Ndugu Rais, mtikisiko uliosababishwa na ukuta wa Septemba mosi, umeitikisa nchi yetu vibaya! Nchi imetapatapa na kuyumbayumba na sasa nyufa zimetokeza! Ni ukweli kwamba tangu tupate Uhuru wananchi hawajawahi kushuhudia serikali yao ikitetemeshwa kwa hofu kama ilivyotetemeshwa kuelekea tishio la Septemba mosi!

Serikali ilijaribu kwa uwezo wake wote kuwatisha wananchi, lakini bila mafanikio. Wananchi hawakutishika! Ukuta kuona Serikali imehemewa wakaifanyia dhihaka. Wakasema sasa ni Oktoba mosi. Serikali ikanyumbuka! Ikamjibu mjinga ili kufanana naye! Ikasema nayo siku hiyo itapanda miti.

Ndugu Rais, mara zote anayepanga ndiye mwenye akili. Anayemjibu kwa kumfuatisha ni boya kama maboya mengine. Hivyo, hali ikiendelea kuwa hivi anayejibu anaweza akaburuzwa mpaka mwisho wa kipindi chake naye akajikuta hana alichowafanyia wananchi. Baba, uongozi unataka busara!

Uongozi unataka hekima, siyo vijembe!

Kwa hofu ambayo ukuta uliijaza Serikali itakuwa vigumu kwa Serikali

kufanya lolote la maendeleo. Nao ukuta unaweza ukawapeleka puta mpaka mwaka 2020. Wananchi waliishuhudia Serikali ikiwa imejaa hofu!

Baadhi ya viongozi wa Serikali walionekana kutetemeka kama utete dhaifu usukumwao na maji ya mkondo! Ikatoa virungu, mabomu ya machozi, bunduki za kivita; vyote hivyo ni kuwakabili raia wake ambao hata hivyo hawakuwa na silaha yoyote! Serikali ilitishwa kidogo lakini, ikatishika sana! Watu wazima wakapoteza fahamu zao kwa kutishwa na ukuta tu! Ni jitu gani hili, ukuta? Si jitu si lolote! Ni asilimia ndogo sana ya wananchi wa nchi hii waliotaka kuandamana na kufanya mikutano huku wakiwa hawana silaha yoyote! Waoga hawa wangekuwa ndio walikuwa viongozi wetu wakati ule wa Vita ya Kagera, kwa madege ya Iddi Amin Dada na askari wake, wangeikimbia nchi wakatuachia Amin na wanajeshi wake watuangamize!

Baba hebu waambie watu wako, kulikuwa na sababu gani iliyowafanya askari wasifanyie mazoezi yao wanakofanyia miaka yote mpaka wakafanyie kwenye mitaa waliko wananchi? Hawaoni kuwa kwa kufanya hivyo wamefanikiwa kujenga chuki kati ya wananchi na wao? Sasa tumefika mahali polisi wakiuawa wananchi wanashangilia! Kwa kukosa

busara viongozi tunadhani tunatisha tunaposema watu hao tutawajumuisha katika uovu huo. Wananchi wanatung’ong’a maana hatutaui tatizo.

Kwa nini wananchi washangilie polisi wakiuawa!

Ndugu Rais, ni wananchi wangapi walishtakiwa mahakamani kwa kumtukana Rais Nyerere katika miaka yake yote 24 ya urais? Na Mwinyi je? 

Na Mkapa na Kikwete je? Sisi wamefika wanne hata mwaka bado. Kwa nini hatujichambui?

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa Burundi alikaririwa akisema: “Siyo hapa Burundi tu palipo na baadhi ya viongozi wapumbavu, hata kwetu Tanzania baadhi ya viongozi wapumbavu wapo.”

Iweje wanajeshi waseme hawatasherehekea kwa kufanya maandamano kwa sababu Serikali imezuia halafu kikundi cha wahuni tu kiseme kitamuunga mkono Rais wetu kwa kuzuia maandamano, kwa wao kuandamana?

Kuviachia vikundi hivi vya wahuni wachache waliokuwa wanafugwa na viongozi mufilisi waliotangulia vitambe, ndiko kunatufanya tuonekane hatuna busara mbele ya watu timamu. Anazuka mtu tu wa mtaani kwa maaana kuwa siyo shekhe, siyo mchungaji, siyo Askofu anasema anaendesha ibada yake. 

Mkuu anapomwinamishia kichwa chake mtu huyo kuonesha kumtii kama afanyavyo mbele ya Baba Askofu, timamu wamueleweje?

Asiyekuwa Mhaya ni Mnyamahanga kama ambavyo asiyekuwa Mchaga ni Chasaka. Na huyu mwendesha ibada asiye, ni mhuni tu!

Mzee Mkapa alituambia kuwa kuna maprofesa uchwara. Wale ambao hawakumwelewa wakati ule, leo wanamwelewa wanapomuona profesa uchwara akijipaka kamasi mwili mzima kwa kuvivuruga vyama vya siasa huku akisindikizwa na walinzi wanaolipwa na mabwana zake! Huyu profesa uchwara aogopwe kama ukoma!

Ndugu Rais, meseji kutoka kwa watu wako ni nyingi. Kutoka Shinyanga mwanamwema Costantino aliandika: “Makala yako ni nzuri na inatoa au kufikisha ujumbe bila shida. Wewe umeishatimiza wajibu wako wakutupa habari na kutuelimisha, lakini je, walengwa ujumbe unawafikia? Bado ninashauri tunu hizi zikusanywe pamoja na kutoa kitabu. Maana imeandikwa kila zama na kitabu chake! Mungu akubariki na kukulinda.”

Huyu nilimjibu nikamwambia kuwa, kila mwenye busara ananiuliza, walengwa wanasoma? Wakisoma wanaelewa? Costantino nisaidie niwajibu nini ikiwa ni pamoja na wewe?

Akaniandikia: “Waambie wewe ni sauti ya wasio na sauti (Sauti iliayo jangwani- mtengenezeeni Bwana njia yake). Kama yeye huyu ndiye tuliyekuwa tunamsubiri, basi wewe ndiye mtangulizi wake. Ayaelewe na kuyakiri maneno yako! Naamini umeishatimiza wajibu wako. Uwe na amani, wawe wanayasoma au la tayari umeishawasemea wasio na sauti. Mungu akubariki.”

Ndugu Rais, tulichokifanya Zanzibar kwa hotuba zetu ni kupanua mfarakano! Mwana wa ibilisi atashangilia na kusifia! Seif Sharrif Hamad hakuukataa mkono wa Dk. Ali Mohamed Shein. Alichokataa Maalim Sefu ni mkono wa Rais wa Zanzibar ambaye kwa mtazamo wake, siye! Alichokikataa Maalim Seif Sharif Hamad ni unafiki! Kutoa meno watu wadhani anacheka kumbe moyoni anaumia. Huu ndiyo unafiki alioukataa mtoto wa marehemu

Wilson Kabwe siku ya maziko ya baba yake! Alijisemea moyoni, ‘ondoka kwangu ewe’. Hakuutoa mkono wake hadi mwisho! Aliukataa unafiki wa wanafiki! Baba nchi yetu imepungukiwa busara na hekima!

Maandiko yanasema busara na hekima huita kwa sauti barabarani. Hupaza sauti yake sokoni; huita juu ya kuta; hutangaza penye malango ya mji; 

Enyi wajinga mpaka lini mtapenda kuwa wajinga? Mpaka lini wenye dharau watafurahia dharau zao na wapumbavu kuchukia maarifa? 

Heri mtu yule aonaye hekima na mtu yule apataye ufahamu. Njia zake ni za kupendeza sana na mapito yake yote ni ya amani.

By Jamhuri