Wiki iliyopita, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, aliibua hoja ya mpango wa taifa wa ardhi ya kuzika wafu.

Mongela alitaja wazo lake hilo wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2015. Mongela aliweka wazi kwamba hakuibua hoja hiyo kama kiongozi wa Serikali, bali ni mtazamo wake binafsi, ambao angependa kuona unafanyiwa kazi.


Alisema; “Ifike wakati Watanzania tuangalie mpango wa kitaifa wa ardhi ya kuzikana (makaburi).” Kwamba Watanzania zaidi ya milioni 44 sasa wanazungukwa na changamoto kubwa ya upatikanaji maeneo rasmi ya kuzika wafu.


“Hili ni wazo langu binafsi, hatuwezi kuwa tunapoteza au kutafuta maeneo ya kuzika kila baada ya miaka kadhaa. Kwamba tukipata eneo moja tunajua baada ya muda litakuwa limejaa na tutatakiwa kununua eneo jingine.


“Kila mkoa nchini makaburi yamejaa, angalia mfano wa Dar es Salaam maeneo ya Kisutu, Kinondoni, Chang’ombe, haya Arusha hapa makaburi ya Njiro yanaelekea kujaa.


“Mimi ni mtu wa dini, lakini mwisho wa siku tutafikia kujadili suala hili hata kama si leo. Lazima tukae kama wadau kwa pamoja kujadiliana jambo hili,” anasisitiza.


Akizungumzia Halmashauri ya Jiji la Arusha, Mongela anasema makaburi ya Njiro yakijaa, halmashauri itawajibika kutafuta eneo na kuwalipa fidia wananchi ili kupata eneo la makaburi.


Mtazamo wa DC Mongela ni kwamba ufike wakati Watanzania tufikirie suala la kuchoma maiti, au aina nyingine ya kuzikana itakayokuwa na matumizi madogo ya ardhi. Anakazia hoja yake kwamba katika dunia ya leo ambayo ardhi imekuwa na thamani kubwa, kuna haja ya Tanzania kujipanga kutumia eneo dogo la ardhi kuzika watu wengi.


Pengine wazo hilo la DC Mongela halijachelewa, bali ni changamoto inayohitaji kuangaliwa na wadau wote kwa mapana na marefu.


Katika mkutano na waandishi wa habari, mmoja wa wadau wa maendeleo jijini Arusha, Nyanga Mawalla, aliwahi kueleza umuhimu wa matumizi ya ardhi katika nchi zilizoendelea. Katika maelezo yake, Mawalla aligusia umuhimu wa kuwa na makaburi yatakayokuwa na mwonekano tofauti na wa sasa.


Kwamba badala ya kuzikana kwa kufuata upana wa eneo la ardhi, basi uwepo utaratibu wa kuanza kuchimba kaburi moja litakalokuwa na uwezo wa kuzika watu wote wa familia moja.


Alitolea mfano wa familia moja ya watu watano kuwa na kaburi lao lililochimbwa kwa urefu wa kwenda chini, ikitokea moja kafariki anatangulizwa chini na kaburi kujengewa usawa ule ule wa jeneza tayari kwa kusubiria mwingine.


Binafsi nakubaliana na mawazo binafsi ya DC Mongela na Mawalla, kwani kadiri idadi ya watu inavyozidi kuongeza, utafika wakati suala la makaburi kugeuka ajenda.


Ninaunga mkono mawazo hayo kwani mpangilio huo ni wazi kuwa unapunguza matumizi ya ardhi yasiyo ya lazima, kwamba katika eneo linalopaswa kuzika mtu mmoja basi wazikwe watu 10. Kama tumeweza kujadili suala la nani aruhusiwe kuchinja, basi ni wakati mwafaka wa kujadili hoja ya binafsi ya DC Mongela.


By Jamhuri