Afrika irejee misingi yake

Kwa wale Watanzania waliokuwapo kwenye ile miaka ya mwanzo ya uhuru wa nchi yetu, bado watakuwa na kumbukumbu ya wimbo ufuatao.

“Bara la Afrika twalilia ukombozi; 

Ukoloni mbaya na ubaguzi wa rangi;

Mataifa hayo ya Ulaya ndiyo Afrika kuivamia; 

Mababu zetu zamani walikataa;

Ukoloni waliukataa; 

Mabeberu waliwatesa; 

Ni vigumu kuyasahau hayo waliyowatendea”

Wimbo huu katika miaka hiyo ulitumika kama kiashiria cha kuanza kwa kipindi kilichokuwa kikitambulika kama “Ukombozi wa Afrika” katika Redio Tanzania ya wakati huo.

Ikumbukwe kuwa wakati huo kituo cha redio kilikuwa ni kimoja nchi nzima na hapakuwa na kituo kingine cha Serikali au cha binafsi.

Ni wakati huo ambapo historia inatueleza kuwa Tanzania ilikuwa mstari wa mbele katika bara hili kuhakikisha kuwa nchi zote zilizokuwa bado mkononi mwa wakoloni zinapata uhuru.

Ni kipindi hicho ambapo vijana wa wakati huo kama aliyekuwa Balozi wa Tanzania huru katika Baraza la Umoja wa Mataifa, Dk Salim Ahmed Salim na Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo, John Samwel Malecela, na wengine kutoka vyama vya ukombozi walisikika kila kona ya bara hili la Afrika na duniani kote wa kielezea umuhimu wa Afrika kuwa huru.

Vijana hawa wa Kiafrika kuanzia kusini, magharibi, kaskzini na mashariki walihaha kuhakikisha zile nchi zote lilizokuwa bado mikononi mwa wakoloni zinakuwa huru.

Tunaona kuwa baada ya nchi hizi kufanikiwa kupata uhuru, viongozi wa wakati huo walikuwa wakikabiliwa na jukumu moja la kuanza kuzijenga nchi zao kiuchumi na kisiasa.

Baada ya viongozi waliopigania uhuru kumaliza mihula yao, ndipo tukaanza kuishuhudia Afrika mpya ambayo imeendelea kuishi kwa kutegemea misaada kutoka nje licha ya kuwa na utajiri wa rasilimali nyingi.

Wengi wa watawala wa kizazi hiki cha baada ya uhuru, wamekubali kuwa vibaraka wa mataifa ya Magharibi kiasi cha kuyasahau majukumu yao ya kuziendeleza nchi zao.

Kinachoshangaza ni kuwa katika nchi nyingi za Kiafrika pamekuwa na ukwapuaji wa kutisha wa pesa nyingi zinazotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo, huku jamii ikiendelea kuishi kwenye umasikini wa kutisha.

Wizi huu wa rasilimali umeendelea kuongezeka kila siku iendayo kwa Mungu katika bara hili na kibaya zaidi wanaohusika nao ni baadhi ya viongozi walioko madarakani kwa kushirikiana na ndugu, wapambe na kampuni za kitapeli kutoka Ulaya na Marekani.

Kwa mfano, kutokana na hali hiyo ya kutisha ya ukwapuaji huo wa rasilimali na pesa barani Afrika, Septemba 2007 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Rais wa Benki ya Dunia,  Robert Bruce, walikuja na mkakati wa pamoja wa kuunda mfumo kwa lengo la kulisaidia bara hili kuokoa rasilimali zinazoibwa na kuhamishiwa ughaibuni.

Taarifa iliyotolewa kwa pamoja na viongozi hao ilionesha kuwa kiasi cha rasilimali zenye thamani ya dola za Marekani zipatazo bilioni 40 huhamishwa kila mwaka na mafiasadi kutoka nchi masikini na kuhamishiwa Ulaya na Marekani, na wengi wa wahusika ni viongozi walioko madarakani kwa kushirikiana na mafisadi wengine.

Taarifa ilienda mbali na kutanabahisha kuwa harakati za mafisadi hao katika bara la Afrika yaani wezi wa kimataifa, wakwepa kodi na watoa rushwa zinaleta hasara inayofikia dola zipatazo trilioni moja hadi sita kwa nchi zinazoendelea barani Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pesa hizo zingeweza kutumika kuondoa umasikini unaoendelea kutamalaki katika bara hili ambalo ndiyo muhanga zaidi wa matukio haya ya uporaji huo.

Ripoti hiyo inasema kuwa kila dola milioni 100 zinazopotea zingeweza kutumika kutoa chanjo kwa watoto wapatao milioni nne au maji safi ya kunywa kwa kaya zipatazo 250,000, au kugharamia dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wenye VVU wapatao 600,000 na zaidi.

Hali kama hii ni hatari kwa bara hili kama kila mwaka ukwapuaji unafanyika kwa kiwango hicho cha kutisha, je, kuna matumaini ya kuliondoa bara hili kwenye lindi la umasikini huu?

Kwa mfano, mwaka 2006 Nigeria ilifanikiwa kuokoa dola za Marekani zipatazo milioni 505 zilizoibwa kipindi cha utawala wa Sani Abacha (1983-1988) zilizokuwa zimefichwa huko Uswisi.

Kiongozi mwingine aliyesifika kwa kupora mamilioni ya dola na kuwaacha wananchi wake wakiogelea kwenye umasikini ni Mabutu Sese Seko wa Zaire sasa DR Congo (1965-1997) na wengine wengi walioko madarakani leo.

Tunaona kuwa viongozi hawa wamekuwa wakishirikiana na marafiki, wapambe na familia zao kuziibia serikali wanazoziongoza na kisha kufungua akaunti za siri huko ughaibuni.

Pamoja na mataifa ya nje kuendelea kupora rasilimali katika nchi nyingi za kiafrika lakini hata misimamo yetu tuliyokuwa nayo wakati ule wa kupigania uhuru wa nchi zetu, tumeiacha kwa kisingizio cha diplomasia ya kiuchumi.

Kwa mfano katika miaka ile ya 1970 Tanzania ilisitisha uhusiano na Israel kutokana na uvamizi wake katika nchi ya Wapalestina.

Msimamo huu wa Tanzania na nchi nyingine marafiki ulitokana na kuamua kufuata siasa za kuwatetea wanyonge kokote kule duniani.

Sidhani kama tutanufaika kwa kuamua kuruhusu hali hii kwa kuachana na misimamo na misingi iliyotufanya tuheshimike ndani na nje ya mipaka yetu.

Tanzania ile iliyokuwa ikifuata siasa za kutofungamana na upande wowote na kulaani ukandamizaji, leo imemezwa na kitu kinachoitwa diplomasia ya uchumi.

Dhana hii ya diplomasia ya uchumi imeigeuza Tanzania kutokuwa na upande unaoeleweka leo inapofikia siasa za kimataifa.

Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo ni kuwa Tanzania ya miaka hiyo haikuwa ya kawaida, historia inaonesha kuwa miaka hiyo ilipofika zamu ya Mwalimu Nyerere kuongea iwe Umoja wa Mataifa au kokote kule kila mtu alikaa kimya kusikiliza.

Kama nchi au bara zima kwa ujumla haiwezi kunufaika na chochote kwa kuwa wahanga wa kulegeza misimamo yetu iliyotupa heshima kiasi cha kuheshimiwa na mataifa mengi Afrika na dunia nzima kwa ujumla.

Mpaka kufikia leo ubadhirifu huu tunaoendelea kuushudia katika baadhi ya nchi nyingi za Kiafrika ni matokeo ya kuachana na ndoto za waasisi wa mataifa yetu haya.