Binadamu anajiendeleza kwa kujifunza au kuiga kutoka kwa vizazi vilivyotangulia. Haipo jamii itakayojihakikishia maendeleo ya uhakika bila kujifunza kutoka jamii nyingine ilimradi wanajamii wanaafikiana juu ya maana ya maendeleo na yapi yawe ya kuiga ili kujiletea maendeleo.

Teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama) imeleta mabadiliko na maendeleo makubwa kwa binadamu duniani kote. Sababu moja ya maendeleo haya ni kuunganisha matumizi ya teknolojia na kusababisha kushuka sana kwa gharama za mawasiliano.

Maendeleo katika Teknohama nayo yakasaidia kubuniwa na kukuzwa kwa matumizi ya mitandao ya jamii, mitandao ambayo kwa kiasi kikubwa imejengwa juu ya msingi huo wa kutamalaki na kushamiri kwa teknolojia mpya mbalimbali.

Teknohama imegusa maisha ya binadamu katika kila suala muhimu la uhai wake na mabadiliko yanazidi kuonekana siku hadi siku. Ubunifu wa binadamu nao unazidi kupanua wigo wa matumizi ya teknolojia hii katika nyanja tofauti.

Si ajabu basi kwamba matumizi hayo yameingia pia kwenye nyanja za mawasiliano kati ya serikali na watu zinazowaongoza; kati ya viongozi na jamii wanazoongoza.

Tunaokumbuka enzi za Mwalimu tunakumbuka kuwa habari muhimu kutoka serikalini ilikuwa inasikika kwenye taarifa ya habari ya saa mbili usiku kutoka Radio Tanzania, Dar es Salaam. Tulitega sikio hapo kusikia nani kateuliwa na nani katimuliwa.

Habari nyingine muhimu, kama zilijiri, tulizisubiri kesho yake kwenye magazeti machache ya serikali na ya TANU, au kwenye taarifa ya habari ya saa saba mchana kupitia Radio Tanzania.

Kati ya taarifa ya habari moja na nyingine, na si zote zilikuwa za kusisimua kila wakati, watu walirudi kwenye shughuli muhimu za kazi na uzalishaji.

Leo hii Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu inatoa taarifa na ndani ya saa moja itakuwa imeenea kwa njia ya mitandao kwenye kila pembe ya dunia. Muda wa taarifa ya habari ukifika ile habari inakuwa imeshachuja tena, si habari.

Na tofauti na zamani, ile hadhira kubwa ya watu ambayo ingerudi kazini na kwenye uzalishaji kusubiri taarifa ya habari nyingine, leo hii imewezeshwa na Teknohama kubaki imeunganishwa na habari saa 24 za kila siku.

Maendeleo kwenye Teknohama na mitandao ya jamii yameipandisha serikali, viongozi na hadhira yao kwenye jukwaa moja. Tofauti na zamani, habari haitoki upande mmoja kwenda kwa hadhira hiyo lakini ni uwanda ambao kila mshirika anayo nafasi ya kusema anachotaka bila kuwepo vizuizi vya zamani.

Zamani haikuwa rahisi kufikisha ujumbe kwa kiongozi mkuu wa nchi. Leo hii unaweza kutumia simu yako ya tochi ukiwa Irigija na kwa uzoefu mdogo tu, ukatuma ujumbe kupitia mtandao na kubahatisha usomwe na mkuu huyo. Au kama si yeye, basi wasaidizi wake.

Lakini si kila kilicho rahisi ni kizuri. Lugha ya Kiingereza ina msemo: panga lenye makali pande zote mbili. Maana yake ni kuwa yapo masuala ambayo yanaleta manufaa lakini yana sifa ya kuibua matatizo pia.

Tumeiga mtindo wa viongozi duniani kote wa kuingia kwenye mitandao na kuanzisha mawasiliano ya moja kwa moja na jamii wanazoongoza. Ni jambo jema sana kwa sababu si rahisi kiongozi atumie njia rasmi za mawasiliano halafu apate uhakika wa taarifa kamili na sahihi juu ya changamoto zilizopo au ufanisi wa utekelezaji wa kazi za serikali.

Akifungua milango anajipa fursa ya kupata taarifa za uhakika zaidi. Lakini milango ikiwa wazi sana basi akubali pia kuwa si yote yatakayopita yatamfurahisha au yatajenga.

Mitandao ya jamii ni kokoro. Ni kapu linalobeba kila aina ya watu, watu ambao wamepishana kwa staha, busara, subira, uvumilivu na kila aina ya sifa unayoweza kumpachika binadamu.

Kwa kiongozi si eneo ambalo utajitumbukiza kwa muda mrefu ukiwa nadhifu na ukaachwa hivyo. Utachafuliwa na utaachwa mtupu na watu ambao ni waraibu wa kuteketeza heshima za watu.

Tuko wengi ambao tunatetea uhuru wa mawazo, lakini si rahisi kutetea uhuru ambao hauna staha hata kama ya ukweli nayo hupenya. Na ndiyo maana iko haja ya kuleta mabadiliko katika kusambaza mawasiliano rasmi ya serikali na taasisi zake.

Kuna sababu nzuri kwanini kuna msemaji rasmi wa serikali, wa wizara au wa taasisi yoyote ya umma au binafsi: ni kuweka msimamo unaofanana katika masuala mbalimbali yanayojitokeza katika utekelezaji wa mipango.

Inawezekana kuwa sababu ya kiongozi mmoja wa serikali kutamka jambo ambalo linakinzana na mwajiri wake au na mwajiriwa mwenzake ni kuwepo mlolongo wa viongozi ambao wamefungua mifumo yao binafsi ya mawasiliano inakosa miongozo mizuri.

Na kwa sababu kwa wengi ya hao mawasiliano si taaluma yao, huo mgongano utaendelea kujitokeza na kushika mizizi. Ingekuwa upo uratibu mzuri wa taarifa hizi haya matatizo yangepungua sana.

Nafahamu uongozi wa awamu hii haupendi mikutano lakini ningeombwa ushauri ningependekeza semina elekezi kufundisha mbinu sahihi za mawasiliano. Kama gharama itakuwa kubwa, dawa iwe kuwanyang’anya simu janja, kuwakabidhi simu za tochi za elfu ishirini na kuwaelekeza kutumia zaidi maofisa habari kuwasiliana na umma.

Barua pepe: barua.muhunda@gmail.com

1097 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!