Na. Edmund Salaho – Dodoma

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Ashatu Kijaji leo Mei, 15 2026 amebainisha kete nne muhimu zitakazotumiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake ili kufikia lengo la watalii millioni nane (8) ifikapo mwaka 2030 pamoja na kuongeza mchango wa Sekta ya Utalii katika pato la Taifa kutoka asilimia 17 mwaka 2025 hadi asilimia 20 mwaka 2030.

Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Bungeni, jijini Dodoma Waziri Kijaji alitaja kete hizo ambazo Wizara imejipanga vilivyo kutumia ili kuongeza idadi ya watalii katika maeneo ya vivutio nchini kuwa ni matukio ya Kimataifa yatakayofanyika nchini.

“Wizara itaendelea kutumia fursa na mikakati mbalimbali ya kukuza utalii kupitia matukio ya kimataifa kama Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Nchi za Afrika (Africa Cup of Nations – AFCON) 2027, Shindano la 74 la Ulimbwende wa Dunia 2027 – Miss World 2027, Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (Inter-Parliamentary Union (IPU) Assembly) Tukio la World Travel Awards (WTA) 2026 ambayo yote yanatarajiwa kufanyika nchini ” alisema Waziri Kijaji

Mkutano wa Umoja wa Mabunge duniani unakutanisha Mabunge ya Nchi wanachama wa umoja wa mabunge Duniani na utafanyika mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu 2026 Jijini, Arusha unatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 1,500 wakiwemo Maspika 183 kutoka nchi mbalimbali duniani ambapo Tanzania ni mwanachama na mwenyekiti wa umoja huo.

“Na kuongeza kuwa Tukio la kimataifa tuzo za ubora katika Sekta ya Utalii duniani (World Travel Awards (WTA) 2026) linatarajiwa kufanyika nchini mwezi Desemba, 2026 nchini linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,000 kutoka Mabara ya Afrika, Ulaya, Asia, Amerika ya Kaskazini na Kusini, huku Shindano la 74 la Ulimbwende wa Dunia 2027 (Miss World 2027) likiwa ni miongoni mwa mashindano makubwa duniani yanayojulikana kama Big Four Beauty Pageants linatarajiwa kufanyika nchini mwezi Mei, 2027 na linatarajiwa kuhudhuriwa na watu takriban 20,000 wakiwemo washindani 120 kutoka nchi mbalimbali Duniani”.

Aidha, Waziri Kijaji aliongeza kuwa kete nyingine ni Mashindano ya AFCON 2027 yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) yanatarajiwa kufanyika kwa pamoja katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania. Mashindano hayo yatahusisha timu 24 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na yanatarajiwa kuvutia zaidi ya watazamaji milioni 1.8 viwanjani pamoja na watazamaji wa televisheni bilioni 1.9 duniani kote kupitia vituo zaidi ya 185 vya utangazaji na yanakadiriwa kuzalisha faida za kiuchumi zinazoweza kufikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 2.

.

Wizara pia imeandaa mkakati maalum wa kuitangaza Tanzania kama kivutio cha kipekee cha utalii kabla na baada ya mashindano ya Kombe la dunia kwa kuandaa kampeni za kimataifa za utangazaji kupitia Mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA 2026 yatakayofanyika nchini Marekani, kwa kushirikisha wadau na mbalimbali wakiwemo watangazaji maarufu wa michezo, watu wenye ushawishi mkubwa pamoja na matumizi ya majukwaa ya kidijitali na mabango katika maeneo ya kimkakati.