sasa hakuna wasiwasi kwamba kuna wizi katika sekta hiyo na mipango iliyopo ni kuimarisha biashara ya madini na kuendelea  kuzuia utoroshaji wake.

Anasema mafanikio na maendeleo ya sekta ya madini kabla na baada ya Uhuru ina historia ndefu  hadi kufikia kipindi cha maadhimisho ya miaka 60 yatakayofanyika mwaka huu.

“Mafanikio ambayo yamepatikana ni pamoja na kuimarisha biashara ya madini pamoja na kuzuia utoroshwaji wa madini nje ya nchi na kwa sasa tumejitahidi kuweka masoko kila eneo  hapa nchini,” anasema na kuongeza:

“Wasiwasi na shaka katika utoroshaji wa madini ni jambo muhimu, hasa kwa mtu mwenye akili timamu kama ilivyo katika ndoa, ambapo wasiwasi ni muhimu ili kuiimarisha.

“Ni muhimu tuwe na wasiwasi. Siku tukiridhika kwamba mambo yapo shwari ujue siku hiyo ndiyo tumeanza kuibiwa, kuwa na wasiwasi na shaka kwa mtu mwenye akili timamu ni bora, lakini twende katika namba. Turudi nyuma tulipotoka ni kesi za watu wangapi walikuwa wakikamatwa wakitorosha madini?” 

Pia anasema zamani wachimbaji na wafanyabiashara walitorosha madini kwa sababu hapa nchini hapakuwa na utaratibu mzuri.

“Tuendelee kuwa na wasiwasi kwa sababu wasiwasi ni sehemu ya maisha muhimu, mtu akisema atatorosha tuujue uchochoro.

“Wito wangu kwa Watanzania, kutorosha madini ni zilipendwa. Hakuna faida, hakuna tija kwa mtu yeyote anayefanya hivyo kwa sababu atakuwa anatafuta vitu viwili tu kati ya jela au umaskini kwenye maisha yake,” amesisitiza.

Changamoto zilizopo

Anazitaja changamoto ambazo wamekutana nazo katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru kuwa ni rasilimali fedha, vitu na watu.

“Changamoto kubwa kwetu ni matokeo ya maendeleo kama ambavyo katika maisha ya kawaida tu ukifanikiwa jambo moja utazalisha jambo jingine. Kwa mfano sekta inapokuwa inavutia watu wengi kuingia ndiyo mwanzo wa kuongezeka kwa fursa kama rasilimali fedha, watu na vitu kwa ujumla,” anasema.

Katika hatua nyingine, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kuajiri watumishi wapya na amesema itapunguza changamoto ya uhaba wa watumishi.

Anaitaja changamoto nyingine kuwa ni utengenezaji wa sheria zinazofanana na akasisitiza ni lazima Waafrika wawe na sheria zinazofanana ili kuendelea kulinda madini katika maeneo yao.

“Mfumo wa usimamizi wa madini sisi Tanzania hatupo peke yetu, tuna majirani zetu ambao wana madini kama sisi, hivyo ni lazima sasa changamoto ninayoiona ni ya Kiafrika zaidi. Ni lazima Waafrika tusimame tuwe tuna sheria zinazofanana,” anasema.

Pia anasema changamoto nyingine ni mtazamo wa wachimbaji wadogo kuvamia maeneo ya wawekezaji na akasema serikali itaendelea kuwalinda wawekezaji wenye leseni.

“Mwekezaji lazima alindwe, ni muhimu Watanzania tuwalinde wawekezaji wetu. Haina maana tunampa mtu leseni halafu anaingiliwa katika biashara zake,” anasema.

Watanzania wapo tayari kuchimba madini

Biteko anasema kwa sasa Watanzania wapo tayari kuchimba madini kwa sababu kuna wataalamu wengi wa kutosha tofauti na miaka ya nyuma ambako Mwalimu Julius Nyerere alisema hadi Watanzania wawe tayari ndipo madini yachimbwe.

“Tumejaribu kuonyesha hata tofauti ya wakati wa wakoloni na sisi, tumepiga hatua kubwa sana na utayari wetu ni kuwa na wataalamu wa kusimamia madini. Nchi hii inazalisha wajiolojia, wahandisi wengi na migodi yetu unayoiona hata wachimbaji wadogo asilimia zaidi ya 80 wana wajiolojia wao. 

“Kwa hiyo kile ambacho Mwalimu Nyerere alisema tukiwa tayari tuchimbe madini yetu, mimi ninaamini wakati ndiyo huu, tupo tayari kwa sababu tuna wataalamu,” anasema.

Uwazi wa mikataba

Anasema mikataba yote inayoingiwa hawajifungii wizarani bali wanaifanya kwa uwazi na inasainiwa hadharani mbele ya waandishi wa habari.

“Mikataba yote tunayoingia waziri hajifungii ndani akaingia mikataba na mwekezaji, tunasaini hadharani na ninyi mnakuwapo (waandishi) na mikataba inawekwa hadharani.

“Isipokuwa lazima katika mikataba wawekezaji hawataki ijulikane, kama nchi zipo taratibu za kufuatwa,” anasema.

Masoko ya madini yaleta faida

Kuhusu masoko anasema ndani ya miaka 60 ya Uhuru kumekuwa na masoko mengi ya madini na yamesaidia kuongeza mapato na kwa sasa kuna masoko 102; makubwa ni 50 na madogo ni 52.

“Dar es Salaam tulikuwa na watu wana viwanda bandia lakini vitafute kwa sasa kama vipo kwa sababu tumebadilika na fedha unaipata siku hiyo hiyo na benki zipo na tunawauliza mnataka mpewe fedha mkononi au kwa njia ya benki.

“Sasa wachimbaji wadogo wananufaika sana, nenda katika mahakama, ilikuwa ni kudhurumiana lakini kwa sasa hakuna, katika masoko watu wenye fedha ndio wananunua,” anasema.

Makinikia

Kuhusu makinikia anasema anawahakikishia Watanzania kutoza kila aina ya madini tofauti na zamani walipotoza katika dhahabu na almasi. 

Anasema katika makinikia yanayozalishwa wanatoza kila aina ya madini yaliyomo, ikiwamo hadi chuma kwa uzito wake na ukubwa wake.

Pia anasema baada ya kukubaliana kutosafirisha makinikia nje ya nchi, kwa sasa wanayachukua na kuyapeleka katika maabara tatu zinazopima na kuonyesha kuna madini kiasi gani.

“Tulikubaliana kubadilisha utaratibu, mwaka 2020 tulisaini mkataba na ule utaratibu wa kusafirisha makinikia tukaachana nao ili yauzwe kama madini,” amesema.

“Tangu mwaka 2020 tulivyosaini mkataba hadi Machi, mwaka huu kulikuwa kuna makontena 1,600 ambayo tayari yalikuwa yameuzwa.

“Mchango wa makinikia katika mapato yake yote katika zile fedha shilingi bilioni 584 na asilimia 2.5 inatokana na mauzo ya makinikia,” anasema.

Migodi

Kulinganishwa na nchi ilipotoka na hivi sasa, anasema nchi ina migodi tisa, huku sita ikiwa ni ya dhahabu, mmoja almasi, mwingine ni tanzanite na mmoja wa makaa ya mawe, pia ipo migodi takriban 28 ya uchimbaji wa kati na mingine mingi ya uchimbaji mdogo.

Ukuta wa Mirerani waongeza mapato

Anasema madini ya tanzanite yameongeza mapato ya serikali kutoka Sh milioni 166 kwa mwaka hadi kufikia Sh bilioni 3.9 baada ya ujenzi wa ukuta wa Mirerani. 

Anasema katika mafanikio hayo yapo mambo mengi wamefanikiwa, ikiwamo kupandisha uchumi, kuongeza ufanisi, kuongeza uwazi na ushiriki wa Watanzania.

By Jamhuri