Tanzania kuna sheria nne ambazo hutumika kugawa mirathi. Kwanza,  sheria za  kimila; pili,  sheria  za Kiislamu;  tatu, sheria ya urithi ya India ( Indian Succession Act) na nne, sheria ya mirathi ya watu wenye asili ya Asia.

Swali la sheria gani kati ya hizo itumike katika kugawa mirathi hutegemea na mambo yafuatayo:  Kwanza, maisha aliyoishi marehemu. Marehemu kama aliishi maisha ya dini, labda alikuwa Mwislamu na maisha yake yalikuwa ya Kiislamu, basi sheria itakayotumika kugawa mali ni ya Kiislamu.

Halikadhalika kama aliishi maisha ya kimila, sheria ya kimila itatumika. Kwa hali ya sasa, maisha ya kimila yako zaidi vijijini.  Kama aliishi kama Mkristo na alikuwa Mkristo, sheria ya urithi ya India (Indian Succession Act) ndiyo itakayotumika.

Pia wenye asili Asia kama wote tunavyojua hupenda kuishi maisha kama ya wenzao wa Asia japo huwa tuko nao nchini humu. Basi nao ikitokea hivyo, sheria ya mirathi ya Asia itatumika kugawa mali.

Makala hii imeangalia mgawo wa mali za marehemu kwa kutumia sheria ya mirathi ya India (Indian Succession Act) ambayo hutumika kwa Wakristo na wale wote walioacha maisha ya kimila lakini wasio Waislamu.

(a) Mgawo ukoje ikiwa mume amefariki dunia akaacha mjane, watoto na ndugu?

Kama mume amefariki dunia na akaacha mjane na watoto, basi moja ya tatu (1/3) ya mali za marehemu zilizo kwenye mirathi anatakiwa apewe mke wake. Mbili ya tatu (2/3) ya mali hizo itakwenda kwa watoto wake.

(b) Mgawo ukoje kama marehemu hakuacha watoto isipokuwa mjane?

Kama hakuna watoto walioachwa  na marehemu katika familia husika lakini kuna mjane, mali ya marehemu hugawanywa katika mtindo ambao ndugu hupewa nusu (1/2), na mjane hupewa nusu (1/2) ya mirathi ya marehemu.

(c) Mgawo endapo marehemu hajaacha ndugu, mtoto isipokuwa mjane

Kama marehemu hajaacha ndugu wala  mtoto au watoto, basi mali yote huchukuliwa na mjane. Ndugu kwa maana ya hapa ni kaka, dada, mama mzazi wa marehemu au baba.

(d) Mke akifariki dunia na kamuacha mume na watoto

Hapo juu tumeona mume akifariki akamuacha mke  na watoto mke huchukua  moja ya tatu na watoto au mtoto mbili ya tatu. Hali iko hivyo hivyo kwa mume naye ana haki kama alizonazo mke wake, yaani kupata mirathi kutoka katika mali za marehemu. Kwa maana hiyo mume hupata moja ya tatu (1/3) ya mali za marehemu mkewe na mbili ya tatu (2/3) huenda kwa watoto.

(e) Mgawo ikiwa mke amefariki dunia na kumuacha mume bila watoto.

Kama mke amefariki dunia na amemuacha mume lakini hakuna watoto, inaangaliwa kama kuna ndugu. Ikiwa kuna ndugu, basi ndugu hao wa mke hutakiwa kupata nusu ya mali (1/2) na nusu inayobaki (1/2) huenda kwa mume. Kwa hiyo ndugu wa mwanamke ambaye ni marehemu hupata sawa kwa sawa na mume wake aliyeachwa.

(f) Mgawo endapo mke amefariki dunia, hakuacha ndugu isipokuwa mume

Ikiwa mwanamke ndiye amefariki dunia na  hakuacha ndugu yeyote wala mtoto yeyote isipokuwa kamuacha mume wake tu, basi mume huyo huchukua mali zote za mkewe.

(g) Mgawo wa  mali endapo wazazi wamefariki dunia na wamebaki watoto/mtoto tu.

Sheria inasema kwamba kama wazazi wote wawili wamefariki dunia, basi mali za marehemu hupewa watoto wao. Kama  mtoto  ni mmoja  na yuko peke yake, mtoto huyo mmoja hutakiwa kuchukua mali zote peke yake. Nasisitiza hapa kuwa haijalishi mali ni nyingi kiasi gani, kama mtoto yupo peke yake atachukua yote. Hapo hakuna ndugu wala wazazi wa marehemu. Pia kama wapo wengi, basi watoto hao hugawana mali hizo sawa kwa sawa bila kujali ni mwanamke au mwanamume.

(H) Mgawo endapo baba na mama na watoto wote wamefariki dunia

Kama wazazi wote baba na mama wamefariki dunia, lakini pia na watoto wao wote nao wamefariki dunia, mali huenda kwa wajukuu. Haijalishi mjukuu wa kike/kiume, mgawo hutakiwa kwenda sawa kwa sawa.

(I) Mgawo endapo mtoto mwenye mali amefariki dunia akawaacha wazazi

Wakati mwingine huwa inatokea wazazi wana mtoto hajaoa/kuolewa na wala hana mtoto lakini ana mali. Mtoto huyu akifariki dunia,  mali zote huenda kwa wazazi wake.

By Jamhuri