Na Kija Elias, JamhuriMedia, Mwanga
KASI ya kuporomoka kwa maadili kwa watoto na vijana nchini imeelezwa kuchangiwa kwa kiwango kikubwa na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano, hali inayosababisha baadhi ya vijana kuiga tamaduni za kigeni zinazokwenda kinyume na mila na desturi za Kitanzania.
Hayo yamebainishwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Kilimanjaro Best Simba wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Wiki ya Jumuiya ya Wazazi kiwilaya yaliyofanyika katika Shule ya Ufundi Kisangara, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Alisema maendeleo ya teknolojia na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yamekuwa na athari kwa watoto na vijana wengi ambao hutumia muda mwingi kwenye simu na majukwaa mbalimbali ya kidijitali bila uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi au walezi wao.
Kwa mujibu wa Simba, alisema baadhi ya maudhui yanayosambazwa kupitia mitandao hiyo yamekuwa yakichochea mmomonyoko wa maadili kwa kuhamasisha tabia zisizokubalika katika jamii ya Kitanzania, ikiwemo utovu wa nidhamu, matumizi ya lugha zisizo na staha pamoja na kupungua kwa heshima kwa wazazi na viongozi wa jamii.
Aidha, aliwakumbusha wazazi na walezi wajibu wao wa msingi katika malezi ya watoto kwa kuhakikisha wanawapatia mahitaji muhimu, kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili pamoja na kujenga utamaduni wa kuzungumza nao mara kwa mara ili kufahamu changamoto zinazowakabili.
Simba ambaye pia ni Katibu wa Elimu, Malezi na Mazingira wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro, alisema changamoto za kiuchumi ndani ya familia zimekuwa chanzo kingine cha mmomonyoko wa maadili, kwani baadhi ya wazazi hutumia muda mwingi katika shughuli za kujitafutia kipato na kushindwa kusimamia malezi ya watoto wao ipasavyo.
Alieleza kuwa kukosekana kwa muda wa wazazi kuwa karibu na watoto kunawafanya vijana wengi kutafuta malezi na ushauri kutoka kwa marafiki au mitandao ya kijamii, jambo ambalo wakati mwingine huwapeleka katika mwenendo usiofaa na hatimaye kuathiri mustakabali wao.
Katika hatua nyingine, aliwataka wazazi, viongozi wa dini pamoja na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kurejesha maadili mema kwa vijana kwa kuhimiza uzalendo, heshima, uwajibikaji na kuthamini utamaduni wa Kitanzania ili kujenga taifa lenye vijana wenye nidhamu na maadili bora.
Katika maadhimisho hayo, washiriki walishiriki pia katika shughuli mbalimbali za kijamii zikiwemo upandaji wa miti ya kivuli na matunda katika mazingira ya Shule ya Sekondari Kisangara kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Aidha, hafla hiyo ilihitimishwa kwa utoaji wa vyeti vya pongezi kwa shule za sekondari za serikali na binafsi zilizofanya vizuri katika masuala mbalimbali ya elimu na nidhamu, hatua iliyolenga kuhamasisha ushindani chanya na kuongeza kiwango cha ufaulu katika wilaya ya Mwanga.
Maadhimisho hayo yalienda sambamba na kauli mbiu isemayo, “Malezi bora ni msingi wa taifa,” ikiwa ni wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya maadili mema, uzalendo na uwajibikaji kwa ajili ya kujenga taifa imara la baadaye.










