Wiki iliyopita nilikuwa mkoani Mara. Nilifika katika Kijiji cha Sabasaba wilayani Butiama, mahali ambako roho takribani 40 za Watanzania zilipotea katika ajali iliyohusisha magari matatu — mawili yakiwa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kati ya miji ya Sirari, Musoma na Mwanza.

Nilipofika mahali hapo, mwili ulinisisimka kwa sababu fikra zangu zilinirejesha ‘kuwaona’ binadamu 40 waliokufa wakiwa wamepangwa pamoja!

Katika hali ya kawaida, hata kama ukikuta mahali kuna miili 40 ya panya waliokufa utashtuka! Pia, huwezi kuona ni jambo la kawaida ukikuta mahali kuna miili 40 ya paka  waliouawa halafu ukashindwa kuonesha mshangao! Kama unaweza kushtuka kwa kuiona miili 40 ya panya, seuze kwa binadamu?

Mmoja wa majeruhi ninaowafahamu, Lucas Sakara, yupo kijijini kwao Butiama akiuguza majeraha aliyoyapata kutokana na ajali hiyo. Simulizi yake kuhusu ajali hiyo ni jambo la kusikitisha mno. Hadi naondoka huko, kiongozi wa ngazi ya juu kutoka serikalini aliyezuru eneo la tukio na kukutana na baadhi ya majeruhi ni Waziri mwenye dhamana na Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe. Kama anavyopongezwa na wananchi, nami nampongeza.

Jirani kabisa na eneo hili la ajali, kuna kijiji ambacho miaka kadhaa iliyopita watu zaidi ya 20 waliuawa kwa kucharangwa mapanga. Yalikuwa mauaji ya kulipiza kisasi. Kama ilivyo ada, hakuna kiongozi mkuu kutoka serikalini aliyefika kuwapa pole wananchi. Najiuliza, hivi watu wa Butiama au Mkoa wa Mara wamewakosea nini viongozi wakuu wa Taifa hili?

Na ukienda mbali zaidi, unajiuliza, iweje sasa mwaka unaelekea ukingoni Mkoa wa Mara ukiwa hauna Mkuu wa Mkoa kutokana na kifo cha aliyekuwapo? Kwanini Mara iendelee kuwa na kaimu Mkuu wa Mkoa kutoka Mwanza? Na ukidadisi zaidi utataka kujua nini kinachomzuia Rais Kikwete kumteua mkuu mpya wa Wilaya ya Serengeti kwa miaka kadhaa sasa, baada ya yule aliyekuwapo kufariki dunia?

Hivi Mkoa wa Mara umemuudhi nini Rais Kikwete ambacho hataki kukitamka ili kama ni kuombwa radhi, basi wananchi wafanye hivyo?

Wakati namjulia hali Sakara, mmoja kati ya ndugu na jamaa wengi waliofika kumjulia hali aliuliza hivi, “Hivi Rais yuko wapi?” Nilijua lile swali limelengwa kwangu kwa sababu wengi wanaamini mwanahabari hapitwi na jambo au ratiba ya mtu mkubwa kama huyo. Sikulijibu swali hilo, badala yake mmoja miongoni mwetu akauliza kwa njia ya swali, “Rais gani? Nchi hii ina marais wengi, lakini kama ni Rais wa nchi, yuko Marekani”.

Sikushangaa kwa jibu hilo kwa sababu hata vijijini nako wananchi wanafuatilia sana taarifa mbalimbali zinazoandikwa na kutangazwa. Huyu mwananchi alisikia habari za Rais kwenda Marekani kupitia kipindi cha magazetini kinachorushwa na Radio Free Africa kila saa 12:30 asubuhi.

Kwenye jibu lake nikaona niongeze kidogo. Nikasema Rais atakuwa Marekani kwa nusu mwezi kukamilisha dhima mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa unaofanyika New York. Kusikia hivyo, mwananchi mwingine akahoji, “Unasema atakuwa Marekani kwa nusu mwezi, yaani siku 15?” Nikamjibu, “ndiyo”.

Basi, kwa kweli mjadala ulioendelea baada ya majibu hayo nisingependa kuuweka kwenye ukurasa huu. Itoshe tu kusema wote waliokuwapo pale walishangaa na kuonesha chuki ya wazi kwa Rais wao kuwaacha kwa nusu nzima ya mwezi.

Ndugu zangu, Watanzania wanajua, na kwa kweli wanafuatilia mambo yanayofanywa na viongozi wao wakuu.

Mjadala huo ambao kwangu ulianzia kwa Sakara, na baadaye nikakutana nao kwenye mitandao ya kijamii, unawagusa mno Watanzania. Kama Rais wetu ana huruma ya kuwajulia hali wafiwa mbalimbali, inakuwaje anashindwa kufika eneo la tukio ambako wapigakura wake zaidi ya 40 wamefariki dunia?

Unaweza kuuliza, kama yeye alikuwa ‘bize’ na dhima nyingine, wasaidizi wake wakuu — Makamu wa Rais na Waziri Mkuu — kwanini hawakuona umuhimu wa kumwakilisha? Ni kweli kabisa safari zao za kwenda eneo la tukio zisingeweza kurejesha uhai kwa walioupoteza, lakini kwa Waafrika hiyo ingekuwa faraja kubwa kwa wafiwa na majeruhi. Rais akaona hilo halina maana isipokuwa kujiandalia nusu mwezi wa kuwa nchini Marekani.

Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi wa nchi hii kukaa ughaibuni kwa muda mrefu kiasi hicho. Rais wa Awamu ya Tatu, Mzee Benjamin Mkapa, alishafanya hivyo. Lakini tofauti na huyu wa sasa, Mzee Mkapa alikuwa mgonjwa.

Wananchi wanahoji uhalali wa Rais Kikwete kuwa nje ya nchi — si kwa sababu ya wivu wa safari — bali uhalali na umuhimu wenyewe wa shughuli za kumkalisha huko kwa nusu mwezi. Kundi la watu alioongozana nao kwenda huko litakuwa mstari wa mbele kuwalaani wote wanaohoji ‘matumbuzi haya’, na kwa kweli wanaojiweka mbele kuhoji wanaweza kujikuta matatani, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa kama Rais si mgonjwa, hakuna sababu ya msingi ya kuwaacha wananchi wake kwa nusu mwezi akiwa ugenini kwa Rais mwenzake.

Hii imenikumbusha vitabu tulivyosoma miaka ile vilivyoeleza “mgeni siku ya kwanza, mgeni siku ya pili, mgeni siku ya tatu, hadi mgeni ile siku ya mwisho ya kuondolewa ugenini kwa fedheha!” Haitashangaza kuona siku moja viongozi wa Tanzania wakifurushwa kutoka Marekani kwa sababu yawezekana sasa tukawa tumechokwa.

Tumekuwa tukihoji safari nyingi za viongozi katika nchi hii kushindia Marekani. Miongoni mwao ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye anaweza kwenda Marekani mara mbili kwa wiki. Lakini kama ‘mwajiri’ wao mwenyewe ndiye anayekuwa wa kwanza kwenda kuishi huko kwa nusu mwezi, hapo tutarajie nini?

Je, ni kweli kwamba Rais wetu ndiye kipenzi cha Rais Barack Obama na Wamarekani kuliko marais wengine Afrika na duniani?

Katika ziara hii tunaambiwa moja ya shughuli iliyo kwenye ratiba yake ni ile ya kuhudhuria ‘Usiku wa Jakaya’ jijini Washington, ambako watakaotaka kuifaidi hafla hiyo watalazimika kulipa dola 100 za Marekani (Sh 170,000). Shughuli ya aina hii ina tija gani kwa Watanzania waliobaki huku nyumbani? Ina msaada gani kwa vijana kama yule wa Sekondari ya Ihungo mkoani Kagera aliyeamua kujitoa uhai kwa sababu ya kukosa matibabu?

Jamani, Watanzania wanauliza, na kwa kweli wanastahili kupata majibu, tija ya hizi ziara za nusu mwezi ndani ya Marekani ni zipi? Hizi ziara zinatokana na ukarimu wa Wamarekani kwa Tanzania, au ni sisi Watanzania kupitia viongozi wetu tulioamua kujipendekeza kwa Wamarekani? Kama ni ukarimu, iweje ukarimu huu uwe wa kiwango cha juu namna hii, hasa wakati huu ambao tunagundua gesi na kuna dalili ya kuwapo mafuta nchini mwetu? Haya mapenzi ya ghafla ya Wamarekani na wakubwa wengine wa Ulaya na Asia kwa Tanzania yanasababishwa na nini?

Juzi tu, Rais wetu alikuwa miongoni mwa marais wa Afrika walioitwa na Rais Obama kwenda Marekani kutafuta mwarobaini wa matatizo ya Afrika. Rais wetu akakaa huko kwa siku zaidi ya 10. Haujapita mwezi anarejea tena; lakini safari hii anakaa kwa nusu mwezi. Hapa ikumbukwe kuwa haya anayafanya akiwa bado hajaanza kuaga. Hivi mwaka kesho akianza kuaga, si nchi itaongozwa na kaimu rais kwa mwaka mzima?

Ni ukweli ulio wazi kuwa dunia ya leo kila nchi inajitahidi sana kuvutia wawekezaji na kwa sababu hiyo kujitangaza ni jambo muhimu pia. Tumetumia vigezo gani kwa Tanzania kumtumia Rais wetu kujitangaza au kuvutia wawekezaji hao? Ina maana Korea Kusini au mataifa mengine ya Asia yalipovutia uwekezaji kutoka Marekani viongozi wake walipiga kambi nchini Marekani kama anavyofanya Rais wetu?

Ziara za Rais Kikwete nchini Marekani au ughaibuni kwa jumla zinaligharimu sana Taifa letu. Gharama za safari hizo zinafanywa na zitaendelea kufanywa siri kwa sababu ni kubwa mno. Kumlaza Rais na ujumbe wake ndani ya hoteli ya hadhi ya nyota tano kwa nusu mwezi ni gharama kubwa sana.

Kama gharama si za kuwakomoa Watanzania, basi wahusika wajitokeze watueleze kwa sababu siamini kama kweli kila ziara anayofanya huko amekuwa akigharimiwa na rafiki yake, Rais Obama.

Kama hizo ziara zinagharimiwa na hao wenyeji wetu, tupewe majibu ya namna au aina ya fadhila tulizoandaa kuwalipa kwa sababu wao wenyewe wanasema katika ulimwengu wa leo hakuna free lunch!

Huku mitaani wananchi wanasema Kikwete kama aliamua kuwa Rais, maana yake alikubali kuwatumikia wananchi akiwa ndani ya nchi. Wanasema miaka 10 aliyokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa huenda ndiyo iliyompa ‘haka kaugonjwa ka kutaka kusafiri kila mara’ akidhani kuwa bado yupo kwenye ofisi hiyo.

Lakini wengine wanakwenda mbali zaidi kwa kusema kama utaratibu wenyewe ndiyo huu, basi mwakani Watanzania wahakikishe wanapambana ili rais awe yeye pia ndiye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Wanasema hivyo kwa kigezo kwamba hatua hiyo itasaidia kuokoa bajeti ya wizara ambayo kwa mtazamo wa mbali ina waziri na naibu, lakini kwa uhalisia ina ‘mawaziri watatu’. Haya ni maneno yanayozungumzwa sana na wananchi, na kwa kweli wana haki ya kuhoji.

Nami kwa upande wangu sioni sababu ya kutoungana nao kuhoji wingi na urefu wa ziara za watawala wetu chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Kikwete.

Nilichotumwa nimfikishie Mheshimiwa Rais kutoka kwa wananchi wa Sabasaba ni kwamba kitakachosalia kwenye ziara yake ya nusu mwezi Marekani, akifikishe pale Sabasaba japo kwa kujenga mnara mdogo wa kuwakumbuka ndugu zetu 40 waliopoteza maisha katika ajali iliyohusisha mabasi ya Mwanza Coach na J4.

Lakini ambalo linahitaji ujasiri kumwambia Rais ni kwamba wananchi wanashangazwa mno kuona kiongozi wao mkuu akiwaacha kwa nusu mwezi nzima — akiwa ughaibuni. Wanasema hii ni rekodi kwa heshima yake,  lakini ni maumivu makali sana kwa walipakodi.

Wanaouliza kama ningekuwamo kwenye msafara huo mnono ningediriki kuhoji? Jibu langu ni: “Ndiyo, ningehoji”.

By Jamhuri