Kuwa na nidhamu utimize ndoto yako

Kama yalivyo muhimu mafuta kwenye gari, ndivyo ilivyo nidhamu kwa mtu yeyote mwenye ndoto. Nidhamu ni kiungo muhimu kwa mtu anayetaka kutimiza ndoto yake. Kuna aliyesema: “Nidhamu ni msingi wa maisha yenye furaha na mafanikio.”

Ni wazi kuwa umesikia watu wengi wakitaja siri za mafanikio neno ‘nidhamu’ huwa halikosi. Vitu vinavyowafanya watu wengi wafanikiwe ni vitu vya kawaida, ambavyo tangu tukiwa wadogo tunaambiwa, lakini kutokana na kuvipuuza ndipo tunaanza kupishana na mafanikio, mafanikio yanakwenda kusini wewe unaelekea kaskazini.

Unapotaka kutimiza ndoto zako hakikisha unaweka nidhamu mstari wa mbele. Kuwa na nidhamu kwa kila mtu, haijalishi awe mkubwa au mdogo, usijali kabila, wala rangi, unaweza kumdharau mtu leo kesho na kesho kutwa ukamkuta akiwa na cheo cha kuweza kukupandisha juu, lakini kwa sababu siku za nyuma ulimdharau, si rahisi wewe kufika unakotaka kufika.

Msalimie kila mtu unayepishana naye njiani bila kujali umri, kazi au mwonekano wake. Ukweli huu unawekwa wazi na Tom Hardy aliyewahi kusema: “Nilikuzwa katika mazingira ya kumpa heshima mfagiaji kama ninavyompa heshima mkurugenzi wa kampuni.”

Ukitaka kuwa na nidhamu kwa wengine, kwanza kuwa na nidhamu kwako mwenyewe, wanasema jiheshimu, uheshimiwe. Ukitaka watu wakuheshimu, lazima kwanza uanze kwa kujiheshimu. Siku zote tunapokea kile tunachokitoa.

“Bila nidhamu, hakuna maisha kabisa,” anasema Katharine Hepburn. Nidhamu yako ianzie katika maneno unayoongea na wakati mwingine maneno unayoyaandika.

Nilipokuwa nikisoma mateso ya Yesu alipokuwa pale msalabani kuna kitu kikubwa nilikigundua; mdomo unaweza kukuponya au kukuangamiza.

Yesu alipokuwa msalabani pembeni yake alisulubiwa pamoja na wahalifu wawili. “Mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema: ‘Je wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.’ Lakini yule wa pili ambaye kwa mapokeo ya Kanisa Katoliki anaitwa Dismas au Demascus, huyu alikaa upande wa kulia wa Yesu, akamkemea yule mhalifu mwenzake akisema:

‘Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu hiyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tunayostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa. Kisha akasema, ‘Ee Yesu nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.’ Yesu akamwambia: ‘Amin, nakuambia leo hii utakuwa nami mbinguni.’” (Luka 23:39-43).

Huyu mhalifu wa pili (Dismas) maneno yake mazuri yalimvusha na kumtoa katika kundi la wahalifu katika dakika za mwisho. Alikuwa amefungwa mikono na miguu lakini alijua kwamba ulimi wake haujafungwa hivyo anaweza kunena neno jema kabla hajakata roho.

Chunga sana maneno unayoyatamka, maneno ni kama risasi, yakitoka yametoka. Ni rahisi sana kuongea bila kufikiri lakini ni vigumu kufanya ulimi urudishe maneno yaliyotamkwa.

Tulipokuwa jeshini kwa mujibu wa sheria, maafande walizoea kutwambia hivi: “Mdomo ukusaidie mesini,” au kwa tafsiri rahisi, mdomo ukusaidie wakati wa kula. Kumbuka: “Unapofungua kinywa chako, unaiambia dunia wewe ni mtu wa namna gani,” anasema Les Brown.

Kuna mtu aliyewahi kusema: “Chunga sana mawazo yako, yanakuwa maneno yako. Chunga sana maneno yako, yanakuwa matendo yako. Chunga sana matendo yako, yanakuwa mazoea yako. Chunga tabia zako, zinakuwa hatima yako.”

“Ukiwa na nidhamu binafsi karibu kila kitu kinawezekana,” alisema Theodore Roosevelt, rais wa zamani wa Marekani. Unahitaji pia nidhamu katika matumizi yako ya muda. Ukiwa na nidhamu ya muda utajipa muda wa kufanyia mazoezi kipaji chako, watu waliofanikiwa wameweka nguvu katika muda wa kuendeleza vipaji vyao. Nakubaliana na David Campbell aliyewahi kusema: “Nidhamu ni kukumbuka kile unachokitaka,” Kama unataka kutimiza ndoto zako, anza kwa kuwa na heshima kwenye matumizi ya muda wako.

“Yule asiyeishi maisha ya nidhamu, atakufa akiwa amekosa heshima,” unaweka wazi msemo wa watu wa Isilandi. Mavazi unayovaa mbele za watu yanaonyesha wazi watu wakuchukulie wewe ni mtu wa namna gani. Kumbuka, “watu wanahukumu kitabu kutokana na jalada lake.” Jinsi unavyovaa watu watakupa maana kutokana na mwonekano wako.

Vaa kwa unadhifu na usafi siku zote. Inalipa kuwa mtanashati, hapa kumbuka simaanishi kwamba uvae mavazi ya gharama, hapana. Vaa kama unavyotamani watu wakuone na waseme kitu kuhusu wewe. Mwisho, kuwa na nidhamu katika matumizi ya pesa, weka akiba unapopata pesa, usisubiri utumie ndipo uweke akiba, hautaweza.

Please follow and like us:
Pin Share