WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na ongezeko la shehena katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuboresha miundombinu ya bandari, reli na maeneo ya kuhifadhi mizigo ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha biashara ya kikanda na kimataifa.
Aidha katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Uchukuzi imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 2.87, ambapo Shilingi bilioni 126.04 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi trilioni 2.74 zikitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma jana, makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Profesa Mbarawa alisema Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kuingia bandarini kupitia mradi wa Port Link pamoja na ujenzi wa eneo la kupakilia mizigo kwenye treni za SGR katika eneo la Malindi Marshalling Yard.
Alisema hatua hizo zinalenga kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
“Serikali pia imekamilisha ujenzi wa kituo cha mizigo Morogoro kitakachounganishwa na reli ya SGR katika eneo la Stesheni ya Morogoro,” alisema Profesa Mbarawa.
Alifafanua kuwa kituo hicho chenye ukubwa wa mita za mraba 68,000 kitakuwa na uwezo wa kuhudumia makasha 600 kwa siku na kitasaidia kusafirisha mizigo kwenda mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Ruvuma na Dodoma pamoja na nchi jirani za Zambia na Malawi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, uondoshaji wa mizigo kutoka eneo la Malindi kupitia reli ya SGR kwenda Kituo cha Mizigo Morogoro unatarajiwa kuanza mwezi Juni 2026.
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeanza ujenzi wa magati mawili mapya katika eneo la Malindi, Bandari ya Dar es Salaam, yatakayokuwa na uwezo wa kuhudumia tani milioni tatu za ziada za shehena kwa mwaka.
Alisema magati hayo ni sehemu ya mpango wa kujenga magati 10 mapya ili kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mizigo inayoongezeka.
“Kati ya magati hayo, manne yataanzia gati namba 12 hadi 15 katika eneo la Kitopeni-Kurasini huku mengine sita yakijengwa Vijibweni-Kigamboni kuanzia gati namba 16 hadi 21,” alisema.
Alieleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza idadi ya magati katika Bandari ya Dar es Salaam kutoka 12 yaliyopo sasa hadi kufikia 22.
Aidha, alisema Serikali inaendelea na upanuzi wa eneo la Kurasini Port Extension lenye ukubwa wa mita za mraba 220,000 kwa ajili ya kuhudumia makasha, ambapo eneo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia makasha 700,000 kwa mwaka.
Profesa Mbarawa alisema awamu ya kwanza ya mradi huo yenye uwezo wa kuhudumia makasha 150,000 imefikia asilimia 92 ya utekelezaji, huku awamu ya pili ikitarajiwa kuanza Juni 2026.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema Serikali kupitia Wakala wa Kuratibu Uwezeshaji wa Usafirishaji na Biashara katika Ukanda wa Kati (CCTTFA) imeendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Ukanda wa Kati kuimarisha usafirishaji na biashara.
Alizitaja nchi hizo kuwa ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Rwanda, Tanzania, Uganda na Zambia.
Alisema kupitia ushirikiano huo, CCTTFA imeendelea kuratibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo upembuzi yakinifu wa reli ya SGR kutoka Musongati–Gitega–Kindu inayounganisha Burundi na DRC, ukarabati wa mabehewa ya mizigo ya reli ya MGR pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta ya usafiri majini kutoka nchi wanachama.
Profesa Mbarawa alisema pia Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Miundombinu ya Usafiri katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika kupitia makubaliano kati ya Tanzania na DRC yaliyosainiwa mwaka 2022.
Alitaja mafanikio yaliyopatikana kupitia ushirikiano huo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Bandari ya Kalemie, ukarabati wa Bandari ya Kigoma na ubadilishanaji wa hekta 60 za ardhi kwa ajili ya kuanzisha bandari kavu kati ya Tanzania na DRC.
Wakichangia bajeti hiyo baadhi ya wabunge wameiomba serikali kuwe na mpango mkakakati wa kufikiria kuweka kongani ya viwanda mbali na Dar es salaam ili kuondoa msongamano katika jiji hilo.
Mbunge wa Kilombero Abubakar Assenga alisema ,kuwe na mpango mkakati wa kiserikali kuhakikisha mji wa viwanda unasogea Morogoro ili bandari iweze kupumua hapo baadaye.


