Baada ya kutambua maana na aina ya uhuru katika sehemu ya kwanza ya makala hii, leo nakamilisha kwa kuangalia kanuni na taratibu za uhuru. Uhuru una thamani unapotekelezwa kwa kuzingatia kanuni zilizopo na kusimamiwa na taratibu zilizokubaliwa na watu walio huru.

Hadhari kuwa si binadamu (mtu) tu ndiye mwenye uhuru. Wanyama, ndege na wadudu kadhalika wanao uhuru. Viumbe vyote duniani vimepewa uhuru tangu zama na zama na muumba mwenyewe, Mwenyezi Mungu. Uhuru ni haki ya kila kiumbe wala si fadhira kwa binadamu.

Kwa vile kila kiumbe kina uhuru, binadamu asitumie uhuru wake kuangamiza uhuru wa viumbe vingine pale anapotumia uhuru vibaya kwa kuanzisha balaa la vita. Vita ni kama mtego wa panya, hunasa mhusika na asiye husika.

Yakini, uhuru utumike katika dhamira njema kuunda umoja na mshikamano, kutoa mawazo, ushauri na uamuzi katika kuleta maendeleo ya watu. Uhuru uwe na uwezo wa kutunza na kulea tabia nzuri, heshima, utu na hifadhi ya mali za watu.

Uhuru wa mtu si kutumia nguvu kukandamiza uhuru wa watu wengine au kutamka kauli za dharau, vitisho, kejeli, hiyana au kutoa amri kuzuia uhuru wa wengine bila ya kufuata taratibu zilizopo. Anayetumia mtindo kama huu, ni wazi hatambui maana, kanuni, taratibu na thamani ya uhuru alionao, na uhuru wa wengine.

Aina zote tatu za uhuru kwa pamoja hutengeneza uhuru wenye nguvu kisheria. Sheria ya kudhibiti, kuzuia na kulinda uhuru wa mtu usipotee. Sheria inayombana mtu au watu wanaodhani wao ndio wenye uhuru na uwezo kufanya makusudi makosa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa na wasibughudhiwe na mtu au mamlaka yoyote.

Katika muktadha kama huu, watendao makosa wanatumia maarifa yao kutimiza juhudi zao za uonevu na dhuluma kwa watu walio huru, badala ya kutumia ukweli katika masuala ya maendeleo na ukombozi wao.

Watu walio huru katika umoja au utaifa wao wanatambua dhuluma si haki, uonevu si haki wala nguvu si haki katika taratibu za uhuru. Hawathubutu kutumia dhana hizi kama maarifa na juhudi za kujiletea maendeleo yao. Wanatambua dhana hizi ni silaha za kuua haki au uhuru wa mtu.

Unapoua haki au uhuru wa mtu (watu) dhahiri unaua haki au uhuru wako. Unakuwa kama pweza anayejipalia makaa ya moto kwa mikono yake akidhani anaondoa makaa ya moto kunusuru mwili wake kuunguzwa, kumbe sivyo. Anaungua.

Si busara mtu kutumia uhuru wake kuvuruga taratibu za uhuru wa mtu binafsi, jumuia au taifa. Huku akitoa maelezo, anatafuta uhuru wake, akidhani ameporwa. Ilhali hajaporwa kwa mujibu wa kanuni na makubaliano ya umoja wao. (kijumuiya au kitaifa).

Iko migogoro inayotokana na matumizi ya uhuru, kuanzia kwenye familia hadi taifa, kwa sababu watu hawataki kutii kanuni na taratibu za uhuru au watu hao hawaelewi mipaka ya uhuru. Haya ni masuala mawili yanayohitaji kufumbuliwa ili kuondoa migogoro hii.

Suala la kutoelewa linaweza kuondolewa na vyombo vyenye dhamana ya kutoa elimu ya maarifa, elimu ya siasa, mafunzo ya uraia, sheria na vyombo vya ulinzi na usalama, bila kusahau itikadi za vyama vya siasa.

Kukataa kutii kanuni na kutofuata taratibu zilizopo ni wazo la mtu binafsi. Baadhi ya watu wapo radhi kudhulumu nafsi zao na za wenzao wakidhi mahitaji au malengo yao. Watu kama hawa wapatiwe mafunzo ya kiroho na taasisi zinazohusika na haki au uhuru utokao kwa Mwenyezi Mungu.

Vyombo vyote hivi vikijitambua viko huru na vina uhuru wa kujenga umoja wa watu, kulea na kurekebisha tabia za watu, suala la kutotii litapungua au kutoweka. Tuseme na kuimba pamoja, “Uhuru una kanuni na taratibu zake, inawezekana twendeni pamoja.”

Please follow and like us:
Pin Share