Salamu nyingi sana wote mliotembelewa na rais, hasa mikoa ya Kusini ambako alikuwepo kuwapa salamu na shukurani za kumchagua, lakini kubwa zaidi kuzindua na kufungua miradi ambayo kwa mujibu wa sera za chama chake waliahidi watatekeleza. Naamini mmefurahi kuona mambo yenu yanakwenda mswanu.

Pamoja na ziara hiyo, kwa sisi tulioko mikoa mingine, naomba tuwe wavumilivu kidogo, naamini atapanga ziara maalumu kuja huko na kutatua kero mbalimbali ambazo zipo na pengine kufungua na kuzindua miradi mingine ambayo iko tayari.

Kusema kweli nimekuwa mfuatiliaji wa ziara yake kwa sababu inarushwa moja kwa moja na vyombo vingi vya habari, pamoja na kwamba mambo ni mengi kwa wakati mmoja, najitahidi kuyapanga kutokana na vipaumbele.

Kilichonifurahisha zaidi katika ziara hii ni uwazi ambao tumeuona kutoka kwa watumishi na wananchi kwa ujumla, sina hakika kama yaliyakuwa yamepangwa kama ambavyo wengi wanadhani, lakini nina uhakika kwa matukio yote yaliyowagusa wananchi ni ‘titi fo tati’, yaani vidole na macho kwa waliokula hela.

Ziara hizi za rais zinanifundisha na kunikumbusha mengi juu ya uongozi ambao wachache wetu tumepitia kwa awamu zote tano. Nataka kuzifananisha ziara hizi na mbio za mwenge za awamu ya kwanza, wakati ule mwenge ukipita ndipo unapoona mabaya yanafichuka, na ilitufanya  tuamini mwenge na imani za macho ya moto, ulikuwa mwenge wa kumulika maovu na uhujumu uchumi kweli.

Leo nijikite katika jambo moja kubwa kidogo kwa uelewa wangu na ninaamini baadhi ya watu hawatakubaliana nami juu ya jambo hili la kujitoa mhanga kwa kiongozi ambaye hayuko madarakani ili kubeba wenzake wapate ulua pamoja.

Sisemi haya eti kwa sababu kuna awamu yoyote ambayo imewahi kufanya hivyo, la hasha! Isipokuwa mfumo wa uongozi kwa awamu zingine, ukiwamo ule wa Mwalimu Julius Nyerere, ulikuwa na upungufu wake, na hata huu ni lazima kutakuwa na upungufu wake, kwa kuwa viongozi si malaika wenye macho katika mioyo yao.

Tumeshuhudia kutojiamini kwa baadhi ya viongozi waandamizi wanaomuwakilisha kiongozi wao mkuu, hasa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Wapo ambao wanakaa ofisini na hawafuatilii utekelezaji wa moja kwa moja kwa wananchi, hawa tunawaona wakishindwa kujibu maswali hadharani, hasa yale ambayo yangeweza kujibika kwa sababu za kiutawala.

Tunajifunza kuwa baadhi bado hawawezi kwenda na kasi ya mabadiliko ambayo yamekuwepo kwa takriban miaka minne tangu awamu hii ilipoingia madarakani. Viongozi wa namna hiyo utawatambua kwa kufanya fitina na kujipendekeza zaidi badala ya kufanya kazi na kusema ukweli.

Wapo viongozi ambao wanadhani wanatakiwa kufanya kazi kwa kumfurahisha aliyewateua badala ya kuwafurahisha anaowaongoza, na hapo ndipo unapoona misuguano na kiongozi wao anapowataka kutoa taarifa mbalimbali.

Mwenyewe alijitanabaisha kwamba yupo kwa ajili ya wananchi na hayupo kwa ajili ya viongozi, na hilo limekuwa fumbo kwao na kushindwa kuelewa kwamba angelipenda kila anapokwenda aone wananchi hawana kero katika mambo muhimu juu yao.

Limekuwa ni jambo la kawaida kuona wananchi wakihoji kuhusu mambo ya maendeleo katika maeneo yao. Kiufupi na si kwa nia ya kuwachongea, nadhani nao wameamua kuungana na ziara ya bosi wao badala ya kufanya wao wakajua kero na kuzitatua.

Hawa ni wachache sana walioibuka katika ziara ya rais na wakawa ziarani, lakini wapo wengi ambao nadhani hata rais hapaswi kwenda kutatua kero za wananchi, kwa kuwa aliyepo anazifanyia kazi japo kuna kasoro ndogondogo za kibinadamu.

Naunga mkono maazimio yote aliyoyafanya, pia ninaunga mkono mambo mengi kuwekwa wazi katika hotuba zake, usiri unaojificha katika mambo mengi unatufanya tukose uaminifu kwa viongozi wetu wachache. Maendeleo katika maeneo yetu kamwe hayawezi kuletwa na mtu kutoka nje, nimeiona hiyo fursa kwa viongozi mliotembelewa pamoja nasi huku Kusini.

Mambo ya ziara ya rais mikoani sasa hivi ni kama mwenge wetu wa zamani ambao ulikuwa ukipita tu utawasikia watu wote waliotuhujumu, utawasikia viongozi wote waliokiuka maadili ya uongozi, utawaona walanguzi na miradi iliyokuwa imedoda inafufuliwa.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

Please follow and like us:
Pin Share