Suala la mazingira na matatizo ya tabia ya nchi, kuondolewa vikwazo nchini Zimbabwe na Bara zima la Afrika kuwa la viwanda ni mambo makuu ambayo Tanzania imeyapeleka katika Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika New York City, Marekani mwezi uliopita.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, amewaeleza wajumbe wa mkutano huo nia ya Tanzania kupeleka mambo makuu hayo ni kusisitiza umuhimu wa kusimamia mambo hayo.

Amesema kuwa asilimia 32.5 ya nchi ya Tanzania imetengwa kuwa hifadhi, mbuga za wanyama na hifadhi ya misitu. Katika kupunguza matumizi ya nishati ya kuni, Tanzania imeamua kuweka mbadala kwa kupeleka umeme vijijini chini ya mradi wa REA kwa wananchi.

Ujenzi wa bwawa la kufua umeme  – Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rufiji ambalo litazalisha MW 2,115 za umeme litakapokamilika utashusha bei ya umeme na kufanya umeme kupatikana hata kwa watu wa kawaida na kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.

Vilevile Tanzania imepeleka suala la kuondolewa vikwazo Zimbabwe. Imeelezwa: “Wakati umefika kuondoa vikwazo ilivyowekewa Zimbabwe ili wanawake na watoto wa Zimbabwe ambao sasa hali yao ya maisha si nzuri kutokana na vikwazo,” alisema Prof. Palamagamba.

Tanzania ikiwa ni Mwenyekiti wa SADC imeamua kuieleza dunia kinagaubaga kuhusu suala hili. Na Rais mpya wa Zimbabwe ameahidi kuendelea kufanya mabadiliko makubwa katika nchi yake.

Kuhusu suala la uchumi na maendeleo ya Afrika, Tanzania imeamua kubeba ajenda ya kuifanya Afrika nzima ni Bara la Viwanda. “Wakati umefika sasa kwa Bara la Afrika kuacha kuendelea kuuza malighafi katika masoko ya Ulaya, na badala yake kujenga viwanda vyake,” ameeleza  Kabudi.

Katika ajenda hii mkazo umewekwa kwa Afrika iweze kutengeneza bidhaa kwa ajili ya matumizi yake yenyewe na iuze nchi za nje. Afrika iweze kuajiri vijana wake takriban asilimia 60 ya watu wote wanaoweza kupata ajira au kujiajiri na kupata maendeleo yao.

Mambo matatu haya yanaonyesha namna gani Tanzania inavyojali watu wake na watu wa Afrika ( Binadamu wote ni sawa) kutokana na misingi ya imani na madhumuni ya Chama Cha Mapinduzi ambacho serikali yake iko madarakani. Hongera CCM, hongera Serikali ya Tanzania.

Msingi mmoja wapo wa Imani ya CCM ni kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Msingi mmoja wapo wa madhumuni ya CCM ni kupigania ukombozi na umoja wa Afrika. Misingi hii na mengineyo ndiyo iliyoisukuma Tanzania kupeleka mambo haya Umoja wa Mataifa.

Suala la mazingira na matatizo ya tabia ya nchi ni nyeti. Halina budi kutazamwa upya na kulitambua ni JANGA la dunia, si TATIZO la nchi moja moja au bara fulani. Naamini nchi zote duniani, hasa Umoja wa Mataifa wanao uwezo wa kuliangalia na kulikabili JANGA hili kwa upana wake.

Wakati umefika pia kwa mataifa ya Ulaya kubaini dunia si mabara ya Ulaya, Marekani na Australia tu. Dunia ni pamoja na Afrika, Bara Arabu na Asia. Kote huko hakutakiwi kuchafuliwa mazingira ( hewa, ardhi na misitu). Narudia kusema mpiga ngoma, mwimbaji na mchezaji ni Umoja wa Mataifa.

Wazimbabwe ni binadamu sawa na binadamu Waingereza, Wamarekani na jamaa zao duniani. Wote hawa mahitaji yao ni aina moja. Wanahitaji chakula bora, kulala mahali safi na salama na kupata mavazi nadhifu. Vikwazo havitoi mahitaji haya abadani. Umoja wa Mataifa ndicho chombo hasa cha kutengua vikwazo. Jukumu liko mlangoni.

122 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!